PSG kombe Arsenal pesa, msimu wa mabingwa ulivyofungwa

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa Arsenal baada ya kupoteza dhidi ya PSG
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2025/26 ilimalizika kwa Paris Saint-Germain (PSG) kuiibuka mabingwa baada ya ushindi wa penati dhidi ya Arsenal kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120. Mechi hiyo iliyochezwa mjini Budapest, nchini Hungary, ilihitimisha msimu uliokuwa na ushindani mkali kuanzia hatua ya makundi hadi fainali, huku ukiacha mjadala mkubwa kuhusu tofauti ya mapato kati ya klabu zilizofika mwisho wa mashindano haya.

Kwa PSG, ushindi huo uliwapa heshima ya kuwa mabingwa wa Ulaya mara mbili mfululizo, pamoja na zawadi kubwa ya kifedha inayoifanya klabu hiyo kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa soka la Ulaya.

Kwa Arsenal, licha ya kupoteza fainali kwa penati, safari yao ya kuvutia ilibeba maana kubwa zaidi ya kisoka na kifedha, hasa kutokana na mfumo mpana wa malipo wa UEFA unaoendelea kuwazawadia hata waliomaliza wa pili.

Kwa ujumla, msimu huu umeonesha wazi kuwa Ligi ya Mabingwa si tu mashindano ya ubingwa, bali pia ni chanzo kikuu cha mapato kinachoweza kubadilisha nguvu ya kifedha ya klabu kwa misimu mingi ijayo.

Utaratibu wa zawadi kwa timu shiriki

Mfumo wa malipo wa UEFA katika Ligi ya Mabingwa unajengwa kwa hatua mbalimbali ambazo kila moja ina thamani yake ya kifedha. Timu zote zinazoingia hatua ya ligi hupokea takribani €18.62 milioni (£16.1m) kama malipo ya msingi ya kushiriki, kabla hata ya matokeo kuanza kuhesabiwa.

Katika hatua ya ligi, kila ushindi unaopatikana huongeza mapato ya klabu, huku malipo ya ziada yakitolewa kulingana na nafasi ya kumaliza msimamo. Timu zinazomaliza nafasi za juu hupata bonasi ya takribani €9.9 milioni (£8.6m), huku zile zinazomaliza nane bora kwenye kundi zikiongezewa €2 milioni (£1.7m).

Kadri timu inavyoendelea mbele, malipo yanaongezeka hatua kwa hatua, ambapo kufuzu 16 bora timu huongezewa €11 milioni (£9.5m), robo fainali - €12.5 milioni (£10.8m), na nusu fainali - €15 milioni (£13.0m).

Ukifika fainali huongezewa €18.5 milioni (£16.1m), na mshindi hupata bonasi ya ziada ya €6.5 milioni (£5.6m), jambo linalofanya bingwa kuzoa takribani €150–160 milioni (£130–£139m) kwa msimu mzima wa mashindano.

Zawadi walizopata PSG

c

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

PSG, kama mabingwa wa Ulaya, wamepata moja ya mgao mkubwa wa fedha kutoka UEFA kutokana na safari yao yenye mafanikio makubwa. Kwa ushindi wao wa fainali dhidi ya Arsenal, klabu hiyo imekusanya karibu €150–160 milioni (£130–£139m) kutokana na michango ya kila hatua waliopita katika mashindano.

Kwa kuongeza thamani ya soka la ndani, PSG pia walishinda Ligue 1 ambapo mabingwa wa ligi hiyo hupata takribani €38.5 milioni (£33.4m).

Hata hivyo, tofauti na ligi nyingine kubwa barani Ulaya, malipo ya fedha kwa mshindi wa Ligue 1 ni ya chini zaidi, jambo linalofanya PSG kutegemea sana mapato ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuongeza nguvu yao ya kifedha na ushindani barani Ulaya.

Kwa ujumla, kutwaa klabu bingwa ulaya mara mbili mfululizo kumeimarisha zaidi nafasi ya PSG kama klabu yenye uwezo mkubwa kifedha na kisoka, huku mapato yao yakichangia moja kwa moja katika ujenzi wa kikosi chenye ushindani wa kiwango cha juu.

Fedha walizoingiza Arsenal

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Arsenal, licha ya kupoteza fainali, wamekuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mfumo wa kifedha wa UEFA msimu huu. Kufikia fainali pekee, klabu hiyo tayari imehakikishiwa takribani €105.6 milioni (£91.5m) kutokana na hatua zote walizopita katika mashindano, ikiwa ni pamoja na makundi na hatua za mtoano.

Zaidi ya hapo, Arsenal bado wanatarajiwa kunufaika na mgawanyo wa thamani "value pillar", ambao hutegemea thamani ya soko la nchi na nafasi ya klabu katika mgawo wa UEFA. Mfumo huu huanza na takribani €1.28 milioni (£1.1m) kwa timu zilizo chini, lakini huweza kufikia hadi €46.08 milioni (£39.9m) kwa timu zenye mvuto mkubwa.

Kwa kuwa Arsenal wana nafasi nzuri katika mgao huo wa thamani ya soko a mvuto kwa kuwa Uingereza ina soko kubwa la matangazo Ulaya, ambapo msimu uliopita walipata takribani €34.585 milioni (£30m) katika kipengele hiki, na msimu huu wanatarajia kuingia zaidi ya kiwango hicho.

Kwa ujumla, mapato ya Arsenal kutokana na Ligi ya Mabingwa yanaweza kufikia takribani €156.9 milioni (£136m), na hiyo bado haijumuishi mapato ya ziada ya msimu ujao wa Ulaya ambapo klabu inatarajiwa kupata angalau €20.2 milioni (£17.5m) kabla hata ya kuanza mashindano.

Zaidi ya hayo, mafanikio yao ya ndani ya nchi pia yameongeza mapato makubwa. Kwa kushinda Ligi kuu England (EPL), Arsenal wamepata takribani £192 milioni kutokana na mgawanyo wa haki za matangazo na nafasi yao ya juu kwenye msimamo, ikiwa ni ongezeko kubwa kutokana na mfumo wa malipo wa ligi.

Kwa pamoja, vyanzo hivi vinaweka klabu hiyo katika nafasi ya kuwa na mapato ya msimu yanayoweza kufikia karibu £770 milioni ($1.04bn), na kuwafanya kuwa miongoni mwa klabu tajiri zaidi duniani.

Kwa mtazamo wa jumla, ingawa PSG ndio mabingwa wa Ulaya, Arsenal wanaweza kujikuta wakiwa mabingwa wa mapato kwa mapato ya jumla kutokana na mfumo mpana wa UEFA, ligi ya ndani na haki za matangazo.

Hili ndilo wanaloringia mashabiki wa Arsenal baada ya kupoteza dhidi ya PSG ; Waache PSG wachukue kombe, sie pesa".