Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanasayansi wamevumbua njia ya kufuta kumbukumbu mbaya: Je, tunapaswa kuitumia?
Maendeleo katika sayansi ya neva (mishipa ya fahamu) na bioteknolojia yameleta elimu kuhusu kumbukumbu kutoka hadithi za kisayansi kuwa hadithi za kweli.
Watafiti sasa wanaweza kudhoofisha, kuandika upya, au kufuta kumbukumbu kwa wanyama, huku wakichunguza uwezekano wa kutumia mbinu kama hiyo kwa wanadamu.
Hata hivyo, wataalamu hao wanasema kwamba kupunguza kumbukumbu mbaya ni jambo bora zaidi na lenye manufaa kuliko kuzifuta moja kwa moja.
Utafiti kwa wanyama
Kumbukumbu huhifadhiwa kwenye ubongo. Kila wakati kumbukumbu inapokumbukwa, huingia katika eneo la ubongo na kukaa kwa saa chache, na hapo kumbukumbu inaweza kubadilishwa, kuimarika, au kuvurugwa.
Watafiti kutoka nchini Canada, wakiongozwa na Dr Sheena Josselyn katika chuo kikuu cha Toronto, walitambua neva maalumu kwenye ubongo wa panya ambazo huhifadhi kumbukumbu za hofu, na kuzishambulia neva hizo kwa kutumia sumu.
Panya waliofanyiwa utafiti huo walipoteza mwitikio wa hofu, na hilo linathibitisha kwamba kumbukumbu inaweza kufutwa.
Mwaka 2013, mwanasayansi wa neva Dkt. Steve Ramirez na mwenzake marehemu Dkt. Xu Liu walitumia nyaya nyembamba na kuziingiza katika ubongo wa panya ili kuamsha seli fulani za kumbukumbu, na hilo lilisababisha hofu isiyokuwepo.
Timu ya Ramirez pia ilionyesha kwamba kuamsha kumbukumbu chanya huku panya akikumbuka ile hasi, kulisaidia kuondosha mwitikio wa hofu kwa miezi kadhaa.
Tiba kwa wanadamu
Kulenga au kubadilisha moja kwa moja seli za ubongo wa binadamu kunaweza kusababisha hatari kubwa kwa afya na maadili ya kimatibabu. Kwa hivyo, utafiti kwa binadamu unazingatia mbinu za kitabia na kisaikolojia za kuvuruga kumbukumbu mbaya.
Tiba ya kitabia hubadilisha kumbukumbu mbaya au hutumia mbinu za mguso wa kihisia, kama vile kupeleka macho kulia na kushoto au kuguswa ili kuvuruga jinsi hofu inavyojiunda katika ubongo.
Mwanasaikolojia na Profesa Emily Holmes aligundua kuwa kumbukumbua mbaya ya matukio ya nyuma hubaki kwa muda mrefu katika ubongo.
Kukumbuka kumbukumbu mbaya, na kucheza gemu katika simu papo hapo kwa dakika 20, huzuia kumbukumbua mbaya za nyuma kubaki kwa muda mrefu,
Katika jaribio hilo la kiutafiti lililofanywa kwa wauguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi, ICU wakati wa COVID-19, mbinu hii ilipunguza matukio ya kumbukumbu mbaya kujirudia kutoka 14 hadi 1 kwa wiki.
Matumizi ya dawa kama vile propranolol, metyrapone, au propofol ili kuondoa kumbukumbu mbaya. Watafiti wamechunguza uwezo wa dawa hizo, katika kudhoofisha kumbukumbu mbaya au kuzuia uundaji mpya wa kumbukumbu mbaya, ingawa matokeo yanabaki kuwa mchanganyiko.
Masuala ya kimaadili
Ingawa karibu 80% ya watu waliohojiwa wanasema hawataki kumbukumbu zao zifutwe, lakini 20% wanaoumizwa na kumbukumbu mbaya wamesema wanaweza kuwa tayari kumbukumbu hizo kufutwa.
Hata hivyo, Ramirez na Holmes wanapinga vikali ufutaji wa kumbukumbu hizo, kwa sababu kadhaa.
Wataalamu hao wanasema kumbukumbu nzuri na mbaya huunda utambulisho binafsi, hufundisha ustahimilivu, na hutuzuia kurudia makosa ya zamani.
Vilevile, kufuta kumbukumbu huondoa ushahidi muhimu unaohitajika kwa ajili ya ushuhuda katika mahakama, na ukweli wa yaliyotokea katika historia.
Watalaamu pia wanasema matukio yenye uchungu mara nyingi huchochea matendo yenye maana, kama vile utunzi wa kazi za fasihi, kuongeza huruma, na mabadiliko ya kijamii.
Badala ya kufuta kabisa kumbukumbu, wanasayansi wa neva wanatetea mbinu ya kupunguza hofu au huzuni inayohusishwa na kumbukumbu mbaya huku watu wakiendeelea kutunza kumbukumbu zao.
Kama Dkt. Ramirez anavyosema kutokana na uzoefu wake mwenyewe kushinda huzuni na uraibu, anasema kushikilia kumbukumbu zenye uchungu huruhusu nyakati ngumu za maisha kupata maana na suluhisho bora zaid.