Mgogoro wa kujiunga na jeshi unaotikisa siasa za Israel

Kwa nini Wayahudi wa Kiorthodoksi wanapinga kujiunga na jeshi wakati Israel ikiendelea kupigana vita vya Gaza?
Mamia ya Wayahudi wa Kiorthodoksi wamekuwa wakijitokeza barabarani nchini Israel kupinga kile wanachokiona kama juhudi za kulazimisha vijana wao kujiunga na jeshi.
Katika moja ya matukio yaliyoibua mjadala mkubwa, waandamanaji walikabiliana na polisi wa kijeshi waliokuwa wakimkamata kijana wa Kiyahudi aliyeshindwa kuripoti kwa huduma ya kijeshi katika mji wa Modi'in, ulioko kati ya Jerusalem na Tel Aviv.
Kwa wengi nchini Israel, tukio hilo lilikuwa ishara ya mgawanyiko unaozidi kuongezeka ndani ya jamii ya nchi hiyo wakati vita dhidi ya Hamas huko Gaza vikiendelea na mahitaji ya wanajeshi yakiongezeka.
Mjadala huo hauhusu tu suala la kujiunga na jeshi. Unagusa maswali makubwa kuhusu usawa, wajibu wa raia kwa taifa, nafasi ya dini katika siasa na mustakabali wa Israel.
Wayahudi wa Kiorthodoksi ni akina nani?

Chanzo cha picha, Reuters
Wayahudi wa Kiorthodoksi, wanaojulikana pia kama Haredi, ni jamii yenye msimamo mkali wa kidini ambayo huishi kwa kufuata kwa karibu mafundisho na mila za dini ya Kiyahudi.
Ingawa kwa muda mrefu walikuwa kundi dogo ndani ya Israel, idadi yao imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika miongo ya karibuni. Inakadiriwa kuwa wanaunda karibu asilimia 14 ya wakazi wa Israel na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kutokana na viwango vya juu vya kuzaliwa katika jamii hiyo.
Wengi wao husoma katika taasisi maalumu za kidini zinazojulikana kama yeshiva. Kwa jamii hii, kujifunza maandiko ya dini si shughuli ya kawaida tu bali ni jukumu muhimu la maisha.
Kutokana na mtazamo huo, vijana wengi wa Haredi wamekuwa wakisamehewa kujiunga na jeshi ili waendelee na masomo ya dini.
Mpangilio huo ulianza katika miaka ya mwanzo ya kuanzishwa kwa taifa la Israel, wakati idadi ya Wayahudi wa Kiorthodoksi ilikuwa ndogo sana na wengi wao walikuwa manusura wa mauaji ya Holocaust waliokuwa wakijaribu kujenga upya maisha yao na taasisi zao za kidini.
Kwa nini wanapinga kujiunga na jeshi?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kwa viongozi wengi wa Haredi, suala la kujiunga na jeshi si tu kuhusu usalama wa taifa bali ni suala la kuhifadhi utambulisho wao wa kidini.
Wanaamini kuwa mazingira ya kijeshi yanaweza kuwaweka vijana wao karibu na mitazamo, tabia na mfumo wa maisha ambao unaweza kuwafanya kuachana na mila za jamii yao.
Kwao, kuendelea kusoma dini na kuhifadhi mafundisho ya Kiyahudi ni jukumu lenye umuhimu mkubwa sawa au hata zaidi kuliko huduma ya kijeshi.
Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakisisitiza kuwa masomo ya dini yana mchango mkubwa katika ulinzi wa taifa kwa njia ya kiroho.
Mtazamo huo unaungwa mkono na sehemu kubwa ya jamii ya Haredi, ambayo inaamini kuwa kulinda urithi wa dini ya Kiyahudi ni jukumu la msingi kwa mustakabali wa Wayahudi duniani kote.
Kutokana na sababu hizo, juhudi za kuwalazimisha vijana wao kujiunga na jeshi zimekuwa zikionekana kama tishio kwa mfumo wao wa maisha.
Kwa nini suala hili limekuwa nyeti zaidi sasa?
Kwa miaka mingi, mjadala kuhusu msamaha wa huduma ya kijeshi ulikuwepo, lakini haukuwa mkali kama ulivyo sasa.
Hali hiyo ilibadilika baada ya mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, na vita vilivyofuata katika Ukanda wa Gaza.
Tangu wakati huo, maelfu ya Waisraeli wameitwa kuhudumu jeshini ama kama wanajeshi wa kawaida au wanajeshi wa akiba.
Familia nyingi zimekuwa na ndugu wanaopigana vitani kwa muda mrefu. Wengine wameuawa huku wengine wakijeruhiwa.
Kutokana na hali hiyo, sehemu kubwa ya umma wa Israel imeanza kuuliza kwa nini baadhi ya vijana hawapaswi kushiriki jukumu ambalo wengine wanalibeba.
Kwa wengi, suala hilo limekuwa la usawa.
Wanaamini kuwa ikiwa taifa liko vitani, basi makundi yote ya jamii yanapaswa kushiriki katika mzigo wa kulilinda.
Mtazamo huo umefanya uungwaji mkono wa kuwajumuisha Wayahudi wa Kiorthodoksi katika mfumo wa huduma ya kijeshi kuongezeka.
Mahakama ilisema nini?
Mjadala huo ulipata nguvu zaidi baada ya Mahakama Kuu ya Israel kuamua kuwa mfumo wa msamaha uliokuwa ukitumika kwa Wayahudi wa Kiorthodoksi haukuwa na msingi wa kutosha wa kisheria.
Uamuzi huo ulifungua njia ya serikali kuanza kuandikisha baadhi ya wanafunzi wa dini kwa huduma ya kijeshi.
Hatua hiyo ilizua hasira kubwa katika jamii ya Haredi.
Maelfu ya watu walishiriki maandamano katika miji mbalimbali ya Israel, huku baadhi ya waandamanaji wakijaribu kuzuia kukamatwa kwa vijana waliokwepa kujiunga na jeshi.
Katika maeneo yenye idadi kubwa ya Wayahudi wa Kiorthodoksi, kumekuwa na mapambano ya mara kwa mara kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.
Kwa nini suala hili linamsumbua Netanyahu?

Chanzo cha picha, Reuters
Mgogoro huu pia umegeuka kuwa tatizo kubwa la kisiasa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Kwa miaka mingi, vyama vya Wayahudi wa Kiorthodoksi vimekuwa sehemu muhimu ya miungano ya kisiasa iliyomsaidia kubaki madarakani.
Kwa sababu hiyo, Netanyahu amekuwa akilazimika kusawazisha maslahi ya washirika wake wa kidini na shinikizo kutoka kwa sehemu kubwa ya wananchi wanaotaka mabadiliko.
Iwapo ataimarisha hatua za kuwalazimisha Haredi kujiunga na jeshi, anaweza kupoteza uungwaji mkono wa washirika wake wa kisiasa.
Lakini iwapo ataendelea kutetea mfumo wa sasa, anaweza kukosolewa na wapigakura wengine wanaohisi kuwa kuna upendeleo usiofaa.
Ndiyo maana suala hili limekuwa moja ya mijadala mikubwa zaidi katika siasa za Israel.
Waisraeli wengine wanaonaje?
Kwa upande mwingine, Waisraeli wengi wasio Haredi wanaona kuwa hali ya sasa haiwezi kuendelea kwa muda mrefu.
Wanahoji kuwa maelfu ya vijana wa Israel hutumia miaka yao ya ujana katika huduma ya kijeshi na huweka maisha yao hatarini.
Kwao, ni vigumu kuelewa kwa nini kundi moja linaweza kuendelea kupata msamaha wakati taifa linakabiliwa na changamoto za usalama.
Wakosoaji pia wanaeleza kuwa baadhi ya wanaume wa Kiorthodoksi hushiriki kwa kiwango kidogo katika soko la ajira kwa sababu ya kuendelea na masomo ya dini kwa muda mrefu.
Kutokana na hilo, mjadala kuhusu jeshi mara nyingi huunganishwa na mjadala mpana kuhusu uchumi na mchango wa kila kundi kwa maendeleo ya taifa.
Je, kuna nafasi ya maelewano?
Licha ya misimamo mikali ya pande zote mbili, baadhi ya watu wanaamini kuwa suluhu inaweza kupatikana.
Wazo moja linalojadiliwa ni kuunda mifumo maalumu ya kijeshi inayowaruhusu vijana wa Haredi kuhudumu bila kuacha mfumo wao wa maisha wa kidini.
Wanaounga mkono pendekezo hilo wanasema linaweza kusaidia kupunguza mvutano huku likihakikisha kuwa jamii hiyo inashiriki katika majukumu ya taifa.
Hata hivyo, bado haijulikani kama viongozi wa dini na wanasiasa wa Haredi wako tayari kukubali mabadiliko hayo.
Mgogoro huu unamaanisha nini kwa mustakabali wa Israel?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mtazamo wa wachambuzi wengi, mgogoro huu ni zaidi ya mjadala kuhusu jeshi.
Unahusu swali la aina ya taifa ambalo Israel inataka kuwa katika miongo ijayo.
Kadiri idadi ya Wayahudi wa Kiorthodoksi inavyoendelea kuongezeka, ndivyo maswali kuhusu nafasi yao katika uchumi, siasa, elimu na jeshi yanavyozidi kuwa muhimu.
Wakati vita vya Gaza vikiendelea, suala hilo limepewa uzito mpya na limekuwa jaribio la uwezo wa Israel kusawazisha mahitaji ya usalama wa taifa na uhuru wa makundi mbalimbali ya jamii yake.
Kwa sasa, hakuna suluhu ya haraka inayoonekana.






























