Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jiwe la kilo 3.1 laondolewa kwenye kibofu cha mwanaume
- Author, BBC Sinhala
- Author, Koh Ewe
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Madaktari nchini Sri Lanka wamefanikiwa kuondoa jiwe kwenye kibofu cha mwanaume lenye uzito wa kilo 3.1 ambalo wanaamini kuwa ndilo kubwa zaidi la aina yake kuwahi kurekodiwa.
Upasuaji huo ulifanyika katika hospitali moja mjini Trincomalee, mashariki mwa nchi hiyo.
Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 55 alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kupata kiharusi. Hata hivyo, wakati akipatiwa matibabu, madaktari waligundua jiwe katika kibofu chake cha mkojo baada ya kubaini kwamba alikuwa akipata shida ya kukojoa.
Wakati wa upasuaji, madaktari waliondoa jiwe hilo la kibofu ambalo lilikuwa na uzito sawa na ule wa mtoto mchanga aliyekamilika kukua tumboni na ukubwa wake ulikuwa karibu na ule wa yai la mbuni.
"Kulingana na rekodi zilizopo, hili ndilo jiwe kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa na kutolewa kwenye kibofu cha mkojo kupitia upasuaji," Dkt. Pragalathan Balakrishnan, aliyeongoza upasuaji huo, aliambia BBC Sinhala.
Aliongeza kuwa mgonjwa huyo ana "afya njema sana".
Madaktari walisema mgonjwa huyo bado yuko hospitalini na anaendelea kupata matibabu kwa ajili ya matatizo mengine ya kiafya aliyonayo.
Dkt. Balakrishnan aliongeza kuwa jiwe hilo huenda lilikuwa ndani ya kibofu cha mgonjwa kwa takriban miaka mitano hadi kumi.
Mawe ya kibofu hutokea wakati madini yaliyomo kwenye mkojo yanapoganda na kuwa vipande vigumu.
Mara nyingi hutokea wakati kibofu hakitoi mkojo wote, na kuacha mkojo uliojaa madini mengi (uliofanya mgando) ambao unaweza kugeuka kuwa mawe madogo.
Mawe madogo ya kibofu, yenye ukubwa wa punje za mchanga, yanaweza kutoka yenyewe. Hata hivyo, mawe makubwa zaidi ya sentimita 1 mara nyingi huziba njia ya mkojo na kuhitaji matibabu. Jiwe la kibofu lenye ukubwa unaozidi sentimita 4 huchukuliwa kuwa kubwa sana.
Kulingana na rekodi za dunia za Guinness, jiwe kubwa zaidi la kibofu liliondolewa kwa mgonjwa nchini Brazil mwaka wa 2003. Lilikuwa na uzito wa kilo 1.9 (pauni 4.2) na urefu wa sentimita 17.9 (inchi 7).
Jiwe la kibofu lililoondolewa nchini Sri Lanka wiki iliyopita lilikuwa na urefu wa takriban sentimita 17.
BBC Tamil ilimuuliza Dkt. Balakrishnan Prahaladhan kuhusu jambo hili. Maswali aliyoulizwa na BBC Tamil pamoja na majibu yake yametolewa hapa chini.
1. Je, ni changamoto zipi zinazokabili utekelezaji wa taratibu hizi za upasuaji?
Hatukuweza kufanya upasuaji mara moja. Sababu ilikuwa ni uzito mkubwa wa jiwe hilo na pia mgonjwa alikuwa amepatwa na kiharusi.
Kama ilivyo kwa mishipa ya fahamu inayoelekea mikononi na miguuni, figo nazo zina mishipa ya fahamu. Kwa kuwa mshipa huo ulikuwa umeharibika, mtiririko wa damu uliathirika.
Kutokana na kiharusi na matatizo ya mzunguko wa damu, shinikizo ndani ya mfuko wa figo liliongezeka, shinikizo la damu likapanda, na mkojo haukutiririka kwenda chini bali ulianza kutiririka kuelekea juu kwenye figo.
Matokeo yake, utendaji kazi wa figo uliathirika. Upasuaji haukuweza kufanyika mara moja. Sababu ni kwamba mgonjwa lazima awe na nguvu mwilini ili kufanyiwa upasuaji. Ili kulinda figo, tulichukua hatua za kupunguza shinikizo ndani ya mfuko wa figo. Kulikuwa na tatizo katika hilo.
Kutokana na uharibifu uliosababishwa na jiwe hilo, ilikuwa vigumu kuingiza mirija kwenye mfuko wa figo. Ikiwa mirija hiyo haikuingizwa kwa usahihi, ilikuwa ikitoka yenyewe.
Kwa kuwa kila kitu, ikiwemo utendaji wa moyo na ubongo, kilikuwa katika hali ya kawaida, tulifanya upasuaji huo. Alilazwa hospitalini mwezi Julai. Tulikuwa tumepanga kufanya upasuaji huo mwezi Agosti.
2. Je, kuna jambo lolote lisilo la kawaida lilitokea wakati wa upasuaji huu?
Ndiyo. Aliwahi kufanyiwa upasuaji kama huu wa kuondoa jiwe dogo hapo awali. Upasuaji huo ulifanyika mwaka wa 1998. Ikiwa ni jiwe dogo, hatulitoi kwa njia ya kukata mwili; badala yake, tunaingiza kamera na kutumia leza kulivunja na kuliondoa. Hata hivyo, ikiwa jiwe ni kubwa zaidi ya sentimita 4, itachukua muda mrefu kuliondoa kwa leza. Kwa hiyo, tutalitoa kwa njia ya upasuaji wa kawaida (kukata).
Mwaka wa 1998, kutokana na ukosefu wa vifaa hivyo, alifanyiwa upasuaji kwa kukatwa tumbo. Hiyo ndiyo sababu ilikuwa na changamoto kidogo.
Kwa upande mwingine, hakukuwa na ugumu wowote katika utaratibu wa upasuaji wenyewe; ulikuwa kama utaratibu wa kawaida wa upasuaji.
3. Ilichukua muda gani kuondoa jiwe hilo kabisa na kukamilisha upasuaji?
"Ilichukua takriban saa moja."
4. Je, jiwe kubwa namna hiyo linajitengenezaje?
"Sababu kuu ya kutokea kwa mawe, hasa kwenye kibofu cha mkojo, ni kutotiririka vizuri kwa mkojo. Kwa wanaume, baada ya umri wa miaka 40 au 50, tezi iliyo chini ya kibofu cha mkojo huwa kubwa.
Inapokuwa kubwa mkojo hautiririki ipasavyo na inakuwa vigumu kukojoa. Mtu huhisi kukojoa mara kwa mara. Hata baada ya kukojoa, bado kuna hisia ya kutaka kukojoa tena, na mtu huhisi kulazimika kuamka usiku. Hii ndiyo sababu ya hali hiyo inayojulikana kama 'Lutz'.
Hali kama hiyo inapokuwepo, kuna uwezekano wa kupata maambukizi ya figo. Sababu hizi mbili zinaweza kusababisha kutokea kwa mawe kwenye mfuko wa figo.
Hii ndiyo sababu mawe hutokea kwenye mfuko wa figo. Vinginevyo, mawe kutoka kwenye figo yanaweza kushuka hadi kwenye kibofu na kutengeneza mawe huko. Hata hivyo, ni nadra sana mawe hayo kuwa makubwa.
Jiwe linaposhuka kutoka kwenye figo, mgonjwa huhisi maumivu. Kwa hiyo, jiwe hilo linaweza kugundulika mapema. Tatizo la kukojoa linapokuwepo, jiwe hilo litaendelea kuwa kubwa zaidi ikiwa halitashughulikiwa.
5. Unadhani ilichukua muda gani kwa jiwe hili kukua na kufikia ukubwa huu?
"Huenda ilichukua takriban miaka 5 hadi 10."
6. Kuna taarifa kwamba jiwe kubwa zaidi duniani limeondolewa kwenye kibofu cha mkojo. Je, hilo ni kweli?
"Hili ndilo jiwe kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa. Tumewasilisha maombi ya kutambuliwa na Rekodi za Dunia za Guinness. Bado kuna hatua chache zilizosalia. Rekodi ya awali katika nyanja hii ni ya jiwe lenye uzito wa kilo 1.9 lililoondolewa nchini Brazil mwaka wa 2003."
7. Je, mgonjwa huyu aliwezaje kuhimili jiwe kubwa kiasi hicho?
Tulizungumza na wanafamilia. Jiwe hilo lilionekana waziwazi. Kulikuwa na uvimbe tumboni ambao hata mtu asiye na ujuzi wa kimatibabu angeweza kuutambua.