Trump amefanya nini tofauti na Obama kuhusu Iran?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rais wa Marekani Donald Trump anasifu makubaliano mapya kati ya Marekani na Iran kama ushindi mkubwa wa diplomasia na usalama ukilinganisha na yaliyoafikiwa wakati wa utawala wa Barack Obama.
Makamu wake, JD Vance, pia amesema mpango wa nyuklia wa Iran "umeangamizwa kikamilifu" na kwamba makubaliano hayo yatahakikisha Tehran haitajenga tena uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Akibainisha kuwa rasimu ya makubaliano ya vipengee 14 kuwekwa wazi na Trump kabla ya ijumaa watakapotia saini mkataba wa maelewano.
Lakini je, makubaliano haya ni tofauti kwa kiwango gani na yale yaliyofikiwa mwaka 2015 chini ya Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama?
Na je, vita hivyo vilivyodumu kwa siku zaidi ya mia moja vimefanikisha lengo lolote?
Tofauti ya mitazamo kati ya Obama na Trump kuhusu Iran
Tofauti ya mitazamo kati ya utawala wa sasa na ule wa zamani wa Marekani inaonekana wazi.
Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump amesema kuwa makubaliano mapya ya Washington na Tehran yanalenga kuhakikisha Iran haitaunda tena uwezo wa nyuklia.
Katika kauli hiyo, Donald Trump alikuwa akikosoa vikali makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA) yaliyosimamiwa na Barack Obama, akidai yalitoa fursa kwa Iran kuendeleza mpango wake wa nyuklia.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Makubaliano ya Obama yalikuwa njia ya kuifanya Iran ipate silaha za nyuklia, yakiambatana na fedha nyingi, na yalikuwa miongoni mwa makubaliano mabaya na ya kipumbavu zaidi kuwahi kufanywa na Marekani. Makubaliano yetu, kwa upande mwingine, ni ngome imara inayozuia kabisa Iran kumiliki silaha za nyuklia. Ni kinyume kabisa cha yale ya Obama."
Kauli iliyoonesha kuwa Trump amebadilisha kabisa kilichokuwa ndani ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, yanayojulikana kama Joint Comprehensive Plan of Action (JCPOA), yaliokuwa makubaliano kati ya Iran na mataifa makubwa duniani yaliyolenga kuzuia Tehran kutengeneza silaha za nyuklia kwa kubadilishana na kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi.
Katika makubaliano yaliyoongozwa na rais wa zamani Barack Obama, Iran ilikubali kupunguza kiwango cha urutubishaji wa urani hadi asilimia 3.67, kiwango kinachofaa kwa matumizi ya kiraia lakini si kwa silaha za nyuklia.
Lakini makubaliano yatakayotiwa saini Uswisi Ijumaa kwa mujibu wa makamu wa rais wa Marekan JD Vance, anasema mpango wa nyuklia wa Iran "umeharibiwa kikamilifu" na kwamba makubaliano mapya yanalenga kuhakikisha Tehran haitaunda tena uwezo huo.
Hata hivyo, tofauti ingine pia inayojitokeza ni ukubwa wa nyaraka hizo.
JCPOA ilikuwa makubaliano ya kina yaliyokuwa na kurasa 18, ilhali makubaliano ya Trump, yanayoelezwa kama hati ya maelewano, yana takriban ukurasa mmoja na nusu pekee, kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance.
Obama anasemaje?
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama anaamini kuwa, licha ya madai ya Ikulu ya White House kwamba imefikia mafanikio mapya dhidi ya Iran, makubaliano yoyote yatakayozaliwa kutokana na juhudi za Donald Trump huenda yakafanana kwa kiasi kikubwa na JCPOA ya mwaka 2015, makubaliano ambayo Trump mwenyewe alijiondoa nayo alipokuwa rais katika muhula wake wa kwanza.
"Kuna uwezekano mdogo kwamba makubaliano yoyote yatakayofikiwa yatakuwa bora zaidi au tofauti kwa kiasi kikubwa na yale tuliyokuwa nayo hapo awali," amesema Obama.
Obama pia alitumia ulinganisho huo kuikosoa sera ya nje ya Donald Trump, ambayo mara nyingi imejengwa juu ya vitisho na matumizi ya nguvu za kijeshi, akisema kuwa matokeo yanayodaiwa kupatikana sasa yangeweza kufikiwa kupitia diplomasia bila kuingia vitani.
"Wazo kwamba tunaweza kuwalazimisha wengine kwa nguvu au kutatua matatizo kwa mabomu linaweza kuonekana la kuvutia wakati mwingine. Hata hivyo, ukweli ni kwamba ni muhimu kutoa muda kwa diplomasia na kutumia kila fursa inayowezekana kufikia makubaliano ambayo, hata kama hayatamaliza tatizo kwa asilimia 100, yanaweza kulitatua kwa asilimia 80 au 90 huku yakiepusha ulazima wa kuingia vitani," alisema Obama.
Aliongeza kuwa dunia ilipaswa kuwa imejifunza somo hilo kufikia sasa, lakini mara kwa mara hujikuta ikirudia makosa yale yale na kulazimika kujifunza upya thamani ya diplomasia katika kutatua migogoro ya kimataifa.
Vita dhidi ya Iran viligharimu Marekani
Tofauti kubwa ambayo Trump pia anaitaja ni kwamba safari hii Marekani imeingia vitani kabla ya kufikia maelewano. Tofauti na Obama ambaye alitegemea diplomasia, Trump aliamuru mashambulizi dhidi ya Iran na sasa anadai miundombinu ya nyuklia ya nchi hiyo imeharibiwa na akiba yake ya urani imeondolewa au kufichwa kabisa.
Kwa mujibu wa Obama wakati huu vita dhidi ya Iran viligharimu Marekani ukilinganisha na utawala wake ambao ulitumia njia ya diplomasia zaidi.
Iran ilijibu kwa kushambulia baadhi ya majirani zake katika Mashariki ya Kati, ikiwemo Israel, jambo lililozidisha ukosefu wa utulivu katika eneo ambalo tayari lilikuwa na migogoro mingi.
Aidha, Iran ilifunga Mlango wa Hormuz, njia muhimu kwa usafirishaji wa mafuta na gesi duniani. Hatua hiyo ilisababisha kupanda kwa bei za nishati na mbolea katika masoko ya kimataifa na kuathiri uchumi wa mataifa mengi.
Vipengee vinavyofanana vya makubaliano ya Trump na Obama

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Licha ya tofauti za kisiasa kati ya Trump na Obama, makubaliano hayo mawili yanafanana katika mambo muhimu.
Yote yanategemea ukaguzi wa kimataifa kuhakikisha Iran haitengenezi silaha za nyuklia. Yote pia yanahusisha kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo na kuruhusu Iran kupata sehemu ya fedha zake zilizozuiliwa.
Tofauti ni kwamba makubaliano ya sasa bado si mkataba kamili wa nyuklia. Ni hati ya maelewano inayolenga kusitisha vita na kufungua dirisha la siku 60 za mazungumzo kuhusu makubaliano ya muda mrefu.
Sio rahisi kulinganisha makubaliano ya Trump na Obama

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni vigumu kusema makuabaliano yalioafikiwa kati ya Marekani na Iran yaliyoongozwa na Trump ni bora kuliko makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 yalioongozwa na Obama.
Makubaliano ya JCPOA yalifikiwa katika mazingira tofauti kabisa na ilihusisha mataifa kadhaa makubwa duniani, yakiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na China pamoja na Iran.
Nayo Makubaliano ya sasa yamehusisha Iran na Marekani na hata kuiacha nje Israel ambayo imekuwa ikitaja Iran kama tishio kwake.
Pili, Makubaliano yaliyotangazwa Jumapili bado hayajawekwa wazi kwa umma, hivyo ni vigumu kwa sasa kubaini yanatofautianaje na makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA).
Muhimu zaidi, hati hii mpya ya maelewano si makubaliano ya kudumu kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Badala yake, ni makubaliano ya kusitisha vita na kutoa muda wa siku 60 kwa pande zote kuendelea na mazungumzo.
Inawezekana mazungumzo hayo yakazaa makubaliano ya muda mrefu zaidi, lakini hakuna uhakika kwamba hilo litafikiwa.
Kurt Volker, aliyewahi kuwa balozi wa Marekani katika NATO, anasema hati hiyo ni mwanzo wa mazungumzo mapya badala ya suluhisho la mwisho.
"Kwa hakika hayajatatua tatizo lolote bado. Ni hati ya muda ya maelewano inayolenga kuweka msingi wa mazungumzo mapya." anasema Volker Kurt.
Kwa mujibu wa wachambuzi, Iran ya mwaka 2026 si Iran ya mwaka 2018.
Baada ya miaka ya vikwazo, mivutano ya kikanda na kuongezeka kwa uwezo wake wa nyuklia, Tehran inaingia kwenye mazungumzo haya ikiwa na nafasi tofauti ya kujadiliana kuliko ilivyokuwa wakati Trump alipojiondoa kwenye JCPOA.
Aidha wachambuzi wa kimataifa wanasema swali muhimu si nani amepata makubaliano bora zaidi, bali kama vita vilivyogharimu maisha, uchumi na uthabiti wa Mashariki ya Kati vimeleta mabadiliko ya kweli ambayo diplomasia peke yake isingeweza kuyafanikisha.














