Mbio za kumrithi Guterres, je UN itapata Katibu Mkuu mwanamke?

Musharaxiinta

Chanzo cha picha, United Nations website: https://news.un.org

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Muhula wa pili wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ukikaribia kukamilika, mchakato wa kumchagua Katibu Mkuu wa kumi, wa Umoja wa Mataifa umeanza tayari.

Wagombea saba kutoka Amerika Kusini na Afrika wamejitosa katika kinyang'anyiro cha kuwania mojawapo ya nyadhfa muhimu zaidi za kidiplomasia duniani.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kuamua mwelekeo wa mojawapo ya taasisi muhimu zaidi za kimataifa katika miaka ijayo.

Baada ya kuhudumu kwa mihula miwili ya miaka mitano, Antonio Guterres anatarajiwa kukabidhi madaraka kwa mrithi wake mwishoni mwa mwaka huu.

Umoja wa Mataifa na mashirika yake yana wafanyakazi pamoja na vikosi vya kulinda amani zaidi ya 100,000.

Mbali na kusimamia taasisi hiyo kubwa, Katibu Mkuu ndiye sura kuu ya diplomasia ya Umoja wa Mataifa. Anatarajiwa kuwa mpatanishi, mwezeshaji wa mazungumzo na msemaji wa jumuiya ya kimataifa wakati wa migogoro ya kimataifa.

Wagombea ni akina nani?

Wagombea saba waliojitosa katika kinyang'anyiro hicho ni:

  • Michelle Bachelet – Rais wa zamani wa Chile.
  • Maria Fernanda Espinosa – Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ecuador na aliyewahi kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
  • Rafael Grossi – Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), kutoka Argentina.
  • Rebecca Greenspan – Makamu wa Rais wa zamani wa Costa Rica.
  • Olara Otunu – kutoka Uganda.
  • Caroline Rodriguez Birkett – Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Guyana.
  • Macky Sall – Rais wa zamani wa Senegal.
QM

Chanzo cha picha, Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huchaguliwa vipi?

Ingawa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hatimaye huidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mchakato wa kumpata huamuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baraza la Usalama lina wajumbe 15, wajumbe watano wa kudumu na wajumbe 10 wasio wa kudumu.

Ili kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu, mgombea anatakiwa kupata angalau kura tisa kati ya 15 za wajumbe wa Baraza la Usalama.

Aidha, mgombea huyo hapaswi kupingwa na mjumbe yeyote kati ya watano wa kudumu, ambao ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China.

Mjumbe yeyote kati ya hao watano wa kudumu ana uwezo wa kutumia haki ya kura ya turufu au veto na kuzuia uteuzi wa mgombea.

Kwa sababu hiyo, uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa si tu kinyang'anyiro kati ya wagombea, bali pia ni kipimo cha kiwango cha makubaliano miongoni mwa mataifa yenye nguvu duniani.

Upinzani kutoka kwa mjumbe yeyote wa kudumu wa Baraza la Usalama unaweza kumzuia mgombea na kupunguza kabisa nafasi yake ya kuchaguliwa.

Baraza la Usalama linapofikia makubaliano kuhusu mgombea, jina lake huwasilishwa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hatua hii mara nyingi huonekana kuwa ya kiutaratibu tu, kwa sababu kwa kawaida Baraza Kuu huidhinisha mgombea aliyependekezwa na Baraza la Usalama.

Ni akina nani wanaoongoza katika kinyang'anyiro cha nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa?

Mgombea Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), amekuwa akitazamwa kwa karibu katika miaka ya hivi karibuni kutokana na nafasi yake katika kushughulikia suala la mpango wa nyuklia wa Iran.

Katika kikao cha maswali na majibu na wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Grossi alizungumzia uzoefu wake katika kushughulikia migogoro ya kimataifa,

"Katika shirika hilo, licha ya vita na migogoro, tumezungumza na viongozi kutoka pande mbalimbali na tumekubalika kuwa wapatanishi. Hii ndiyo nafasi ambayo Umoja wa Mataifa inaweza kutekeleza."

Hata hivyo, kwa mujibu wa matokeo ya duru ya kwanza ya kura, Rebecca Greenspan wa Costa Rica ndiye aliyeonekana kuwa na uungwaji mkono mkubwa zaidi. Katika hotuba yake, alisisitiza kupungua kwa imani ya kimataifa kuhusu uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani, pamoja na umuhimu wa kujenga upya imani katika taasisi hiyo.

Caroline Rodriguez Birkett, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Guyana, pia anaonekana kuwa miongoni mwa wagombea wanaoongoza katika kinyang'anyiro hicho.

UN itamchagua mwanamke wake wa kwanza kuwa Katibu Mkuu?

Musharixiin dumar ah

Chanzo cha picha, United Nations

Tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, taasisi hiyo imekuwa na Makatibu Wakuu tisa, ambao wote wamekuwa wanaume.

Hata hivyo, safari hii, wanawake wanne kati ya wagombea saba wanawania nafasi hiyo, na nchi nyingi zinaamini kwamba baada ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, umefika wakati nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa taasisi hiyo ikabidhiwe mwanamke.