Kwanini Tanzania inaweza kufuzu Kombe la Dunia 2030?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Saa 12 alfajiri, nikiwa namsindikiza jirani yangu kurudi nyumbani baada ya kuangalia mechi mbili za ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 zilizochezwa Marekani, Mexico na Canada, tulitembea polepole katika ukimya wa usiku uliokuwa unaanza kukabidhi nafasi kwa alfajiri.
Tulikuwa tumekesha tangu saa nne usiku. Kwanza tukiitazama Mexico v Afrika Kusini, kisha Korea Kusini v Jamhuri ya Czech. Maelfu ya kilomita kutoka Tanzania, mataifa hayo yalikuwa yanatimiza ndoto ambayo Watanzania wanaiota na kusubiri kwa miongo na miongo toka taifa hilo liumbwe.
Ghafla jirani yangu akavunja ukimya. "Yaani mimi nakesha kuwaangalia Wakorea?"
Alikuwa anatania. Lakini ndani ya utani huo kulikuwa na swali kubwa zaidi: Kwa nini si Tanzania?
Nilimjibu haraka: "Ipo siku utaikesha ukiiangalia Taifa Stars."
Akacheka kidogo.
Kisha akanirushia swali ambalo limekuwa mjadala mkubwa katika wiki za hivi karibuni.
"Unadhani kweli Tanzania inaweza kufuzu Kombe la Dunia?"
Swali hili si la jirani yangu huyu pekee. Ni swali la mamilioni ya Watanzania wanaokesha kwenye mabaa, sebuleni, mabweni ya vyuo na kwenye simu zao za mkononi wakishangilia Argentina, Ureno, Ufaransa au Brazil huku wakisubiri siku ambayo bendera ya Tanzania itapeperuka kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.
Na pengine ndiyo maana, wiki chache baada ya Serengeti Boys kufika fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON-U17), kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kwamba vijana hao watawekwa kambi maalumu kuelekea ndoto ya Kombe la Dunia 2030, ilizua mjadala mkubwa kuliko hata ushindi wenyewe.
Tanzania haijawahi kufuzu fainali za Kombe la dunia kwa timu ya wakubwa wanaume, na kwa miaka mingi, swali la Tanzania kufuzu Kombe la Dunia lingeonekana kama ndoto ya mbali. Lakini safari hii, kwa mara ya kwanza, linaonekana kama jambo linaloweza kujadilika.
Safari ya misingi na mifumo

Chanzo cha picha, Micky Jnr
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa miongo mingi Tanzania ilikuwa inategemea vipaji vya asili. Kulikuwa na wachezaji wazuri, lakini hakukuwa na mfumo wa kuwatafuta, kuwalea na kuwafikisha kwenye viwango vya juu vya ushindani.
Katika miaka ya hivi karibuni hali hiyo imeanza kubadilika. Kupitia vituo vya maendeleo ya vipaji vya TFF vya Kigamboni na Tanga, Tanzania imeanza kujenga kile ambacho wataalamu wa maendeleo ya michezo wanakiita mfumo wa muda mrefu wa kuzalisha wachezaji.
Hapa vijana hawaishi kama wanasoka pekee. Wanasoma darasani asubuhi, wanafanya mazoezi mchana na kurejea kwenye masomo jioni. Ni mfumo unaofanana na ule unaotumiwa katika baadhi ya nchi zilizofanikiwa duniani.
Kupitia mpango wa FIFA Forward, Tanzania ilipata zaidi ya dola milioni 4.1 kwa ajili ya miundombinu na zaidi ya dola milioni 1.6 kwa ajili ya maendeleo ya timu za taifa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2022.
Fedha hizo zimesaidia kujenga vituo vya maendeleo ya vijana, kuboresha viwanja na kuongeza uwezo wa kiufundi wa soka la Tanzania.
Mwandishi maarufu wa michezo kutoka Ghana, Micky Jnr, alipotembelea Kituo cha TFF Tanga alikiri kushangazwa na kile alichokiona.
"Niliona kazi inayofanyika nyuma ya pazia. Kuanzia watoto wanaporudi kutoka shule, wanavyofanya mazoezi hadi wanavyorudi darasani jioni. Mustakabali wa soka la Tanzania haujengwi kwa bahati. Unajengwa kwa makusudi kila siku."
Matokeo ya uwekezaji huo tayari yanaanza kuonekana. Mmoja wa vijana waliopitia mfumo huo ni Dismas Athanas, mfungaji bora wa michuano ya AFCON kwa vijana mwaka 2025 na zao la Kituo cha Maendeleo ya Vipaji cha TFF kilichopo Tanga.
Athanas amekaa kituoni hapo kwa miaka minne. "Kituo kimetusaidia sana kupata ujuzi mzuri na kufikia malengo tuliyojiwekea ya kufuzu Kombe la Dunia," anasema.
Ndoto yake ni kucheza soka Ulaya. Lakini zaidi ya hayo, anataka kuwa sehemu ya kizazi kitakachoandika historia ya Tanzania kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Morocco imefikaje ilipo? Somo ambalo Tanzania inaanza kulifuata

Chanzo cha picha, Getty Images
Kama kuna taifa moja ambalo Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwake, basi ni Morocco. Leo Morocco ni moja ya mataifa yenye mafanikio makubwa zaidi katika soka la Afrika.
Mwaka 2022 ilifika nusu fainali ya Kombe la Dunia na kuwa taifa la kwanza Afrika kufikia hatua hiyo. Mwaka 2025 ilitwaa Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya Senegal kupokwa ushindi wa uwanjani.
Lakini mafanikio hayo hayakuanza mwaka 2022. Yalianza karibu miaka 20 iliyopita.
Kupitia Mohammed VI Football Academy, kituo cha kukuza vipaji, Morocco iliamua kubadili kabisa namna ya kuendesha soka lake. Kwa mujibu wa taarifa za CAF, zaidi ya watoto 15,000 walikusanywa na kufanyiwa tathmini kutoka sehemu mbalimbali za nchi.
Walipatikana watoto 37 na kuingia katika kundi la kwanza na kukuza vipaji kwa mpango maalumu. Mkurugenzi wa kwanza wa masuala ya uufundi wa kituo hicho academy hiyo, Nasser Larguet, amesema walipoanza hawakuwa wanajenga timu. Walikuwa wanajenga mfumo.
"Tulianza na sifuri. Tulitakiwa kwanza kujenga mfumo kabla ya kutengeza wachezaji", Larguet.
Leo matokeo yanaonekana wazi. Wachezaji kama Youssef En-Nesyri, Nayef Aguerd, Azzedine Ounahi na wengine wengi wa timu ya taifa ya Morocco wametokana na mfumo huo.
Kilichoifanya Morocco kuwa nguvu ya soka Afrika si kizazi cha vipaji pekee. Ni uwezo wa kubadili vipaji kuwa mfumo, na mfumo kuwa matokeo. Mfuatiliaji wa soka la Afrika, Boniface Charles, anaamini Tanzania inaanza kufuata njia hiyo.
"Wanachokifanya Morocco ni kutafuta vipaji mapema, kuvilinda, kuviendeleza na kuhakikisha havipotei. Mafanikio yao si bahati."
Lakini Morocco haikuishia kwenye kituo hicho na vingine kama hivyo vilivyofuata ( Academies). Ilihakikisha vipaji vyake vinaingia kwenye mazingira yenye ushindani mkubwa duniani. Hapo ndipo Tanzania inapoonekana kutaka kwenda sasa.
Lakini safari hii sio rahisi kama inavyoonekana kwa wengine. Siasa za U-simba na Yanga, rushwa na wanasiasa kuingilia michakato, inaweza kuwa sehemu ya vikwazo.
Soko na soka la Ulaya

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Soka la kisasa limebadilika. Limetoka kwenye burudani, sasa ni kazi, ni taaluma, hivyo linafuata misingi yote ya taaluma. Nchi za Ulaya ni baba katika eneo hilo. Ni soko kubwa na wanasoka wengi. Mataifa mengi yanayofanya vizuri hayategemei tena ligi zao za ndani pekee.
Morocco ina zaidi ya asilimia 70 ya wachezaji wake waliopo kwenye michuano ya Kombe la dunia mwaka huu wanacheza nje ya nchi. Senegal inategemea zaidi wachezaji waliopo England, Ufaransa na Hispania. Ivory Coast imejenga nguvu yake kupitia wachezaji wanaocheza kwenye ligi kubwa za Ulaya.
Cape Verde, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Uruguay yenyewe karibu wote wote walioko kwneye kombe la dunia mwaka huu wanacheza nje ya mipaka yao.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo aliyeifundisha Tanzania kati ya 2006-2010, amewahi kusema changamoto kubwa ya Tanzania kimataifa ni kuwa na idadi ndogo ya wachezaji wanaocheza katika ligi za kiwango cha juu duniani. Lakini anaamini vipaji vipo.
Ndiyo maana Waziri Paul Makonda amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuwapeleka vijana wa Serengeti Boys kupata uzoefu wa kimataifa. "Tunahitaji waende wakacheze Ufaransa, Hispania, Uingereza na sehemu nyingine. Vipaji wanavyo. Kinachohitajika ni uzoefu wa ushindani wa kimataifa."
Vituo vya kukuza soka na kuchanganya wachezaji wanaocheza soka nje, kumeanza kuonekana kama mkondo unaopitika na mataifa mengi na Tanzania inakwenda huko. Kikosi cha Taifa Stars sasa kina angalau sura za wachezaji wanaocheza nje ya nchi kama Haji Mnoga, Cypria Kachwele, Simo Msuva, Said Khamis, Mohamed Sagaf, Charles William M'Mombwa, Tarryn Allarakhia, Alphonce Mabula na Nahodha Mbwana Samatta.
Japo wanacheza kwenye ligi ndogo na za kati, lakini tofauti inajionyesha na ushahidi ni AFCON ya 2025.
Miaka 40 ya kusubiri na kuamini

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika kipindi cha karibu miaka 40 baada ya kufuzu AFCON mwaka 1980, Tanzania ilionekana kuwa taifa linalopenda mpira wa miguu lakini lenye matokeo ya kusikitisha.
Lakini katika miaka michache iliyopita picha imeanza kubadilika. Taifa Stars imefuzu AFCON mara tatu ndani ya kipindi kifupi -2019, 2023 na 2025. Mwaka 2025 ilifika hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Serengeti Boys, timu ya vijana hii imefuzu AFCON za vijana mara kadhaa na sasa imefuzu Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 litakalofanyika Qatar mwaka 2026.
Tanzania pia imefuzu CHAN mara mbili na itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda. Kwa mara ya kwanza, mafanikio haya hayaonekani kama matukio ya bahati. Yanaonekana kuwa sehemu ya mwelekeo.
Kocha wa vijana Boniface Pawassa anaamini Tanzania ipo kwenye njia sahihi. "Tunaitengeneza Tanzania ya kesho. Naam, tuna safari, lakini naamini kati ya mwaka 2030 na 2040 Tanzania inaweza kufuzu Kombe la Dunia."
Rais wa TFF Wallace Karia naye anaamini mafanikio ya sasa yanatokana na uwekezaji wa muda mrefu. "Tuna vijana zaidi 100 kule Tanga (umri miaka 10-17) kule kutoka sehemu mbalimbali, tunawapeleka shule na tunawalipia ada".

Chanzo cha picha, caf/bsnsports
Hakuna anayesema safari imekwisha. Morocco ilihitaji karibu miaka 20. Senegal ilihitaji mabadiliko ya mfumo. Ghana na Nigeria ziliwekeza kwa muda mrefu kwenye vipaji vinavyocheza Ulaya.
Lakini tofauti na miaka iliyopita, Tanzania sasa inaonekana kuwa na ramani. Hakuna anayejua kama Tanzania itafuzu Kombe la Dunia mwaka 2030. Lakini kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania, swala hilo linaaanza kuonekana kama linaweza kujadiliwa. Cape Verde, Curacao, Jordan na Uzbekistan zinashiriki kwa mara ya kwanza mwaka huu, Tanzania itaweza mwaka 2030? Nafasi za timu kutoka Afrika kwenye kombe la dunia zimeongeza kutoka 5 mpaka 10, Tanzania inakosaje?
Godfrey Madegwa, mchambuzi wa michezo anasema" "Tanzania tunaweza kushiriki kombe la dunia 2030 kwakuwa timu za U17 na U20 wa kike wameshakuwa kwenye Kombe la Dunia. Hiyo inaonyesha vipaji vipo. Ikiwa TFF na serikali watawekeza kwenye vituo vye kuendeleza soka la vijana, watoe wachezaji wengi kwenda Ulaya, na kutumia AFCON 2027 kama maandalizi, basi 2030 tunaweza kuwepo.. kwa wenzetu Morocco na senegal wamefanikiwa katika hayo maeneo".
Kwa maneno ya Madegwa, kauli ya Waziri Makonda na ndoto inayoanza kuzungumzwa sasa, huenda miaka michache ijayo, wakati Kombe la Dunia litakaporejea tena, Watanzania hawatakuwa wanajiuliza kwa nini wanakesha kuwaangalia Wakorea, Wafaransa au Wabrazil.
Watakuwa wanakesha kuiangalia Tanzania na yule rafiki yangu nadhani atakesha tumbo wazi kushangilia kwa shangwe hata kama Taifa Stars haitapata matokeo.














