Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bidhaa 8 zilizobadilisha dunia
Hapa tunaangazia baadhi ya bidhaa maarufu zaidi za kampuni hiyo, bidhaa zilizoshindwa lakini zikawa na mchango katika kuijenga Apple, na kile ambacho huenda kikafuata.
Apple ilipotimiza miaka 50 mwezi Aprili 2026, tuliona ni wakati mwafaka wa kuangazia baadhi ya bidhaa maarufu zaidi za kampuni hiyo, bidhaa zilizoshindwa lakini zikasaidia kuijenga, pamoja na kile ambacho huenda kikaja baadaye.
Bidhaa zilizofanikiwa
1. Apple II
Ilizinduliwa mwaka 1977, Apple II ndiyo iliyobadilisha Apple kutoka kampuni changa ya kiteknolojia na kuwa kampuni kubwa na yenye ushawishi.
Tofauti na kompyuta za wakati huo zilizokuwa zikilenga zaidi wapenda teknolojia waliokuwa wakijenga mashine zao wenyewe, Apple II iliwasili ikiwa tayari imeunganishwa na kutumika, ikiwa na michoro ya rangi na uwezo wa kuunganishwa kwenye televisheni ya nyumbani.
Hata hivyo, programu za Apple II ndizo zilizokuwa siri ya mafanikio yake makubwa. VisiCalc, programu ya kwanza ya lahajedwali iliyopata matumizi makubwa, ilizinduliwa kwa ajili ya Apple II pekee, na kuifanya kuwa maarufu miongoni mwa biashara ndogo.
Mapato yaliyopatikana yaliisaidia Apple kuingia kwenye soko la hisa mwaka 1980, na kuiwezesha kupata msingi imara wa kifedha ambao ulifadhili kwa kiasi kikubwa maendeleo yake yaliyofuata.
2. Macintosh 128K
Ingawa Apple II iliipa kampuni hiyo mafanikio yake ya kwanza kibiashara, Macintosh 128K ndiyo iliyosaidia kuunda Apple tunayoijua leo.
Iliyotolewa mwaka 1984, Macintosh ilibadilisha namna watu wa kawaida walivyotumia kompyuta, kwa kuondoa hitaji la kutumia mfululizo wa amri za maandishi na badala yake kuleta mfumo rahisi wa kutumia uliodhibitiwa kwa kipanya.
Ingawa mauzo yake hayakuwa makubwa sana, kwa kiasi fulani kutokana na bei yake kuwa juu kuliko kompyuta za IBM zilizokuwa zikishindana nayo, Macintosh ilisaidia kuchochea ukuaji wa uchapishaji wa kidijitali na kuimarisha utambulisho wa Apple kama kampuni iliyotilia mkazo usanifu na uzoefu wa mtumiaji.
3. iMac G3
iMac G3 iliisaidia Apple kurejea kutoka ukingoni mwa kuporomoka chini ya uongozi wa Steve Jobs aliyerejea.
Wakati iMac G3 ilipozinduliwa mwaka 1998, Apple ilikuwa katika hali mbaya. Steve Jobs alikuwa amerejea katika kampuni hiyo muda mfupi tu kabla, baada ya kulazimishwa kuondoka na bodi ya kampuni zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Apple ikiwa karibu kufilisika, ilihitaji kwa haraka bidhaa iliyofanikiwa. iMac G3 yenye rangi angavu na mwonekano wa uwazi ikawa jibu. Ilikuwa kompyuta iliyounganishwa katika kifaa kimoja, iliyobuniwa na Jony Ive, mtu ambaye baadaye alihusishwa sana na mtindo wa Apple wa vifaa vyenye mwonekano maridadi na rahisi.
Pia ilikuwa bidhaa iliyotazama mbele kwa wakati wake, ikiondoa matumizi ya diski za floppy na kukumbatia teknolojia ya USB.
Kipanya chake chenye umbo lililofanana na mpira wa hoki kilizua maoni tofauti, lakini iMac G3 bado ikawa mojawapo ya kompyuta za Apple zilizouzwa kwa kasi zaidi. Iliisaidia kampuni kuondoka kwenye ukingo wa kuporomoka na kuunda upya utambulisho wake chini ya Jobs.
4. iPod ya kizazi cha kwanza
Mwaka 2001, Apple bado ilikuwa kampuni ndogo katika soko lililotawaliwa na kompyuta binafsi. Uzinduzi wa iPod ulibadilisha hilo, na kuifanya Apple kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa kisasa.
Ikiwa na gurudumu rahisi la kusogeza na muunganisho mzuri na iTunes, iPod ilifanya vichezeshi vingine vya MP3 vilivyokuwa sokoni vionekane kuwa vigumu na visivyo rahisi kutumia — jambo ambalo Apple ingeendelea kufanya mara kwa mara.
Zaidi ya mauzo, iPod na baadaye iTunes Store, iliyozinduliwa miaka miwili baadaye, vilibadilisha namna watu walivyonunua na kusikiliza muziki, na kuweka msingi wa vifaa vya simu vilivyofuata.
5. iPhone 3G
Ingawa iPhone ya kwanza iliweka msingi wa mipango ya Apple katika soko la simu janja, iPhone 3G ndiyo iliyofanya mawazo hayo yaanze kutimia kikamilifu.
Pamoja na kuja na huduma muhimu ya intaneti ya kasi zaidi ya 3G, siri kubwa ya mafanikio yake ilikuwa App Store, iliyozinduliwa kwenye kifaa hicho. Ghafla, iPhone haikuwa simu tu, bali kifaa cha burudani na matumizi mbalimbali ambacho kingeweza kufanya karibu kila kitu.
Ndani ya miezi michache, watengenezaji walikuwa wameunda maelfu ya programu na michezo, na kuwapa watumiaji uwezo wa kubinafsisha vifaa vyao kwa kiwango kikubwa.
Mauzo yaliongezeka kwa kasi, washindani wakaanza kukimbizana na Apple, na enzi ya simu janja za kisasa ikaanza — huku Apple ikipanda hadi kilele cha ulimwengu wa teknolojia.
Bidhaa zilizoshindwa
1. Apple III
Katika jaribio la kutumia mafanikio ya Apple II, Apple III iliingizwa sokoni kwa haraka bila kufanyiwa majaribio ya kutosha, huku kampuni ikilenga kushindana na IBM katika soko la kitaalamu.
Muundo wake usiotumia feni ya kupooza ulikuwa wa kimapinduzi, lakini ulisababisha matatizo ya joto kupita kiasi na kutokuwa thabiti kwa mashine.
Kompyuta hiyo ilishindwa kibiashara na kuharibu sifa ya Apple katika miaka yake ya mwanzo, kosa la gharama kubwa lililofundisha kampuni hatari za kukua kwa haraka kupita kiasi.
2. Apple Pippin
Pippin ilikuwa jaribio la Apple kuleta uzoefu wa kutumia Mac sebuleni, huku ikiunganisha teknolojia hiyo na michezo ya kampuni nyingine kwa mfumo wa aina ya koni ya michezo.
Ingawa ilikuwa na uwezo mzuri kiteknolojia, iliingia sokoni wakati PlayStation ikiwa katika kilele cha mafanikio. Bei yake ya juu, ukosefu wa michezo ya kutosha na kutokuwa na nafasi iliyoeleweka sokoni kulifanya ishindwe kushindana.
Apple ilitarajia kuuza vifaa 500,000 lakini iliuza 42,000 pekee.
3. Apple Vision Pro
Ikiwa na teknolojia ya hali ya juu ya lenzi na programu, kifaa cha kwanza cha Apple cha uhalisia mseto kilivutia wakosoaji, na bado kinachukuliwa na wengi kuwa miongoni mwa vifaa bora zaidi katika kundi hili.
Hata hivyo, bei yake ya juu sana, muundo wake mzito na matumizi machache ya kila siku kwa watumiaji wa kawaida yameathiri mauzo. Ripoti zinaonyesha kuwa mustakabali wa kifaa hicho bado hauna uhakika.
Nini kinafuata?
Kwa hiyo, Apple inajiandaa na nini? Miongoni mwa tetesi ni miwani janja inayotumia AI, kifaa cha kisasa cha kuonyesha taarifa nyumbani, na hata kamera za usalama zenye chapa ya Apple. Lakini tetesi kubwa zaidi, pamoja na taarifa nyingi zilizovuja, zinaashiria kwamba iPhone inayokunjika huenda hatimaye ikawasili mwaka huu.
Kwa sasa inatajwa kama iPhone Fold, na inatarajiwa kuwa simu inayokunjika kwa mtindo wa kitabu, ambayo hufunguka kutoka kwenye skrini ya inchi 5.3 (sentimita 13) hadi skrini yenye ukubwa unaokaribia ule wa iPad mini.
Hilo si jambo jipya, bila shaka. Google, Samsung na kampuni kadhaa za China tayari zimezindua simu zinazofanana katika miaka ya hivi karibuni.
Lakini kama historia inavyotuonyesha, hata kama washindani watafika sokoni kwanza, hiyo haimaanishi Apple iko nyuma.
Ripoti zinaeleza kuwa Apple imekuwa ikichukua muda kuhakikisha hatimaye inaondoa mstari wa kukunjia skrini ambao umekuwa tatizo katika skrini zinazonyumbulika.
Hata hivyo, haitakuwa nafuu, iPhone Fold inasemekana inaweza kugharimu hadi dola 2,500, sawa na karibu pauni 1,900.