Unataka ngozi yenye afya na mwonekano wa ujana? Hivi ndivyo vyakula vya kula

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Melissa Hogenboom
- Nafasi, Senior Health Correspondent
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ngozi ndiyo kiungo kikubwa zaidi katika mwili wa binadamu na inapaswa kudumu nasi maisha yetu yote. Mbali na kutusaidia kuonekana vijana, kuitunza ngozi vizuri pia kuna manufaa kwa afya yetu kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa kuwa ngozi ndiyo kinga inayotenganisha miili yetu na mazingira ya nje, hukabiliwa na mambo mbalimbali yanayoweza kuisababisha kuharibika. Mambo mengi ya kimazingira huchangia kuzeeka kwa ngozi, yakiwemo uchafuzi wa hewa, ozoni na mabadiliko ya tabianchi, anasema Jean Krutmann, profesa wa magonjwa ya ngozi katika Taasisi ya Leibniz ya Utafiti wa Tiba ya Mazingira.
"Kwa miongo kadhaa tuliamini kuwa mionzi ya urujuanimno (UV) ndiyo sababu kuu ya kuzeeka kwa ngozi kunakosababishwa na mazingira, lakini sasa tunajua kuwa hilo si sahihi," anasema Krutmann.
Mionzi ya UV ni aina ya nishati inayotoka kwenye jua.
"Urefu mwingine wa mawimbi ya mwanga wa asili wa jua unaweza kuchangia kuzeeka kwa ngozi, kwa mfano mwanga unaoonekana kwa macho na mionzi ya infrared." Anasema hata ongezeko la joto linaweza kuchangia mchakato huo.
Kuzeeka kwa mwili wenyewe pia ni sababu nyingine. Kadiri tunavyozeeka, kiwango cha kolajeni mwilini hupungua taratibu. Kolajeni ni protini inayoupa ngozi muundo wake na kuisaidia kubaki imara.
Jambo moja ambalo mara nyingi halizingatiwi, lakini linaweza kusaidia kuitunza ngozi, ni aina ya vyakula tunavyokula. Kuanzia mafuta yenye afya hadi vyakula vilivyochachushwa, baadhi ya vyakula vinaweza kusaidia kudumisha afya ya ngozi.
1. Matunda na mboga za rangi mbalimbali
Kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa lishe yenye vyakula vingi vinavyotokana na mimea ni muhimu kwa kudumisha afya ya ngozi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ni vizuri kula matunda na mboga za rangi mbalimbali kwa sababu zina viambata vya antioxidant vinavyosaidia kulinda ngozi dhidi ya madhara yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira na mwanga wa jua.
Karoti, pilipili hoho na nyanya zina kiasi kikubwa cha carotenoids, ikiwemo lutein, lycopene na beta-carotene.
"Viambata hivi huhifadhiwa kwenye tishu za mafuta mwilini na husaidia kulinda ngozi dhidi ya mionzi ya UV," anasema Volker Böhm, profesa wa kemia ya chakula katika Chuo Kikuu cha Friedrich Schiller, Jena.
Ingawa matumizi ya krimu ya kuzuia mionzi ya jua (sunscreen) bado ni muhimu, Böhm anasema watu wengi huwa wanaitumia wanapokuwa nje kwa muda mrefu badala ya kuitumia kila siku.
Anasema ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vyenye carotenoids unaweza kutoa kiwango cha msingi cha ulinzi dhidi ya mionzi ya UV kinachokadiriwa kuwa sawa na SPF ya takribani 2 hadi 3 mwaka mzima.
Kuongeza kiasi kidogo cha mafuta yenye afya, kama mafuta ya zeituni, kwenye nyanya au karoti husaidia mwili kufyonza viambata hivi vya antioxidant kwa urahisi zaidi.
Beta-carotene pia inaweza kubadilishwa na mwili kuwa vitamini A, ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa seli za ngozi na kusaidia kulinda ngozi dhidi ya maambukizi.
Carotenoids zinaweza kusaidia seli za ngozi kuzalisha asidi ya hyaluronic. Molekuli hii husaidia kudumisha uimara na unyumbufu wa ngozi, na hupatikana katika vilainishi vingi vya ngozi na krimu zinazodai kupunguza dalili za kuzeeka.
Rangi hizi za asili zinaweza pia kusaidia kuongeza uzalishaji wa kolajeni. Katika utafiti mdogo, wanawake waliotumia virutubisho vya carotenoids kila siku kwa miezi 10 walionyesha kuongezeka kwa kolajeni na elastini kwenye ngozi zao. Matokeo hayo yanaashiria kuwa virutubisho hivyo vinaweza kusaidia kuzuia kuvunjika kwa kolajeni.
Mwisho, imebainika kuwa ulaji wa matunda na mboga nyingi za rangi mbalimbali unaweza kuifanya ngozi ionekane yenye afya na mng'ao wa asili.
Ili kupata manufaa haya, ni muhimu kula vyakula hivyo mara kwa mara, anasema Krutmann.
"Kwa antioxidant yoyote unayokula, kwa kawaida huchukua wiki nane hadi 10 kabla ya kuona matokeo yanayoweza kupimika katika ulinzi dhidi ya madhara ya kimazingira."

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Embe limebainika kuwa linaweza kusaidia ngozi kuendelea kuonekana changa kadiri mtu anavyozeeka.
Katika utafiti uliofanywa kwa wanawake waliokoma hedhi, ukiongozwa na Vivien Fam wa Chuo Kikuu cha California, Davis, washiriki walikula gramu 85 za embe mara nne kwa wiki kwa muda wa wiki 16.
Watafiti walibaini kuwa ulaji huo ulipunguza ukubwa wa mikunjo iliyokuwepo kwenye ngozi na pia kupunguza idadi ya mikunjo mipya.
Ingawa tafiti zaidi zinahitajika, watafiti walidhani kuwa manufaa hayo yanaweza kutokana na carotenoids pamoja na viambata vya antioxidant vinavyoitwa flavonoids na mangiferin.
Kwa kushangaza, utafiti huo ulibaini kuwa kula takribani gramu 250 za embe kwa siku kuliongeza mikunjo ya ngozi.
Mmoja wa waandishi wenza wa utafiti huo, Robert Hackman, profesa wa lishe katika Chuo Kikuu cha California, Davis, anasema bado haijulikani kwa nini hali hiyo ilitokea. Hata hivyo, huenda ikahusiana na kiwango kikubwa cha sukari ya asili kilichomo kwenye maembe.
"Tunadhani sukari ilisababisha madhara fulani kwenye molekuli za ngozi," anasema Hackman.
Ingawa utafiti huo ulikuwa mdogo, anasema utafiti mwingine wa ufuatiliaji, ambao bado haujachapishwa, ulipata matokeo yanayofanana.
Maembe na matunda jamii ya machungwa pia yana vitamini C kwa wingi. Vitamini hii husaidia mwili kuzalisha kolajeni na pia hufanya kazi kama antioxidant inayoweza kulinda ngozi dhidi ya madhara ya jua.
Tafiti zinaashiria kuwa vitamini C inaweza kusaidia kuongeza unyevunyevu wa ngozi na kupunguza mabadiliko ya rangi ya ngozi. Kwa sababu hiyo, vitamini C hutumika sana katika bidhaa za kutunza ngozi na virutubisho, anasema Krutmann.
2. Mafuta yenye afya
Kula karanga na mbegu kwa wingi kunaweza kuwa na manufaa kwa ngozi.
Utafiti mdogo uliotumia ugawaji wa washiriki kwa njia ya nasibu na kundi la udhibiti ulibaini kuwa watu waliokula lozi kama kitafunwa kwa wiki 16 walikuwa na mikunjo isiyoonekana sana ikilinganishwa na wale waliokula kitafunwa kingine.
Vitamini E, ambayo hupatikana kwa wingi katika karanga na mbegu, inaweza pia kulinda ngozi dhidi ya uharibifu wa seli na kuzeeka.
Upungufu wa vitamini hii unaweza kuathiri afya ya ngozi, ikiwemo kuchelewesha kupona kwa majeraha. Vyanzo vizuri vya vitamini E ni pamoja na lozi, karanga za hazelnut, karanga za pine na aina nyingi za mafuta yatokanayo na mbegu.
Karanga pia zina asidi ya mafuta ya omega-6, ambayo inaweza kuimarisha tabaka la kinga la ngozi na kuisaidia kuhifadhi unyevunyevu.
Aina nyingine ya mafuta yenye afya yanayojulikana kuwa mazuri kwa ngozi ni omega-3, ambayo hupatikana katika samaki wenye mafuta mengi na mwani.
Samaki wenye omega-3 kwa wingi ni pamoja na salmon, sardini na makrili. Tafiti ndogo zinaashiria kuwa samaki hao wanaweza kupunguza unyeti wa ngozi dhidi ya jua na hivyo kusaidia kuilinda dhidi ya madhara ya mionzi ya jua.
Samaki wenye mafuta mengi pia husaidia kuhifadhi kolajeni iliyopo kwenye ngozi na kupunguza uvimbe.
3. Vyakula vinavyosaidia afya ya utumbo

Chanzo cha picha, Getty
Tunapokula mlo wenye aina mbalimbali za vyakula vibichi, karanga na mbegu, vijidudu rafiki vinavyoishi kwenye utumbo hunufaika, na ngozi yetu pia hunufaika.
Hii ni kwa sababu afya ya utumbo na afya ya ngozi vina uhusiano wa karibu. Watafiti huita uhusiano huu "gut-skin axis", yaani uhusiano kati ya utumbo na ngozi.
Tunapokula aina mbalimbali za vyakula vinavyotokana na mimea, vijidudu vya utumbo huzalisha viambata vyenye uwezo wa kupunguza uvimbe na kufanya kazi kama antioxidants. Viambata hivyo huathiri pia afya ya ngozi, anasema Hackman.
Mfumo wa vijidudu rafiki kwenye utumbo ulio katika hali nzuri unaweza pia kusaidia kuboresha hali ya ngozi kwa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili.
Njia mojawapo ya kupata manufaa haya ni kula aina nyingi za vyakula vinavyotokana na mimea. Hivi ni pamoja na matunda, mboga, kunde, nafaka zisizokobolewa, mimea ya viungo na viungo vya chakula.
Lishe hii inaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo, kuboresha usingizi na kulinda dhidi ya baadhi ya magonjwa ya ngozi, kama psoriasis, ambayo husababisha mabaka ya ngozi kuwa makavu, yenye magamba, kuwasha na kuuma.
Vyakula vilivyochachushwa, kama sauerkraut, kimchi, kombucha na mtindi, pia vina manufaa makubwa kwa sababu husaidia kulisha vijidudu rafiki vilivyopo kwenye utumbo.
Huenda usiweze kuonekana mwenye umri wa miaka 30 milele, lakini kula lishe bora kutasaidia kuipa ngozi yako nafasi nzuri zaidi ya kubaki na afya kwa miaka mingi ijayo.
Pia, ni muhimu kutumia krimu ya kuzuia mionzi ya jua ili kusaidia kulinda ngozi dhidi ya madhara ya jua.



































