Yıldırımhan: Lifahamu kombora la kwanza la masafa marefu la Uturuki

s

Chanzo cha picha, Cem Tekkeşinoğlu/Anadolu Ajansı/Getty Images

Maelezo ya picha, Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imeonesha kombora la kwanza la masafa marefu la nchi hiyo katika maonesho ya Saha-2026.
Muda wa kusoma: Dakika 3

Kituo cha Utafiti na Maendeleo cha Wizara ya Ulinzi ya Uturuki kimetambulisha kombora la kwanza la masafa marefu la nchi hiyo, linaloitwa "Yıldırımhan".

Kombora hilo lilioneshwa siku ya kwanza ya Maonesho ya Kimataifa ya Sekta ya ulinzi, anga na teknolojia ya anga za Juu ya Saha-2026 yaliyofanyika mjini Istanbul.

Katika sehemu kombora hilo, kuna picha ya Bayezid I, sultani wa Dola ya Ottoman anayejulikana kwa jina la "Yıldırım" likimaanisha "Radi".

Pia, saini ya Mustafa Kemal Atatürk inaweza kuonekana kwenye sehemu ya mbele ya kombora hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yaşar Güler, amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba kombora hilo ni silaha ya kwanza katika ghala la kijeshi la Uturuki kutumia mafuta ya roketi, na lina uwezo wa kuruka kwa kasi ya ajabu.

Pia alisema kuwa kombora la Yıldırımhan ndilo kombora lenye uwezo wa kufika umbali mrefu zaidi kuwahi kutengenezwa na taifa hilo.

Hata hivyo, taarifa chache za kiufundi zimewekwa wazi kuhusu kombora hilo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokuwa kwenye jedwali lililowekwa mbele ya mfano wa kombora uliooneshwa kwenye maonesho hayo, Yıldırımhan lina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 6,000.

Makombora ya balistiki katika ghala ya silaha ya Uturuki

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya ulinzi ya Uturuki imevutia dunia kupitia maendeleo ya silaha za masafa marefu, pamoja na ndege zisizo na rubani na mifumo ya kujitegemea.

Katika Maonesho ya Kimataifa ya Sekta ya Ulinzi yaliyofanyika mjini Istanbul mwezi Julai 2025, kombora la balistiki la Typhoon Block-4 lililotengenezwa na Roketsan lilioneshwa.

Kombora hilo lenye urefu wa mita 10 na uzito wa kilogramu 7,200 lilielezwa wakati huo kuwa "kombora la balistiki lenye uwezo wa kufika umbali mrefu zaidi lililotengenezwa kwa uwezo wa ndani wa Uturuki."

Kwa mujibu wa mtengenezaji, makombora mengine ya aina ya Typhoon yana uwezo wa kufika umbali wa takriban kilomita 280, huku toleo la Block-4 likikadiriwa kuwa na uwezo wa kufika kilomita 1,000.

Kombora la balistiki la masafa ya kati la "Genk", ambalo linaendelezwa na Roketsan, pia linatarajiwa kuwa na uwezo wa kufika umbali wa takribani kilomita 2,000.

Utengenezaji na usafirishaji wa makombora ya balistiki ya masafa marefu huathiriwa na vikwazo mbalimbali, baadhi yake vikiwa vinawekwa kupitia makubaliano ya kimataifa ambayo Uturuki imejiunga nayo.

Katika miaka ya karibuni, Urusi imetumia makombora ya balistiki ya masafa ya kati kushambulia maeneo nchini Ukraine.

Vilevile, Iran imefyatua makombora ya balistiki ya masafa ya kati na marefu kuelekea Israel.

Kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu, ili kuepuka vikwazo vinavyotokana na mikataba ya kimataifa, uwezo halisi wa makombora hayo mara nyingi hutajwa kuwa mdogo kuliko ulivyo kwa uhalisia.

Kombora la masafa marefu ni nini?(Intercontinental Ballistic Missile)

Makombora ya intercontinental ballistic missiles (ICBM) ni silaha zinazotengenezwa kushambulia maeneo ya umbali mkubwa sana.

Kila kombora linaweza kubeba vichwa almaarufu (warheads) kadhaa, na kila kichwa kina uwezo wa kuelekezwa kujitegemea na kupiga malengo tofauti.

Nchi kama Urusi, Marekani, na China zipo katika orodha ya juu ya wamiliki wa aina hii ya silaha.

Pia nchi kama Uingereza, Ufaransa, India, Korea Kaskazini, Israel, na Iran pia zinamiliki idadi ndogo ya makombora ya aina hii , ambayo hufyatuliwa kutoka ardhini au kwenye manowari.

Baadhi ya makombora haya yanaweza kubeba vichwa vya nyuklia, lakini pia yanaweza kutumika na vilipuzi vya kawaida.

Tofauti kuu kati ya makombora ya intercontinental na makombora ya kawaida ya balistiki ni umbali na kasi yake.

Makombora ya kawaida ya balistiki huwa na uwezo wa kilomita 300 hadi 5,500, wakati baadhi ya makombora ya intercontinental yanaweza kuzidi umbali wa kilomita 10,000.