Moja kwa moja, Trump akanusha Marekani kuishiwa silaha za kivita
Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa kwamba Marekani imepungukiwa na silaha na risasi, akisema nchi hiyo ina akiba kubwa ya silaha na kwamba nyingine zinaendelea kutengenezwa.
Muhtasari
Trump akanusha Marekani kuishiwa silaha za vita
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid
CENTCOM yafichua meli zilizozuiwa tangu kuanza kwa vikwazo vya Marekani
Chanzo cha picha, CENTCOM
Kamandi Kuu ya Marekani CENTCOM, inayosimamia operesheni za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati, imesema tangu kuanza kwa zuio la baharini dhidi ya Iran, imezuia meli 55 za kibiashara na kusimamisha meli mbili kwa kutumia mashambulizi ya risasi.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, CENTCOM imesema zaidi ya meli 20 za kivita za Marekani zinafanya shughuli katika Mashariki ya Kati kuunga mkono operesheni za kijeshi, ikiwemo utekelezaji na ufuatiliaji wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.
CENTCOM pia imesema vikosi vya Marekani viliingia na kukagua meli mbili wakati wa utekelezaji wa zuio hilo la baharini.
Trump: Iran imekuwa na utovu wa nidhamu kwa miaka 51
Chanzo cha picha, truthsocial.com/@realDonaldTrump
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran imekuwa na utovu wa nidhamu kwa miaka 51.
Trump amesema hayo katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, akidai Iran imeiongoza dunia katika kile alichokiita tabia mbaya kwa kipindi cha miaka 51.
Trump pia alichapisha picha inayoonyesha kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya Iran, rial, tangu mwanzoni mwa mwaka 2025 hadi sasa.
Akiambatanisha picha hiyo, Trump amesema, “Iran haina pesa,” na kuongeza, “fedha yao haina thamani.”
Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa kwamba Marekani imepungukiwa na silaha na risasi, akisema nchi hiyo ina akiba kubwa ya silaha na kwamba nyingine zinaendelea kutengenezwa.
Trump pia ameonya kuwa watu wanaoshukiwa kuvujisha taarifa za siri za serikali wataadhibiwa vikali.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye X Alhamisi, Trump amesema Marekani ina “idadi kubwa ya silaha na risasi”, hasa za aina fulani, huku akisema uzalishaji wa silaha hizo unaendelea na zinatumwa pale zinapohitajika.
Trump na Wizara ya Ulinzi ya Marekani wanakabiliwa na maswali kuhusu hali ya akiba ya silaha nchini humo, huku vita vikiingia mwezi wa sita na makubaliano ya amani yakitarajiwa kuchukua muda kufikiwa.
Kwa upande mwingine, Iran imesema silaha zinazozalishwa nchini humo zinaiwezesha kukabiliana na “tishio lolote”.
Waziri wa Ulinzi wa Iran, Majid Ibn Reza, amesema dalili za kupungua kwa uwezo wa adui zinaendelea kuonekana kila siku, huku akisisitiza kuwa majeshi ya Iran yako tayari kukabiliana na hatari yoyote.
Amesema teknolojia inayozalishwa nchini Iran ni bora kuliko teknolojia nyingine yoyote ya kijeshi katika eneo hilo.
Taarifa hiyo inafuatia mashambulizi makubwa ya makombora yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Iran katika operesheni iliyopewa jina Epic Fury, pamoja na mashambulizi mengine ya kijeshi.
Kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC, Marekani imetumia sehemu kubwa ya akiba yake ya kimataifa ya makombora ya masafa marefu na makombora yanayoongozwa kwa usahihi. Taarifa hiyo ilinukuu vyanzo viwili vinavyofahamu hali hiyo, vilivyozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina.