Cristiano Ronaldo amuoa Georgina Rodríguez baada ya miaka 10
Nyota wa soka Cristiano Ronaldo amemuoa mpenzi wake wa muda mrefu, mwanamitindo na mshawishi Georgina Rodríguez, katika hafla ya kiraia nchini Ureno.
Ronaldo alichapisha picha kwenye akaunti yake ya Instagram ikionyesha mikono miwili, unaodhaniwa kuwa wake ukiwa juu ya wa mke wake, huku wote wakiwa wamevalia pete za ndoa.
Vyombo vya habari nchini Ureno vimeripoti kuwa wawili hao walifunga ndoa tarehe 11 Agosti katika mji wa pwani wa Cascais, karibu na Lisbon, huku watoto wao watano wakihudhuria.
Picha hiyo ilipata uungwaji mkono wa mitandaoni milioni tatu ndani ya dakika 30 baada ya kuchapishwa.
Ronaldo na Rodríguez wamekuwa pamoja kwa miaka 10, baada ya kukutana katika duka la Gucci mjini Madrid, ambako Rodríguez alikuwa akifanya kazi. Wakati huo Ronaldo alikuwa akiichezea Real Madrid.
Wawili hao walitangaza uchumba wao tarehe 11 Agosti mwaka jana.
Ronaldo amefunga karibu mabao 1,000 katika maisha yake ya soka, akichezea Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid, Juventus, Al Nassr ya Saudi Arabia na timu ya taifa ya Ureno.
Hivi karibuni alishiriki katika Kombe lake la Dunia la sita, rekodi ya ushiriki katika fainali za Kombe la Dunia kwa upande wa wanaume, ambayo anaishikilia pamoja na Lionel Messi wa Argentina.