Kwa nini Kenya inapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa magenge ya wahuni?

    • Author, Laillah Mohammed
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 10

Alhamisi ya Julai 16, 2026 ni siku ya kawaida kwa wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki ila ina umuhimu mkubwa kwa eneo-bunge la Ol Kalau, lililo katika kaunti ya Nyandarua nchini Kenya.

Siku hii wapiga kura takribani 72,997 watashiriki katika uchaguzi mdogo kuchagua mwakilishi wao katika bunge la kitaifa nchini Kenya baada ya kufariki kwa aliyekuwa mbunge wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mnamo mwezi Machi mwaka huu baada ya kuugua.

Na huku wengi hasa nchini Kenya wakifuatilia uchaguzi huo mdogo unaofanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, matukio ya ghasia yaliyoshuhudiwa wakati wa kampeni zimetia doa shughuli nzima na kuliacha wingu jeusi kuhusiana na suala la uhuni unaofanyika wazi, mchana peupe na ambao wengi nchini kenya wanahisi umewashinda maafisa wa usalama kuudhibiti.

'Ishara za ghasia zilizoshuhudiwa Kenya mwaka wa 2007/08 zilianza kuonekana wazi mapema na wahusika wakuu wakashindwa kufanya lolote. Walisubriri hadi maafa yakatokea, watu kupoteza makazi na mali ndipo wakaanza kusisitiza umuhimu wa taifa kuwa na uwiano, umoja na wote kuishi na amani,' alisema mchambuzi wa siasa nchini Kenya Barrack Muluka katika mahojiano na BBC.

Ni kwanini uhuni wa kisiasa umekithiri Kenya?

Mwaka wa 2026 umeshuhudia visa vya kutisha vya uhuni ambavyo mpaka leo ni wachache ambao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kukabiliwa na mashtaka.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Kenya, kijana aliyejitambulisha kama 'mhuni wa kukodisha' alikiri kwamba 'njaa ndio sababu kubwa ya wao kukubali kupokea kati ya shilingi mia tano na elfu moja na mia tano za Kenya, sawia na shilingi 10,177 na 30,533.06/= za Tanzania kama malipo ya kutekeleza vurugu.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari mapema mwaka huu, Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Kipchumba Murkomen alisema kwamba serikali ina ufahamu wa ni kina nani wanaofadhili makundi ya vijana kutekeleza uhuni na kwamba wangechukuwa hatua kali dhidi yao kwa ajili ya kukabiliana na utovu wa aina hiyo wa nidhamu, wengi nchini kenya wanasubiri kuona hatua hiyo ikichukuliwa hasa kwa waathiriwa wa machafuko yanayotekelezwa na makundi hayo ya vijana ambao wanaonekana kupata ujasiri mkubwa jinsi siku zinavyokwenda.

Ghasia za uchaguzi mdogo wa Ol Kalaou

Tuiangazie katiba ya Kenya ambayo inaipa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini kenya IEBC uwezo wa kuandaa uchaguzi mdogo ikiwa imesalia mwaka mmoja kwa uchaguzi mkuu wa nchi kufanyika.

Na ikiwa na siku tisini kisheria kuandaa uchaguzi mdogo, IEBC ilitangaza kuwa kiti cha Ol Kalou kipo wazi na kuwapa fursa wenye hamu kujitosa uwanjani kuwania kiti hicho. Lakini katika mwezi mmoja uliopita Ol Kalou imegeuka kuwa uwanja wa makabiliano kati ya makundi ya wahuni,na polisi huku baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vina pigania kiti hicho vikishambuliwa na kuwaacha wengi wakikadiria hasara au hata kujeruhiwa.

Matukio ya ghasia Ol Kalau

1: Mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki ashambuliwa

Dereva wa Mbunge wa EALA kutoka Kenya Kanini Kenga amefunguliwa mashtaka ya kuendesha gari ambalo halina nambari za usajili na kwa sasa ameachiliwa huru kwa dhamana ya shilingi elfu 15 za Kenya sawia na shilingi 305,661.16 za Tanzania.

Dereva huyo anaripotiwa kunusurika kifo katika shambulizi lililotokea katiaka eneo-bunge la Ol Joro Oroko ambalo lipo pia katika kaunti ya Ndaraua ambapo alikuwa safarini kurejea nyumbani baada ya kumaliza kufanya kampeni katika eneo-bunge jirani la Ol Kalou.

Kanini alidai kufuatwa na magari mawili ambayo alidai yalikuwa ya polisi wakati ambapo gari lake lilifyatuliwa risasi kadhaa ambazo amedai zilivunja kioo cha nyuma cha gari hilo. Kanini na dereva wake walitoroka na kujificha katika nyumba moja mjini Kasuku ambapo alirekodi video akisema kwamba amenusurika jaribio dhidi ya maisha yake.

'Mungu amenijaalia kukwepa mtego ulioweka kunimaliza. Hawa watoto wamenificha na kuniokoa, na nimeshuruku. Ila tunawajuwa waliojaribu hili na Mungu hatakubali matendo yao kukithiri,' Kanini alisema kwenye video hiyo iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.

2: Kanisa lazingirwa na wahuni Kisumu

Jumapili hiyo ya Julai 12, kundi la vijana waliojihami kwa mipini na mishale, walivamia kanisa la Kianglikana jijini Kisumu ambapo waliwajeruhi watu kadhaa.

Polisi waliingilia kati na kudhibiti hali hasa wakati ambapo kundi la pili lilizingira kanisa hilo ambapo wanasiasa wa mrengo wa LINDA MWANANCHI wanaoongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna walikuwa wakihudhuria ibada ya Jumapili.

Makabiliano makali kati ya makundi hayo mawili yalisababisha watu kadhaa kujeruhiwa huku waliokuwa ndani ya kanisa wakijawa na hofu hasa kina mama waliokuwa wanahudhuria ibada hiyo ya Jumapili wakiwa na watoto wadogo.

Seneta Sifuna alisema kwamba tukio hilo lilikuwa la kisasa na kwamba kundi hilo halingetishiwa kwa vyovyote na uhuni wa kisiasa.

Usiku huo, msemaji wa polisi nchini Kenya Muchiri Nyagah alitoa taarifa kuhusianiana na matukio hayo amwili akitaka kuihakikishia taifa kwamba huduma ya polisi haitakubali visa vya ina hiyo vya jinai kuendelezwa nchini.

'Huduma ya polisi inaisitiza kwamba, hakuna mtu yeyote, bila kuzingatia hadhi yake katika jamii, chama cha kisiasa anachokiunga mkono wala ikiwa anashikilia kiti cha uongozi wa umma, yupo juu ya sheria za nchi.

Mtu yeyote atakaye patikana na hatia ya kujihusisha, kufadhili, au kuwa mwanachama wa kundi la kihuni, kuchochea ghasia au chuki na kutatiza vikao vya hadhara ambavyo ni halali,' alisema bwana Muchiri.

Watu 14 wamefikishwa mahakani Kisumu Jumatatu Julai 13 na kusomewa mashtaka ya kushiriki kwenye ghasia na kutokuwa na vurugu zinazochochewa kisiasa.

3: Gavana wa Muranga ashambuliwa

Wiki moja kabla ya Mbunge Kanini Kega kushambuliwa, mkutano wa kisiasa uliokuwa ukifanyika huko Ol Kalou ulitibuliwa na kundi la wahuni ambalo lilisababisha kufyatuliwa risasi kwa dereva wa Gavana wa kaunti ya Murang'a Irungu Kangata ambaye alikuwa anafanya kampeni kuuza sera za muungano wa kisiasa wa Linda Nchi katika eneo hilo.

Siku moja kabla ya tukio hilo, aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gashagua alikuwa amemuonya Kangata kutoingia siasa za ndani za Ol Kalou akisema kwamba hakupendelea jinsi ambavyo vyama vingine vya 'mbali ' vilikuwa vinapendekeza mgombea wa kiti hicho ambacho kwa sasa kimeonekana kuwa na mafahali wawili wakuu ambao wanawania kiti hicho kupitia tiketi za vyama vya UDA {Chama tawala anachokiongoza Rais Williama Ruto} na DCP {Anachokiongoza Rigathi Gachagua}

Mchambuzi Barack Muluka ametambua kwamba siasa za ubabe wa kisiasa katika eneo lilozingira mlima Kenya zimesheheni kampeni za uchaguzi wa Alhamisi hii, huku Gachagua aliyekuwa mwandani mkuu wa Ruto 2022 na kumsaidia kupata uungwaji mkono katika eneo la mlima Kenya, akijaribu mara kadhaa kuonesha ushawishi wake katika eneo hilo katika Uchaguzi mdogo mwingine bila mafanikio.

4: Ghasia katika uchaguzi mdogo wa Mbeere North

Siasa za matumizi ya wahuni zilianza kupamba moto katika uchaguzi huu uliofanyika mwezi Novemba 2025. Aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Geoffrey Ruku aliteuliwa katika baraza la mawaziri baada ya Justin Muturi kutimuliwa mamlakani kwa kuikosoa vikali serikali ambayo alikuwa akiifanyia kazi.

Vigogo wa kisiasa akiwemo Naibu Rais, Prof Kithure Kindiki walitumwa katika eneo hilo na kupiga kampeni ambayo ilionekana kama ya kufa kupona, kwa Ruto na Gachagua. Ni hapa ambapo visa vya wahuni kushambulia mikutano ya hadhara ya kisiasa ilianza kushuhudiwa.

5: Gachagua ashambuliwa kanisani

Mwezi Januari mwaka huu wa 2026, siku ya Jumapili, ilikuwa siku ngumu kwa waumini wa kanisa la Witima Anglican Church of Kenya ambapo makundi ya wahuni ambao walidaiwa kuwa maafisa wa polisi walishambulia kanisa hilo na kurusha mabomu ya kutoa machozi ndani ya kanisa hilo.

Kina mama, watoto na wakongwe ambao hawajiwezi waliathirika pakubwa na hali hiyo huku milio ya risasi ikirindima hewani kwa saa kadhaa. Hadi leo, hakuna anayekabiliwa na shtaka la utovu wa nidhamu, uvunjani wa amani wala kuhatarisha maisha ya raia ambao hawajajihami kwa silaha.

Akihojiwa katika kituo kimoja ya televisheni, mtaalamu wa usalama Hassan Khanenje amesema kwamba; ' Makundi ya kihuni yanazaliwa, kulelewa na kustawishwa n wanasiasa. Na ikiwa wenye kuyamiliki watashindwa kuyadhibiti basi huwashinda na kuwa kidonda ndugu mwilini mwa wamiliki wao na kitaifa. Kwa mfano makundi kama Janjaweed ambayo hadi leo yanatekeleza ukatili mkubwa nchini Sudan, na mengine mengi ambayo yameshuhudiwa kote duniani.' Alisema Khannenje.

6: Kikao cha kisiasa chavurugwa All Saints Cathedral

Mnamo Juni 2026, kundi la wahuni lilivamia kanisa la All-Saints Cathedral jijini Nairobi na kuvuruga mkutano wa umma uliokuwa ukijadili bajeti. Washukiwa kadhaa walikamatwa na maafisa wa upelelezi wa DCI, huku mmoja wa washukiwa akifichua kuwa walilipwa KSh 2,000 kila mmoja kutekeleza uhuni huo.

Tukio hilo ambalo lilinakiliwa na kamera za CCTV liliwashtuwa wengi ambao waliwachwa vichwa wazi kuwatazama polisi wakishindwa kuwadhibiti vijana hao ambao walifika pale na silaha wakiwa na pikipiki na baada ya kutekeleza vurugu kwenye kikao hicho walitoka nje na kupora mali kwa raia waliokuw awakitembea nje kwenye Barabara ya Kenyatta Avenue.

Tamko la Kanisa

Mkuu wa kanisa Anglikana nchini Kenya, Askofu Jackson Ole Sapit akikashifu tukio hilo na kuitaka serikali kudhibiti hali kabla ya usalama nchini kuwa mbaya. Katika vikao kadhaa na wanahabari, muungano wa maaskofu katika kanisa katoliki pia wamelaani vikali matukio hayo na kusisitiza kwamba wizara ya usalama wa ndani inapaswa kuingilia kati mara moja.

7.Uchumi wa Uhuni wa kisiasa Kenya

Katika utafiti wake Mkuu wa masuala ya wanafunzi katika chuo kikuu cha Daystar Mutinda Musyimi ameelezea kwa undani mfumo wa uhuni wa kisiasa nchini humo akiufananisha na taasisi inayoongozwa na mfumo wa mstatii ambao uko na viwango kadhaa – kule juu kukiwa na viongozi wa vijana ambao husakwa na wanasiasa na kupokea hela za kuwakodisha vijana wengine kutekeleza ghasia katika maeneo kadhaa.

Makundi hayo yanayotekeleza majukumu kadhaa kama vile kuwalinda wanasiasa hutoza viongozi hao kati ya shilingi laki tano za kenya na Milioni moja sawia na 10,189,493.42 - 20,379,218.87 za Tanzania.

Siasa za 'uchochole na kukata tamaa zimesheheni nchini Kenya kulingana na utafiti huu ambao sasa unasema kwamba viongozi wenye kutojali wanatumia mbinu hii kimabavu kama mbinu ya kuendeleza ajenda zao kisiasa.

Hali ya wengi wa vijana kutokuwa na ajira pia imeonekana pakubwa kama kigezo ambacho wanasiasa wanatumia kuwatumia vibaya kwa ajili ya kuwapa 'kitu kidogo.'

Musyimi anasema 'kimya cha polisi' kinatoa sauti kubwa ya aibu kwa kuwa polisi hawaonekani kutekeleza majukumu yao kama inavyohitajika.

Historia ya makundi ya kihuni ya kisiasa nchini Kenya

Kwa mujibu wa mchambuzi Barack Muluka, hii sio mara ya kwanza kwa Kenya kushuhudia makundi ya kihuni ambayo yanatokana na siasa nchini, Nyakati za uongozi wa awamu ya pili wa Daniel Toroitich Arap Moi, kulikuwa na kundi lililofahamika kama JESHI LA MZEE.

Kundi hili lilichipuka mwishoni mwa muongo wa miaka ya themanini na kusheheni sana siasa za uchaguzi wa 1992 ambapo kulikuwa na msukumo mkubwa w akuifungulia nchi kuwa na mfumo wa vya vingi.

Wakati huo, katiba ya Kenya ilikuwa inatambua chama kimoja pekee , 'Cha Baba na Mama, Chama cha KANU' ambacho wengi wakati huo walihisi kwamba kilikuwa kinazima sauti za wale ambão walikuw ana msimamo unaokinzana na ser aza uongozi wa Moi.

Muluka anasema,' wakati huo, Jeshi la Mzee likilukwa na kitovu chake jijini Nairobi na lilitumwa kusambaratisha mikutano ya kisasa kama vile mikutano iliyoandaliwa katiak uwanja wa Kamukunji.

Mtaalamu wa usalama Hassana Khannenje naye amelitaja kundi la MUNGIKI ambalo lilitajwa kama 'watoto wa MAUMAU' waliotokea kabila moja nchini Kenya na kudaiwa kuendeleza ghasia nchini. Kundi hili lilihusishwa na kiongozi mmoja mkuu wa kisiasa nchini Kenya ambaye aliwahi kufunguliwa kesi katika mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC.

Katika kesi dhidi yake, kiongozi wa mashtaka wakati huo Louis Ocampo alimtaja mwanasiasa huyo kuwa mfadhili wa kundi hilo ambalo lilidaiwa kutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasai dhidi ya wafuasi wa Raila Odinga katika maeneo ya Naivasha, Nakuru, Eldoret na hata katika baadhi ya vitongoji duni vya jiji la Nairobi.

Khannenje anasema, 'Japo aliyekuwa Waziri wa Usalama wa ndani John Michuki alijaribu kukabiliana na kundi hilo, bado kunao wafuasi wake waliosalia nchini na wao hutumika kutoza 'ushuru' kwa wafanyabiashara, na wahudumu wa matatu' katika baadhi ya maeneo wakidai kulipwa ada ya 'ulinzi wa maeneo hayo.'

Viongozi wawili wa kundi hilo Ndura Waruinge na Maina Njenga wamejihusisha na sias aza kitaifa mara kadhaa. Maina amewahi kuwania Usenata wa kaunti ya Laikipia 2017 na 2022 akijihusisha pakubwa na vyama vha KANU na Jubilee ambayo inaongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Je, Kenya inapaswa kuwa na hofu kuhusu usalama wake 2027?

Japo mwandishi huyu sio mtabiri wa jinsi mambo yatakavyokwenda mwakani, suali hili pia lisikosolewe kuashiria kwamba Kenya itajipata katika ghasia wakati wa uchaguzi wa 2027.

Lakini, ikiwa hali itaendelea kuwa ilivyo basi wataalamuw anahisi kwamba matukio ya 2027 {miongo miwili iliyopit} huenda yakajitokeza tena ikiwa tasisi za ujajusi , usalama na hata Ulinzi wa taifa hazitachukuwa hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili.

Waziri Murkomen amenukuliwa mara kadhaa akionya 'wachochezi' mara kadhaa kuhusiana na kufadhili makundi hayo akisema kwamba watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Hata hivyo wakfu wa Kofi Anan {Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mpatanishi mkuu wa ghasia za Kenya 2007 } imeripoti kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba historia inaweza kujirudia mwakani.

Kulingana na ripoti hiyo, viwango vya ghasia kutokea kwa sasa vipo asilimia 84 kutokana na visa vya uhuni kuzidi kutokea.

'Tangu 2023 Kenya imeshuhudia maandamano ya kupinga miswada ya fedha, kupanda kw agharama ya maisha, na hivi maajuzi wengi walipinga kupanda kwa bei ya mafuta, hali ambayo ilisababisha ghasia kushuhudiwa, watu kuuawa, wengi kupotea na mamia kujeruhiwa,' ilisema ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa mchambuzi Barack Muluka, hali ya kiusalama nchini Kenya ilizna kuwa mbaya zaidi baaada ya maandamano ya 2024 ambapo watu walianza kutekwa na kupotea au kupatikana baada ya muda wakiwa wameteswa na hali mbaya kiafya.

'Alipolizungumzia suala hilo katika kikao cha wanahabari, Rais William Ruto alisema kwamba 'hakuna mtu mwengine yeyote atakayepotea mikononi mwa kikosi cha polisi ambacho awali kilitumiwa kuwadhulumu wakenya kwa misingi ya kisiasa,' Ila akaendelea kuwaonya wazazi kwamba ni jukumu lao kuwapa malezi bora watoto wao la sivyo! Serikali haitakosolewa

ikichukuwa hatua za kuwaadhibu wanaovuja sheria na kutishia usalamw a kitaifa,' alisema Muluka.

Wakati huo, Rais Ruto aliyekuwa mwenye kujawa na hasira alitaja hatua ya kuvamiwa kwa bungee la Kenya na vijana , kama jaribio dhidi ya serikali yake na kuitaka idara ya sheria na usalama wa ndani kuwafungulia mashtaka ta uhaini wahusika.