Nani hufanya maamuzi nchini Iran?

Chanzo cha picha, EPA
Swali ambalo limekuwa likitawala Tehran tangu kuanza kwa mashambulizi katika mzozo wa sasa wa Iran dhidi ya Marekani na Israel ni hili: Nani hasa yuko madarakani?
Kwa macho rasmi jibu liko wazi. Mojtaba Khamenei alichukua nafasi ya kiongozi mkuu baada ya kuuawa kwa baba yake, Ali Khamenei, siku ya kwanza ya vita mnamo Februari 28. Katika mfumo wa nchi hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu, nafasi hiyo imeundwa kuwa ya mwisho katika kufanya maamuzi ikiwemo kuhusu vita, amani na mwelekeo wa kimkakati wa serikali.
Lakini kwa vitendo, hali halisi inaonekana kuwa tata zaidi.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameielezea uongozi wa Iran kuwa "umevunjika vipande vipande" na kusema Marekani inasubiri Tehran kuwasilisha "pendekezo lenye umoja."
Umoja huo ulionekana kuwa muhimu kwa viongozi wa Iran walipotuma ujumbe kwa wananchi kupitia simu zao wakisema:
"hakuna tena mgawanyiko wa wenye misimamo mikali au ya wastani, kuna taifa moja na njia moja."
Uongozi usioonekana
Mojtaba Khamenei hajaonekana hadharani tangu achukue madaraka. Mbali na matamko machache ya maandishi, ikiwemo msimamo wake kuwa Mlango wa Hormuz utaendelea kufungwa, hakuna ushahidi wa wazi kuhusu uongozi wake wa kila siku.
Maafisa wa Iran wamekiri kuwa alijeruhiwa katika mashambulizi ya awali, lakini hawajatoa maelezo ya kina. Gazeti la New York Times limeripoti kuwa huenda alipata majeraha kadhaa, ikiwemo ya usoni yaliyomfanya kushindwa kuzungumza vizuri.
Kutokuwepo kwake kuna athari kubwa. Katika mfumo wa Iran, nguvu haipo tu kwenye taasisi bali pia inaonekana kupitia uwepo na vitendo vya kiongozi.
Baba yake marehemu alikuwa akitoa mwelekeo kupitia hotuba, mikutano iliyopangwa na wapatanishi kati ya makundi tofauti. Sasa jukumu hilo linaonekana kukosekana.
Hali hii imeacha nafasi ya tafsiri tofauti. Wengine wanasema Mojtaba Khamenei hakupata muda wa kujenga nguvu zake kutokana na kuingia madarakani wakati wa vita. Wengine wanahoji kama hali yake ya kiafya inamruhusu kuongoza kikamilifu.
Kwa sasa, inaonekana maamuzi yanachukuliwa kwa upana zaidi ama kugawanyika zaidi kuliko hapo awali.
Diplomasia ipo, lakini yenye mipaka
Diplomasia ni jukumu la serikali. Waziri wa mambo ya nje Abbas Araghchi anaendelea kuiwakilisha Iran katika mazungumzo na Marekani, chini ya Rais Masoud Pezeshkian.
Hata hivyo, hakuna dalili kuwa wao ndio wanaopanga mkakati mkuu. Nguvu yao imepungua zaidi kutokana na ujumbe wa Iran kuongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad-Bagher Ghalibaf.
Nafasi ya Araghchi inaonekana kuwa ya utekelezaji tu. Kubadilika kwake kwa haraka kuhusu kufunguliwa au kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kunaonyesha jinsi diplomasia ilivyo na ushawishi mdogo katika maamuzi ya kijeshi.
Kwa upande wake, Rais Pezeshkian anaonekana kufuata mwelekeo uliopo bila kuunda mkakati wake binafsi.
Mazungumzo yaliyokwama kati ya Iran na Marekani yanaonyesha wazi kuwa hata diplomasia ikiwa wazi, maamuzi ya mwisho hayajaweza kufikiwa.
Jeshi limeongeza mamlaka yake
Udhibiti wa Mlango wa Hormuz ni moja ya silaha kuu ya Iran. Lakini uamuzi wa kuufunga uko mikononi mwa Jeshi la walinzi wa mapinduzi ya kiislamu (IRGC), linaloongozwa na Ahmad Vahidi.
Hii inaweka nguvu halisi kwa watu wanaofanya kazi nyuma ya pazia. Tofauti na zamani, hakuna mtu mmoja anayeonekana wazi kuwa msimamizi mkuu wa mkakati.
Kwa vitendo, IRGC inaonekana kuongoza mwelekeo wa mgogoro, iwe ni kufunga njia hiyo au kufanya mashambulizi katika Ghuba, huku majibu ya kisiasa na kidiplomasia yakifuata baadae.
Hii haimaanishi mfumo umevunjika, lakini inaonyesha kuwa jeshi limeongeza uhuru wake katika kufanya maamuzi.
Ghalibaf aibuka kwenye ombwe la uongozi

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mohammad-Bagher Ghalibaf, aliyewahi kuwa kamanda wa IRGC na sasa Spika wa Bunge, ameibuka kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa kwa sasa.
Amehusika kuratibu mazungumzo, kuzungumza na umma, na kutoa maelezo ya hali ya vita kwa mtazamo wa uhalisia zaidi kuliko ule wa kisiasa au kiitikadi.
Hata hivyo, msimamo wake ni hatari kisiasa. Anasema anatekeleza matakwa ya Khamenei, lakini hakuna ushahidi wa wazi wa mawasiliano ya moja kwa moja kati yao.
Katika mfumo unaotegemea ishara kutoka juu, hali hii ya kutokuwa na uwazi ina maana kubwa.
Kwa ujumla, mabadiliko haya yanaonyesha mfumo unaoendelea kufanya kazi, lakini bila uratibu ulio wazi na unaoeleweka. Kiongozi mkuu yupo, lakini haonekani. Rais yupo, lakini haongozi kikamilifu. Diplomasia ipo, lakini haina maamuzi ya mwisho.
Jeshi lina nguvu, lakini hakuna kiongozi mmoja anayeonekana wazi. Wanasiasa wanajitokeza, lakini hawana uhalali kamili.
Hii si dalili ya kuanguka kwa mfumo. Jamhuri ya Kiislamu bado ipo na inasimama.
Lakini inaonyesha changamoto kubwa zaidi, ugumu wa kubadili nguvu iliyonayo kuwa mkakati ulio wazi wakati wa shinikizo kubwa.
Kwa sasa, mfumo unaendelea kudumisha utulivu na kuzuia kuporomoka. Lakini swali linaongezeka: Je, umoja huo ni wa kweli au ni wa kuonekana tu?













