Kwa nini Austria ilibadilisha mahali alipozaliwa Hitler kuwa kituo cha polisi?

.

Chanzo cha picha, Bethany Bell/BBC

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Austria imefungua kituo cha polisi katika nyumba ambayo Adolf Hitler alizaliwa. Jengo hilo liko katika mji wa Braunau am Inn, ulioko kaskazini mwa Austria, ambao una wakazi wapatao 17,000.

Hatua hiyo inajiri baada ya miaka mingi ya mjadala na kutokubaliana kuhusu hatima ya jengo hilo, ambalo hapo awali lilitumiwa na wageni kama sehemu ya kujipumzisha katika karne ya 17 na mahali ambapo Hitler, kiongozi wa Ujerumani wa Nazi, alizaliwa mnamo Aprili 1889.

Jengo hilo limefanyiwa ukarabati mkubwa na muonekano wake wa nje umebadilishwa, lakini kwa miaka mingi limekuwa changamoto kubwa kwa mamlaka za Austria, ambazo zinajaribu kuzuia mahali hapo alipozaliwa Hitler kugeuka kuwa eneo la mikusanyiko na mahali pa hija kwa wafuasi wa itikadi za 'neo-Nazi'.

Hitler aliishi katika nyumba namba 15, Saltsburger Forststadt, kwa wiki chache tu kabla ya familia yake kuhamia nyumba nyingine huko Braunau, mji ulioko mpakani mwa Ujerumani. Waliondoka katika mji huo wakati alipokuwa na umri wa miaka mitatu.

Mnamo mwaka wa 1938, baada ya Austria kuunganishwa na Ujerumani ya Nazi, Hitler alirejea Braunau kwa muda mfupi akiwa njiani kuelekea Vienna.

Hafla ya ufunguzi wa kituo hicho cha polisi, ambayo ilihudhuriwa na bendi ya muziki ya polisi, ilihudhuriwa pia na Gerhard Karner, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria, pamoja na maafisa kadhaa wa eneo hilo.

Karner alisema kuwa Austria inachukua jukumu na kuwajibikia historia yake mambo mabya yaliyotokea, akiongeza kuwa ingawa uamuzi kuhusu hatima ya jengo hilo haukuwa rahisi, aliamini kuwa kuanzisha kituo cha polisi hapo kungeashiria "sura mpya" kwa nchi hiyo.

"Sasa nyumba hii itakuwa mahali pa demokrasia, utawala wa sheria, usalama, uhuru na utu wa binadamu," alisema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images/ EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadaye, padri wa kanisa la katoliki alibariki misalaba miwili ambayo itawekwa katika kituo kipya cha polisi.

Kwa miongo kadhaa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Austria ilikuwa imepangisha jengo hilo kutoka kwa mmiliki wake wa awali, mwanamke aliyeitwa Gerlinde Pommer. Kwa kulipa kodi ya juu, mamlaka za Austria zilijaribu kuzuia jengo hilo kuwa mahali pa watu kuzuru na kukusanyikia na wafuasi wa mrengo wa kulia pamoja na wale wenye itikadi za Kinazi-mamboleo.

Jengo hilo lilimilikiwa na shirika la hisani kwa miaka mingi na kutumika kama kituo na mahali pa watu walio na matatizo na mahitaji malaum ya kiafya.Hata hivyo, shirika hilo lililazimika kuhama jengo hilo mwaka wa 2011 kwa sababu mmiliki alipinga mipango ya ukarabati. Mmiliki huyo pia alikataa mara kwa mara kuliuza jengo hilo kwa serikali.

Matokeo yake, nyumba hiyo ilibaki wazi kwa miaka kadhaa huku migogoro kati ya maafisa wa serikali na mmiliki ikiendelea kuhusu masharti ya uhamisho wa umiliki wake.

Mwaka wa 2016, bunge la Austria lilipitisha sheria iliyoruhusu serikali kutwaa nyumba ya Gerlinde Pommer. Serikali ilimlipa fidia ya euro 812,000 ili kupata umiliki wa mali hiyo.

Baadaye, mmiliki wa jengo hilo alifungua kesi dhidi ya serikali akidai kuwa malipo hayo hayakutosha, lakini hatimaye alishindwa katika kesi hiyo.

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria wa wakati huo, Wolfgang Sobotka, hapo awali alisema kwamba jengo hilo linapaswa kubomolewa na kujengwa upya. Pendekezo hili lilikuwa sawa na mpango uliotolewa mapema na mwakilishi wa Urusi ambaye alisema angependa kununua nyumba hiyo na kuilipua.

Lakini wazo hilo lilikabiliwa na wimbi la ukosoaji, huku wengi wakisema kwamba kubomoa nyumba hiyo kungekuwa sawa na kukana kipindi cha nyuma cha Nazi cha Austria.

Mnamo mwaka wa 2019, serikali ilitangaza mipango ya kubadilisha jengo hilo kuwa kituo cha polisi, na shindano la EU kote lilifanyika kwa wasanifu kuwasilisha miundo yao.

Mamilioni ya Euro yalitumiwa kukarabati jengo hili la zamani la rangi ya manjano, ambalo sasa linaonekana tofauti kabisa.

Jengo hilo, ambalo sasa limepakwa rangi nyeupe ndani na nje, limepambwa kwa sehemu za mbao ya mwaloni zinazong'aa. Pia, ngazi ya zamani ya iliyozunguka eneo la kuingilia lenye umbo la tao zimehifadhiwa.

Mkaguzi Mkuu wa Polisi Ludwig Heise alisema anafurahi kufanyia kazi katika "jengo zuri na la kisasa kama hili."

"Tuna nafasi zaidi, lakini mbali na hayo, ni kama kituo kingine chochote cha polisi nchini Austria," aliongeza.

.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Hata hivyo, si kila mtu anayefurahishwa na uamuzi wa kubadilisha jengo hilo kuwa kituo cha polisi, na baadhi wanaamini hatua hiyo inatoa ujumbe usio sahihi.

Baadhi walitaka kulifanya jengo hilo kuwa kituo cha kukiri uwajibikaji wa kihistoria na kukabiliana na historia ya enzi ya Nazi. Wengine, akiwemo mwanahistoria Florian Kotanco, walipendekeza shirika la hisani lirejee katika jengo hilo.

"Lakini hata shirika hilo la hisani lenyewe lilisita kurejea, likiamini kuwa lingeweza kutumiwa kama chombo cha mjadala wa kisiasa, hivyo serikali ililazimika kuchagua njia nyingine," Florian Kotanco aliambia BBC.

Hakuna mabango au alama yoyote kwenye nyumba hiyo inayoonyesha historia yake, na kamera za usalama zimewekwa kuzunguka jengo hilo ili kufuatilia mienendo ya watu wanaoweza kulitembelea wakiwa na nia zinazohusiana na itikadi ya 'neo-Nazi'.

Alama pekee inayounganisha mahali hapa na Hitler ni jiwe la kumbukumbu lililowekwa mwaka 1989 kwenye barabara iliyo mbele ya jengo hilo.

Sentensi ifuatayo imechorwa kwenye jiwe hilo la kumbukumbu: "Fashisti kamwe isijirudie; kwa kumbukumbu ya mamilioni ya wahanga."

Jiwe hilo lilihamishiwa hapo kutoka kwenye kambi ya zamani ya mateso ya Mauthausen, iliyo karibu na eneo hilo.

Jina la Hitler halionekani popote. Hata hivyo, Florian Kotanko anaamini kuwa historia ya mahali hapo haitasahaulika kamwe, hata kama idadi ya wafuasi wa itikadi ya 'neo-Nazi' wanaokitembelea itapungua.

"Ni lazima tukabiliane nayo, na sote tumejaribu kushughulikia suala hili kwa uwazi na uaminifu," anasema. "Suala si kujivunia, bali ni kukubali uhalisia."