Israel yalaani vikali makubaliano ya Libya na Uturuki

Chanzo cha picha, Reuters
Israel imesema kuwa “inalaani vikali” uamuzi wa bunge la mashariki mwa Libya kuidhinisha makubaliano ya mipaka ya baharini na Uturuki, hatua iliyokosolewa kwa haraka na Ugiriki, mshirika wa karibu wa Israel.
Makubaliano hayo yaliyoidhinishwa Jumanne ni sehemu ya mgogoro wa muda mrefu kuhusu madai yanayokinzana ya mipaka ya bahari na haki za uchunguzi wa rasilimali za nishati katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania.
“Kwa masikitiko, kwa mara nyingine tunaona Uturuki ikifanya kazi za kudhoofisha utulivu wa eneo la mashariki mwa Mediterania,” Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilisema.
Viongozi wa Israel na Uturuki wamekuwa wakibadilishana maneno makali katika miezi ya hivi karibuni kutokana na tofauti zao kuhusu Syria na vita vya Gaza.
Ugiriki na Uturuki, ambazo zote ni wanachama wa muungano wa NATO lakini zimekuwa wapinzani wa muda mrefu, zimekuwa zikibishana kuhusu mipaka ya baharini katika Bahari ya Aegean na mashariki mwa Mediterania.
Kwa muda mrefu, Ugiriki, Misri na Cyprus zimekuwa zikipinga makubaliano ya baharini kati ya Libya na Uturuki, zikidai kuwa yanakiuka madai yao ya maeneo ya baharini.
Mwaka 2020, Athens na Cairo zilitia saini makubaliano yanayobainisha eneo lao maalum la kiuchumi katika mashariki mwa Mediterania, hatua ambayo Uturuki imekuwa ikiipinga.
Pia unaweza kusoma:
































