Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani ikubali masharti sita - Iran

Kauli hiyo inakuja wakati Iran na Oman zikisema mazungumzo kuhusu utaratibu mpya wa kuruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz yamekuwa ya “chanya na yenye kujenga” katika siku za hivi karibuni.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. JD Vance: Marekani imeharibu mpango wa nyuklia wa Iran

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema Marekani imeharibu mpango wa nyuklia wa Iran, kuangamiza uwezo wake wa kijeshi wa kawaida na kudhoofisha kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kijeshi wa kutumia makundi washirika.

    Vance amesema hayo katika mahojiano na Fox News Jumamosi, akieleza kuwa Washington kwa sasa inatathmini ikiwa Iran iko tayari kufanya mabadiliko ya muda mrefu ambayo yanaweza kuboresha uhusiano kati ya Iran na Marekani.

    Amesema iwapo Iran haitakuwa tayari kufanya mabadiliko hayo, Marekani itaendelea kuongeza shinikizo dhidi ya Tehran.

    Vance pia amesema serikali ya Marekani inalenga kuongeza uzalishaji wa mafuta na gesi katika Mashariki ya Kati ili kupunguza gharama za mafuta na nishati kwa Wamarekani, huku ikiimarisha upatikanaji wa nishati.

    Soma zaidi:

  2. Oman: Mazungumzo kuhusu Hormuz yapiga hatua

    Oman imesema mazungumzo yake na Iran kuhusu makubaliano ya kuhakikisha usalama wa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz yanaendelea vyema, huku Tehran ikionya kuwa makubaliano hayo hayamaanishi kwamba njia hiyo muhimu ya majini itafunguliwa mara moja.

    Pande zote mbili zimesema Jumamosi kwamba mazungumzo hayo yanaendelea kwa matumaini, ingawa bado haijafahamika ni lini makubaliano yanaweza kufikiwa.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman imeonya kuhusu mashambulizi dhidi ya meli, ambayo yanaweza kuvuruga juhudi hizo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mazungumzo yako katika hatua za mwisho, lakini akasema kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz bado kunategemea masharti mengine.

    Tehran imezuia kwa kiasi kikubwa matumizi ya njia hiyo ya majini, ambayo kwa kawaida hupitisha takriban theluthi moja ya biashara ya mafuta na gesi duniani, tangu Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi mwezi Februari.

    Soma Zaidi:

  3. FIFA yakosoa kampeni ya kutaka Infantino ajiuzulu

    FIFA imekosoa vikali kile ilichokiita juhudi zinazoendelea za kuidhoofisha taasisi hiyo pamoja na rais wake, Gianni Infantino. Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti zilizomuhusisha Infantino na madai kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi, ambayo FIFA imesema ni madai yasiyo na msingi na ya uongo.

    Infantino pia anakabiliwa na shinikizo kutoka UEFA na baadhi ya vyama vya soka barani Ulaya kufuatia mpango wake uliositishwa wa FIFA Forward Enterprise, uliolenga kuanzisha kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za FIFA, huku sehemu ya kampuni hiyo ikiuzwa kwa mwekezaji binafsi.

    Rais wa Shirikisho la Soka la Norway, Lise Klaveness, ametaka Infantino ajiuzulu, huku UEFA ikisema bado iko tayari kususia baadhi ya matukio ya FIFA ikiwa haitapewa uhakikisho kwamba mpango huo hautafufuliwa.

    FIFA imemtetea Infantino ikisema alichaguliwa kidemokrasia na vyama wanachama na anaendelea kuhudumu kwa mamlaka waliompa. Shirikisho hilo limeonya kwamba wanaopinga uongozi wake wanapaswa kutumia taratibu rasmi za kidemokrasia za FIFA badala ya madai au taarifa potofu.

    Upinzani dhidi ya Infantino unatoka zaidi Ulaya, huku Mexico, Conmebol na CAF zikimuunga mkono. CAF, inayowakilisha nchi 54 za Afrika, imesema inaunga mkono Infantino kwa kauli moja.

  4. Masharti ya Iran yapunguza matumaini ya kufikiwa haraka kwa makubaliano

    Masharti yaliyotolewa na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Baqer Zolghadr, kwa kiasi kikubwa yanarudia masharti yaliyokuwa sehemu ya makubaliano ya mfumo yaliyofikiwa kati ya Iran na Marekani mwezi Juni. Lakini sasa, Zolghadr ameyawasilisha masharti hayo kama sharti la lazima ili Mlango wa Hormuz urejee kufanya kazi kikamilifu kama kawaida.

    Masharti hayo yanajumuisha kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran, kulipwa fidia kwa uharibifu uliosababishwa na vita, pamoja na kusitishwa mara moja kwa kizuizi cha Marekani dhidi ya bandari za Iran.

    Iwapo kauli hizo zitatumika kama ishara ya msimamo wa sasa wa Tehran, huenda zikapunguza zaidi matumaini ambayo Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ameyaibua kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano na Iran hivi karibuni.

    Wakati huo huo, Iran na Oman zinaendelea na mazungumzo kuhusu njia mpya ya kuruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz. Mpango huo unatarajiwa kusimamiwa kwa pamoja na Iran na Oman, huku nchi hizo zikitoza ada kwa matumizi ya njia hiyo.

    Makubaliano kama hayo, iwapo yatafikiwa, yangefungua sehemu tu ya njia kuelekea suluhisho pana la mzozo huo. Hata hivyo, yanaweza kumpa Donald Trump njia ya kujiondoa katika vita bila kuhitaji kufikia mara moja makubaliano kamili ya kumaliza mzozo.

    tofauti hizo ni za aina gani.

  5. Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani ikubali masharti sita - Iran

    Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Bagher Zolghadr, amesema Iran haitafungua tena Mlango wa Hormuz hadi Marekani itakapokubali masharti sita yaliyowekwa na Tehran.

    Masharti hayo yanajumuisha kupunguza vikwazo dhidi ya Iran, kulipa fidia za uharibifu wa vita, kusitisha mara moja kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran, kuacha vitisho dhidi ya Iran na kuachilia mali za Iran zilizogandishwa. Kauli yake inaashiria msimamo mkali zaidi wa Tehran katika mazungumzo kuhusu ufunguzi wa njia hiyo muhimu ya mafuta.

    Kauli hiyo inakuja wakati Iran na Oman zikisema mazungumzo kuhusu utaratibu mpya wa kuruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz yamekuwa ya “chanya na yenye kujenga” katika siku za hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema mazungumzo hayo yako katika hatua za mwisho, lakini amesisitiza kuwa makubaliano hayatamaanisha mlango huo utafunguliwa mara moja, kwa kuwa ufunguzi wake utategemea masharti mengine.

    Ripoti ya Axios siku moja kabla ilisema, ikinukuu mwanadiplomasia kutoka moja ya nchi zinazosaidia upatanishi, kwamba wajumbe wa Iran walikuwa wakisubiri idhini ya mwisho kutoka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ili kukamilisha makubaliano na Oman pamoja na Marekani. Mwanadiplomasia huyo alisema idhini hiyo ilitarajiwa kutolewa “hivi karibuni”.

    Reuters pia iliripoti, ikimnukuu afisa wa Marekani, kwamba kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo kati ya Iran na Oman na Washington inatarajia makubaliano kufikiwa hivi karibuni.

    Kwa mujibu wa afisa huyo wa Marekani, Washington itaondoa kizuizi dhidi ya bandari za Iran baada ya kutangazwa kwa makubaliano yatakayohakikisha meli za kibiashara zinapita bila kizuizi katika Mlango wa Hormuz. Kauli ya Zolghadr ni muhimu kwa sababu ametoka katika taasisi hiyo hiyo inayotarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kwa upande wa Iran kuhusu makubaliano hayo.

    Wakati huo huo, kuna taarifa kwamba Zolghadr amewasilisha barua ya kujiuzulu kutoka nafasi yake, lakini Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amepinga hatua hiyo na kumuomba aendelee na kazi. Pezeshkian alipoulizwa kuhusu taarifa hizo amesema kuna “tofauti kadhaa” ambazo wanaendelea kujaribu kuzitatua, bila kueleza zaidi tofauti hizo ni za aina gani.

  6. Salaam na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo 09.08.2026