Meli ya miaka 5,000 yafichua siri za biashara za dunia ya kale

.
Maelezo ya picha, Wazamiaji walichimba na kuyatoa kwa uangalifu mkubwa mabaki ya vitu vya kale vya kiakiolojia kutoka chini ya bahari.
    • Author, ਐਲੀਸਨ ਫਰਾਂਸਿਸ, ਰੈਬੇਕਾ ਮੋਰੇਲੇ ਅਤੇ ਕੇਵਿਨ ਚਰਚ
    • Nafasi, ਬੀਬੀਸੀ ਪੱਤਰਕਾਰ
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa maelfu ya miaka, mabaki ya meli hiyo yalilala kimya chini ya maji ya Bahari ya Mediterania. Sasa, ugunduzi wake katika pwani ya Uturuki unawapa wanaakiolojia fursa adimu ya kufichua siri za biashara na maisha ya watu walioishi karibu miaka 5,000 iliyopita.

Wataalamu wanaamini mabaki hayo yanaaminika kutoka Enzi ya Awali ya Shaba na kinafanana takribani na kipindi ambacho Piramidi Kuu ya Giza nchini Misri ilijengwa.

Muundo wa mbao wa meli hiyo haukuhifadhiwa, lakini vyombo vya udongo ilivyokuwa imebeba vilibaki chini ya bahari. Cha kushangaza, baadhi ya vyombo hivyo bado vina mabaki ya vitu vilivyokuwa ndani yake.

Wanaakiolojia walioigundua meli hiyo wanasema ilikuwa na urefu wa takribani mita 10 na ilitumika kusafirisha bidhaa katika Bahari ya Mediterania.

"Mabaki haya ya meli ni kama kapsuli ya muda iliyo chini ya bahari," alisema Profesa Hakan Öniz wa Chuo Kikuu cha Akdeniz nchini Uturuki, aliyeongoza msafara wa utafiti kwa niaba ya Chama cha Akiolojia ya Mediterania.

Nini kimegunduliwa?

.
Maelezo ya picha, Vyombo vya amfora vilitolewa baharini na kupandishwa ndani ya meli, ambako vinafanyiwa uchunguzi.

Mabaki ya meli hiyo yalipatikana katika pwani ya Kisiwa cha Kekova, katika mkoa wa Antalya nchini Uturuki. Yakiwa katika kina cha mita 30 tu kutoka usawa wa bahari, mabaki hayo ya kiakiolojia yametawanyika kwenye mteremko wa chini ya maji.

Mbali na miundo mitatu mikubwa ya mawe, zaidi ya vyombo 30 vikubwa vya udongo vilivyotumika kuhifadhi chakula na vinywaji, vinavyojulikana kama amfora, pia vilipatikana katika eneo hilo.

Kwa kuwa hakuna mabaki ya mbao za meli yaliyopatikana, mbinu kama vile upimaji wa umri kwa kutumia kaboni ya redio (radiocarbon dating), ambayo hupima aina maalumu ya kaboni katika vitu hai, hazikuweza kutumika kubaini umri wake.

Badala yake, wanaakiolojia walichunguza muundo wa vyombo hivyo vya amfora. Mitindo ya utengenezaji wa vyombo vya udongo hubadilika kadiri muda unavyopita, na mabadiliko hayo huakisi vipindi maalumu vya kihistoria.

Vyombo vya udongo vilivyopatikana Kekova vina muundo wa kipekee. Vina mishikio miwili, mstari ulioinuka katikati na sehemu ya chini iliyo bapa.

Öniz alisema muundo huo unafanana na wa vyombo vingine vya amfora vilivyopatikana Misri na Mashariki ya Kati, ambavyo vinaaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 4,400 na 4,700.

"Kwa kulinganisha mbinu za urembo, tunaweza kusema bila shaka yoyote kwamba mabaki haya ni ya Enzi ya Awali ya Shaba. Tuna uhakika wa asilimia 100 kuhusu hili," alisema.

Wataalamu wanafanya uchunguzi gani?

.
Maelezo ya picha, Wazamiaji wamegundua nanga tatu zilizotengenezwa kwa mawe, ambazo zilihifadhiwa kama vifaa vya ziada kwenye meli wakati wa safari ndefu za baharini.

Wazamiaji walioshiriki katika msafara huo walivileta vyombo hivyo juu ya uso wa bahari. Baada ya kukaa chini ya maji kwa maelfu ya miaka, sasa vinahifadhiwa kwa uangalifu.

Mwanaakiolojia Karin Sowada wa Chuo Kikuu cha Macquarie nchini Australia alichunguza vyombo hivyo baada ya kutolewa baharini. Baadhi vilikuwa vizima kabisa. Alishangazwa kuona kuwa bado vilikuwa na mabaki ya dutu nzito na inayong'aa.

"Karibu nizimie nilipotazama ndani," alisema. "Sikuamini kwamba kulikuwa na mabaki mengi kiasi hicho ndani yake. Hayakuwa madoa tu... bado kulikuwa na mabaki mengi sana ndani."

.

Sasa timu ya utafiti inajaribu kubaini ni bidhaa gani hasa zilizokuwa zikisafirishwa katika vyombo hivyo vya amfora.

"Inawezekana ilikuwa mafuta ya zeituni, divai au dutu iliyotokana na miti," alisema Sowada.

"Pia inawezekana kwamba mabaki hayo yalitokana na matumizi ya mara kwa mara ya vyombo hivyo. Ninamaanisha, vyombo hivi ni vikubwa sana. Havikuwa vikitumika kusafirisha bidhaa mara moja tu kisha kutupwa. Watu walipovipata, walivimwaga na huenda waliendelea kuvitumia tena kwa miaka mingi sana," alisema.

Ni taarifa gani zimepatikana kuhusu biashara za kale?

.
Maelezo ya picha, Baada ya kukaa baharini kwa maelfu ya miaka, vitu hivi dhaifu vya kiakiolojia vinachunguzwa kwa uangalifu mkubwa na kuhifadhiwa ili visiharibike.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Taarifa mpya kuhusu biashara katika ulimwengu wa kale pia zinafichuliwa kupitia mabaki ya meli hiyo na bidhaa ilizokuwa imebeba.

Wanaakiolojia wanasema meli hiyo ilianza safari yake kutoka eneo fulani katika pwani ya mashariki ya Bahari ya Mediterania.

Wanaamini bidhaa hizo zilikuwa zikisafirishwa kwenda katika jiji la kale la Troy, lililopo kaskazini-magharibi mwa Uturuki ya sasa, au kwa watu wa ustaarabu wa Minoan katika Kisiwa cha Krete.

Kusafiri baharini kulikuwa na hatari nyingi, hasa katika maeneo yanayozunguka Kisiwa cha Kekova, ambako mawimbi makubwa na upepo mkali vimesababisha kuzama kwa meli nyingi.

Kuna mamia ya mabaki ya meli zilizozama katika eneo hilo. Chama cha Akiolojia ya Mediterania kina utaalamu wa kugundua na kuchunguza mabaki hayo.

Öniz anasema anapozamia hadi kwenye mabaki ya meli hiyo, jambo la kwanza linalomjia akilini ni maisha ya watu waliokuwa na uhusiano fulani na meli hiyo.

"Sisi ndio binadamu wa kwanza baada ya miaka 5,000 kugusa vitu hivi," alisema.

"Siku zote tunawafikiria mabaharia... watu waliotengeneza amfora hizi na mtu aliyezibeba mabegani mwake hadi kwenye meli. Pia tunawafikiria wanawake waliowasubiri waume zao, lakini kwa masikitiko, waume hao hawakurudi kamwe," alisema.

.
Maelezo ya picha, Kutokana na kina cha bahari, wazamiaji waliweza kuchunguza eneo hilo kwa dakika 30 tu kwa kila mzunguko wa kuzamia.

Mabaki ya meli hiyo yako chini ya umiliki wa Wizara ya Utamaduni ya Uturuki.

Waziri wa Utamaduni wa Uturuki, Mehmet Nuri Ersoy, alisema vitu vilivyopatikana baharini vitaonyeshwa katika Jumba Jipya la Makumbusho ya Akiolojia ya Chini ya Maji ya Mediterania, mjini Antalya, ambalo litafunguliwa katika miezi ijayo.

Ugunduzi huu wa Kekova sasa umeiweka meli hiyo katika nafasi ya kwanza katika orodha ya mabaki ya meli za kale zaidi duniani.

Rekodi ya awali ilikuwa inashikiliwa na mabaki ya meli yaliyopatikana katika pwani ya Kisiwa cha Dokos, kusini mwa Ugiriki, ambayo yana umri wa takribani miaka 4,200.

Meli ya kale zaidi inayojulikana ambayo bado iko katika hali nzuri, ikiwa na mbao zake za awali, ilipatikana katika pwani ya Bulgaria, katika Bahari Nyeusi. Meli hiyo ina umri wa takribani miaka 2,400.