Sir Wicknell alipataje utajiri wake?

c
    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kifo cha ghafla cha mfanyabiashara mashuhuri wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, kimeacha nyuma historia ya biashara, utajiri na maisha ya kifahari yaliyomfanya kuwa mmoja wa wafanyabiashara waliozungumziwa zaidi nchini humo na hata Afrika Mashariki.

Chivayo amefariki baada ya kupata ajali ya helikopta, na kifo chake kimeibua tena maswali kuhusu safari yake ya kibiashara na chanzo cha utajiri mkubwa alioujenga.

Kwa miaka kadhaa, jina lake lilihusishwa na sekta mbalimbali, zikiwemo nishati, miundombinu, mawasiliano, mafuta na usafirishaji.

Lakini Chivayo hakujulikana kwa biashara pekee.

Aliishi maisha ya kifahari yaliyovuta macho ya umma, kuanzia magari ya gharama kubwa, mali na safari za kifahari hadi tabia yake ya kutoa magari na fedha taslimu kama zawadi kwa watu mbalimbali.

Na kusema kweli, alijua namna ya kuonyesha ukwasi wake katika mtandao wa instagram.

Na lililokuwa likishangaza wengi ni namna Chivayo alionyesha ukaribu na watu wenye mamlaka. Mara kwa mara alikuwa akichapisha picha akiwa na wanasiasa mbalimbali, kuanzia marehemu Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na mrithi wake, Emmerson Mnangagwa, hadi viongozi wengine wa Afrika, akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya William Ruto.

Kwa hiyo, Wicknell Chivayo aliupataje utajiri wake, na ni biashara zipi zilizokuwa nyuma ya mafanikio yake?

Taarifa zinazopatikana hadharani zinatoa sehemu ya majibu. Hata hivyo, hakuna takwimu iliyothibitishwa kwa kujitegemea inayoweza kutaja kwa uhakika thamani halisi ya mali zake binafsi.

Maisha ya Kifahari mitandaoni

h
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika nchi (Zimbambwe) ambayo watu wengi wanahangaika kumudu maisha ya kila siku, utajiri wake mkubwa uliendelea kuvuta hisia na kuibua maswali kuhusu chanzo chake.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Instagram yake imejaa pia machapisho ya zawadi anazowapa watu.

Mara nyingi simulizi huwa lilelile.

Unaona picha ya gari jipya, linalong'aa, limefungwa puto na wakati mwingine utepe mkubwa kwenye boneti. Kisha Chivayo anaandika ujumbe wa kumpongeza mtu aliyemchagulia zawadi hiyo na kumwelekeza mahali pa kwenda kulichukua.

Mara nyingi ni kwenye moja ya maduka ya magari ya kifahari jijini Harare.

Mwezi uliopita, kwa mfano, alimwandikia mwanamuziki maarufu Jah Prayzah:

"Tafadhali mwende mkamuone Victor huko Exquisite Motors. Range Rover Autobiography yako mpya ya mwaka 2025 imelipiwa kikamilifu na iko tayari kuchukuliwa."

Na huo ndio mtindo wa "Sir Wicknell" - maisha ya kifahari, magari ya bei kubwa na zawadi zinazoweza kumshangaza mtu yeyote.

Kampuni ya Intatrec ya Zimbambwe

Wicknell alijitangaza kama mfanyibiashara nguli.

Na miongoni mwa majina yanayohusishwa kwa karibu na safari yake ya biashara ni Intratrek Zimbabwe.

Kampuni hiyo, kwa kushirikiana na kampuni ya China, ilishinda zabuni yenye thamani ya dola milioni 172.8 ya kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa jua chenye uwezo wa megawati 100 huko Gwanda.

Mradi huo, hata hivyo, baadaye uliingia kwenye utata.

Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha kuwa Intratrek ililipwa fedha za awali ili kuanza kazi, lakini haikufanikisha mradi huo kwa kiwango kilichotarajiwa na Zimbabwe Power Company, ZPC.

Mgogoro ukaibuka.

ZPC ilivunja mkataba, na Chivayo akaishtaki kampuni hiyo.

Alishinda kesi hiyo.

Baadaye pia aliachiliwa katika mashtaka yote ya jinai yaliyokuwa yamefunguliwa dhidi yake kuhusiana na suala hilo.

Mnamo Septemba 2026, Zimbabwe Power Company iliipa Intratrek kibali cha kuanza utekelezaji wa mradi huo. Thamani ya mkataba uliorekebishwa iliwekwa katika takriban dola milioni 132 za Marekani, huku mradi ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.

Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya thamani ya mkataba na kipato binafsi cha Chivayo. Mkataba wenye thamani ya dola milioni 132 haumaanishi kwamba Chivayo mwenyewe alipata dola milioni 132.

Biashara ya Mawasiliano

Chivayo hakuishia kwenye nishati na miundombinu. Baadaye, alipanua shughuli zake hadi kwenye sekta ya mawasiliano.

Mwezi Mei 2024, Zimbabwe iliidhinisha Starlink kuanza kutoa huduma ya intaneti ya satelaiti nchini humo. Katika mpango huo, kampuni ya IMC Communications ilitajwa kuwa mshirika wa Starlink nchini Zimbabwe.

Taarifa za wakati huo zilimtaja Chivayo kama mmiliki wa IMC Communications.

Ikawa mshirika wa Starlink, huduma ya intaneti ya satelaiti inayohusishwa na kampuni ya SpaceX ya Elon Musk.

Hivyo, biashara yake ikaingia katika sekta mpya inayokuwa kwa kasi, mbali na miradi ya nishati na miundombinu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na jina lake.

Mfanyabiashara mmoja ambaye amewahi kufanya biashara na Chivayo, lakini akaomba jina lake lisitajwe, aliiambia BBC kuwa Chivayo anahusika kwa karibu sana na shughuli za biashara zake.

"Yuko karibu sana na biashara zake. Yuko mwenyewe uwanjani, akifuatilia kwa karibu jinsi kila senti inavyotumika," alisema.

Mfanyabiashara huyo aliongeza:

"Ni wazi kwamba ana ulinzi wa kisiasa."

Siasa, Zanu-PF na utajiri wake

c

Chivayo ni mfuasi wa wazi wa chama cha Zanu-PF nchini Zimbambwe.

Amehusisha mafanikio yake na sera ya uwezeshaji wa wazawa iliyoanzishwa na chama hicho mwaka 2013.

Sera hiyo ililenga kuongeza umiliki na udhibiti wa kiuchumi wa Wazimbabwe weusi katika kampuni nchini humo.

Kwa baadhi ya watu, Chivayo ni mfano wa mafanikio ya sera hiyo - mfanyabiashara mweusi aliyeweza kujenga utajiri mkubwa.

Lakini si kila mtu ana mtazamo huo.

Wakosoaji wake wameibua madai kwamba sehemu ya utajiri wake inaweza kuwa imejengwa kupitia rushwa au uhusiano usio wazi na watu wenye mamlaka.

Hata hivyo Chivayo aLIkanusha vikali madai hayo.

Lakini fedha zinatoka wapi kufadhili biashara zake?

s

Hili ndilo swali ambalo Chivayo alikuwa akikabiliwa nalo mara kwa mara.

Yeye si mtu anayependa sana mahojiano na waandishi wa habari. Ameeleza pia hapo awali kwamba hapendi waandishi wa habari.

Lakini katika mahojiano machache aliyofanya kwenye kipindi cha redio cha asubuhi mwaka 2024, aliulizwa swali hilo moja kwa moja.

Jibu lake lilikuwa kwamba biashara yake kubwa inahusu zabuni za serikali anazopata kwa kushirikiana na washirika wa kigeni.

Alitaja sekta za nishati jadidifu, uhandisi, ununuzi na ujenzi pamoja na miradi ya umeme.

Pia alisema ana biashara nchini Kenya, Afrika Kusini na Tanzania.

Kwenye Instagram, Chivayo amekuwa akizungumza kwa kujiamini zaidi kuhusu mafanikio yake.

Anajiita "hustler" - mtu anayepambana na kufanya kazi kwa bidii.

Pia anasema yeye ni "self-made millionaire", yaani milionea aliyejijengea utajiri wake mwenyewe.

Anarejea maisha yake ya utotoni huko Chitungwiza, mji ulio karibu na Harare, ambako anasema familia yake ilipitia kipindi kigumu baada ya baba yake kufariki alipokuwa na umri wa miaka 10.

Uchunguzi wa madai ya rushwa

Mnamo 2024, Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zimbabwe, ZACC, ilianzisha uchunguzi baada ya shirika la uchunguzi kutoka Afrika Kusini, Open Secrets, kutoa madai kuhusu Chivayo.

Shirika hilo lilidai kwamba Chivayo alipata mamilioni ya dola kwa kuwezesha zabuni ya kusambaza vifaa vya uchaguzi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe, ZEC, mwaka 2023.

Mambo yalizidi kuwa mazito baada ya sauti iliyodaiwa kuwa ya Chivayo kuvuja.

Katika sauti hiyo, alidaiwa kuzungumza kuhusu mkataba huo na kuwafariji wafanyabiashara wengine wawili ambao, kwa mujibu wa madai hayo, walikuwa wamekosa malipo waliyotarajia.

Sauti hiyo pia ilionekana kudokeza kwamba kulikuwa na mikataba mingine mingi iliyokuwa njiani.

Lakini ZEC ilikanusha kuwa na uhusiano wowote wa kibiashara na Chivayo au wafanyabiashara hao.

Chivayo na watu wengine waliotajwa pia walikanusha madai hayo.

Na mwaka mmoja baadaye, ZACC haikuwa imemfungulia mtu yeyote mashtaka kuhusiana na suala hilo.

Chivayo alisema sauti hiyo huenda ilikuwa "deepfake", yaani rekodi iliyotengenezwa au kubadilishwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.

Pia alimuomba msamaha rais kwa kile alichosema kuwa huenda sauti hiyo ilileta taswira kwamba familia ya kwanza ilihusika katika vitendo vya rushwa.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, wafanyabiashara wawili waliotajwa katika sauti hiyo walikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kutumia vibaya takriban dola milioni 7.

Wafanyabiashara hao walikanusha mashtaka hayo, ambayo yanahusishwa na zabuni ya mpango wa serikali wa kusambaza mbuzi kwa wananchi.

Wamekuwa rumande kwa karibu mwaka mmoja wakisubiri kuanza kwa kesi yao.

Kitendawili cha utajiri wake

d

Wicknell Chivayo atakumbukwa kwa maisha yake ya kifahari, biashara kubwa, ukaribu wake na watu mashuhuri na wenye ushawishi, pamoja na tabia yake ya kutoa magari na fedha kama zawadi.

Na wengi aliowazawadi alitaja kuwa alikuwa anawapongeza kwa uzalendo wao wa kuunganisha jamii kupitia masuala tofauti.

Kwa mtu ambaye alipenda kuonyesha ulimwengu jinsi alivyotumia fedha zake, huenda baadhi ya majibu kuhusu jinsi alivyotengeneza utajiri huo na ni nini hasa kilichomfikisha kwenye kilele cha maisha ya kifahari yameondoka naye.

Hata hivyo, historia ya biashara zake, kampuni alizohusishwa nazo na mahusiano yake katika ulimwengu wa siasa na biashara vinaacha vipande vya simulizi vinavyoweza kusaidia kuelewa safari yake.

Na pengine hapo ndipo urithi wa Chivayo unapobaki, si tu katika mali alizoacha, bali pia katika maswali ambayo kifo chake kimeyaacha wazi.