Siri ya wosia wa Ayatollah Ali Khamenei: Kwa nini Iran haijaitoa hadharani?

Ayatollah Ali Khamenei
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Miezi saba baada ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, wosia wake wa kisiasa bado haujatangazwa hadharani, jambo ambalo limeendelea kuzua maswali na mijadala ndani na nje ya nchi.

Katika kipindi hicho chote, kilichotolewa kwa umma ni wosia wa zamani aliouandika mwaka 1342 kwa kalenda ya Iran. Wakati huo huo, kumekuwapo na ucheleweshaji wa kutolewa kwa rekodi za sauti au video zinazohusiana na mchakato wa urithi wake, hali iliyoongeza sintofahamu kuhusu suala hilo.

Maelezo yaliyotolewa na baadhi ya taasisi za serikali hayajamaliza sintofahamu kuhusu suala hilo, na badala yake yamezua maswali mapya kuhusu kilichoupata wosia huo muhimu.

Miongoni mwa nadharia zilizojitokeza ni kwamba wosia huo ulipotea au kuharibiwa wakati makazi ya Khamenei yaliposhambuliwa. Gazeti la Ettelaat lilidai kuwa huenda hati hiyo bado iko chini ya vifusi vya majengo yaliyobomoka katika shambulio hilo.

Naye Meya wa Tehran, Alireza Zakani, alisema inawezekana wosia huo uliathiriwa na uharibifu uliotokea katika maktaba na mkusanyiko wa maandishi ya Khamenei.

Hata hivyo, maelezo hayo yamekutana na shaka kutoka kwa baadhi ya wachambuzi na wananchi. Wengi wanaona ni vigumu kuamini kuwa hati nyeti kama wosia wa kisiasa wa kiongozi mkuu wa nchi ingewekwa mahali ambapo ingeweza kupotea au kuharibiwa kwa urahisi.

Mashaka hayo yanachochewa na jinsi wosia wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini, ulivyohifadhiwa. Wosia wake uliandaliwa kwa nakala mbili tofauti zilizotiwa muhuri na kuhifadhiwa katika maeneo salama tofauti ili kuhakikisha usalama wake.

Kutokana na historia hiyo, wengi wanaamini kuwa ni jambo lisilo la kawaida kwa hati yenye uzito wa kisiasa na kidini kama wosia wa Khamenei kupotea au kuharibiwa kirahisi, jambo linaloendelea kuzusha maswali kuhusu sababu halisi za kutowekwa kwake hadharani.

Miongoni mwa mambo muhimu yaliyosisitizwa katika wosia wa Ruhollah Khomeini ni kwamba kauli yoyote inayodaiwa kutoka kwake haipaswi kuaminika mpaka iwe imethibitishwa na maandishi yenye saini yake au imetolewa rasmi kupitia redio na televisheni ya taifa la Iran.
Maelezo ya picha, Miongoni mwa mambo muhimu yaliyosisitizwa katika wosia wa Ruhollah Khomeini ni kwamba kauli yoyote inayodaiwa kutoka kwake haipaswi kuaminika mpaka iwe imethibitishwa na maandishi yenye saini yake au imetolewa rasmi kupitia redio na televisheni ya taifa la Iran.

Wosia wa Ruhollah Khomeini ulikuwa na nini?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kutaka kujua yaliyomo katika wosia wa Ayatollah Ali Khamenei hakuashirii kwamba kuchapishwa kwake kutaleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa uongozi wa Iran. Hata kama wosia huo utawekwa hadharani, athari zake zitategemea namna viongozi wa nchi watakavyoutafsiri na kuutekeleza.

Historia ya Iran inaonyesha kwamba hata maelekezo yaliyoandikwa wazi kwenye wosia wa viongozi wakuu si lazima yafuatwe kikamilifu. Hali hiyo ilionekana baada ya kifo cha mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini, mwezi Juni 1989.

Ingawa viongozi wa Iran walisisitiza utii na heshima yao kwake, baadhi ya mapendekezo muhimu aliyoyaacha kwenye wosia wake hayakutekelezwa kikamilifu bila kusababisha mvutano mkubwa wa kisiasa.

Wosia wa Khomeini ulikuwa mrefu na ulijadili masuala mbalimbali, yakiwemo historia ya Iran, hali ya dunia, masuala ya kidini na mustakabali wa Jamhuri ya Kiislamu. Aidha, ulijumuisha maelekezo ya moja kwa moja kuhusu mfumo wa uongozi wa taifa hilo.

Moja ya maelekezo yake muhimu zaidi lilikuwa marufuku kwa vyombo vya usalama kujihusisha na shughuli za kisiasa. Khomeini alisisitiza kuwa jeshi, polisi, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Basij na taasisi nyingine za usalama hazipaswi kushiriki katika kile alichokiita "michezo ya kisiasa".

Hata hivyo, katika kipindi cha uongozi wa Ali Khamenei, IRGC na hasa Basij zimejijengea ushawishi mkubwa katika siasa za Iran. Taasisi hizo zimekuwa na nafasi kubwa katika mijadala ya kisiasa, kampeni za uchaguzi na mchakato wa kufanya maamuzi ya kisera nchini humo.

Wosia wa Khomeini pia ulikuwa na tahadhari muhimu kuhusu kauli ambazo zingehusishwa naye baada ya kifo chake. Aliandika kwamba kauli yoyote inayodaiwa kutoka kwake haipaswi kukubaliwa isipokuwa iwe imethibitishwa kupitia sauti yake, maandishi yenye saini yake au tamko rasmi lililotolewa kwa niaba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hata hivyo, saa chache baada ya wosia huo kusomwa mbele ya Baraza la Wataalamu, aliyekuwa Rais wa zamani wa Iran, Akbar Hashemi Rafsanjani, alieleza kuwa Khomeini aliwahi kumwambia yeye na mwanawe Ahmad Khomeini katika mazungumzo ya faragha kwamba Ali Khamenei alikuwa mtu anayefaa kumrithi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kikao hicho, kauli hiyo ilitumika kama moja ya hoja muhimu katika mchakato wa kumchagua Khamenei kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran. Jambo hilo limeendelea kutajwa na baadhi ya wachambuzi kama mfano wa jinsi tafsiri na matumizi ya urithi wa viongozi yanaweza kutofautiana na maelekezo yaliyoandikwa kwenye wosia wao.

Ndiyo maana, hata iwapo wosia wa Ali Khamenei utachapishwa siku zijazo, swali kubwa halitakuwa tu kuhusu yaliyomo ndani yake, bali pia kuhusu namna mamlaka za Iran zitakavyouchukulia na kuutekeleza.

Andiko hilo, ambalo baadaye lilijulikana kama "Wosia wa Vladimir Lenin", lilitoa onyo kali kuhusu hatari za madaraka kujilimbikiza mikononi mwa mtu mmoja, hasa Joseph Stalin.

Kutoka Umoja wa Kisovieti wa Lenin hadi China ya Mao

Wosia wa viongozi wanaobaki madarakani hadi mwisho wa maisha yao mara nyingi huwa miongoni mwa nyaraka nyeti na muhimu zaidi za serikali. Tofauti na marais wanaochaguliwa kwa muda maalumu na baadaye kuondoka madarakani, viongozi wa aina hii huwa na mamlaka makubwa ya kufanya maamuzi yanayoathiri mustakabali wa taifa kwa miongo kadhaa.

Ndiyo maana makundi ya kisiasa yanayowania ushawishi baada ya kifo cha kiongozi yanaweza kuona umuhimu wa kuchapisha, kutafsiri au hata kuficha wosia wake, kutegemea maslahi yao katika kipindi kinachofuata.

Moja ya mifano maarufu zaidi katika historia ni wosia wa Vladimir Lenin, kiongozi wa Mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917. Kwa hakika, wosia huo ulikuwa barua aliyoiandikia Chama cha Kikomunisti cha Umoja wa Kisovieti.

Katika waraka huo, Lenin alitoa tathmini kali kuhusu baadhi ya viongozi wakuu wa chama na akaonya kuhusu hatari ya mamlaka makubwa kujilimbikiza mikononi mwa Joseph Stalin.

Baada ya kifo cha Lenin, waraka huo ulisomwa kwa viongozi waandamizi wa chama pekee katika vikao vya faragha. Baadaye, Stalin na washirika wake wa kisiasa walihakikisha hauwekwi wazi kwa umma.

Ingawa gazeti la The New York Times lilifanikiwa kuupata na kuuchapisha mwaka 1926, wosia huo haukuchapishwa rasmi ndani ya Umoja wa Kisovieti hadi mwaka 1956, miaka 32 baada ya kifo cha Lenin.

Hatua hiyo ilikuja wakati wa kampeni ya Nikita Khrushchev ya kupunguza ushawishi wa Stalin na kukosoa urithi wake wa kisiasa.

Hali kama hiyo ilijitokeza pia nchini China baada ya kifo cha Mao Zedong mwaka 1976, wakati taifa hilo lilipoingia katika mvutano wa kisiasa kuhusu urithi wake na nani angechukua nafasi ya uongozi.

Tofauti na Lenin, Mao hakuacha wosia wa kisiasa ulioandikwa. Hata hivyo, karibu miaka 20 kabla ya kifo chake, alisaini pamoja na viongozi wengine wa juu wa Chama cha Kikomunisti waraka uliotaka viongozi wa chama wachomwe moto baada ya kufariki dunia na kupinga ujenzi wa makaburi makubwa au maeneo maalumu ya kumbukumbu kwa ajili yao.

Hatua hiyo ililenga kupunguza desturi za kuwatukuza viongozi baada ya kifo chao, jambo ambalo lilikuwa limejikita katika baadhi ya mila za China hata kabla ya utawala wa Kikomunisti.

Hata hivyo, baada ya kifo cha Mao, mrithi wake Hua Guofeng na washirika wake hawakuweka wazi msimamo huo. Wakiwa wanatafuta kuimarisha uhalali wao wa kisiasa dhidi ya wapinzani ndani ya chama, waliamua kujenga ukumbi mkubwa wa kumbukumbu ya Mao na kuhifadhi mwili wake kwa njia maalumu.

Hatua hiyo ilimgeuza Mao kuwa ishara ya kudumu ya taifa, jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wanasema lilizidi hata desturi zilizowahi kupewa watawala wa kale wa China.

Ilikuwa miaka minne baadaye ndipo Deng Xiaoping, aliyekuja kuwa kiongozi mkuu wa China na kujulikana kwa mtazamo wake wa kisiasa wa pragmatiki, alipoeleza hadharani kuwapo kwa pendekezo hilo la Mao na sababu zilizofanya lisitekelezwe baada ya kifo chake.

Mifano ya Lenin na Mao inaonyesha kwamba kilichoandikwa au kuachwa na kiongozi kabla ya kufariki si mara zote huamua mwelekeo wa taifa. Mara nyingi, kilicho muhimu zaidi ni jinsi warithi wake wanavyochagua kukitafsiri, kukitumia au kukipuuzia katika mapambano ya kisiasa yanayofuata.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi