Misheni 3 za Marekani zilizotikisa dunia

Gaddafi, Sadam na Osama

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa miaka kadhaa, Marekani imekuwa ikiongoza operesheni zinazolenga kuwakamata au kuwaua viongozi wa makundi ya kigaidi au marais wa zamani wanaotuhumiwa kwa uhalifu mbalimbali.

Miongoni mwa watu waliotafutwa kwa muda mrefu na kwa nguvu kubwa ni Rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi na aliyekuwa kiongozi wa kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden.

Idara za ujasusi za Marekani zilifanya kila lililowezekana kuhakikisha zinafanikisha malengo ya kuwakamata au kuwatokomeza viongozi hao.

Lakini operesheni hizi za kipekee dhidi ya viongozi hao zilifanyikaje?

Operesheni dhidi ya Osama bin Laden

Vyombo vya usalama na ujasusi vya Marekani vilifanya operesheni iliyolenga kumkamata au kumuua Osama bin Laden.

Kiongozi huyo wa zamani wa Al-Qaeda alikuwa akiwindwa kwa miaka kadhaa kutokana na uhalifu mbalimbali, ikiwemo mashambulizi maarufu ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani.

Operesheni hiyo iliyopewa jina la "Neptune Spear" ilikuwa imepangwa kwa miezi kadhaa, lakini ilitekelezwa ndani ya dakika chache tu mwezi Mei mwaka wa 2011.

Kikosi cha wanajeshi maalum wa Marekani kiliondoka Afghanistan na kusafiri usiku, hadi kufika takriban kilomita 192 ndani ya Pakistan, ambako Osama bin Laden alikuwa amejificha.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanajeshi hao walifika kwa helikopta na, katika giza la usiku, wakavamia nyumba waliyokuwa wakiilenga. Waliwaua watu watano, akiwemo Osama bin Laden.

Baada ya takriban dakika 40, waliondoka na mwili wa Bin Laden pamoja na vifaa vya kompyuta vilivyokuwa na taarifa za kijasusi kuhusu Al-Qaeda na mipango yake ya operesheni.

Miili mingine iliwaachwa hapo, ikiwemo ya mwanamke mmoja na mmoja wa watoto wa Bin Laden.

Pia waliwaacha wanawake watatu na watoto mvulana na wasichana wawili ambao wote walikuwa wamefungwa pingu.

Operesheni hiyo ilifanyika tarehe 2 mwezi Mei mwaka wa 2011, baada ya Rais wa Marekani wa wakati huo, Barack Obama, kuidhinisha shambulizi hilo. Obama alitoa idhini hiyo asubuhi ya Ijumaa, tarehe 29 mwezi Aprili.

Kabla ya operesheni kuanza, wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani kinachojulikana kama SEAL Team Six waliondoka katika kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko Jalalabad, Afghanistan, wakiwa ndani ya helikopta mbili aina ya Black Hawk zilizokuwa zimefanyiwa marekebisho maalumu kwa ajili ya operesheni hiyo.

Kulikuwa pia na helikopta nyingine zilizofuatana na kikosi hicho, kwa maandalizi ya kukabiliana na hali yoyote isiyotarajiwa ambayo ingeweza kujitokeza.

Helikopta hizo ziliingia Pakistan usiku wa manane, kwa siri na bila kelele, hadi kufika Abbottabad, ambako Osama bin Laden aliaminika kuwa amejificha.

Osama

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Osama bin Laden

Wanajeshi wa SEAL team, kikosi maalumu kilichotekeleza shambulizi hilo, walikuwa 23.

Walikuwa pamoja na mkalimani na mbwa aliyefunzwa kwa ajili ya shughuli za kijeshi, aliyejulikana kwa jina la Cairo.

Oparesheni hiyo ilikuwa helikopta moja itue juu ya paa la jengo kubwa ambako Osama aliaminika kuwa anaishi, kisha wanajeshi washuke kwa kutumia kamba kutoka kwenye helikopta hiyo.

Lengo lilikuwa kutekeleza operesheni hiyo kwa siri na kimya, bila mtu yeyote kugundua. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyopangwa, kwani moja ya helikopta hizo ilipata hitilafu na kutua kwa nguvu. Hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyefariki.

Walipofika katika eneo hilo, ambalo lilizungukwa na ukuta mrefu wa ulinzi, waliingia ndani na kuanza kupekua vyumba kimoja baada ya kingine, hadi walipompata Osama bin Laden na kumuua.

CIA ilipoanzisha operesheni hiyo mwezi Mei mwaka wa 2011, serikali ya Marekani iliamua kutoijulisha Pakistan kwamba helikopta zake zingeingia katika anga ya nchi hiyo.

Marekani iliogopa kwamba kuna mtu angeweza kumpa Bin Laden taarifa kuhusu operesheni hiyo na hivyo kumpa nafasi ya kutoroka.

Operesheni ya Kumkamata Saddam Hussein

Tarehe 13 mwezi Disemba mwaka wa 2003, wanajeshi wa Marekani walianzisha operesheni iliyojulikana kama Operation Red Dawn, karibu na mji wa Ad-Dawr, kusini mwa Tikrit nchini Iraq. Operesheni hiyo ilisababisha kukamatwa kwa Saddam Hussein akiwa hai.

Operesheni hiyo ilipewa jina kutokana na filamu iliyotolewa mwaka 1984.

Baada ya Saddam Hussein kuondolewa madarakani wakati wa vita vya Iraq, jeshi la Marekani lilianza msako mkali wa kumtafuta yeye pamoja na maafisa wengine waliohudumu katika utawala wake.

Msako huo uliendelea kwa miezi kadhaa, huku taarifa za kijasusi zikikusanywa kutoka kwa wafungwa, jeshi na raia wa eneo hilo.

Taarifa kutoka kwa mtu aliyekuwa na uhusiano wa karibu na Saddam Hussein, ambaye alikuwa amekamatwa, ziliwaelekeza wanajeshi wa Marekani kwenye shamba lililokuwa maeneo ya vijijini karibu na mji wa Tikrit, alikozaliwa Saddam.

Wanajeshi walianza kwa kupekua maeneo mawili yaliyodhaniwa kuwa Saddam Hussein alikuwa amejificha, kabla ya kumpata akiwa amejificha kwenye shimo lililochimbwa chini ya ardhi, lililojulikana kama "spider hole".

Kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi, Saddam hakukataa au kupinga kukamatwa kwakwe alipogunduliwa. Badala yake, alijisalimisha.

Saddam Hussein

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Saddam Hussein

Kanali James Hickey, ambaye alikuwa akiongoza operesheni hiyo, alisema taarifa zilizowasaidia kumkamata Saddam Hussein zilitoka kwa mtu aliyekuwa mshirika wake wa karibu na ambaye alikuwa amekamatwa mjini Baghdad.

Ingawa eneo hilo lilikuwa limepekuliwa hapo awali, inawezekana Saddam hakuwa hapo wakati huo, kwa sababu alikuwa akihama kutoka sehemu moja hadi nyingine ili asipatikane. Hali hii ilifanya iwe vigumu kwa wanajeshi waliokuwa wakimsaka kubaini mahali alipokuwa.

Wakati wanajeshi wa Marekani walipomkamata Saddam Hussein, hawakupata vifaa vyovyote vya mawasiliano ambavyo vingeonyesha kuwa bado alikuwa akiongoza wanajeshi. Hata hivyo, hilo halikuweza kuthibitisha kwamba hakuwa tena na uhusiano na wafuasi wa utawala wake wa zamani.

Wanajeshi waliokuwa wakipekua eneo alimokuwa amejificha walipata dola za Marekani 750,000 taslimu, pamoja na bunduki mbili aina ya Kalashnikov (AK-47).

Muammar Gaddafi

Gaddafi
Maelezo ya picha, Picha za Muammar Gaddafi

Wakati vuguvugu la Arab Spring lilipoanza nchini Tunisia mwezi Desemba mwaka 2010, Libya haikuwa miongoni mwa nchi zilizotarajiwa kuathiriwa na wimbi la maandamano lililokuwa likienea katika nchi za Kiarabu.

Muammar Gaddafi alikuwa akiiongoza Libya tangu mwaka 1969, ambapo alitawala nchi hiyo kiimla kwa zaidi ya miongo minne. Ingawa baadhi ya wafuasi wake waliona utawala wake kama chanzo cha usalama na utulivu, wakosoaji wake walimtuhumu kwa utawala wa udikteta na ukiukaji wa haki za binadamu.

Maandamano yalipofika Libya mwanzoni mwa mwaka wa 2011, yaligeuka kuwa vita ambapo makundi yenye silaha yalianza kupigana dhidi ya serikali ya Gaddafi.

Waasi hao baadaye waliungana chini ya mwavuli wa taasisi iliyojulikana kama National Transitional Council (NTC), ambayo ilifanikiwa kuteka maeneo makubwa ya nchi hiyo.

Vita vilivyozidi kuwa vikali, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililoruhusu kuingiliwa kijeshi kwa taifa hilo kwa lengo la kuwalinda raia.

Mwezi Machi mwaka wa 2011, vikosi vya muungano wa NATO, uliokuwa ukijumuisha nchi mbalimbali za eneo la Atlantiki Kaskazini vilitumwa Libya. Vikosi hivyo vilijumuisha wanajeshi kutoka Marekani, Ufaransa na Uingereza.

Katika oparesheni yao, walitekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya serikali ya Gaddafi.

Mashambulizi hayo ya anga ya NATO yaliwasaidia waasi kusonga mbele dhidi ya vikosi vya serikali, hatimaye Gaddafi akapoteza madaraka.

Gaddafi aliondoka katika mji mkuu Tripoli na kukimbilia katika mji alikozaliwa wa Sirte, ambao ulikuwa miongoni mwa maeneo ya mwisho yaliyokuwa yakidhibitiwa na wanajeshi waliokuwa wakimuunga mkono.

Tarehe 20 mwezi Oktoba 2011, Gaddafi alijaribu kutoroka Sirte akiwa katika msafara wa magari. Ndege ya NATO ilishambulia msafara huo, na safari hiyo ikakatizwa huku waliokuwa ndani ya msafara huo wakitawanyika.

Baada ya shambulizi hilo la anga, wapiganaji wa NTC walimpata Gaddafi akiwa amejificha ndani ya bomba la kupitisha maji chini ya ardhi karibu na Sirte. Alikamatwa akiwa hai lakini alikuwa amejeruhiwa.

Alifariki muda mfupi baadaye katika mazingira ambayo hadi wa leo yanazua utata.