Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanasayansi 5 waliookoa maisha ya mamilioni ya watu kupitia uvumbuzi wao
Sayansi imeboresha kwa kiasi kikubwa umri wa kuishi na ubora wa maisha duniani kote, kupitia kutibu magonjwa, kuwezesha taratibu mpya za kitabibu na kuboresha lishe.
Hawa ni wanasayansi watano katika historia ambao wameokoa maisha ya watu wengi.
1. Maurice Hilleman
Mtaalamu wa virusi kutoka Marekani, Maurice Hilleman, alitengeneza chanjo 40 katika kipindi cha kazi yake, zikiwemo chanjo dhidi ya mabusha (mumps), tetekuwanga, uti wa mgongo (meningitis) na surua. Chanjo zake zinakadiriwa kuwa zimechangia kuokoa zaidi ya maisha milioni 130.
Pia aligundua kuwa virusi vya mafua hubadilika, na hivyo kubadilisha protini ambazo mwili hutumia kuvitambua na kuanzisha kinga. Ugunduzi huo ulisaidia kuwezesha utengenezaji wa chanjo za mafua zinazotolewa kila mwaka.
Mwaka wa 1957, Hilleman alitabiri uwezekano wa kutokea kwa janga la mafua na akatengeneza haraka chanjo mpya, hatua iliyosaidia kupunguza ukali wa mlipuko huo.
2. Alexander Fleming
Huenda ugunduzi mkubwa zaidi katika historia ulitokea mwaka 1928, wakati mwanabiolojia wa Scotland, Sir Alexander Fleming, aliporejea kutoka likizo na kugundua kwamba moja ya sahani zake za maabara zilizokuwa na bakteria ilikuwa imechafuliwa na ukungu.
Alipotambua kuwa kulikuwa na eneo lililozunguka ukungu ambalo halikuwa na bakteria, aligundua kwamba huenda ukungu huo ulikuwa ukitoa dutu iliyozuia ukuaji wa bakteria.
Aligundua kuwa dutu hiyo, aliyoiita penicillin, ingeweza kuua aina mbalimbali za bakteria hatari. Hata hivyo, alikumbana na changamoto katika kuitenganisha na kuiboresha ili iweze kutumika kitabibu. Zaidi ya muongo mmoja baadaye, mtaalamu wa dawa kutoka Australia, Profesa Howard Florey, pamoja na wenzake, hatimaye walifanikiwa kuitengeneza penicillin. Tangu wakati huo, antibiotiki hiyo imechangia kuokoa zaidi ya maisha milioni 200.
3. Sir Frederick Banting
Kisukari ni kundi la magonjwa yanayoathiri uwezo wa mwili kudhibiti matumizi ya sukari kutoka kwenye damu. Zamani, kulikuwa na njia chache za kukitibu, kisukari cha aina ya kwanza mara nyingi kilisababisha kifo utotoni.
Kisha, mwaka wa 1921, mtaalamu wa dawa kutoka Canada, Sir Frederick Banting, aligundua insulini , homoni inayosaidia kudhibiti kiwango cha sukari mwilini na akaonyesha kuwa inaweza kutumika kutibu kisukari kwa wanyama.
Mwenzake, James Collip, alibuni njia ya kuiboresha insulini ili iweze kutumiwa na binadamu. Kwa pamoja, uvumbuzi wao unakadiriwa kuwa umechangia kuokoa zaidi ya maisha milioni 200.
Timu hiyo iliuza hati miliki ya insulini kwa dola moja, ili kuhakikisha kwamba kila aliyekuwa akiihitaji angeweza kupata tiba hiyo iliyookoa maisha.
4. Profesa Norman Ernest Borlaug
Kati ya miaka ya 1950 na 1960, mtaalamu wa kilimo kutoka Marekani, Profesa Norman Ernest Borlaug, alibuni aina za ngano zenye mavuno mengi na zinazostahimili magonjwa, ambazo alizisambaza kwa wakulima nchini Mexico, Pakistan na India.
Wakati huo, wakulima wengi walilima aina za mazao zilizozalishwa kutoka kwa mbegu za aina moja, ambazo zilitoa mavuno mengi lakini zilikuwa na jeni chache za kustahimili magonjwa. Hali hiyo ilizifanya kuwa katika hatari kubwa ya kushambuliwa na milipuko ya magonjwa.
Borlaug alianzisha mbinu ya kuzalisha aina mbalimbali za mazao zinazohusiana. Mbinu hiyo ilizalisha aina za mazao zilizopewa jina "multiline varieties", ambazo ziliunganisha jeni za kustahimili magonjwa kutoka kwa mimea asili.
Kazi yake iliongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao na inakadiriwa kuwa iliokoa maisha ya watu milioni 245 kupitia kuboresha lishe.
5. Profesa Karl Landsteiner
Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, majeraha na magonjwa yaliyosababisha mtu kupoteza kiasi kikubwa cha damu mara nyingi yalikuwa yanasababisha kifo.
Madaktari walikuwa wamejaribu kufanya uongezaji wa damu, lakini wagonjwa wengi walipata madhara makubwa na wakati mwingine kufa kutokana na damu waliyopewa kutoka kwa wafadhili.
Mwaka wa1901, mwanabiolojia mwenye asili ya Austria na baadaye raia wa Marekani, Profesa Karl Landsteiner, aligundua sababu iliyokuwa nyuma ya hali hiyo.
Aligundua kwamba watu mbalimbali wana damu yenye sifa tofauti, ambazo sasa zinajulikana kama makundi ya damu au blood groups, na tofauti hizo zilifanya damu ya mtu mmoja isiendane na ya mwingine.
Ugunduzi wake uliweka msingi wa kufanikisha uongezaji wa damu kwa usalama zaidi.
Hata hivyo, ilikuwa hadi mwaka 1914, wakati daktari kutoka Ubelgiji, Albert Hustin, alipogundua mbinu ya kuzuia damu kuganda wakati wa kuhifadhiwa na kusafirishwa, ndipo utaratibu huu muhimu wa kitabibu ulipoweza kutumika kwa ufanisi.