Christa Pike hajitambui baada ya hukumu ya kifo kushindikana

Chanzo cha picha, Tennessee Department of Corrections
Tahadhari: Makala hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuyapata ya kushtua
Mfungwa wa kunyongwa nchini Marekani, Christa Pike, alikuwa hajitambui na alikuwa amewekewa mashine ya kumsaidia kupumua siku ya Alhamisi usiku, baada ya jaribio la kutekeleza hukumu yake kifo kwa sindano ya sumu kushindikana, kwa mujibu wa mawakili wake.
Pike, mwenye umri wa miaka 50, alidungwa dozi mbili za dawa ya pentobarbital siku ya Jumatano katika jaribio la kutekeleza hukumu yake ya kifo. Hata hivyo, aliendelea kuwa hai na baadaye alikimbizwa hospitalini kwa gari la wagonjwa.
Hali yake bado ni mbaya na anaendelea kupata matibabu katika hospitali moja eneo la Nashville, Tennessee.
Mawakili wake sasa wanataka hukumu yake ya kifo ibadilishwe, wakisema jaribio hilo lililoshindikana linaibua maswali makubwa kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo. Pike alihukumiwa kifo mwaka 1996 kwa mauaji ya Colleen Slemmer.
Ijumaa, mawakili wake waliwasilisha ombi la dharura mahakamani wakitaka ushahidi wote unaohusiana na tukio hilo uhifadhiwe. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, madaktari walikuwa wakijaribu kuokoa maisha yake huku wakifanya jitihada za kuondoa dawa hiyo mwilini mwake.
‘Sindano moja ilipinda kabisa’
Mawakili wa Pike wanasema wakati wa maandalizi ya utekelezaji wa hukumu, maafisa wa gereza walijaribu mara kadhaa kupata mshipa wa kumdunga dawa hiyo.
Walisema takriban sindano saba zilitumika, na wakati mmoja Pike mwenyewe alielekeza sehemu ambazo zingeweza kutumika kupata mshipa.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa mahakamani, sindano moja ilitolewa ikiwa imejipinda kabisa baada ya jaribio hilo kushindikana.
Pia walidai kuwa Pike alikuwa akilia, akigugumia na kupumua kwa nguvu wakati akidungwa dozi hizo mbili.
Kufuatia tukio hilo, Gavana wa Tennessee, Bill Lee, ameagiza uchunguzi huru kufanyika na kusitisha utekelezaji wote wa adhabu za kifo katika jimbo hilo kwa kipindi kilichosalia cha mwaka.
Hata hivyo, Idara ya Magereza ya Tennessee imetetea utaratibu uliotumika, ikisema ulifuatwa kulingana na kanuni zilizopo.
Mamlaka bado hazijaeleza kwa nini utekelezaji huo ulishindikana wala kama zitajaribu tena kutekeleza hukumu ya Pike.
Soma Zaidi:




















