Kwa nini dawa za kupunguza uzito zinaathiri biashara ya urembo?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rachel Clun
- Nafasi, Business reporter
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kampuni kubwa ya urembo ya L'Oréal imesema kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kupunguza uzito kumeathiri mauzo ya bidhaa za urembo na utunzaji wa ngozi, huku ikibuni bidhaa zinazolenga kukabiliana na baadhi ya athari za kupungua uzito kwa haraka.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Nicolas Hieronimus, amesema soko la urembo limeendelea kuwa imara licha ya changamoto katika uchumi wa dunia, na kwamba matumizi ya dawa za kundi la GLP-1 ni "jambo muhimu sana kwetu".
Akizungumza katika kikao na wawekezaji, alisema kuongezeka kwa matumizi ya dawa hizo "kunaathiri matumizi ya bidhaa za urembo na hasa bidhaa za utunzaji wa ngozi".
L'Oréal, ambayo inamiliki pia chapa maarufu zikiwemo Maybelline na La Roche-Posay, ilitangaza Alhamisi kuwa mauzo yake katika kipindi cha miezi mitatu hadi Septemba yaliongezeka kwa asilimia 7.7, kiwango kilichozidi matarajio ya wachambuzi.
Matumizi ya dawa za GLP-1 yameongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, baada ya dawa zilizotengenezwa kutibu kisukari, kama vile Ozempic, Wegovy na Mounjaro, kubainika pia kusababisha kupungua kwa uzito kwa kiasi kikubwa kutokana na kupunguza hamu ya kula.
Ingawa ngozi kulegea hakusababishwi moja kwa moja na dawa za GLP-1, kupungua uzito kwa haraka kunaweza kusababisha athari hiyo kwa baadhi ya watu, ikiwemo ngozi ya usoni kulegea.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hieronimus alisema chapa za L'Oréal, SkinCeuticals na Kiehl's, zina bidhaa "zilizobuniwa kutumika sambamba na matumizi ya dawa za GLP-1 na kusaidia kukabiliana na athari zake kwenye kulegea kwa ngozi", pamoja na athari nyingine zinazohusiana na kupungua uzito kwa haraka.
L'Oréal pia imepanua uwekezaji wake katika sekta ya matibabu ya urembo, kwa kuongeza hisa zake katika kampuni ya tiba ya magonjwa ya ngozi ya Galderma hadi asilimia 20 mwezi Desemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kampuni hizo mbili zimekuwa zikifanyia majaribio bidhaa zao kwa watumiaji wa dawa za GLP-1 ambao wana wasiwasi kuhusu ngozi kulegea, kupitia tafiti tofauti za kitabibu.
Galderma inamiliki bidhaa maarufu za matibabu ya urembo, zikiwemo Sculptra, sindano inayolenga kuchochea uzalishaji wa kolajeni mwilini, na Restylane, kichujio cha ngozi kinachodungwa ili kuongeza ujazo na kuboresha mwonekano wake.
Mwaka jana, kampuni hiyo ya urembo ilitoa ripoti kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya dawa za GLP-1 na wasiwasi unaohusiana na mabadiliko ya mwonekano wa uso.
Utafiti wake wenyewe uliohusisha watumiaji wa dawa za kupunguza uzito ulibaini kuwa idadi kubwa ya washiriki walikuwa wameona mabadiliko katika mwonekano wa nyuso zao baada ya kutumia dawa hizo.
Dawa maarufu za kupunguza uzito hufanyaje kazi?
Dawa za kutibu unene uliopitiliza hupunguza hamu ya kula kwa kuiga utendaji wa homoni zinazoupa mwili ishara kwamba umeshiba.
Mara nyingi, dawa hizo hufanya kazi kupitia homoni za GLP-1 (glucagon-like peptide-1) na GIP (glucose-dependent insulinotropic polypeptide).
Dawa hizo hupunguza kasi ya chakula kutoka tumboni kwenda kwenye utumbo, hali inayofanya mtu ajisikie ameshiba kwa muda mrefu zaidi. Pia huathiri mfumo mkuu wa neva ili kupunguza hamu ya kula na kutamani chakula, anaeleza Stojanović.
Dawa hizo huungana na vipokezi vinavyohusika na udhibiti wa njaa na kushiba, hupunguza kasi ya tumbo kumeng'enya na kusafirisha chakula kwenda kwenye utumbo, na kupunguza hamu kubwa ya kula. Ndiyo maana watumiaji kwa kawaida huanza kupungua uzito ndani ya wiki za kwanza za matibabu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Madhara ya dawa hizi ni yapi?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Madhara yanayojitokeza mara nyingi ni pamoja na kichefuchefu, kuharisha, kutapika na matatizo mengine ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula. Madhara haya kwa kawaida huwa ya muda mfupi.
Katika hali zisizojitokeza mara nyingi, dawa hizi zinaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi, kama vile uvimbe wa kibofu cha nyongo, kuvimba kwa kongosho na baadhi ya matatizo ya kuona.
Kwa mujibu wa uzoefu wa kitabibu, dawa hizi huchukuliwa kuwa salama zinapotumiwa kwa kipimo kilichoelekezwa na daktari na chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Hata hivyo, hazifai kwa kila mtu.
Kwa kawaida, dawa hizi za kupunguza uzito zinaweza kuzingatiwa kwa watu wenye fahirisi ya uzito wa mwili (BMI) inayozidi 30.
Kwa watu wenye BMI inayozidi 27, kunaweza kuwa na vigezo vya ziada, kama vile uwepo wa magonjwa yanayohusiana na uzito wa mwili. Kutaka tu kupunguza kilo chache si sababu ya kitabibu inayotosha kutumia dawa hizi.
BMI ni kipimo kinachotumia uwiano wa uzito wa mwili na urefu wa mtu kutathmini hali ya uzito wake.
Huhesabiwa kwa kugawanya uzito wa mtu kwa kilogramu kwa mraba wa urefu wake kwa mita.
Matumizi ya dawa hizi kwa watoto na vijana, pamoja na watu wenye uzito wa kawaida wanaozitumia kwa sababu za urembo pekee, yanahitaji kuzingatiwa kwa umakini. Ni muhimu kutathmini umri wa mtumiaji, sababu za kitabibu za kutumia dawa, kipimo kinachofaa na uwiano kati ya manufaa na hatari zinazoweza kutokea.
Jambo la kuzingatia si tu ikiwa dawa inaweza kusaidia kupunguza uzito, bali pia ni nani anayeitumia, kwa sababu gani, kwa kipimo gani, anapata dawa hiyo kutoka wapi na ikiwa matibabu yanafanyika chini ya uangalizi wa daktari.



































