Moja kwa moja, Trump ataka marekebisho yafanywe katika mkataba kati ya Marekani na Iran

Mabadiliko yanahusiana na Mlango-Bahari wa Hormuz na kuondolewa kwa madini ya Urani iliyorutubishwa, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Brazil inawafuatilia wagonjwa wawili kwa uwezekano wa kuambukizwa Ebola

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa afya nchini Brazil wamesema wanachunguza kisa cha pili kinachoshukiwa kuwa cha Ebola mjini Rio de Janeiro ambapo raia wa Ubelgiji hivi karibuni aliwasili kutoka Uganda.

    Raia huyo alionyesha"dalili za virusi kama vile kikohozi, baridi na kuhara".

    Kisa kingine kinachoshukiwa kiligunduliwa Jumamosi katika jimbo la São Paulo. Matokeo ya vipimo kwa wagonjwa wote wawili yanatarajiwa kupatikana wiki ijayo.

    Iwapo yatathibitishwa, hii itakuwa mara ya kwanza kwa maambukizi hayo kuripotiwa nje ya Afrika tangu mlipuko ulipoanza nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Mlipuko wa sasa kuna zaidi ya maambukizi 1,000 yenye kushukiwa kuwa Ebola nchini DR Congo, huku vifo vikishukiwa kuwa takriban 246. Uganda imeripoti maambukizi tisa yaliothibitishwa na kifo kimoja.

    Mlipuko wa sasa umesababishwa na aina adimu ya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo haina chanjo iliyothibitishwa.

    Awali, mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwataka watu nchini DRC kutafuta matibabu haraka iwapo watahisi dalili za ugonjwa huo.

    Soma zaidi:

  2. Mlipuko mkubwa waua makumi ya watu katika kijiji kinachoshikiliwa na waasi Myanmar

    .

    Chanzo cha picha, Shwe Phee Myay

    Mlipuko mkubwa umewaua watu wasiopungua 55 na kuwajeruhi wengine kadhaa katika kijiji kimoja katika eneo la Myanmar lililo chini ya udhibiti wa waasi, BBC imeambiwa.

    Chanzo kinachofahamu hali iliyopo eneo la Kaung Tat, kijiji kilichopo katika Mji wa Namkham katika Jimbo la Shan, karibu na mpaka wa China, kilisema wanawake 25 na wanaume 30 wamefariki. Ripoti zingine zilitoa takwimu tofauti kidogo.

    Wingu kubwa la moshi lilionekana likitanda juu ya kijiji muda mfupi baada ya mlipuko kutokea Jumapili.

    Jeshi la Kitaifa la Ta'ang Liberation ambalo linadhibiti eneo hilo na limekuwa likipigana na utawala wa kijeshi, lilisema vilipuzi vinavyotumika katika uchimbaji madini na uchimbaji mawe vimelipuka.

    Soma zaidi:

  3. Polisi Nigeria waonya mashambulizi dhidi ya raia wa Afrika Kusini

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Polisi nchini Nigeria wamewataka wananchi kutojihusisha na “mashambulizi ya kulipiza kisasi” dhidi ya raia au biashara za raia wa Afrika Kusini kufuatia “taarifa za mashambulizi ya chuki dhidi ya raia wa wageni yaliyowalenga raia wa Nigeria nchini Afrika Kusini.

    Katika taarifa, msemaji wa polisi, Anthony Okon Placid, amesema vyombo vya usalama vilifanya tathmini ya hali hiyo baada ya mkutano ulioongozwa na mshauri wa usalama wa taifa, na kuwahakikishia raia wa Nigeria kwamba “hakuna sababu ya kuwa na hofu”.

    Amesema serikali inaendelea kushirikiana na mamlaka za Afrika Kusini pamoja na wadau wengine kupitia njia za kidiplomasia na kiusalama ili kushughulikia hali hiyo na kuhakikisha usalama wa raia wa Nigeria.

    “Ingawa wasiwasi kuhusu mashambulizi dhidi ya Wanigeria nchini Afrika Kusini unaeleweka, wananchi wanashauriwa kutokuchukua sheria mkononi mwao. Mashambulizi ya kulipiza kisasi, vurugu, vitisho, uharibifu wa mali, matamshi ya chuki au vitendo vyovyote vinavyotishia amani ya umma na usalama wa taifa ni kinyume cha sheria na havitavumiliwa,” Bwana Placid amesema.

    Polisi wamesema hatua za ziada za kiusalama zimewekwa katika balozi na misheni za kigeni, miundombinu muhimu pamoja na maeneo mengine nyeti.

    Onyo hilo linatolewa wakati mvutano ukiendelea kuongezeka nchini Afrika Kusini kufuatia maandamano dhidi ya wahamiaji.

    Waandamanaji wamewashutumu wahamiaji wasiokuwa na stakabadhi halali kwa kuongeza shinikizo kwenye huduma za umma na wametoa wito kwa serikali kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

    Soma zaidi:

  4. Wagonjwa 5 wapona virusi vya Ebola nchini Congo - WHO

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefurahia kupona kwa wagonjwa watano walioambukizwa aina ya nadra ya virusi vya Ebola.

    Wanasema hatua hii ni matokeo chanya katika kukabiliana na mlipuko ambao umesababisha vifo vya takriban watu mia mbili arobaini na sita mashariki mwa nchi.

    Hakuna chanjo au matibabu yaliyokubaliwa kwa spishi ya Ebola ya Bundibugyo inayosababisha mlipuko wa sasa.

    Wagonjwa wanne wameruhusiwa kurejea makwao huko Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri, na kufanya jumla ya waliopona kufikia watano.

    Wagonjwa hao -- wauguzi -- walitoka katika kituo cha matibabu huko Bunia jana. Waliambukizwa walipokuwa wakiwahudumia wagonjwa wa Ebola na walisema kwamba wanashukuru kuwa hai.

    Mtu mwingine aliyenusurika, mfanyakazi wa maabara, alienda nyumbani siku ya Ijumaa. Dk Mwamba Kazadi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Umma amewaita waliopona kuwa ni ushindi unaostahili kusherehekewa.

    Amesema ugunduzi wa mapema na utunzaji thabiti ulikuwa msingi wa mafanikio hayo.

    Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye anazuru mkoa wa Ituri, kitovu cha mlipuko huo, amesema uaminifu ni hatua muhimu.

    Amezitaka jamii kushirikiana na wafanyikazi wa matibabu baada ya wakaazi wengine kushambulia vituo vya afya juu ya sheria kali za mazishi ambazo zinakinzana na mila za wenyeji.

    Mbali na Ituri, maambukizi ya Ebola pia yameripotiwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa DRC, pamoja na nchini Uganda.

    Takribani watu 246 wamefariki dunia kutokana na Ebola, huku wengine zaidi ya 1,000 wakishukiwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo.

    Nchi jirani ya Uganda imeripoti kifo kimoja na kuthibitisha watu tisa mpaka sasa wameambukizwa Ebola.

    Soma zaidi:

  5. Trump ataka marekebisho yafanywe katika mkataba kati ya Marekani na Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Donald Trump wa Marekani ameomba marekebisho yafanywe kwenye makubaliano kati ya Marekani na Iran yanayolenga kukomesha mapigano yaliyoanza mapema mwaka huu, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti.

    Mabadiliko hayo yanahusiana na Mlango-Bahari wa Hormuz na kuondolewa kwa madini ya urani, CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, iliripoti. Ikulu ya White House haikujibu ombi la kutoa maoni.

    Mohammad Bagher Ghalibaf, mpatanishi mkuu wa Iran, alisema Jumapili kwamba Tehran haitakubali makubaliano yoyote isipokuwa haki za Iran zipatikane kikamilifu.

    Rais na wasaidizi wake wakuu walikutana Ijumaa kufanya "uamuzi wa mwisho" juu ya mfumo wa kuongeza muda katika suala la kusitisha mapigano na Iran, lakini mkutano huo ulimalizika bila ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata.

    Makubaliano hayo yaliyoripotiwa kwa mara ya kwanza na Axios siku ya Jumamosi, yanajumuisha kusitishwa kwa vurugu kwa siku 60, wito wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na mfumo wa kufungua tena na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, kulingana na CBS.

    Ikiwa diplomasia itaendelea, makubaliano hayo pia yanaripotiwa kuhusisha uwezekano wa kupunguzwa vikwazo kwa Iran ambavyo vinaweza kuiruhusu kupata mabilioni ya dola katika mali zilizozuiliwa, CBS ilisema.

    Ripoti za Jumapili za marekebisho zaidi ni hatua ya hivi karibuni katika mazungumzo ya siku nyingi kati ya Ikulu ya White House na Iran kuhusu mfumo wa makubaliano yanayolenga kukomesha vita vya miezi kadhaa.

    Siku ya Alhamisi, maafisa wa Marekani walisema nchi hizo mbili zimekubaliana kuhusu mfumo - unaojulikana kama mkataba wa makubaliano - unaosubiri idhini ya Trump na uongozi wa Iran.

    Soma zaidi:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya Tarehe 01/06/2026.