Waliouawa na polisi Kasarani wakati wa kumuaga Raila Odinga hawakuhusika na vurugu -Uchuguzi wa BBC

"Kulikuwa na watu wengi sana, kwa nini yeye?" Yvonne Akinyi anakumbuka siku ambayo mume wake aliuawa kwa kupigwa risasi
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Waombolezaji watatu waliouawa wakati polisi wa Kenya walipofyatua risasi katika hafla ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga hawakuhusika na vurugu zilizochochea matumizi ya nguvu hiyo, uchunguzi wa BBC Africa Eye umebaini.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Oktoba mwaka jana kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa Odinga, watu watatu walifariki kwa kupigwa risasi baada ya baadhi ya waombolezaji kujaribu kuingia kwa nguvu katika eneo la wageni mashuhuri (VIP) kwenye Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

Uchambuzi wa BBC wa picha na video zilizorekodiwa ndani ya uwanja unaonyesha kuwa watu hao walikuwa umbali wa kati ya mita 60 na 160 kutoka eneo ambako vurugu zilikuwa zikiendelea.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen, aliiambia BBC kuwa polisi walichukua hatua hiyo ili " kujilinda" baada ya baadhi ya watu kuanza kurusha mawe.

Hata hivyo, uchambuzi wa BBC wa matukio hayo unaonyesha kuwa ingawa vitu mbalimbali, ikiwemo viti vya plastiki, vilirushwa kuelekea eneo la VIP, hakuna ushahidi wa wazi unaoonyesha kuwa mawe yalirushwa.

Katika picha na video zilizochungunzwa na BBC, vitu mbalimbali, ikiwemo viti vya plastiki, vinaonekana kurushwa wakati wa vurugu hizo. Hata hivyo, hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa mawe yalikuwa miongoni mwa vitu vilivyorushwa.

Ili kufuatilia kwa kina kilichotokea siku hiyo, BBC ilikagua zaidi ya picha na video 1,500 za tukio la Oktoba 16, 2025, na pia kuzungumza na baadhi ya ndugu wa waliouawa. Uchunguzi huo uliwezesha kubaini mahali walipokuwa wahanga wakati risasi zilipofyatuliwa.

Uchambuzi wa wataalamu ulioagizwa na BBC unaashiria kuwa huenda risasi zilizosababisha vifo hivyo zilifyatuliwa na kikosi maalum cha polisi kinachohusika na ulinzi wa rais.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Odinga, aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani na mmoja wa viongozi wa upinzani wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Kenya, alifariki dunia siku moja kabla ya hafla hiyo akiwa nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwaka mmoja baada ya tukio hilo, Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) bado inaendelea na uchunguzi kuhusu vifo hivyo na namna polisi walivyoshughulikia hali hiyo. Hadi sasa, hakuna afisa aliyewajibishwa.

Akijibu maswali kuhusu tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, aliwatetea maafisa wa polisi akisema walikuwa chini ya "shinikizo kubwa" baada ya kufanya kazi kwa saa nyingi bila mapumziko na kuhamishiwa eneo hilo dakika za mwisho.

"Uchunguzi unafanywa na mamlaka huru ya kusimamia polisi, na tunaamini matokeo yake yatatusaidia kuchukua hatua stahiki za kisheria," alisema Murkomen.

Kuhusu matumizi ya risasi, alisema haamini kuwa kulikuwa na amri ya moja kwa moja ya kufyatua risasi, akieleza kuwa huenda uamuzi huo ulifanywa na afisa mmoja wa polisi kulingana na hali ilivyokuwa wakati huo.

Evans Kiche (kushoto) na Jidah Burka (kulia) walipigwa risasi kichwani, huku Vincent Ogutu (katikati) akipigwa risasi kifuani.
Maelezo ya picha, Evans Kiche (kushoto) na Jidah Burka (kulia) walipigwa risasi kichwani, huku Vincent Ogutu (katikati) akipigwa risasi kifuani.

Yvonne Akinyi, ambaye mumewe alikuwa miongoni mwa waliouawa, aliambia BBC kuwa familia nyingi bado zinaendelea kubeba mzigo wa maumivu yaliyosababishwa na tukio hilo.

"Watu tunaowategemea kutulinda ndio wanaotusababishia maumivu haya. Hao ndio wanaotugeuza kuwa wajane na watoto kuwa yatima wakiwa bado wadogo," alisema.

Kifo cha Raila Odinga akiwa na umri wa miaka 80 kilitikisa Kenya na kuzua maombolezo makubwa kote nchini. Maelfu ya waombolezaji walifurika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi kuupokea mwili wake uliporejeshwa nchini.

Awali, mwili huo ulitarajiwa kuagwa katika majengo ya Bunge. Hata hivyo, kutokana na wingi wa watu na hofu ya changamoto za kiusalama, mamlaka zilihamishia hafla hiyo katika Uwanja wa Kasarani dakika za mwisho. Maafisa walikiri kuwa walikuwa na muda mfupi wa kuandaa usalama katika uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu 48,000, huku maelfu ya waombolezaji wakifanikiwa kuingia bila udhibiti madhubuti.

Baada ya kusubiri kwa saa kadhaa chini ya joto kali bila kupatiwa taarifa rasmi kupitia mfumo wa sauti, baadhi ya waombolezaji walianza kurusha vitu mbalimbali, ikiwemo viti vya plastiki, kuelekea maafisa waliokuwa wakilinda eneo la wageni mashuhuri (VIP).

Polisi walijibu kwa kufyatua risasi halisi huku kundi dogo la watu likisonga kuelekea eneo hilo. Hata hivyo, picha zilizochambuliwa na BBC zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya umati katika maeneo mengine ya uwanja ilibaki tulivu.

Watu watatu waliuawa katika mkasa huo.

Mmoja wao alikuwa Evans Kiche, mpishi mwenye umri wa miaka 40 na baba wa watoto saba. Uchambuzi wa BBC unaonyesha kuwa alipigwa risasi kichwani akiwa takriban mita 60 kutoka eneo la vurugu.

Waathiriwa wengine wawili, Vincent Ogutu na Jidah Burka, walikuwa katika majukwaa ya upande wa pili wa uwanja, umbali wa angalau mita 160 kutoka eneo la mtafaruku na mbali kabisa na jukwaa la VIP.

Uchanguzi wa BBC Africa Eye unaonyesha kuwa wote watatu waliuawa wakiwa mbali na eneo ambako vurugu zilikuwa zikishuhudiwa.

A graphic of a stadium showing the VIP Pavilion and then the three spots were the people were when they were shot.

Ripoti za uchunguzi wa maiti zinathibitisha kuwa Vincent Ogutu aliuawa na jeraha la risasi kifuani, huku Jidah Burka, mwenye umri wa miaka 42, akifariki baada ya kupigwa risasi kichwani.

Kwa kutumia uchambuzi wa video, picha na ratiba ya matukio ya siku hiyo, BBC Africa Eye iliwatambua angalau maafisa wanane wa polisi waliokuwa wakifanya kazi kwa pamoja ndani ya uwanja. Maafisa hao walikuwa wamevalia mavazi ya kimkakati ya kijeshi, nyuso zao zikiwa zimefunikwa na bila nembo zozote za utambulisho zinazoonekana. Walikuwa pia na bunduki za kivita.

BBC inasema mavazi na mienendo yao vilifanana na kikosi cha usalama kilichokuwa kikimlinda Rais William Ruto na viongozi wengine wa ngazi za juu kabla na baada ya risasi kufyatuliwa. Uchambuzi huo unaonyesha kuwa takribani maafisa watatu kutoka kundi hilo walionekana wakifyatua silaha zao.

BBC ilifanikiwa kuwatambua maafisa watatu kati yao kuwa ni wanachama wa kikosi maalum cha polisi kinachohusika na ulinzi wa rais.

Hata hivyo, shirika hilo linasema haliwezi kuthibitisha ni risasi gani hasa zilizowaua wahanga hao watatu, wala kuondoa uwezekano kwamba maafisa wengine ndani ya uwanja walifyatua risasi wakati wa mkasa huo.

Kwa upande wake, Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya iliiambia BBC kuwa matukio ya siku hiyo yalitoa mafunzo muhimu kwa jeshi la polisi, na kwamba yaliyotokea yamekuwa msingi wa kuboresha namna operesheni za aina hiyo zitakavyosimamiwa kwa weledi zaidi siku zijazo.

Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) haikujibu ombi la BBC la kutaka maoni kuhusu matokeo ya uchunguzi huo.

Risasi hizo zilisababisha taharuki na sintofahamu miongoni mwa maelfu ya watu waliokuwa wamekusanyika uwanjani.
Maelezo ya picha, Risasi hizo zilisababisha taharuki na sintofahamu miongoni mwa maelfu ya watu waliokuwa wamekusanyika uwanjani.

Vincent Ogutu, baba wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 36, hakuwa na mpango wa kuhudhuria hafla ya Kasarani siku hiyo, mkewe Yvonne Akinyi aliiambia BBC. Asubuhi ya Oktoba 16, alikuwa katikati ya jiji la Nairobi pamoja na marafiki zake walipoona umati wa watu ukielekea uwanjani na kuamua kujiunga nao.

Saa chache baadaye, alikuwa amefariki kwa risasi.

Akinyi alisema kifo cha mumewe kimeiacha familia yao katika majonzi makubwa, huku watoto wao wakikua bila baba.

Mwaka mmoja baada ya tukio hilo, bado hajapata majibu kuhusu kilichosababisha mumewe kuuawa akiwa amehudhuria hafla ya kitaifa iliyoandaliwa na serikali.

"Nitajaribu kuwa imara, imara sana. Lakini ndani ya moyo wangu kuna pengo ambalo haliwezi kuzibika," alisema.

"Inauma sana. Wakati mwingine unaketi na kujiuliza. Kulikuwa na maelfu ya watu Kasarani siku hiyo. Kwa nini yeye? Kwa nini ilimtokea yeye?" alisema.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi