Manchester City yapatikana na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Klabu ya Manchester City imepatikana na hatia ya kukiuka idadi kubwa ya kanuni 115 za kifedha ambazo ilikuwa inatuhumiwa kuvunja.

Kwa mujibu wa ripoti ya The Athletic, hatua za adhabu bado hazijaamuliwa, lakini jopo huru lililokuwa likichunguza kesi hiyo limefikia uamuzi wake na kuikuta klabu hiyo na hatia katika mashtaka yote isipokuwa shtaka moja.

Ligi Kuu ya England imekataa kutoa maoni kuhusu taarifa hiyo.

Ilipoulizwa iwapo ripoti hiyo ni sahihi, Manchester City nayo haikuthibitisha wala kukanusha.

Badala yake, klabu hiyo ilitoa taarifa ikisema kuwa "mchakato wa Premier League bado unaendelea, huku baadhi ya vipengele muhimu vikiwa bado havijakamilika na vikibaki kuwa vya siri."

Taarifa hiyo iliongeza kuwa:

"Klabu imeheshimu ipasavyo mchakato wa kisheria kwa kipindi cha miaka minane, kwa msingi kwamba bodi na uongozi wa Premier League utafanya kazi kama mdhibiti huru, asiye na upendeleo na mwenye haki."

BBC Sport pia imeelezwa kuwa iwapo Manchester City itapatikana na hatia rasmi, klabu hiyo itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Inaaminika pia kwamba klabu nyingine za Premier League zimejulishwa kuhusu uamuzi wa jopo hilo huru na zimeanza kutafuta ushauri wa kisheria kuhusu uwezekano wa kudai fidia.

Historia ya kesi hiyo ni ipi?

.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwezi Februari 2023, Manchester City ilishtakiwa kwa zaidi ya ukiukwaji 100 wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu ya England (Premier League) kufuatia uchunguzi uliodumu kwa miaka minne.

Klabu hiyo iliwasilishwa mbele ya tume huru kutokana na tuhuma kwamba ilikiuka kanuni za kifedha kati ya mwaka 2009 na 2018.

Usikilizwaji wa kesi hiyo ulianza mwezi Septemba 2024 kwa faragha na kukamilika mwezi Desemba 2024, baada ya takriban wiki 12 za vikao.

Premier League ilidai kuwa Manchester City ilikiuka kanuni zinazotaka klabu kutoa taarifa sahihi za kifedha zinazoonyesha hali halisi ya kifedha ya klabu hiyo.

Ligi hiyo ilisema City ilishindwa kutoa taarifa za kifedha zenye uwazi na usahihi, jambo ambalo ni hitaji muhimu katika kuhakikisha ushindani wa haki miongoni mwa klabu zinazoshiriki Premier League.

Manchester City imekuwa ikikanusha vikali tuhuma zote ilizokabiliwa nazo na imesema kuwa utetezi wake unaungwa mkono na "ushahidi mpana usioweza kupingwa".

Katika kipindi kinachohusishwa na kesi hiyo, klabu hiyo ilitwaa mataji manane, yakiwemo mataji matatu ya Ligi Kuu ya England, matatu ya Kombe la Ligi (League Cup), moja la Community Shield na moja la Kombe la FA (FA Cup).

Mashtaka hayo yanahusu vipindi vya ukocha vya Roberto Mancini na Manuel Pellegrini, pamoja na miaka miwili ya mwanzo ya Pep Guardiola, ambaye aliondoka klabuni baada ya misimu 10 mwishoni mwa kampeni ya 2025-26.

Kesi nyingine tofauti kati ya Manchester City na Premier League pia ilisikilizwa mwaka jana.

Mwaka 2024, jopo huru la usuluhishi liliamua kuwa baadhi ya vipengele vya kanuni za Associated Party Transactions (APTs) za Premier League havikuwa halali, baada ya Manchester City kufungua kesi ya kuyapinga.

APTs ni kanuni zinazolenga kusimamia mikataba ya kibiashara na udhamini kati ya klabu na kampuni zinazohusishwa na wamiliki wake, ili kuhakikisha mikataba hiyo inazingatia thamani halisi ya soko.

Aidha, mwezi Februari 2025, mahakama ya usuluhishi iliamua kuwa baadhi ya kanuni za Premier League zilizokuwa zikisimamia mikataba ya udhamini kati ya mwaka 2021 na 2024 zilikuwa "batili na haziwezi kutekelezwa kisheria."

Manchester City na Ligi Kuu ya England (Premier League) zilifikia mwafaka mwezi Septemba 2025, ambapo klabu hiyo ilikubali kwamba kanuni za Associated Party Transactions (APTs) ni halali na zina nguvu kisheria. Pande zote mbili pia zilikubaliana kusitisha mashauri ya kisheria yaliyokuwa yakiendelea.

Kanuni hizo ziliwekwa na Premier League kwa lengo la kuzuia klabu kunufaika kupitia mikataba ya kibiashara au ya udhamini na kampuni zinazohusishwa na wamiliki wao, pale mikataba hiyo inapozidi kile kinachoonekana kuwa thamani halisi ya soko

Kwa mujibu wa Premier League, sheria hizo zinalenga kuhakikisha ushindani wa haki kati ya vilabu na kuzuia baadhi ya klabu kupata faida isiyo ya kawaida kupitia kampuni zinazohusiana na wamiliki wao.

Mashtaka 115 dhidi ya Manchester City yalikuwa yapi?

54: Kushindwa kutoa taarifa sahihi za kifedha kati ya misimu ya 2009-10 na 2017-18.

14: Kushindwa kutoa taarifa sahihi kuhusu malipo ya wachezaji na mameneja kati ya 2009-10 na 2017-18.

5: Kushindwa kuzingatia kanuni za UEFA, ikiwemo Financial Fair Play (FFP), kati ya 2013-14 na 2017-18.

7: Kuvunja kanuni za Profitability and Sustainability Rules (PSR) za Premier League kati ya 2015-16 na 2017-18.

35: Kushindwa kushirikiana na uchunguzi wa Premier League kati ya Desemba 2018 na Februari 2023.

Ingawa kesi hiyo imekuwa ikijulikana kama ya "mashtaka 115", ripoti kutoka gazeti la The Times na mtaalamu wa masuala ya fedha katika soka Kieran Maguire zimependekeza kuwa idadi halisi ya mashtaka inaweza kufikia 130. Hata hivyo, BBC Sport haijaweza kuthibitisha taarifa hiyo.