Edward Rukidi Kijanangoma: Kutoka uwanahabari hadi ufalme wa Tooro Uganda

.
    • Author, Basillioh Rukanga
    • Author, Bella Twine
    • Nafasi, BBC Focus on Africa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mwanmfalme Edward Rukidi Kijanangoma Nyabongo II, anayetarajiwa kutawazwa kuwa mfalme wa Ufalme wa Tooro nchini Uganda baadaye leo, amekuwa mtu anayefahamika kwa muda mrefu nchini humo.

Kwa Waganda wengi, hakufahamika kama mrithi wa kiti cha ufalme, bali kama msimulizi, mtangazaji na mhariri wa muda mrefu katika shirika la utangazaji la serikali.

Lakini sasa Kijanangoma, mwenye umri wa miaka 56, amekuwa chanzo cha habari, huku kupanda kwake kwenye kiti cha ufalme wa Tooro kukizua utata na hisia mbalimbali ndani na nje ya Uganda.

Tooro ni mojawapo ya falme nne kuu za kihistoria zinazotambuliwa rasmi nchini Uganda. Kwa miaka 31 iliyopita, ufalme huo ulikuwa ukiongozwa na Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV, aliyewahi kujulikana kama "mfalme mtoto" baada ya kurithi kiti hicho akiwa mchanga.

Oyo alikua mfalme mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka mitatu tu, baada ya kifo cha baba yake. Wakati huo akiwa mfalme mwenye umri mdogo zaidi duniani, aliendelea kutawala hadi alipofariki mwezi uliopita kutokana na saratani, akiwa na umri wa miaka 34.

Sherehe za kutawazwa ni siku ya kusherehekea, zikihusisha taratibu za jadi zinazoanza usiku wa manane. Mfalme mpya kisha hutembea umbali wa takriban kilomita nne hadi katika kasri rasmi la kifalme la Karuziika ambako hutawazwa.

Baada ya hapo hufanyika mapambano ya kuigiza, yanayoashiria kwamba kupata ufalme si jambo rahisi. Kisha hubarikiwa na wanachama wa ukoo wa kifalme wa Babiito, ambao ni ukoo wa kifalme wa Ufalme wa Tooro, Waziri wa Habari wa Tooro Charles Mwanguhya aliiambia podikasti ya BBC Focus on Africa.

Hufanya sherehe nyingine zinazoashiria kuchukua kwake rasmi madaraka ya ufalme, kabla ya kuketi kwenye kiti cha enzi na taji halisi kuwekwa kichwani mwake, kuashiria mamlaka yake mapya na nafasi yake kama mfalme mpya wa Tooro.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini kuchaguliwa kwa Kijanangoma kuwa mfalme hakukuwa jambo lililokwenda moja kwa moja.

Kwa mujibu wa mila, mwana anayemtambua mfalme aliyefariki anapaswa kumrithi. Wanafamilia wa karibu wa kifalme walisema Oyo aliacha mtoto wa kiume na wosia uliokuwa na maelekezo kwamba mtoto huyo ndiye anayepaswa kuwa mfalme anayefuata.

Hata hivyo, mtoto huyo hajawahi kutambulishwa hadharani, wala hakutambuliwa na kamati ya wajumbe 21 wa ukoo wa Babiito ambao huchagua mfalme na hatimaye kumchagua Kijanangoma.

Mfalme Oyo hakuwahi kufunga ndoa hadharani, na machache yanajulikana kuhusu mke wake au mtoto wao wa kiume.

Hata hivyo, mama yake, Malkia Best Kemigisa, alisisitiza kwamba wosia wa mfalme huyo aliyefariki ulipaswa kuheshimiwa.

Lakini kamati ya urithi wa kifalme ilipuuza msimamo wake, ikisisitiza kuwa mchakato wao wa kumchagua mfalme ulifanyika kwa kuzingatia mila na desturi za Tooro.

Hivyo, mfalme mpya amejikuta katikati ya mzozo wa urithi, huku Kemigisa na ndugu zake wa karibu wakiwa hawajaridhishwa na matokeo hayo.

.
Maelezo ya picha, Mama wa marehemu Mfalme Oyo ameeleza maumivu yake kuhusu mzozo wa urithi.

Kemigisa alitaja kuchaguliwa kwa Kijanangoma kuwa "kutangazwa kwa mfalme wa pili" baada ya "wosia wa Mfalme Oyo kusomwa mbele ya wanafamilia wa kifalme".

"Kama mama, hilo lilikuwa jambo lenye kuumiza sana," alisema, akielezea jinsi sherehe za mfalme anayefuata zilivyokuwa zikifanyika "umbali wa mita chache tu kutoka mahali mwili wa mwanangu ulipokuwa".

Baadaye malkia huyo alisema mtoto wa Oyo, aliyekuwa katika jimbo la Texas nchini Marekani, alitarajiwa kurejea nyumbani lakini hilo halikuwezekana kutokana na "mzozo mkali na wenye mgawanyiko kuhusu urithi".

"Hakuna mtoto anayepaswa kuwekwa katika mazingira ambayo kurejea katika nchi ya baba yake kunaweza kumfanya ajikute akivutwa katika uhasama na mzozo," Kemigisa alisema katika chapisho kwenye X.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa Tooro, mtoto anayezungumziwa "hajawahi kuwasilishwa popote, jambo linalomaanisha kwamba kuna ongezeko la kukubalika kwamba, ingawa ni jambo la kusikitisha, Mfalme Oyo hakuacha mtoto wa kiume".

Wakati Mfalme Oyo aliporithi taji kutoka kwa baba yake, Mwanguhya aliiambia BBC kwamba "taji sasa limehamia katika ukoo mwingine ndani ya ukoo wa watawala".

Mfalme lazima atoke katika ukoo wa Babiito, hususan katika kizazi cha Mfalme George David Matthew Kamurasi Rukidi III, kwa mujibu wa vyanzo vya ikulu ya kifalme.

Kijanangoma na Mfalme Oyo aliyefariki walikuwa binamu. Wote ni wajukuu wa Rukidi III, mfalme wa 11, au Omukama, aliyeongoza Ufalme wa Tooro kuanzia mwaka 1928 hadi 1965.

Kijanangoma alikuwa miongoni mwa watu kadhaa waliozingatiwa kwa nafasi hiyo, akiwemo Prince George Desmond Kamurasi, anayekipigia soka moja ya klabu maarufu za soka za ngazi ya chini nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa kamati ya urithi, nahodha na kipa wa South East Dons alikataa ofa ya kuwa mfalme, akitaja majukumu mengine aliyonayo.

Baada ya kutangazwa rasmi kuwa mfalme, Kijanangoma aliahidi kuwa ikulu itakuwa wazi kwa wananchi, huku akisema atazingatia umoja na maendeleo.

"Naomba jambo moja kutoka kwenu - wamekunipa cheo hiki cha mfalme lakini siwezi kufanya kazi peke yangu, ni lazima nifanye kazi pamoja nanyi," alisema.

Rais Museveni (kushoto), aliyerejesha falme za jadi katika miaka ya 1990, akiwa katika picha na Mfalme Oyo wa Tooro (kulia) mwaka 2010.
Maelezo ya picha, Rais Museveni (kushoto), aliyerejesha falme za jadi katika miaka ya 1990, akiwa katika picha na Mfalme Oyo wa Tooro (kulia) mwaka 2010.

Wafalme wa jadi nchini Uganda hawana mamlaka rasmi ya kisiasa, lakini wanaendelea kuwa na ushawishi mkubwa wa kitamaduni na uaminifu mkubwa katika jamii wanazoongoza.

Uganda ina falme nne kuu, huku mkubwa na maarufu zaidi ukiwa Buganda, uliopo katikati mwa nchi na unaojumuisha mji mkuu Kampala.

Falme hizo zilifutwa mwaka 1967, lakini serikali chini ya Rais Yoweri Museveni ilizirejesha mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Serikali ilisema hatua hiyo ililenga kukuza fahari ya kitamaduni na umoja wa kitaifa, lakini hatua hiyo pia imetafsiriwa kuwa njia ya kuwaridhisha baadhi ya jamii na kukuza uaminifu wa kisiasa.

Katikati ya mzozo wa urithi, serikali iliunga mkono chaguo la Kijanangoma lililofanywa na ukoo wa Babiito. Mwanasheria Mkuu Sam Mayanja alisema Ufalme wa Tooro ulipewa ruhusa ya kuendelea na sherehe za kutawazwa, kwa kuwa hakukuwa na malalamiko rasmi dhidi ya Kijanangoma.

Tarehe ya kutawazwa ilitangazwa na serikali na Rais Museveni anatarajiwa kuhudhuria.

Mwana wa rais huyo na mkuu wa jeshi, Muhoozi Kainerugaba, pia ameiunga mkono hadharani Kijanangoma. "Atawale kwa muda mrefu," aliandika kwenye X.

Jina la Kijanangoma lenyewe linaashiria urithi wake wa kifalme.

Baba yake, Kijanangoma wa kwanza, alizaliwa mwaka ambao Mfalme Rukidi III alikalia kiti cha ufalme. Mfalme huyo alimpa jina hilo, linalomaanisha "anayekuja na ngoma ya kifalme".

Ngoma ya kifalme, iliyotabiriwa vizazi viwili vilivyopita, sasa inarejea kwa mwenye jina lake.

Kijanangoma alizaliwa mwaka 1970 na kukulia katika nyumba ya familia yao katika kijiji cha Kidukuru, Fort Portal, takriban kilomita 300 kutoka Kampala.

Aliondoka kijijini hapo kwenda kuendelea na masomo na kuhitimu shahada ya mawasiliano ya umma kutoka Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 1999.

Alifanya kazi kama mtangazaji katika taaluma iliyodumu zaidi ya miongo miwili, ikiwemo nchini Rwanda jirani na Uganda, na katika Shirika la Utangazaji la Uganda.

Kijanangoma amekuwa mwanahabari kwa sehemu kubwa ya maisha yake ya utu uzima.
Maelezo ya picha, Kijanangoma amekuwa mwanahabari kwa sehemu kubwa ya maisha yake ya utu uzima.

Miaka aliyotumia kushirikiana na wananchi, kukutana na viongozi na kufahamu masuala ya kitaifa kupitia kazi yake ya uandishi wa habari huenda ikamsaidia anaporejea katika jamii alikotoka, safari hii akiwa kiongozi wao.

Baada ya kutangazwa kuwa mfalme, Kijanangoma alisema atatumia mahusiano aliyojenga katika miaka 21 ya kufanya kazi kama mwanahabari "kuwaletea watu wetu mambo mazuri".

Mama yake, Assimwe Yusta Kijanangoma, anaamini mwanawe yuko tayari kwa jukumu lake jipya. Anasema malezi yake yalijikita kwa kina katika mila na desturi.

"Nilimlea kwa mafundisho ya ufalme wa zamani, kwa kutumia fimbo, maelekezo na kukemewa. Wakati mwingine tunacheka pamoja, na wakati mwingine namkemea," aliiambia BBC.

Aliongeza: "Eddy ana tabia nzuri, hapigani wala kupaza sauti. Hata anapokosewa, husema maneno machache na haendelei sana kulizungumzia."

Anasema anafurahia kwa ajili ya mwanawe, ingawa anakiri kuwa ana hisia mchanganyiko, hasa kwa kuwa mwanawe anachukua nafasi hiyo baada ya kifo cha "mtu mkubwa".

Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Ambia Hirsi