Mambo muhimu 14 waliyokubaliana Iran na Marekani

Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Makubaliano ya Marekani na Iran ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano kati ya nchi hizo mbili yamesainiwa na sasa yameanza kutekelezwa, afisa mmoja kutoka ikulu ta White House ameiambia BBC.

Rais wa Marekani, Donald Trump, alitia saini makubaliano hayo wakati akihudhuria mkutano wa viongozi wa nchi Tajiri duniani G7 mjini Evian-les-Bains nchini France.

Makubaliano hayo yenye vipengele 14, yanabainisha kuwa Iran haitamiliki silaha za nyuklia. Pia yanaanzisha mfuko wa dola bilioni 300 kwa ajili ya "ujenzi upya na maendeleo ya kiuchumi" ya Iran, ingawa Marekani haitatoa pesa hizo kutoka kwa walipa kodi wake

Makubaliano hayo yanakuja miezi minne baada ya kuzuka kwa mzozo kati ya Marekani na Israel, dhidi ya Iran.

Utawala wa Trump umeelezea makubaliano hayo kuwa yanategemea utendaji ikimaanisha kuwa Iran itanufaika tu ikiwa itatekeleza kikamilifu ahadi zake chini ya mkataba huo.

Ingawa maandishi ya makubaliano hayo yanaacha maswali mengi bila majibu bila kutatua masuala kadhaa muhimu, ila yanaweka msingi wa kuendelea kwa usitishaji mapigano na kufunguliwa tena kwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Mlango bahari wa Hormuz.

Kumalizika kwa mzozo

Kifungu cha kwanza cha makubaliano kinaelezea kuwa Marekani, Iran na washirika wao watatangaza kusitishwa kwa operesheni za kijeshi katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo nchini Lebanon.

Kwa upande wa Marekani, Rais Donald Trump amekuwa akionyesha wasiwasi mkubwa kwamba operesheni za kijeshi za Israel dhidi ya kundi la Hezbollah zinaweza kuhatarisha makubaliano yaliyoafikiwa na Iran.

Kwa upande wake, Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa Lebanon inapaswa kujumuishwa katika makubaliano ya usitishaji mapigano.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Iran alisema Jumatano kuwa kuendelea kwa operesheni za kijeshi za Israel nchini Lebanon kutachukuliwa kuwa ukiukaji wa makubaliano hayo, na kwamba "hatua zinazohitajika zitachukuliwa".

Makubaliano hayo yanaeleza kuwa kuanzia sasa, hakuna upande utakaoanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya mwingine wala kutoa vitisho vya kijeshi, na kwamba pande zote zitaheshimu uhuru na mamlaka ya Lebanon.

Hata hivyo, bado haijulikani jinsi Israel itakavyoipokea kipengele hiki cha makubaliano.

Kuheshimu mamlaka ya kila upande

Hati hiyo inaelezea kuwa Marekani na Iran zitaheshimu mamlaka ya kila mmoja, mipaka yao, na kuepuka kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, pande zote mbili zimekubaliana kutoshiriki katika vitendo vinavyoweza kutafsiriwa kama kuingilia siasa za ndani, utawala au masuala ya kitaifa ya upande mwingine.

Hatua hii huenda ikapokelewa kwa mtazamo hasi na makundi ya wapinzani wa serikali ya Iran, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitarajia kuungwa mkono na Marekani katika juhudi zao za kuishinikiza serikali ya Tehran kufanya mabadiliko ya kisiasa.

Mapema mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump, aliwaahidi waandamanaji wa Iran kwamba "msaada uko njiani" wakati maandamano makubwa dhidi ya serikali yalipozuka katika miji mbalimbali ya Iran.

Pezeshkian

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku 60 ya mazungumzo

Marekani na Iran zimejitolea kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya kipindi cha siku 60.

Hata hivyo, muda huo unaweza kuongezwa ikiwa pande zote mbili zitakubaliana kufanya hivyo.

Hesabu ya siku hizo 60 imeanza rasmi baada ya viongozi wa nchi hizo kusaini hati ya maelewano.

Marekani kusitisha kizuizi cha kijeshi

Kwa mujibu wa kipengele cha nne cha makubaliano hayo, Marekani ilikubali kuanza kuondoa kizuizi cha kijeshi vilivyowekwa kwenye bandari za Iran.

Makubaliano hayo yanaeleza kuwa kizuizi hicho kitasitishwa kikamilifu ndani ya siku 30. Katika kipindi hicho, idadi ya meli zitakazoruhusiwa kupita katika bandari za Iran na Marekani italingana na kiwango cha usafiri wa majini ambacho Iran itakuwa imerejesha katika mlango bahari wa Hormuz.

Aidha, ndani ya siku 30 baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya mwisho, Marekani imeahidi kuondoa majeshi yake kutoka maeneo yaliyo karibu na Iran.

Mlango bahari wa Hormuz

Sehemu ya makubaliano inaeleza kwamba mara tu Hati ya Maelewano itakapotiwa saini, Iran itachukua hatua kwa kutumia "jitihada zake zote" kuhakikisha usafiri salama wa meli za kibiashara kupitia Mlango bahari wa Hormuz bila kutozwa ada yoyote.

Hili limekuwa lengo muhimu la Marekani tangu kuanza kwa mzozo huo, hasa baada ya mlango huo kufungwa na kusababisha ongezeko kubwa la bei ya mafuta duniani.

Fedha za ujenzi upya wa Iran

Kipengele cha sita kinaelezea kuwa Marekani na washirika wake wa kikanda wataandaa mpango wa mwisho na uliokubaliwa kwa pamoja wenye thamani ya angalau dola bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi upya na maendeleo ya kiuchumi ya Iran.

Mfumo wa mwisho wa utekelezaji wa mpango huo utakubalika ndani ya siku 60 baada ya makubaliano ya mwisho kusainiwa, na Marekani itatoa leseni, ruhusa na msamaha wa vikwazo vinavyohitajika ili kuwezesha utekelezaji wake.

Hata hivyo, makubaliano haya hayaashirii kuwa Marekani itachangia kifedha moja kwa moja.

Kuondolewa kwa vikwazo

Marekani itasitisha vikwazo vyote vya kiuchumi dhidi ya Iran, ikiwemo vikwazo vilivyowekwa chini ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia zile zilizowekwa moja kwa moja na Marekani kwa upande wake.

Hata hivyo, ratiba ya utekelezaji wa hatua hiyo bado haijawekwa wazi.

Iran imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na vikwazo hivyo, huku kampeni ya Marekani ijulikanayo kama "Operation Economic Fury" ikilenga kuikata Tehran kutoka kwenye mfumo wa kifedha wa kimataifa.

Kutokuwa na silaha za nyuklia

Iran imekubali kutotafuta, kutopata au kununua silaha za nyuklia, huku pande zote mbili zikikubaliana kushughulikia madini ya urani yaliyoboreshwa ambayo tayari yako mikononi mwa Tehran.

Hata hivyo, njia ya kusimamia nyenzo hizo bado haijafafanuliwa kikamilifu.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa kuzuia Iran kupata silaha ya nyuklia ndilo lilikuwa takriban asilimia 99 ya lengo lake alipoanzisha operesheni ya "Epic Fury" mapema mwaka huu.

Hali ya sasa

Vipengele 9 na 10 vya mwisho vya makubaliano vinaeleza kuwa Marekani na Iran wamekubaliana kudumisha "hali ya sasa" ya mpango wake wa nyuklia kwa muda, hadi wakati ambapo urani iliyoboreshwa itashughulikiwa kikamilifu.

Hii inamaanisha kuwa Marekani haitaanzisha vikwazo vipya katika kipindi hicho cha mpito.

Badala yake, Marekani itaendelea kutoa misamaha kwa ajili ya usafirishaji wa mafuta ya Iran, bidhaa za petroli, pamoja na huduma nyingine zinazohusiana.

Ufuatiliaji na mazungumzo ya mwisho

Vipengele vya mwisho kutoka 12 hadi 14 vya hati hiyo vinaweka jinsi makubaliano yatakavyotekelezwa kwa vitendo na jinsi yatakavyosimamiwa.

Kwanza, Marekani na Iran wataunda "utaratibu" wa kufuatilia utekelezaji wa Hati ya Maelewano na kuhakikisha kuwa pande zote zinazingatia masharti ya makubaliano ya baadaye. Hata hivyo, haijabainishwa wazi jinsi mfumo huo utakavyofanya kazi kivitendo.

Hati ya makubaliano yatakapotiwa Saini na utekelezaji kuanza, pande zote mbili zitaanza mazungumzo rasmi ya kufikia makubaliano ya mwisho ya kudumu.

Hati hiyo inaelezea kuwa makubaliano ya mwisho yatapokelewa rasmi na kuidhinishwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hii ina maana kuwa makubaliano hayo yatapata nguvu ya kisheria ya kimataifa, yakihusisha uangalizi na utekelezaji chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.