Ni vyakula gani unapaswa kuhifadhi kwa ajili ya dharura?

.
    • Author, أنابيل راكهام
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Je, unakumbuka siku za mlipuko wa virusi vya corona? Na jinsi tulivyolazimika kuhifadhi baadhi ya vyakula kutokana na muda wa amri ya kutotoka nje uliowekwa wakati huo?

Sababu mbalimbali zinaweza kutulazimisha kuhifadhi vyakula vya msingi kwa ajili ya kukabiliana na dharura zinazoweza kutokea.

Mapema mwezi huu, serikali ya Uingereza iliwashauri watu kuongeza bidhaa zinazoweza kukaa kwa muda mrefu kwenye orodha zao za manunuzi, kwa kujiandaa na uwezekano wa kukwama kwa mnyororo wa usambazaji wa chakula.

Mabadiliko ya tabianchi, kwa mfano, mashambulizi ya mtandaoni, milipuko ya magonjwa na bila shaka vita na migogoro, vinaweza kuvuruga mnyororo wa usambazaji wa chakula au hata kuzuia kabisa chakula kuwafikia wafanyabiashara na majumbani mwetu.

Tazama hapa
Maelezo ya video, Tazama: Vyakula unavyopaswa kuhifadhi kwenye kabati lako

Profesa Richard Wilding, mtaalamu wa mikakati ya mnyororo wa usambazaji, anasema hakuna sababu kubwa ya kuwa na wasiwasi, kwa kuwa wataalamu wa usafirishaji wa bidhaa duniani wanaendelea kuzoea mabadiliko. Hata hivyo, anasema watu wanapaswa kuwa tayari kununua bidhaa tofauti endapo itakuwa muhimu.

Anasema: "Bidhaa ambazo hapo awali zilipatikana kwa wingi madukani zinaweza ghafla kuwa adimu."

Kwa hiyo, ni kwa kiwango gani ni rahisi kuhifadhi chakula, na ni mambo gani yanapaswa kuepukwa wakati wa kuhifadhi?

.
Maelezo ya picha, Samaki wenye mafuta waliowekwa kwenye makopo, wakiwemo salmon, makrill na tuna, ni miongoni mwa vyakula muhimu kwa watu wanaotaka kuhifadhi akiba ya chakula.

Ni vyakula gani ninapaswa kuhifadhi?

Dkt. Sammy Gill, kutoka British Nutrition Foundation, anasema baadhi ya makundi ya vyakula yanapaswa kupewa kipaumbele:

  • Wanga tata kama biskuti za ngano, nafaka zisizokobolewa, crackers, mkate, pamoja na shayiri, mchele na pasta.
  • Protini kama njegere zilizowekwa kwenye makopo, dengu, maharagwe mekundu, karanga zisizo na chumvi, siagi ya karanga na samaki wenye mafuta waliowekwa kwenye makopo kama tuna, makrill na dagaa.

Rebecca McManumon, mtaalamu wa lishe, anataja pia mambo yafuatayo:

  • Unaweza kula matunda yaliyowekwa kwenye makopo pamoja na juisi yake ili kupata maji zaidi, vitamini na nyuzinyuzi.
  • Vyakula vilivyowekwa kwenye siki au chumvi kama mboga na mayai.

Wataalamu hao wawili pia wanashauri kuhifadhi maziwa yenye muda mrefu wa matumizi, ili kupata protini na kalsiamu.

.

Ni nini ninachopaswa kuepuka ninaponunua mahitaji?

Gill anasema unapaswa kuzingatia kiwango cha chumvi na sukari wakati wa kununua vyakula vilivyowekwa kwenye makopo:

  • Epuka vyakula vya makopo vilivyohifadhiwa kwenye maji yenye chumvi nyingi au sharubati yenye sukari; chagua vilivyowekwa kwenye maji, ambavyo ni bora zaidi kiafya.
  • Epuka noodles za kupikwa haraka na supu za makopo, kwa kuwa mara nyingi huwa na kiwango kikubwa cha chumvi.
  • Epuka nafaka za kifungua kinywa zenye sukari iliyoongezwa na zenye thamani ndogo ya lishe.
  • Chagua samaki wa makopo badala ya nyama za makopo kama soseji, hot dog au nyama ya ng'ombe ya makopo, kwa kuwa mara nyingi huwa zimechakatwa na zina chumvi nyingi pamoja na mafuta yaliyoshiba.
  • Punguza matumizi ya vitafunwa vitamu kama biskuti na chokoleti, kwa kuwa vina kiwango kikubwa cha sukari.

Je, kuna njia ya kufanya vyakula vya msingi viwe na ladha nzuri?

McManumon anasema unaweza kuhifadhi karanga kama mbadala wa vyakula vitamu, lakini unapaswa kufahamu kuwa muda wake wa kukaa bila kuharibika unaweza kuwa mfupi.

Pia anapendekeza kuhifadhi viungo vya majani vilivyokaushwa, viungo mbalimbali na chumvi, kwa kuwa vyakula vya makopo vinaweza kuwa na ladha isiyo na mvuto.

.
Maelezo ya picha, Wataalamu wanasema: Boresha kidogo ladha ya vyakula vya msingi kwa kutumia siagi ya karanga na vyakula vilivyowekwa kwenye siki.

Maji na vitamini: Ni mambo gani mengine yanapaswa kuzingatiwa?

McManumon anasema tunapaswa kulenga kutumia takribani mililita 1,500 hadi 2,500 za maji na vinywaji kwa siku, bila kujali hali ya hewa.

Kiasi hicho kinaweza kupatikana kupitia maji ya chupa, pamoja na vyakula vya makopo vyenye majimaji, iwapo upatikanaji wa maji mengine utakuwa mdogo.