Mabilionea duniani wanavyopambana kuishi milele

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Matajiri wakubwa wanaendelea kutumia mamilioni ya dola kutafuta njia ya kuishi milele kwa nini basi mafanikio halisi ya kisayansi hayapati ufadhili?

Unataka kuishi milele? Huu hapa mpango wa hatua mbili: kwanza, tengeneza mabilioni ya dola huko Silicon Valley; pili, tumia mabilioni hayo kugharamikia matibabu ya kuongeza maisha marefu, kisha usubiri hadi siku ya kutokufa ifike.

Huu unaonekana kuwa mtazamo unaotumiwa na baadhi ya mabilionea wa teknolojia.

Kwa mfano, Sam Altman, mkurugenzi mtendaji wa OpenAI, kampuni inayomiliki ChatGPT, hutazama mwanga mkali wa LED kila asubuhi anapofanya kazi zake.

Kisha yeye hukaa masaa 15 kila siku bila chakula na hutumia dawa ya kisukari aina ya metformin dawa ambayo inadaiwa inaweza kusaidia kupunguza kasi ya kuzeeka.

Niliiuliza ChatGPT, "Je, ninapaswa kutumia metformin ili kuishi maisha marefu?" Jibu lake lilikuwa: "Kwa kifupi: si wazo zuri."

Kisha kuna Peter Thiel, bilionea na mwanzilishi mwenza wa PayPal, ambaye aliwahi kusema kwamba anachunguza mambo yanayohusiana na parabiosis, eneo lenye utata la utafiti ambapo damu ya wanyama wachanga hutumiwa kuchunguza uwezekano wa kufufua au kurejesha nguvu za wanyama wazee, na huenda siku moja ikatumika hata kwa binadamu.

Mwanzilishi wa PayPal na Palantir, Peter Thiel
Maelezo ya picha, Mwanzilishi wa PayPal na Palantir, Peter Thiel

Bryan Johnson anadai kuwa ana utajiri wa dola milioni 200, sawa na takriban pauni milioni 150, lakini anachokosa kwa upande wa utajiri anakifidia kwa wingi wa maudhui anayochapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yeye huchapisha kuhusu kila kitu anachokifanya, kuanzia kwa ratiba yake ya sauna hadi kifaa anachotumia kupima nguvu ya kusimama kwa uume wake na ya mwanawe wakati wa usiku.

Anaeleza kwamba ratiba yake ina mchanganyiko wa lishe kali, mazoezi na usingizi wa kupindukia, virutubisho kadhaa na hata tiba ya jeni, ambayo imemsaidia kupunguza umri wake wa kibayolojia kiasi kwamba sasa anadai kuwa "mtu mwenye afya zaidi duniani." Ingawa kauli hiyo haiwezi kuthibitishwa.

Bilionea wa mpira wa kikapu LeBron James anaripotiwa kutumia dola milioni 1.5 kila mwaka kwa ajili ya afya yake.

Matumizi hayo yanajumuisha kukaa kwenye chumba maalumu cha oksijeni yenye shinikizo alichonacho nyumbani, pamoja na kufanyiwa cryotherapy, tiba inayohusisha kukabiliwa na baridi kali ya hadi nyuzi joto -160°C.

Familia ya Kardashian imewahi kufanyiwa uchunguzi wa mwili mzima kwa kutumia MRI, ambao unadaiwa kusaidia kugundua saratani na matatizo mengine mapema. Hata hivyo, uchunguzi huo haupendekezwi na baadhi ya taasisi za kitabibu.

Bilionea wa Urusi Dmitry Itskov alianzisha mpango unaoitwa "2045 Initiative", ambao unalenga kuwezesha akili za binadamu kuhamishiwa kwenye kompyuta.

Bilionea wa China mwenye umri wa miaka 97, Li Ka-shing, anaamini katika kirutubisho kinachodaiwa kupunguza kasi ya kuzeeka kinachoitwa nicotinamide riboside, na amewekeza dola milioni 25 katika kampuni inayoitengeneza.

Wanafanana kwa jambo gani?

Je, taratibu hizi zote tofauti za kuongeza maisha marefu miongoni mwa matajiri wakubwa zinafanana kwa kiasi gani?

Hakuna ushahidi thabiti kwamba matibabu hayo yatawasaidia watumiaji wake kuishi muda mrefu zaidi kuliko wastani.

Mambo ambayo yameonyeshwa kuwasaidia watu matajiri kuishi kwa muda mrefu, kwa kushangaza, ni yale yale yanayowasaidia kila mtu kuishi maisha marefu: kutovuta sigara, kuwa na lishe bora, kufanya mazoezi, kupunguza msongo wa mawazo na kupata huduma bora za afya.

Na jambo la kufurahisha ni kwamba, hakuna hata moja kati ya mambo hayo yanahitaji kutumia mamilioni ya dola kila mwaka.

Na mafanikio ya kweli ya kisayansi yatakayoweza kuongeza muda wa maisha ambayo bado hayajapatikana, hayatapatikana kwa mabilionea kujifanyia majaribio wao wenyewe.

Yatapatikana kupitia utafiti wa kisayansi unaofadhiliwa ipasavyo jambo ambalo, kwa kushangaza, matajiri wengi wameshindwa kuwekeza vya kutosha katika utafiti huo.

Kufuata pesa

Watu matajiri kwa hakika huishi muda mrefu zaidi. Nchini Marekani, watu walio katika asilimia 1 ya juu zaidi kwa utajiri huishi kwa miaka 10 hadi 15 zaidi kuliko wale walio katika asilimia 1 ya chini zaidi.

Hata hivyo, si kwa sababu ya vyumba vyao vya kugandisha mwili, metformin au parabiosis, bali kwa sababu ya mambo yale ya kawaida na yanayofanywa na watu wengine wa kawaida.

Hata ukiwa na fedha zisizo na kikomo, ukweli ni kwamba hakuna mengi ya ziada unayoweza kufanya kwa kutumia teknolojia ya sasa ya tiba ili kuongeza maisha yako kuwa marefu.

Wanasayansi wana mawazo mengi ya kuvutia kuhusu namna ya kupunguza kasi ya kuzeeka. Baadhi ya mbinu hizo zimeonyesha matokeo katika minyoo, nzi na panya, lakini hadi sasa hakuna matibabu ambayo yamefikia hata hatua ya kufanyiwa majaribio ya kitabibu ili kubaini kama yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mchakato wa kuzeeka kwa binadamu.

Huenda Sam Altman akaishi muda mrefu zaidi kutokana na kutumia metformin, au huenda asiishi muda mrefu, kwa sasa hakuna ushahidi thabiti unaothibitisha kile kinachoweza kutokea.

Faida za metformin bado hazijathibitishwa kikamilifu, na matumizi yake ya muda mrefu huenda yakaleta madhara.

.

Vivyo hivyo, kujinyima chakula au kudhibiti mlo unaotumia kupita kiasi pia kumeonekana kuwa na madhara, kwani kunaweza kudhoofisha mifupa na kuathiri mfumo wa kinga katika maisha ya baadaye.

Kisha kuna zile zinazoitwa "supplement stacks" mchanganyiko mkubwa wa vidonge, unga na kemikali za majaribio vinavyotumiwa kwa wakati mmoja kwa matumaini kwamba kwa namna fulani vitaongeza muda wa maisha.

Badala ya kuongeza muda wa kuishi, virutubisho hivi mara kwa mara huhusishwa na uharibifu wa ini na madhara mengine.

Na kuchanganya aina kadhaa za matibabu kwa wakati mmoja huleta tatizo jingine. Tunajua kwamba matibabu mengi yanapotumiwa kwa pamoja yanaweza "kuingiliana" na kuleta madhara.

Kwa mfano Viagra, ikichanganywa na baadhi ya dawa za moyo, inaweza kusababisha kifo kutokana na kushuka kwa kiwango cha shinikizo la damu.

Biolojia ya binadamu ni jambo tata, na ni rahisi zaidi kuvuruga mfumo kuliko kuurekebisha.

Ili kubaini ni nini hasa kinafanya kazi, haitoshi kuwa na mamilioni ya dola pekee kunahitajika majaribio sahihi kwa binadamu.

Bei ya kutokufa

Ikiwa bado una wasiwasi kwamba mabilionea kwa siri wananunua fursa ya kutokufa, huku sisi wengine tukijikita katika kufanya mazoezi, kupata usingizi wa kutosha na kula mboga, kuna jambo la kutia moyo: matajiri wengi sana hawaishi kana kwamba matibabu ya mapinduzi dhidi ya kuzeeka yako karibu kupatikana.

Kwa kweli, ukizingatia tabia zao, kwa kushangaza hawajaonekana kuwa na msukumo mkubwa sana wa kuongeza muda wa maisha.

Pia kuna mabilionea wenye mawazo tofauti. Elon Musk amewahi kusema mara kadhaa kwamba kuishi maisha marefu zaidi kunaweza kuwa jambo baya.

Alipoulizwa mjini Cannes mwaka 2024, alisema: "Sina uwekezaji wowote katika kuongeza muda wa maisha. Ikiwa tutaishi kwa muda mrefu sana, nadhani jamii inaweza kuganda na kushindwa kubadilika."

.
Maelezo ya picha, Elon Musk

Kuna wachache wanaowekeza katika eneo hili. Mfano unaojulikana zaidi ni Altos Labs, kampuni ya siri inayojikita katika utafiti wa kuongeza muda wa maisha, ambayo ilipokea uwekezaji wa awali wa dola bilioni 3, ambao inasemekana kwa sehemu kubwa ilifadhiliwa na Jeff Bezos anayemiliki Amazon.

Kampuni hiyo ilivutia zaidi baada ya kumwajiri mwanasayansi aliyeshinda Tuzo ya Nobel, Shinya Yamanaka, ambaye utafiti wake ulijikita katika kuchunguza namna seli za watu wazima zinavyoweza kubadilishwa na kurudishwa katika hali inayofanana na seli shina, kama zile zinazopatikana katika hatua za mwanzo za ukuaji wa kiumbe.

Jeffrey Bezos
Maelezo ya picha, Jeffrey Bezos

Lakini ingawa hiyo inaonekana kuwa kiasi kikubwa cha fedha, kwa kweli ni kidogo sana ukilinganisha na utajiri wake.

Utajiri wa Bezos unakadiriwa kuwa dola bilioni 270 mwaka 2026, ikimaanisha kwamba hata kama angeifadhili Altos Labs peke yake jambo ambalo hakufanya ingekuwa takriban asilimia 1 ya utajiri wake.

Pia, kiasi hicho kiko karibu na fedha anazotumia kila mwaka katika kampuni yake ya roketi, Blue Origin.

Akiwa na umri wa miaka 62, huenda Bezos akawa na miaka 20 hadi 30 zaidi ya kuishi. Kwa hiyo, ikiwa kweli aliamini kwamba sayansi ya kuongeza muda wa maisha ndiyo tiketi yake ya kutokufa, ungeweza kutarajia angewekeza zaidi ya asilimia 1 tu ya utajiri wake katika jambo hilo.

Tiba halisi ya kuzeeka

Kinaya kikubwa ni kwamba mabilionea ambao kwa dhati wanataka kuishi muda mrefu zaidi huenda wakafanya zaidi kwa kufadhili majaribio makubwa ya kisayansi kuliko kujifanyia majaribio kwa kutumia matibabu ambayo bado hayajathibitishwa vya kutosha.

Kwa sasa, utafiti wa aina hiyo unapata ufadhili mdogo sana. Nchini Marekani, utafiti wa kuelewa mchakato wa kuzeeka hupata takriban mara 20 chini ya fedha za serikali ikilinganishwa na utafiti wa saratani licha ya ukweli kwamba saratani nyingi husababishwa na kuzeeka.

Na licha ya uwekezaji unaovutia vichwa vya habari katika kampuni kama Altos Labs, utafiti wa kuongeza muda wa maisha bado unachukua sehemu ndogo sana ya uwekezaji wote katika teknolojia ya tiba.

Jambo hilo linashangaza zaidi ikizingatiwa kwamba, kulingana na utafiti, matajiri wanauwezo wa kutoa karibu nusu ya utajiri wao ili kupata miaka 10 ya ziada yenye afya.

Kwa ujumla, mabilionea duniani wanakadiriwa kuwa na utajiri wa jumla wa dola trilioni 20.

.

Nusu ya kiasi hicho ni dola trilioni 10 kiasi ambacho huenda kikawa kikubwa kuliko fedha zote ambazo tumewahi kuwekeza katika utafiti wa afya katika historia nzima ya binadamu.

Hatimaye, ingehitaji sehemu ndogo tu ya mabilionea duniani kuamua kufadhili utafiti wa kuongeza muda wa maisha ili kuwapa wao na sisi wengine nafasi nzuri ya kupata miaka 10 ya ziada ya kuishi kwa afya njema.

Na hiyo ndiyo hoja muhimu: mara tu zitakapogunduliwa na kuendelezwa, matibabu ya kupunguza kasi ya kuzeeka hayatapatikana kwa matajiri pekee.

Ili kurejea kwa mara ya mwisho katika matumizi ya metformin ya Sam Altman, hii si dawa maalumu ya gharama kubwa inayogharimu dola milioni 1 kwa mwaka ni kidonge cha bei nafuu kinachotengenezwa kwa wingi, ambacho gharama yake ni ndogo sana kwa kila kidonge.