Je, vita na Iran kuathiri ushirika wa miaka mingi kati ya Ghuba na Marekani?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 10

Kwa miongo kadhaa, mwamvuli wa usalama wa Marekani katika Ghuba umechukuliwa kama jambo la kawaida lisilo na mashaka, lakini vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinaweza kubadilisha hilo.

Wakati wa vita hivyo, na changamoto za ulinzi zilizotokana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizokuwa na rubani za Iran dhidi ya mifumo ya ulinzi iliyokuwa ikijaribu kuzuia kulenga miundombinu muhimu katika nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC), nchi hizo hazikuwa tu zikifuatilia mwelekeo wa makombora, bali pia zilikuwa zikifuatilia majibu ya Washington, baada ya kujikuta zikiwa eneo la vita ambalo viongozi wa Ghuba wanasema hawakushirikishwa.

Je, mgogoro huu umebaini mapungufu ya mipango ya usalama kati ya Washington na nchi za Ghuba? Na je, utapunguza au kuongeza utegemezi wa miji mikuu ya Ghuba kwa nguvu ya kijeshi ya Marekani?

Ushirikiano wa miongo mingi

Nchi zote zinazounda baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) zina ushirikiano wa kiusalama na Marekani, ambapo Saudi Arabia, Qatar, Bahrain na Kuwait zimeainishwa kama "washirika wakuu nje ya NATO," huku Falme za Kiarabu ikitambuliwa kama "mshirika mkuu wa masuala ya ulinzi."

Maslahi ya Marekani katika eneo la Ghuba yaliongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya Vita kuu ya pili ya dunia, ambapo Marekani ilianza taratibu kuchukua nafasi ya Uingereza kama taifa lenye nguvu nje ya eneo hilo.

Mpangilio wa usalama ulioongozwa na Washington katika Ghuba ulishinikizwa na mambo mawili: umuhimu wa kijiografia wa eneo hilo na akiba kubwa ya mafuta, pamoja na lengo la kimkakati la kukabiliana na ushawishi wa Muungano wa Kisoviet.

Hata miaka miwili kabla ya kumalizika kwa vita, Rais wa Marekani wakati huo Franklin D. Roosevelt alitabiri umuhimu ambao mafuta na eneo la Ghuba vingekuwa navyo kwa nchi yake katika siku zijazo, akitangaza mwaka 1943 kwamba "kulinda Saudi Arabia ni jambo la umuhimu mkubwa kwa ulinzi wa Marekani," akihalalisha haja ya kutoa msaada wa kijeshi na kiuchumi kwa Ufalme huo na kuimarisha uhusiano nao.

Mwaka 1945, Roosevelt alikutana na Mfalme Abdulaziz Al Saud akiwa ndani ya meli ya kivita USS Quincy katika eneo la Great Bitter Lake la Mfereji wa Suez nchini Misri.

Ingawa rekodi rasmi hazitaji mafuta katika mazungumzo yao, mkutano huo mara nyingi unaelezwa kama mwanzo wa "uhusiano maalum" kati ya nchi hizo mbili.

Dkt. Jeffrey F. Gresh, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa na mwandishi wa kitabu "Gulf Security and the US Military: Regime Survival and the Politics of Basing", aliambia BBC News Arabic kwamba mwishoni mwa Vita kuu ya pili ya dunia, Marekani "ilikuwa na moja ya mifumo mikubwa na ya kina zaidi ya kambi za kijeshi na msaada wa vifaa duniani."

Aliongeza kuwa jeshi la Marekani wakati huo "lilibadilisha lugha na sera zake ili kulenga hasa eneo la Ghuba.

Kufikia mwaka 1949, isipokuwa kambi za usafiri wa anga nchini Ujerumani, kambi ya anga ya Dhahran ilikuwa kambi ya ng'ambo ya Marekani iliyokuwa na shughuli nyingi zaidi na ilionekana kuwa muhimu kwa operesheni na uratibu wa Marekani duniani kote katika kipindi cha baada ya vita."

Gresh anaeleza kwamba ahadi za Marekani za msaada wa kijeshi na kiuchumi zilisaidia kupata makubaliano ya kambi za kijeshi wakati huo.

Zaidi ya hayo, Marekani "ilikuwa tayari kukubali maombi ya Saudi Arabia ya risasi na vifaa vya kijeshi kwa sababu ilihofia kwamba ikiwa ingekataa, Ufalme huo ungeamua kununua vifaa vya kijeshi kutoka Muungano wa kisovieti."

Kwa mujibu wa Gresh, masuala ya usalama wa nje na ya kikanda yaliendelea kuwa "sababu muhimu nyuma ya kukamilishwa kwa makubaliano ya kuongeza uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Saudi Arabia katika muongo uliofuata vita," licha ya upinzani wa ndani dhidi ya muungano huo na Washington "kutokana na uungaji mkono wake kwa Israel na mgawanyiko uliofuata wa Palestina."

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mkutano kati ya Mfalme Abdulaziz Al Saud na Rais Franklin D. Roosevelt mara nyingi unaelezwa kama mwanzo wa "uhusiano maalum" kati ya Riyadh na Marekani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulikuwa na ushirikiano wa kijeshi wa kiwango kidogo kati ya Marekani na nchi nyingine za Ghuba kuanzia mwisho wa Vita kuu ya pili ya dunia hadi miaka ya 1980, ambao ulichukua sura mbalimbali kama mikataba ya ushirikiano wa kiusalama, mafunzo ya kijeshi, au kuruhusu majeshi ya Marekani kutumia kambi za kijeshi za ndani.

Kwa mfano, mwaka 1971 kulikuwa na makubaliano kati ya Washington na Bahrain yaliyoiwezesha Marekani kutumia miundombinu ya zamani ya kijeshi ya baharini ya Uingereza ili kuanzisha bandari katika eneo la Juffair.

Mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970, Rais wa Marekani Richard Nixon alifuata sera kuelekea eneo la Ghuba iliyoziona Iran na Saudi Arabia kama "nguzo pacha" za usalama na utulivu wa Marekani, pamoja na kulinda maslahi ya mafuta ya Marekani, ambayo Washington ilitambua kuwa muhimu kwa kudumisha nafasi yake dhidi ya Muungano wa Kisoviet katika vita Baridi.

Sera hii ya "nguzo pacha" ilisababisha Marekani kuzisambazia silaha nchi hizo mbili na kuwapa mafunzo ya kijeshi majeshi yao.

Uhusiano kati ya Marekani na Ghuba ulidorora wakati wa vita vya 1973, wakati Taasisi ya nchi za Kiarabu zinazouza Mafuta (OAPEC) ilipoweka zuio la mafuta kwa nchi zilizounga mkono Israel katika vita hivyo, hasa Marekani.

Mwaka 1979, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalimaliza sera ya "nguzo mbili" baada ya kumuangusha mshirika wa karibu wa Marekani, Shah Mohammad Reza Pahlavi.

Hali hiyo ilifuatiwa na uvamizi wa Muungano wa Kisoviet nchini Afghanistan mwaka huohuo. Matukio haya yaliongeza wasiwasi wa Washington kuhusu uwezekano wa upanuzi wa ushawishi wa Kisoviet katika Ghuba na hitaji la kuwepo kwa miundombinu ya kijeshi ya hali ya juu kulinda maslahi yake ya mafuta katika eneo hilo.

Mwaka 1980, Rais wa wakati huo Jimmy Carter alitangaza kwamba "jaribio lolote la nguvu ya nje kutawala eneo la Ghuba ya Uajemi… litakabiliwa a njia zote muhimu, ikiwa ni pamoja na nguvu za kijeshi." Wataalamu wengi wa masuala ya Marekani wanaamini sera hii iliendelea chini ya marais Ronald Reagan na George H. W. Bush

Uanzishwaji wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) mwaka 1981 wakati wa vita kati ya Iran na Iraq uliweka mfumo wa usalama wa pamoja unaojumuisha Saudi Arabia, UAE, Qatar, Bahrain, Kuwait na Oman, lakini uwezo wake ulikuwa mdogo na Marekani ikaendelea kuwa nguzo kuu ya ulinzi wa eneo hilo.

Miaka ya 1980 ilishuhudia mvutano kati ya Iraq na nchi za Ghuba, ambao ulifikia kilele mwaka 1990 wakati Iraq ilipoivamia Kuwait.

Mwaka 1990–1991 vita vya Ghuba vilibadilisha sera ya Marekani chini ya "Carter Doctrine," ambapo muungano ulioongozwa na Marekani uliendesha Operesheni Desert Shield na Desert Storm, ukilenga kulinda Saudi Arabia na kuikomboa Kuwait, jambo lililoanzisha uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani katika eneo la GCC.

Mwaka 2003 uvamizi wa Iraq na kuangushwa kwa Saddam Hussein uliibadilisha tena nafasi ya Marekani, ambapo iliongeza uwepo wake wa kijeshi lakini pia kuibua wasiwasi mpya baada ya Iran kupata nafasi ya kupanua ushawishi wake.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Ghuba zimeanza kutafuta washirika wengine kama China na Ulaya, huku zikihoji utegemezi wao kwa Marekani kutokana na majibu yanayoonekana kuwa hafifu katika baadhi ya mashambulizi ya kikanda kama yale ya Houthi dhidi ya Saudi Arabia na UAE.

Hali hii imeongeza mjadala kuhusu ikiwa uhusiano wa muda mrefu kati ya Ghuba na Marekani bado ni wa kuaminika, huku nchi za Ghuba zikijaribu kusawazisha ushirikiano wao kati ya Marekani na mataifa mengine ili kupunguza hatari za kiusalama na kiuchumi.

Hasira na kutoridhika katika eneo la Ghuba

Saa chache kabla ya kuanza kwa vita kati ya Israel na Marekani dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr al-Busaidi, ambaye nchi yake ilikuwa mpatanishi wa mazungumzo kati ya Marekani na Iran, alisema kuwa mazungumzo hayo yalikuwa yamepiga hatua "kubwa na ya kihistoria" na kwamba kufikia makubaliano kulikuwa "karibu sana."

Nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) zilijikuta zikiingia moja kwa moja katika mzozo huo, na uhusiano na Iran ukadhoofika baada ya miaka ya jitihada za kuurekebisha, ambazo zilifikia kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tehran na nchi nyingi za GCC.

Uchumi wa Ghuba uliathirika pakubwa kutokana na mashambulizi ya Iran dhidi ya miundombinu ya nishati na maeneo mengine muhimu, na nafasi ya kanda hiyo kama kituo muhimu cha utalii, usafiri wa anga, uwekezaji na teknolojia ya habari ikaanza kutetereka.

Al-Busaidi aliishutumu Washington katika makala iliyochapishwa katika jarida la The Economist tarehe 18 Machi, akisema kuwa "imepoteza udhibiti wa sera yake ya mambo ya nje" na akaita vita hivyo "janga."

Baadhi ya wachambuzi wa Kiarabu na wa Magharibi waliona machapisho ya bilionea wa UAE Khalaf Al Habtoor kwenye mtandao wa X mnamo Machi 9 (ambayo baadaye alifuta) kama ishara ya hasira ya wasomi wa Ghuba dhidi ya Marekani na wasiwasi wao kuhusu athari za vita.

Machapisho hayo yalijibu kauli za seneta wa Marekani Lindsey Graham ambaye alitoa wito kwa nchi za Ghuba kujiunga na vita pamoja na Marekani na Israel, na akatishia kupitia upya makubaliano ya ulinzi kama zisingeshiriki.

Katika maudhui hayo, Al Habtoor alieleza kuwa wanajua kwa nini wanashambuliwa na pia wanajua ni nani aliyesababisha mzozo huo bila kushauriana na washirika wake, akisema hawahitaji yeyote anayejifanya kuwa amekuja kuwaokoa, akitaja kuwa ingawa Iran ni tishio, vita hivyo ni mchezo mchafu unaoathiri eneo lao, na kwamba hawataingia katika vita hivyo kwa maslahi ya wengine.

Mtaalamu wa masuala ya Qatar Naif bin Nahar pia alikosoa jinsi Rais wa Marekani alivyoshughulikia mzozo huo, akisema katika chapisho la Machi 23 kwamba Trump aliahirisha kushambulia miundombinu ya nishati nchini Iran kwa sababu ya hofu ya bei katika soko la Marekani, huku jamii za Ghuba zikiwa chini ya mashambulizi ya makombora kwa zaidi ya siku 20 na uchumi wao ukipoteza mabilioni ya dola bila hatua kubwa kuchukuliwa.

Kubadili washirika na mkakati wa kujilinda

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Ghuba zimeanza kupanua ushirikiano wao wa kiuchumi na kiteknolojia na mataifa kama China, India, Urusi, Ufaransa na Ujerumani, na mwelekeo huu umeanza pia kuingia kwa kiwango fulani katika sekta ya usalama na ulinzi.

Wakati wa mzozo wa hivi karibuni kati ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, nchi za Saudi Arabia, UAE na Qatar zilitia saini makubaliano na Ukraine wakati wa ziara ya Rais Volodymyr Zelenskyy katika Ghuba mwishoni mwa Machi.

Chini ya makubaliano hayo, Kyiv itawapatia nchi hizo ndege zisizo na rubani za kijeshi na teknolojia za vita vya kielektroniki pamoja na kukabiliana na droni.

Zelenskyy pia alitangaza awali kwamba nchi yake ilikuwa ikisaidia mataifa matano UAE, Saudi Arabia, Qatar, Kuwait na Jordan katika kukabiliana na ndege zisizokuwa na rubani za Iran.

Tovuti ya habari ya Axios iliripoti hivi karibuni, ikinukuu maafisa wawili wa Israel na afisa mmoja wa Marekani, kwamba Israel iliiuzia UAE mfumo wa ulinzi wa anga unaofanana na Iron Dome, pamoja na wanajeshi wa kuusimamia mwanzoni mwa vita.

Swali linalojitokeza ni kama mzozo wa sasa utaifanya nchi za Ghuba zipitie upya dhamana za usalama za Marekani, au utaongeza utegemezi wao kwake.

Dkt. Andreas Krieg anasema kuwa mzozo huo huenda ukaongeza utegemezi wenye masharti zaidi kwa Marekani badala ya kuvunja kabisa uhusiano huo.

Anaeleza kuwa nchi za Ghuba hazielekei kuvunja uhusiano wa kimkakati na Washington, bali kuelekea katika uhusiano wa tahadhari zaidi na wa vitendo.

Anaongeza kuwa nchi za Ghuba zimeanza kujifunza kutokana na vita hivyo kwa kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea kimkakati, ikiwa ni pamoja na kuongeza akiba ya silaha, kuimarisha viwanda vya ulinzi vya ndani, kuboresha mifumo ya ulinzi wa anga wenye tabaka nyingi, na kuongeza uratibu wa kikanda lakini bado chini ya mwamvuli wa Marekani.

Kwa hiyo, kwa mtazamo wake, vita vinaweza kuongeza utegemezi wa muda mfupi kwa Marekani, lakini wakati huohuo kupunguza kiwango cha imani kamili katika ulinzi wake.

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Volodymyr Zelenskyy alihitimisha makubaliano ya kijeshi na Saudi Arabia, UAE na Qatar, akiwa na Emir wake Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani wakati wa ziara yake ya Ghuba mwezi uliopita.

Dk. Al-Amer anaamini kuwa nchi za Ghuba zitaendelea kusonga mbele kwa kuibadilisha na kuongeza ushirikiano wao wa kijeshi.

Anaona kuwa si suala la kuacha kabisa uhusiano na Marekani au kuchagua nchi nyingine badala yake, bali ni kuendelea na ushirikiano huo huku wakiuimarisha na kuufanya uwe na vyanzo vingine vya usalama pia.

Moja ya sababu zinazofanya kuvunjika kabisa kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili kuwa jambo lisilowezekana ni mashambulizi ya Iran ambayo yameongeza imani kwa baadhi ya nchi za Ghuba kuhusu umuhimu wa ulinzi wa Marekani.

Wataalamu wanasema kuwa nchi nyingi za GCC bado zinaona uwepo wa kijeshi wa Marekani kuwa kinga muhimu dhidi ya Iran, hata katika hali ya sasa ya mivutano.

Kwa mtazamo huo, uwepo wa kambi za kijeshi za Marekani katika nchi kama Bahrain na Qatar unaendelea kuonekana kuwa na umuhimu mkubwa.

Baadhi ya viongozi wa zamani wa eneo hilo pia wamesema mashambulizi ya Iran yamezisukuma nchi za Ghuba kuwa karibu zaidi na Marekani na hata Israel katika masuala ya kiusalama na kisiasa.

Sababu nyingine ni kwamba hakuna mbadala wa moja kwa moja unaoweza kuchukua nafasi ya Marekani kwa sasa. Ingawa China na Urusi ni washirika muhimu kisiasa, bado hawana uwezo wa kutoa ulinzi wa haraka wa anga, ushirikiano wa kijasusi, na uzuiaji wa vitisho kwa kiwango sawa na Marekani.

Dk. Craig anaeleza kuwa juhudi za kuleta washirika wengine zinaendelea, lakini zinakabiliwa na changamoto za uwezo, jiografia na muda. Hivyo, hata kama kuna mpango wa kupunguza utegemezi kwa Marekani, bado haiwezi kufanyika kwa haraka au kwa urahisi.

Dk. Al-Amer pia anasema kuwa mifumo ya ulinzi wa anga iliyonunuliwa kutoka Marekani imeonyesha ufanisi mkubwa, ikiwa na kiwango cha kuzuia makombora kinachozidi asilimia 90.

Anaongeza kuwa mifumo hii inaweza kuongezewa teknolojia nyingine za bei nafuu zaidi, lakini kubadilisha mfumo mzima wa kijeshi uliopo ni jambo litakalochukua muda mrefu sana.

Hatimaye, inabainika kuwa nchi za Ghuba hazina msimamo mmoja kuhusu mustakabali wa usalama wao na Marekani. Mgogoro wa hivi karibuni umeonyesha pengo kati ya matarajio na uhalisia, na changamoto kubwa ni jinsi ya kusawazisha utegemezi wao kwa Marekani huku wakijaribu pia kuimarisha njia mbadala za usalama.