Moja kwa moja, Zaidi ya watu 1000 wakamatwa katika maandamano yaliyoitikisa Ufaransa

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imesema inakadiria kuwa watu 410,000 walishiriki katika maandamano ya hapo jana huku vyama vya wafanyakazi vikikadiria idadi hiyo kufikia takriban 800,000.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Israel kufunga vivuko vya Ukingo wa Magharibi wakati wa uchaguzi

    .

    Vivuko vyote vya mpakani vya kuingia na kutoka eneo la Ukingo wa Magharibi vitafungwa siku ya Jumanne wakati wa uchaguzi nchini Israel, jeshi la nchi hiyo limesema.

    Aidha, wafanyakazi wa Kipalestina hawataruhusiwa kuingia katika makazi yoyote ya walowezi wa Israel.

    Vikwazo hivyo vinakuja wakati Israel imeimarisha operesheni zake za usalama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, baada ya kuuawa kwa wanajeshi wawili wa Israel na wanamgambo wa Kipalestina katika eneo hilo.

    Jeshi la Israel (IDF) lilitangaza kupiga marufuku kuingia na kutoka kwa wafanyakazi wa Kipalestina katika maeneo yote ya Yudea na Samaria pamoja na Bonde la Mto Jordan, yakiwemo maeneo ya viwanda. Pia, vivuko vyote vya mpakani vitafungwa siku ya Jumanne.

    Kabla ya shambulio lililoongozwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, zaidi ya wafanyakazi 100,000 wa Kipalestina waliruhusiwa kuingia Israel kufanya kazi. Tangu wakati huo, ni idadi ndogo tu ambayo walipewa vibali vyao vya kufanya kazi.

    Soma pia:

  2. Brazil kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais wenye ushindani mkali

    .

    Raia wa Brazil wanatarajiwa kupiga kura hii leo, kumchagua rais wao mpya, katika duru ya pili ya uchaguzi uliokumbwa na ushindani mkali.

    Chaguo la raia wa Brazil ni kati ya rais wa sasa mwenye umri wa miaka 80, Luiz Inácio Lula da Silva, wa mrengo wa kushoto, ambaye anawania muhula wa nne usiofuatana madarakani, na seneta wa mrengo wa kulia Flávio Bolsonaro, mwenye umri wa miaka 45.

    Bolsonaro ni mwanawe rais wa zamani wa mrengo wa kulia, Jair Bolsonaro, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kupanga njama ya kupindua serikali baada ya kushindwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka wa 2022.

    Flávio Bolsonaro ndiye anayeonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo, au kupoteza ushindi alioukaribia, baada ya kuongoza katika duru ya kwanza ya upigaji kura iliyofanyika Oktoba 4. Rais wa Marekani Donald Trump alielezea matokeo hayo kuwa ushindi “mkubwa sana.”

    Aidha katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, hakuna kiongozi aliyepata Zaidi ya asilimia 50 za kura katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba huku duru ya pili ya uchaguzi huo ukiwa na ushindani mkali tayari.

    Soma pia:

  3. Obama amkosoa Trump kuhusu vita vya Iran na kupanda kwa gharama ya maisha

    Picha ya Rais wa zamani wa Marekani, Barrack Obama
    Maelezo ya picha, Picha ya Rais wa zamani wa Marekani, Barrack Obama

    Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ameikosoa serikali ya Donald Trump kuhusu vita vya Iran na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

    Obama aliikosa serikali ya Marekani alipokuwa akifanya kampeni ya kuwaunga mkono wagombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.

    “Uchaguzi huu ndio fursa yetu ya mwisho na bora zaidi ya angalau kudhibiti baadhi ya mambo yasiyo na busara yanayofanywa na serikali hii,” Obama aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni katika jimbo la Ohio.

    Aidha, Rais wa Marekani Donald Trump,ametetea sera za serikali yake kuhusu uhamiaji na ushuru wa bidhaa katika mkutano wa kampeni alioufanya katika jimbo la Georgia.

    Uchaguzi wa katikati ya muhula, utakaofanyika tarehe 3 mwezi Novemba, utaamua ni chama gani kitakachodhibiti Bunge la Marekani kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Trump. Matokeo hayo yataathiri pia urahisi wa rais kutekeleza mipango yake.

    Upigaji kura wa mapema tayari umeanza, na Trump alipiga kura yake siku ya hapo jana katika jimbo la Florida, akiwa ameandamana na mkewe, Melania Trump.

    Soma pia:

  4. Zaidi ya watu 1000 wakamatwa Ufaransa katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha

    .

    Maafisa wa usalama nchini Ufaransa, wamesema wamewakamata Zaidi ya watu elfu moja, baada ya mamia ya maelfu ya watu kushiriki maandamano nchini humo, ambayo yalishuhudia makabiliano makali ya polisi hapo jana.

    Baada ya siku nzima ya maandamano yaliyokuwa kwa kiasi kikubwa ya amani, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na magari ya kunyunyizia maji kuwatawanya waandamanaji katika miji kadhaa, ikiwemo Paris.

    Hata hivyo, vizuizi vya barabarani vilichomwa moto katika mji wa Marseille, huku baadhi ya watu wakivunja mbao zilizokuwa zimefunika duka moja katika mji wa Bordeaux.

    Hadi kufikia sasa, maafisa wa usalama wamefanikiwa kuzuia ghasia na uporaji ikilinganishwa na kiwango kilichoshuhudiwa mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo kulishuhudiwa matukio mabaya zaidi ya uharibifu wa amani katika historia ya kisasa ya Ufaransa.

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imesema inakadiria kuwa watu 410,000 walishiriki katika maandamano ya hapo jana huku vyama vya wafanyakazi vikikadiria idadi hiyo kufikia takriban 800,000.

    Mapema wiki hii, Rais Emmanuel Macron alikuwa ameamuru kuwa maandamano yatakayoruhusiwa ni yale tu yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi vinavyotambuliwa rasmi.

    Katika siku za hivi karibuni, mamia ya watu wamehukumiwa vifungo vya jela kwa makosa ya uharibifu wa mali, uchomaji moto na uporaji, kufuatia kusikilizwa kwa kesi zao kupitia taratibu za haraka za mahakama.

    Soma pia:

  5. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumapili ya leo