Wakosoaji wa serikali ya Rwanda ambao vifo vyao vimezua maswali

Chanzo cha picha, Robert Kabera
Kifo cha Robert Kabera, mwanajeshi wa zamani wa Rwanda na mwanablogu aliyekuwa akiishi uhamishoni nchini Uganda, kimezua mjadala mpya kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi nje ya nchi. Polisi wa Uganda wanasema uchunguzi kuhusu mazingira ya kifo chake bado unaendelea.
Kwa miaka kadhaa, vifo vya baadhi ya watu waliokuwa wakosoaji wa serikali ya Rwanda, au waliokuwa wametofautiana hadharani na mamlaka, vimevutia uangalizi wa kimataifa. Katika baadhi ya matukio, mamlaka zimetoa maelezo rasmi kuhusu sababu za vifo hivyo, huku familia, wanaharakati na mashirika ya haki za binadamu wakitaka uchunguzi huru au kuhoji maelezo yaliyotolewa.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika katika vifo vya wakosoaji wake na kusisitiza kuwa tuhuma hizo hazijathibitishwa. Hata hivyo, baadhi ya matukio yameendelea kufuatiliwa na mashirika ya haki za binadamu na mamlaka za nchi nyingine kutokana na maswali yaliyoibuliwa kuhusu mazingira ya vifo hivyo.
Hawa ni baadhi ya wakosoaji wa serikali ya Rwanda ambao vifo vyao vilizua maswali, mjadala au wito wa kufanyika kwa uchunguzi zaidi, kwa mujibu wa taarifa za mamlaka husika na rekodi za umma.
Robert Kabera, 2026

Chanzo cha picha, Ssgt Robert Kabera / Facebook
Robert Kabera alikuwa sajenti mkuu wa zamani wa jeshi la Rwanda, mwanamuziki na mtayarishaji wa maudhui ya YouTube aliyekuwa akiishi uhamishoni nchini Uganda. Baada ya kuondoka Rwanda, alijenga hadhira kubwa mtandaoni kupitia mtandao wake YouTube uliokuwa ukijadili masuala ya kisiasa na kuikosoa serikali ya Kigali.
Kabera alikuwa ameomba hifadhi nchini Uganda akidai kuwa alikuwa akikabiliwa na mateso ya kisiasa nchini Rwanda. Pia alikanusha mashtaka yaliyokuwa yakimkabili kabla ya kuondoka nchini humo.
Mwezi Oktoba 2026, mwili wake ulipatikana katika eneo karibu na Kampala. Tukio hilo liliripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa na kuibua wasiwasi mpya kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi uhamishoni.
Msemaji wa polisi wa Uganda, Kituuma Rusoke, alisema polisi walikuwa wakichunguza mauaji ya mwanaume aliyepatikana amefariki karibu na Kampala. Polisi walithibitisha kuwa ndugu wa marehemu walimtambua mwili huo kuwa wa Robert Kabera na kwamba uchunguzi ulikuwa ukiendelea.
Kwa mujibu wa familia yake, Kabera alikuwa ameondoka kwenda kukagua eneo la ujenzi kabla ya kifo chake. Mke wake alisema alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa familia baada ya tukio hilo. Wakati huohuo, kundi la upinzani la Rwanda National Congress (RNC) lilitaka uchunguzi wa kina na wahusika kuwajibishwa.
Kwa nini kifo chake kilizua maswali?
Kabera alikuwa mmoja wa wakosoaji wa hivi karibuni wa serikali ya Rwanda waliokuwa wamejijengea hadhira kubwa mtandaoni. Kifo chake kilitokea nje ya Rwanda na wakati uchunguzi ukiwa bado unaendelea, jambo ambalo limefanya tukio hilo kufuatiliwa kwa karibu na wanahabari, wanaharakati wa haki za binadamu na makundi ya upinzani.
Aimable Karasira, 2026

Aimable Karasira alikuwa mhadhiri wa zamani wa chuo kikuu, mchambuzi wa masuala ya kijamii na mkosoaji wa serikali ya Rwanda. Alijipatia umaarufu kupitia video alizokuwa akichapisha mtandaoni, ambamo alizungumza kuhusu historia ya familia yake wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na kipindi kilichofuata.
Mwaka 2021, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka kadhaa, yakiwemo yanayohusiana na kile ambacho mamlaka zilisema ni kuchochea mgawanyiko na kukanusha mauaji ya kimbari. Baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, huku upande wa mashtaka ukiendelea kukata rufaa katika baadhi ya mashtaka mengine.
Mwezi Mei 2026, Karasira alifariki akiwa karibu kuachiliwa kutoka gerezani baada ya kutumikia karibu kifungo chake chote. Kifo chake kilizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Rwanda, huku wanaharakati wa haki za binadamu wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu mazingira ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa Idara ya Magereza ya Rwanda, Karasira alitumia kiwango kikubwa cha dawa alizoandikiwa kwa ajili ya tatizo la kiafya alilokuwa nalo. Msemaji wa magereza, Hillary Sengabo, alisema alipelekwa hospitalini baada ya kutumia dawa hizo kupita kiwango kilichopendekezwa na baadaye akafariki.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema kulikuwa na sababu za kuhoji mazingira ya kifo chake kutokana na kile ilichodai kuwa miaka ya manyanyaso, vitisho na mateso aliyopitia akiwa chini ya uangalizi wa mamlaka. Shirika hilo lilitaka kufanyika kwa uchunguzi huru na kusema serikali ilikuwa na wajibu wa kuthibitisha kwamba hakuuawa kinyume cha sheria.
Kwa nini kifo chake kilizua maswali?
Karasira alifariki siku ambayo alitarajiwa kuachiliwa au muda mfupi kabla ya kuondoka rasmi mikononi mwa magereza, jambo lililoongeza maswali kutoka kwa wanaharakati na baadhi ya wachambuzi. Kifo chake pia kilikuja baada ya miaka kadhaa ya mvutano kati yake na mamlaka kuhusu maoni aliyokuwa akiyatoa hadharani.
Kizito Mihigo, 2020

Chanzo cha picha, Kizito Mihigo/Facebook
Kizito Mihigo alikuwa mmoja wa wanamuziki maarufu wa nyimbo za injili nchini Rwanda na alijulikana kwa ujumbe wake wa maridhiano baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Akiwa manusura wa mauaji hayo, muziki wake ulijikita katika msamaha, umoja na uponyaji wa jamii.
Umaarufu wake ulianza kupungua katika uhusiano na mamlaka baada ya kuandika na kuimba wimbo uliotafsiriwa na serikali kuwa unapingana na simulizi rasmi kuhusu mauaji ya kimbari. Mwaka 2014 alikamatwa na kufunguliwa mashtaka yanayohusiana na usalama wa taifa. Baadaye alipata msamaha wa rais mwaka 2018, lakini kwa mujibu wa Human Rights Watch, aliendelea kusema kuwa alikuwa chini ya uangalizi wa karibu wa mamlaka.
Mwezi Februari 2020, Kizito Mihigo alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi siku chache baada ya kukamatwa tena alipokuwa akidaiwa kujaribu kuvuka mpaka wa nchi. Kifo chake kilizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Rwanda kutokana na hadhi yake kama msanii maarufu na mtetezi wa maridhiano.
Serikali ya Rwanda ilisema kuwa Kizito Mihigo alijiua akiwa mahabusu. Mamlaka zilieleza kuwa alikutwa amefariki katika kituo cha polisi baada ya kujinyonga kwa kutumia mashuka.
Human Rights Watch na watetezi wengine wa haki za binadamu walitaka uchunguzi huru kuhusu kifo hicho. Shirika hilo limesema kuwa kabla ya kifo chake, Mihigo alikuwa amelieleza kuwa alikuwa akipokea vitisho na alihofia usalama wake. Pia lilisema hakujakuwa na uchunguzi huru unaokubalika hadharani kuhusu mazingira ya kifo hicho.
Kwa nini kifo chake kilizua maswali?
Tofauti na wakosoaji wengi wa kisiasa, Kizito Mihigo alikuwa msanii mwenye ushawishi mkubwa na aliyekuwa akiheshimika ndani na nje ya Rwanda. Kifo chake akiwa chini ya ulinzi wa polisi, pamoja na historia ya mvutano wake na mamlaka kuhusu baadhi ya kauli zake, kilisababisha mashirika ya haki za binadamu na wanaharakati kuendelea kuhoji mazingira ya tukio hilo na kutaka uchunguzi huru
Patrick Karegeya, 2013

Aliyekuwa mkuu wa zamani wa ujasusi wa Rwanda, Patrick Karegeya alikuwa miongoni mwa wanachama wa Rwandan Patriotic Front (RPF) walioingia madarakani baada ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994. Kwa zaidi ya muongo mmoja, alihudumu katika nyadhifa za juu za ujasusi kabla ya kuingia katika mvutano na uongozi wa Rwanda. Alivuliwa baadhi ya madaraka yake, akakabiliwa na mashtaka mbalimbali na hatimaye kwenda uhamishoni nchini Afrika Kusini mwaka 2007, ambako aligeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali.
Tarehe 31 Desemba 2013, Karegeya alipatikana amefariki katika chumba cha hoteli mjini Johannesburg. Kifo chake kilivutia uangalizi mkubwa wa kimataifa na kuibua hofu kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi uhamishoni.
Baada ya kifo hicho, Paul Kagame alitoa matamshi yaliyotafsiriwa na baadhi ya wachambuzi na wakosoaji kama onyo kwa wanaompinga. Wakati huo huo, familia ya Karegeya na makundi ya upinzani yaliendelea kudai uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya kifo chake.
Mwaka 2019, mamlaka za Afrika Kusini zilitoa hati za kukamatwa kwa raia wawili wa Rwanda kuhusiana na mauaji hayo, hatua iliyofufua tena mjadala kuhusu tukio hilo miaka kadhaa baada ya kutokea.
Mamlaka za Afrika Kusini zilichukulia kifo cha Karegeya kama mauaji na baadaye zikatoa hati za kukamatwa kwa washukiwa wawili kuhusiana na tukio hilo.
Kwa nini kifo chake kilizua maswali?
Karegeya alikuwa miongoni mwa maafisa waandamizi wa zamani wa Rwanda waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini kabla ya kugeuka wakosoaji wa utawala huo akiwa uhamishoni. Kifo chake kiliibua mjadala mkubwa kuhusu usalama wa wapinzani wa kisiasa wa Rwanda wanaoishi nje ya nchi, na kimeendelea kuangaziwa katika ripoti na mijadala inayohusu mazingira ya wakosoaji wa serikali ya Kigali.
Abdallah Seif Bamporiki, 2021
Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini Rwanda na mwanachama wa chama cha Rwanda National Congress, alipigwa risasi na kuuawa nchini Afrika Kusini, ambako alikuwa akiishi uhamishoni. Polisi wa Afrika Kusini awali walisema wanachunguza tukio hilo kama mauaji yaliyotokana na wizi. Wiki moja kabla ya kuuawa kwake, Bamporiki alikuwa ameongoza ibada ya kumbukumbu kwa ajili ya wanaharakati wa upinzani wa Rwanda waliouawa katika maeneo mbalimbali duniani.
Revocant Karemangingo, 2021
Mfanyabiashara tajiri Revocant Karemangingo alishambuliwa kwa risasi na watu wenye silaha karibu na nyumbani kwake jijini Maputo. Mkosoaji huyo wa Kagame, ambaye alikuwa akimkosoa Kagame wazi wazi, alikuwa akiishi Msumbiji baada ya kuondoka nchini Rwanda mwake mwaka 1994. Serikali ya Rwanda imekanusha kuhusika na mauaji hayo.
Ntamuhanga Cassien, 2021
Mwandishi wa habari, Ntamuhanga Cassien, alitoweka jijini Maputo mwezi Mei baada ya kukamatwa na polisi wa Msumbiji, na tangu wakati huo hakuna taarifa zozote kumhusu. Kuna uvumi kwamba alikabidhiwa kwa Rwanda, madai ambayo yamekanushwa.
Anselme Mutuyimana, 2019
Msaidizi wa Victoire Ingabire, rais wa chama cha upinzani cha United Democratic Forces (FDU-Inkingi), alikutwa amefariki msituni mnamo mwaka 2019. Mwaka mmoja kabla, Mutuyimana alikuwa ameachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka sita gerezani kwa kosa la "shughuli za kisiasa."
Jean Damascene Habarugira
Mwanasiasa huyo wa upinzani alitoweka baada ya kuitwa kwenye mkutano na afisa anayesimamia usalama katika eneo hilo. Siku chache baadaye, mamlaka ziliiambia familia ya Habarugira kwenda kuchukua mwili wake katika hospitali ya eneo hilo.
Kwa upande wa serikali ya Rwanda imekua ikikanusha kuhusika na matukio hayo.
Theogene Turatsinze, 2012
Aliyekuwa mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Rwanda alikutwa amefariki dunia mwaka 2012 katika mto mmoja karibu na Maputo, siku chache baada ya kutoweka. Kabla ya kuondolewa katika wadhifa wake, Turatsinze aliaminika kuwa aliondoka na kwenda Msumbiji akiwa na orodha ya malipo ya siri yaliyofanywa na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Rwanda.
Charles Ingabire, 2011
Mwandishi huyo wa habari kutoka Rwanda alianzisha tovuti ya *Inyenyeri News*, ambayo ilikuwa ikikosoa vikali serikali ya Rwanda. Ingabire alipigwa risasi na kuuawa nchini Uganda, ambako aliishi kama mkimbizi wa kisiasa.
Andre Kagwa Rwisereka, 2010
Makamu mwenyekiti wa Chama cha Democratic Green Party cha Rwanda alikutwa ameuawa na kukatwa kichwa kwa sehemu nchini Rwanda mwaka 2010. Uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda (RIB) kuhusiana na mauaji yake haukuwahi kuleta matokeo yoyote ya wazi.
Illuminee Iragena,
Mwanaharakati huyo wa upinzani alitoweka mwaka 2016 na hajawahi kuonekana tangu wakati huo. Kuna hofu kwamba alitekwa na kutoweshwa kwa nguvu.
Jean-Leonard Rugambage, 2010
Mwandishi huyo wa habari alipigwa risasi na kuuawa mwaka 2010 baada ya kuchapisha makala mtandaoni kuhusu jaribio la mauaji dhidi ya aliyekuwa mkuu wa jeshi, Luteni Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa. Rugambage alijulikana kwa kukosoa vikali serikali ya Kagame.
Mashirika ya haki za binaadamu yamesisitiza juu ya haki za wakosoaji wa serikali nchini Rwanda.
Shirika la human rights watch limesema kuwa Uhuru wa kujieleza au uhuru wa kukosoa serikali au chama tawala – umekandamizwa vikali nchini Rwanda. Hata hivyo, vyombo vya habari huru na upatikanaji wa taarifa ni mambo muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo na kuzifanya serikali ziwe na uwajibikaji.





























