Rekodi 11 na historia zilizoandikwa EPL msimu huu, Arsenal ikitwaa ubingwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Msimu wa 2025/26 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umefungwa rasmi Jumapili hii kwa Arsenal kutwaa ubingwa wa ligi baada ya miaka 22. Nyuma yao, Manchester City, Aston Villa, Liverpool pamoja na Manchester United zimefanikiwa kufuzu michuano ya Ligi ya mabingwa Ulaya, huku Bournemouth na Sunderland zikiiandika historia kwa kufuzu michuano ya Ulaya.
Bournemouth imefuzu Europa League kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake miaka 127 iliyopita. Sunderalnd ikifuzu michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka zaidi ya 50, ikimaliza nafasi ya 7 kwenye ligi, ikifunga Chelsea mabao 2-1 huku Chelsea ikimaliza nafasi ya 10 na kukosa michuano ya Ulaya msimu ujao.
Kwa upande mwingine, msimu huo ulihitimisha safari ya Tottenham Hotspur waliomaliza nafasi ya 18 katika moja ya misimu mibaya zaidi katika historia yao ya EPL. Sambamba nao, West Ham United, Wolverhampton Wanderers pamoja na Burnley zilishuka daraja baada ya kushindwa kuhimili presha ya ligi hiyo ngumu zaidi duniani.
Lakini mbali na mbio za ubingwa, vita vya Ulaya na majonzi ya kushuka daraja, msimu wa 2025/26 utakumbukwa zaidi kwa rekodi nyingi zilizovunjwa. Kuanzia kwa wakongwe waliodumu kwa zaidi ya miongo miwili hadi vijana wadogo waliotikisa dunia kwa mafanikio makubwa, EPL imeandika upya historia yake katika msimu ambao mashabiki hawatausahau kwa haraka.
Max Dowman na rekodi tatu za 'kinda'

Chanzo cha picha, Getty Images
Kinda mwenye kipaji wa Arsenal mwenye miaka 16, Max Dowman, alivunja rekodi na kuandika historia tatu: Mosi kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kushinda ubingwa wa EPL akiwa na miaka 16 na siku 144. Dowman alivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Phil Foden ambaye alitwaa ubingwa akiwa na miaka 17 na siku 350 akiwa Manchester City.
Kinda huyo pia aliweka rekodi nyingine kadhaa ikiwemo kuwa mfungaji mdogo zaidi EPL baada ya kufunga dhidi ya Everton akiwa na miaka 16 na siku 73. Rekodi ya awali ilikuwa ikishikiliwa kwa zaidi ya miaka 20 na James Vaughan aliyefunga akiwa na miaka 16 na siku 270 mwaka 2005. Pia nyota huyu akitokea kufanya mitihani shuleni ameweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuanza mchezo wa Ligi kuu , akicheza dakika 62 katika mchezo wa mwisho wa ligi Jumapili dhidi ya Crystal Palace, Arsenal ikishinda 2-1 ugenini.
Bruno Fernandes avunja rekodi mbili kwa pasi za mabao

Chanzo cha picha, Getty Images
Rekodi ya nne na ya tano zimewekwa na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, aliweka historia baada ya kufikisha pasi za mabao 21 ndani ya msimu mmoja wa EPL.
Idadi hiyo ilimfanya avunje na rekodi iliyowahi kuwekwa na manguli Thierry Henry wa Arsenal katika msimu wa 2002/03 pamoja na Kevin De Bruyne wa Manchester City katika msimu wa 2019/20.
Mbali na hilo, pasi zake za mabao zilichangia alama 24 kwa Manchester United ndani ya msimu mmoja, rekodi mpya EPL iliyovunja rekodi ya alama 17 iliyowekwa msimu wa 1994/95 na kiungo wa zamani Tottenham Hotspur, Darren Anderton .
Haaland na rekodi ya mabao 100 ya haraka

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa wa Manchester City, Erling Haaland, alivunja rekodi ya kufikisha mabao 100 EPL kwa haraka zaidi. Kwa maneno rahisi katika rekodi hii ya sita, alifikisha mabao 100 kwa kucheza mechi chache zaidi ukilinganisha na mchezaji yeyote yule kwenye ligi hiyo
Mshambuliaji huyo alifikia idadi hiyo ndani ya mechi 111 pekee na kumpita Alan Shearer, nyota wa zamani wa Blackburn Rovers na Newcastle United aliyefikisha mabao hayo 100 ndani ya miechzo 124.
Haaland pia alimaliza msimu akiwa kinara wa mabao kwa kufunga mabao 27 na kutwaa kiatu cha dhahabu kwa mara nyingine kama mfungaji bora wa ligi.
Raya na rekodi mbili za kipekee za 'Golden Glove'

Chanzo cha picha, Getty Images
Kipa wa Arsenal F.C., David Raya ameweka rekodi mbili za kipekee baada ya kuwa kipa pekee katika historia kushinda tuzo ya Goligipa bora (Golden Glove) katika ligi kuu EPL na ile ya Championship.
Raya pia ameandika historia pia kwa kushinda tuzo hiyo ya Golden Glove kwa misimu mitatu mfululizo ya 2023/24, 2024/25 na 2025/26. Mafanikio hayo yamemuingiza kwenye orodha ya makipa wanne pekee waliowahi kufanya hivyo katika historia ya EPL, akiwafuata nyayo za Pepe Reina (Liverpool), Joe Hart na Ederson (Man City).
Katika msimu wa 2025/26, Raya hajaruhusu bao (clean sheets) katika michezo 19 kati ya 37 alizoichezea Arsenal, akifikia rekodi ya kipa nguli wa klabu hiyo David Seaman aliyoweka katika misimu ya 1993/94 na 1998/99.
James Milner na rekodi tatu za utu uzima

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkongwe James wa Brighton & Hove Albion anafunga dimba kwa rekodi 3 muhimu. Aliweka rekodi kwa kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika historia ya EPL akicheza mechi 658 na kumpita Gareth Barry aliyecheza mechi 653. Alivunja rekodi hii mwezi Machi, 2026.
Kiungo huyo wa zamani wa Liverpool, Man City na Aston Villa pia aliweka rekodi ya kucheza misimu 24 mfululizo EPL tangu alipoanza kucheza akiwa na miaka 16 mwaka 2002.
Milner aliweka pia rekodi ya pengo la muda mrefu zaidi kati ya bao lake la kwanza kufunga na la mwisho kufunga ndani ya EPL. Pengo hilo ni miaka 22 na siku 248.
Historia zingine zilizowekwa EPL msimu huu

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mbali na rekodi binafsi za wachezaji, msimu wa 2025/26 wa ligi kuu ya England (EPL) , uliandika historia nyingine kubwa kupitia vilabu na makocha walioonyesha ubora wa kipekee ndani ya England.
Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal waliweka rekodi mpya ya klabu kwa kushinda mechi 42 katika mashindano yote ndani ya msimu mmoja, mafanikio yaliyowasaidia kutwaa ubingwa wa EPL na kujithibitisha kama moja ya timu bora zaidi barani Ulaya msimu huo. Arteta pia aliingia kwenye historia ya EPL baada ya kuwa mmoja wa watu wachache waliowahi kucheza EPL na baadaye kushinda ubingwa huo kama kocha.
Kabla yake, mafanikio hayo yaliwekwa na Roberto Mancini aliyecheza Leicester City kwa mkopo mwaka 2001 na baadaye kushinda taji la EPL kama kocha akiwa Manchester City, lakini Arteta ameweka historia ya kipekee zaidi kwa kuwa kocha wa kwanza kushinda EPL akiwa ameichezea klabu hiyo hiyo aliyokuja kuipa ubingwa katika zama za EPL.
Kwa upande mwingine, Bournemouth waliandika rekodi yao baada ya kucheza mechi 17 mfululizo bila kupoteza, jambo lililowapa nafasi ya kufuzu michuano ya Europa League kwa mara ya kwanza katika historia yao. Nao Aston Villa waliweka rekodi ya ushindi wa mechi nane mfululizo na kujihakikishia nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa ulaya msimu ujao.
Msimu huo pia uliingia kwenye historia kwa kuwa na asilimia kubwa zaidi ya mechi zilizoamuliwa na mabao ya dakika za mwisho, hali iliyoonyesha ushindani mkubwa uliokuwepo EPL kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kampeni hiyo ya kihistoria.














