Moja kwa moja, Iran yatafakari pendekezo la Marekani kumaliza vita

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema Tehran bado inapitia pendekezo hilo na baadaye itawasilisha msimamo wake kupitia wapatanishi kutoka Pakistan.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu & Mariam Mjahid

  1. Iran inatarajiwa kujibu mapendekezo ya Marekani ya kumaliza vita leo - vyombo vya habari vya Marekani

    f

    Chanzo cha picha, Tasnim

    Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti, vikinukuu vyanzo, kwamba Iran inatarajiwa kutoa jibu lake kwa wapatanishi leo kuhusu pendekezo la Marekani la kumaliza vita.

    Televisheni ya CNN imenukuu chanzo kikiarifu kwamba pande za Marekani na Iran zinaelekea kufikia makubaliano ya kumaliza vita, huku Tehran ikichambua pendekezo lililotolewa na Marekani.

    Vyombo vya habari vya Iran pia vimeripotiwa kuarifiwa na vyanzo kwamba kwa sasa Iran inapitia upya mapendekezo ya Marekani kabla ya kuijulisha nchi mpatanishi, Pakistan.

    Shirika la habari la nusu rasmi la Iran, Tasnim, limesema vyanzo vya kuaminika vimeeleza kuwa Iran imeanza tena kulichambua suala hilo baada ya kile kilichoelezwa kama hatua ya kurudi nyuma kwa Rais wa Marekani Donald Trump, na itatoa taarifa kwa mpatanishi mara uamuzi utakapofikiwa.

    Vyanzo vinavyofahamu suala hilo vimeiambia The Guardian kwamba licha ya madai ya vyombo vya habari vya Marekani kuwa Iran na Marekani wako karibu kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita, Tehran bado haijajibu rasmi pendekezo la hivi karibuni la Washington, kwa kuwa lina vifungu vinavyochukuliwa kuwa visivyokubalika.

    Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kampeni ya propaganda inayofanywa na vyombo vya habari vya Marekani inalenga zaidi kuhalalisha hatua ya hivi karibuni ya Trump kujiondoa kwenye hatua za uhasama. Vimeongeza kuwa hatua hiyo ilikosewa tangu mwanzo na haikupaswa kuchukuliwa.

    Vimeendelea kueleza kuwa haijulikani ni mara ngapi Marekani italazimika kugonga ukuta ili kuelewa hali halisi ilivyo ardhini, vikisisitiza kuwa uzoefu unapaswa kuwa umefundisha Marekani kwamba lugha ya nguvu na vitisho si tu haifanyi kazi dhidi ya Iran bali pia huzidisha hali kuwa mbaya kwa Marekani na maadui wake wengine.

    Vyanzo hivyo vimefafanua kuwa baada ya Iran kuwasilisha pendekezo lake la vipengele 14 lililoelezwa kuwa la busara na lenye mantiki kupitia mpatanishi wa Pakistan, Marekani ilijibu kwa pendekezo lake, lakini mara moja baadaye ilianza hatua mpya ya kile kilichoelezwa kama ubabe na uhasama.

    Vimesema kuwa Iran ilikuwa inaendelea kulichambua jibu lake, lakini Marekani ilichukua tena mkondo usio wa busara, jambo lililosababisha kusitishwa kwa mchakato wa mapitio.

    Mohsen Rezaei, aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi na mshauri wa kiongozi mpya wa Iran, amesema Iran “haitafanya mazungumzo na mtu yeyote kuhusu suala la nyuklia” na kwamba udhibiti wa Mlango wa Hormuz unapaswa kubaki mikononi mwa Iran.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa la Iran ISNA, Rezaei ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Umma la Nia ya Iran ameonya kuwa iwapo udhibiti na usimamizi wa Mlango wa Hormuz utatoka mikononi mwa Iran, adui atautumia tena kama silaha dhidi ya Iran na wananchi wake.

    Soma zaidi:

  2. Jaji wa Marekani aidhinisha kufichuliwa kwa barua inayodaiwa kuwa ya kujiua ya Jeffrey Epstein

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Onyo: habari hii ina maudhui ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuyapata kuwa ya kushtua

    Jaji wa Marekani ameamuru kufichuliwa kwa hati inayodaiwa kuwa barua ya kujiua iliyoandikwa na mhalifu wa ngono aliyepatikana na hatia, Jeffrey Epstein, mwezi mmoja kabla ya kifo chake.

    Nakala ya barua hiyo iliyoandikwa kwa mkono na kufunguliwa hadharani Jumatano inataja uchunguzi uliodumu kwa miezi kadhaa ambao “haukupata chochote”, na inaeleza kuwa “ni jambo la kufurahisha kuwa na uwezo wa kuchagua muda wa kuaga dunia.”

    Aliyekuwa mfungwa mwenzake wa Epstein anadai aliipata barua hiyo ikiwa imewekwa ndani ya kitabu baada ya Epstein kujaribu kujiua Julai 2019. Epstein alikutwa amekufa katika seli yake mwezi mmoja baadaye.

    BBC haijathibitisha kama barua hiyo iliandikwa na Epstein, na mamlaka za Marekani hazijatoa maoni yoyote.

    Kifo chake, ambacho kilitangazwa kuwa ni kujiua na mamlaka, kilitokea akiwa anasubiri kesi ya ulanguzi wa ngono.

    Barua hiyo inayodaiwa iliwekwa chini ya ulinzi wa mahakama kama sehemu ya kesi za jinai zinazomhusisha aliyekuwa mfungwa mwenzake, Nicholas Tartaglione, ambaye wakati huo alikuwa akizuiliwa gerezani akisubiri kesi ya mauaji manne.

    Tartaglione, aliyekuwa afisa wa polisi na aliyepatikana na hatia ya mauaji ya watu wanne, wakati fulani alishutumiwa na Epstein kumshambulia, jambo alilolikanusha. Aliwahi kutaja kuwepo kwa barua hiyo mwaka jana katika kipindi cha podikasti.

    Soma zaidi:

  3. Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Marekani awasili Vatican kukutana na Papa Leo

    d

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio amesafiri hadi Vatican leo Alhamisi Mei 7 kukutana na Papa Leo wa Kumi na Nne, kiongozi wa Wakatoliki duniani.

    Ziara hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani imekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumkosoa vikali Papa kutokana na misimamo yake dhidi ya vita.

    Shirika la habari la AFP, likiripoti kuhusu kuwasili kwa Rubio Vatican, limesema kuwa Rubio ambaye amejitambulisha kuwa Mkatoliki mwenye imani thabiti, alijaribu kupunguza tofauti zilizopo kati ya Trump na Vatican kabla ya mkutano huo wa faragha.

    Katika muendelezo wa ziara yake, Rubio amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Jimbo la Vatican.

    Balozi wa Marekani katika Vatican alikuwa amesema awali kuwa mkutano huo ungetarajiwa kuwa na mazungumzo ya wazi na ya moja kwa moja.

    Kardinali Pietro Parolin aliwaambia waandishi wa habari Vatican jana kuwa watasikiliza kile ambacho mgeni wao atakisema, akibainisha kuwa mkutano huo umefanyika kwa ombi la Washington.

    Soma zaidi:

  4. Rais wa Iran asema amekutana na Mojtaba Khamenei

    g

    Chanzo cha picha, IRNA

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametangaza kuwa amefanya mkutano na Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu, Mojtaba Khamenei.

    Akizungumza Alhamisi Mei 7, Pezeshkian hakutaja tarehe ya mkutano huo lakini amesema mkutano ulidumu kwa “saa mbili na nusu.”

    Katika kile alichokitaja kuwa mkutano “usio rasmi” na wawakilishi wa wafanyabiashara na vyama vya sekta mbalimbali katika Wizara ya Viwanda mjini Tehran, Pezeshkian alisema jambo lililomgusa zaidi ni “namna ya mazungumzo, mtazamo na unyenyekevu pamoja na uaminifu mkubwa” aliouona kutoka kwa Mojtaba Khamenei.

    “Mtazamo huo uliibadili hali ya mazungumzo na kuwa mazingira ya kuaminiana, utulivu, uelewano na mazungumzo ya moja kwa moja,” alisema.

    Wiki moja baada ya kuuawa kwa Ali Khamenei katika mashambulizi ya Marekani na Israel, mwanawe Mojtaba Khamenei alitangazwa kuwa kiongozi wa tatu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Tangu mashambulizi hayo dhidi ya makazi ya kiongozi mkuu, hakuna sauti wala video ya Mojtaba Khamenei iliyotolewa hadharani, huku vyombo vya habari vya Iran vikichapisha ujumbe wa maandishi pekee unaodaiwa kutoka kwake.

    Baadhi ya ripoti pia zimeeleza kuwa huenda alijeruhiwa katika shambulio hilo.

    Haijafahamika iwapo huu ulikuwa mkutano wa kwanza kati ya Pezeshkian na Mojtaba Khamenei tangu ateuliwe kuwa kiongozi wa Iran.

    Soma zaidi:

  5. Idadi ya Wakenya wanaopigana katika jeshi la Urusi yafikia 291 huku 19 wakifariki vitani

    Clinton Mogesa alisajiliwa akiwa Qatar

    Chanzo cha picha, Ukraine Defence Intelligence Maelezo ya picha,

    Maelezo ya picha, Clinton Mogesa alisajiliwa akiwa Qatar

    Idadi ya Wakenya waliothibitishwa kujiunga na jeshi la Urusi imefikia 291, huku serikali ya Kenya ikionya kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka kutokana na baadhi yao kusafiri bila kuarifu mamlaka.

    Akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Leba na Ustawi wa Jamii Alhamisi, Musalia Mudavadi amesema takwimu hizo zimeongezeka kutoka 252 alizowasilisha katika Bunge la Taifa Aprili 1.

    Kwa mujibu wa serikali, Wakenya 53 tayari wamerejeshwa nchini, 19 wanaaminika kufariki vitani huku wengine 42 wakiripotiwa kutoweka. Wawili wanashikiliwa nchini Ukraine kama wafungwa wa vita.

    Serikali pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu Wakenya wanaosafiri kuelekea Urusi kupitia njia zisizo rasmi, ikiwemo kupitia mataifa ya Afrika Kaskazini.

    Maseneta wameitaka serikali kueleza hatua zinazochukuliwa kuwaokoa Wakenya waliokwama katika maeneo ya vita, lakini Mudavadi alisema mazingira ya mapigano ni hatari hata kwa maafisa wa serikali.

    “Ni eneo la vita, droni zinaruka kila mahali. Huwezi kumtuma balozi kwenda mstari wa mbele,” amesema.

    Mnamo Machi, Mudavadi alifanya ziara mjini Moscow kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, ambapo pande hizo mbili zilikubaliana kuwaondoa Wakenya katika huduma ya kijeshi ya Urusi.

    Aidha, serikali ya Kenya imesema inaandaa sheria mpya za kudhibiti uhamiaji haramu na kuziba mianya inayotumiwa kuwasafirisha vijana kwenda maeneo hatari.

    “Serikali imetoa msamaha kwa Wakenya kurejea nyumbani, lakini hatua hiyo haitadumu kwa muda mrefu,” Mudavadi ameonya.

    Mbali na Urusi, serikali ya Kenya imezitaja Golden Triangle ya Kusini Mashariki mwa Asia, njia ya Afrika Kaskazini na mataifa ya Ghuba kuwa maeneo hatari kwa Wakenya wanaotafuta kazi kupitia njia zisizo rasmi.

    Soma zaidi:

  6. Wanawake wenye uhusiano na Islamic State warejea Australia

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanawake 13 na watoto wenye uhusiano na kundi la Islamic State (IS) wamewasili nchini Australia baada ya kuishi kwa miaka kadhaa kizuizini nchini Syria.

    Kundi hilo, ambalo lilikuwa linaishi katika kambi ya al-Roj tangu mwaka 2019, limekuwa likizua mjadala mkali wa kisiasa nchini Australia, huku serikali ikisema haitatoa msaada wowote kwao kurejea nchini humo.

    Wanawake watatu pamoja na watoto wanane wanaoaminika kuwa wa familia moja waliwasili mjini Melbourne Alhamisi.

    Mwanamke mwingine pamoja na mtoto wake waliwasili muda mfupi baadaye mjini Sydney.

    Polisi wamesema baadhi ya wanawake hao watakamatwa na kufunguliwa mashtaka mara baada ya kuwasili, huku wengine wakiendelea kuchunguzwa na vyombo vya usalama.

    Kundi lililowasili Melbourne walifahamika kama Kawsar Abbas pamoja na mabinti zake Zeinab na Zahra Ahmed, na watoto wao wanane.

    Abbas ameolewa na Mohammad Ahmad ambaye alikuwa akiendesha shirika la misaada ambalo polisi wa Australia wanashuku lilitumika kutuma fedha kwa kundi la IS.

    Ahmad alikanusha tuhuma hizo katika mahojiano na shirika la utangazaji la Australia ABC mwaka 2019, baada ya kupatikana akiwa gerezani nchini Syria.

    Soma zaidi:

  7. Watu 3 waokolewa baada ya mlipuko wa Hantavirus kwenye meli ya kitalii

    g

    Watu watatu wameokolewa kutoka kwenye meli ya kitalii ya MV Hondius baada ya kuzuka kwa mlipuko wa virusi hatari vya hantavirus wakati meli hiyo ikielekea Visiwa vya Canary nchini Hispania.

    Kampuni ya Oceanwide Expeditions imesema watu wawili waliokuwa katika hali mahututi tayari wamewasili nchini Uholanzi kwa ajili ya kupatiwa matibabu maalumu.

    Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mtu wa tatu aliyekuwa katika hali ya kawaida alikuwa akisafirishwa kwa ndege ya uokoaji ambayo ilichelewa kuondoka.

    Meli hiyo ilisimama kwa siku tatu karibu na Cape Verde, taifa la visiwa lililopo katika pwani ya Afrika Magharibi, kabla ya kuendelea na safari yake kuelekea Canary.

    Waliookolewa ni raia wa Uingereza, Uholanzi na Ujerumani.

    Kampuni hiyo imeeleza kuwa mwanaume Mjerumani mwenye umri wa miaka 65 alikuwa na uhusiano wa karibu na mwanamke Mjerumani aliyefariki dunia ndani ya meli hiyo tarehe 2 Mei kutokana na maambukizi yanayohusishwa na virusi hivyo, Hantavirus.

    Raia wa Uingereza aliyeokolewa ametajwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa ni Martin Anstee, mwenye umri wa miaka 56 na aliyewahi kuwa askari polisi. Inadaiwa kuwa yuko katika hali tulivu nchini Uholanzi.

    Aidha, mfanyakazi wa meli kutoka Uholanzi mwenye umri wa miaka 41 naye ni miongoni mwa waliohamishwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

    Soma zaidi:

  8. Kamanda mwandamizi wa Hezbollah auawa katika mashambulizi ya Israel mjini Beirut

    f

    Chanzo cha picha, Social Media

    Chanzo kilicho karibu na Hezbollah kimeiambia AFP kuwa mmoja wa makamanda wakuu wa kundi hilo ameuawa katika shambulio la Israel lililolenga viunga vya kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon, jana.

    Hili ni shambulio la kwanza la Israel dhidi ya Beirut tangu kutangazwa kwa usitishaji mapigano Aprili 16.

    Chanzo hicho kimemtaja kamanda aliyeuawa kuwa Malik Balout na kusema alikuwa kamanda wa operesheni wa kikosi maalum cha Ridwan cha Hezbollah.

    Ripoti ambazo bado hazijathibitishwa pia zinaeleza kuwa shambulio hilo lililenga nyumba moja ambapo viongozi wa kikosi hicho walikuwa wakikutana.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia amesema kuwa aliyelengwa katika shambulio hilo alikuwa kamanda wa kikosi cha Radwan cha Hezbollah.

    Soma zaidi:

  9. Iran yakana kuishambulia meli ya Korea Kusini huko Hormuz

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imekanusha kuhusika kwa namna yoyote na mlipuko pamoja na moto uliotokea kwenye meli ya mizigo ya South Korea katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, inayodaiwa kushambuliwa.

    Kupitia taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Iran mjini Seoul, Tehran ilisema “inakataa kabisa madai yoyote” yanayohusisha vikosi vya kijeshi vya Iran na tukio hilo.

    Siku tatu zilizopita, meli hiyo ya Korea Kusini ililipuka na kushika moto katika Ghuba ya Uajemi, lakini hakuna watu waliofariki au kujeruhiwa katika tukio hilo.

    Kwa mujibu wa Reuters, mshauri wa usalama wa taifa wa Korea Kusini, Lee Song-hock, amesema bado haijafahamika kama mlipuko huo ulisababishwa na shambulio au hitilafu nyingine.

  10. Israel iko tayari kwa lolote kuhusu Iran- Netanyahu

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa Israel iko “tayari kwa kila hali” kuhusiana na Iran, kufuatia kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump kuashiria uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa makubaliano na Tehran, huku pia akitishia kurejea kwa mashambulizi.

    Akizungumza mwanzoni mwa mkutano wa Baraza la Usalama wa Israel, Netanyahu alisema amevielekeza vikosi vya jeshi na vyombo vya usalama kuwa tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza.

    “Tumekuwa tayari kwa kila hali, na hayo ndiyo maelekezo niliyoyatoa kwa jeshi na vyombo vyetu vya usalama,” alisema Netanyahu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

  11. Bei ya mafuta yashuka soko la dunia, kufuatia taarifa za kukaribia kwa makubaliano ya Marekani na Iran

    v

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bei ya mafuta duniani imeshuka katika saa 24 zilizopita huku masoko ya hisa yakipanda baada ya taarifa kuwa Marekani na Iran wako karibu kufikia makubaliano ya kumaliza vita vinavyoendelea.

    Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ilishuka hadi dola 97 kwa pipa kabla ya kupanda tena juu ya dola 101, kutoka zaidi ya dola 108 mapema katika kipindi hicho. Wakati huohuo, masoko makubwa ya hisa Ulaya na Asia yalimaliza siku ya jana kwa mafanikio makubwa.

    Mabadiliko hayo yamechochewa na ripoti kwamba Marekani inaamini ipo karibu kufikia makubaliano ya awali na Iran yatakayofungua njia ya mazungumzo mapya kuhusu nyuklia na kumaliza vita.

    Hata hivyo, Iran imesema bado inatafakari pendekezo hilo, huku Rais wa Marekani Donald Trump akionya kuwa kushindwa kufikiwa kwa makubaliano kutasababisha mashambulizi “makubwa zaidi” dhidi ya Tehran.

    Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vimeathiri kwa kiasi kikubwa biashara ya mafuta duniani, hasa baada ya Iran kutishia kushambulia meli zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia inayopitisha karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi duniani.

  12. Trump atishia ‘kuishambulia’ upya Iran isipokubali mapendekezo ya amani

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Iran kuwa itakabiliwa na mashambulizi mapya na makali zaidi endapo haitakubali mapendekezo ya amani yanayojadiliwa kati ya pande hizo mbili.

    Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema Marekani ilisimamisha kwa muda operesheni yake ya kijeshi katika Mlango wa Hormuz ili kutoa nafasi kwa juhudi za kidiplomasia, lakini akaonya kuwa mashambulizi yatarejea kwa “nguvu na kiwango kikubwa zaidi” ikiwa makubaliano hayatapatikana.

    Kauli hiyo imekuja wakati Iran ikisema bado inatafakari pendekezo la Marekani lenye masuala 14, yanayolenga kumaliza vita pamoja na mvutano wa miezi miwili kuhusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za Marekani, pendekezo hilo linajumuisha kusitishwa kwa urutubishaji wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo na kurejeshwa kwa usafiri wa meli katika njia hiyo muhimu ya biashara ya mafuta duniani.

    Hata hivyo, Trump amesema bado ni mapema kwa mazungumzo mapya ya moja kwa moja licha ya kile alichokiita “maendeleo makubwa” katika majadiliano ya siku za karibuni.

  13. PSG kukutana na Arsenal Budapest fainali ya Ulaya

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Paris Saint-Germain (PSG) imefuzu fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya, baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Ujerumani.

    PSG ilianza kwa kasi baada ya Ousmane Dembélé kufunga bao la mapema dakika ya tatu akimalizia pasi ya Khvicha Kvaratskhelia. Bayern walipata bao la kusawazisha kupitia Harry Kane katika dakika za mwisho, lakini halikutosha kuipeleka mechi muda wa nyongeza.

    Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Paris, PSG iliibuka na ushindi wa mabao 5-4, matokeo yaliyoisaidia kutinga hatua ya mwisho kwa jumla ya mabao 6-5.

    Kwa upande mwingine, Arsenal ilifuzu fainali hiyo baada ya kuiondoa Atlético Madrid kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1, ikifika fainali hiyo kwa mara ya pili katika historia ya klabu hiyo tangu mwaka 2006.

    Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2025/2026 itachezwa Mei 30 katika Puskás Aréna nchini Hungary, ambapo PSG na Arsenal zitachuana kuwania taji kubwa zaidi la klabu barani Ulaya.

    Mwaka jana PSG iliiondosha Arsenal katika hatua ya nusu fainali ya mchuano hiyo.

  14. Meli ya kitalii iliyokuwa na wagonjwa wa Hantavirus yaondoka Cape Verde

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meli ya kitalii ya Uholanzi, MV Hondius, imeondoka nchini Cape Verde kuelekea Visiwa vya Canary baada ya watu watatu waliokuwa ndani yake kuhamishwa kwa matibabu kufuatia mlipuko wa virusi vya hantavirus.

    Waliohamishwa ni raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 56, mfanyakazi wa meli kutoka Uholanzi mwenye miaka 41 na raia wa Ujerumani mwenye miaka 65. Wawili kati yao tayari wamewasili hospitalini nchini Uholanzi huku mmoja akichelewa kutokana na matatizo ya safari ya ndege.

    Tangu meli hiyo iondoke Argentina mwezi mmoja uliopita, watu watatu waliokuwa ndani yake wamefariki dunia. Maafisa wamesema mmoja wa waliofariki alithibitika kuwa na hantavirus huku uchunguzi ukiendelea kwa vifo vingine viwili.

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema hadi sasa visa nane vimegunduliwa miongoni mwa waliokuwa ndani ya meli hiyo, tatu vikiwa vimethibitishwa rasmi na vitano vikihisiwa. Wataalamu wanaamini maambukizi hayo yanaweza kuwa yalisambazwa kupitia muingiliano wa karibu wa watu.

    Hata hivyo, mamlaka za afya zimesema hatari ya maambukizi kwa umma bado ni ndogo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini iwapo watu wengine waliokuwa ndani ya meli hiyo wameambukizwa virusi hivyo.

  15. Iran yatafakari pendekezo la Marekani kumaliza vita

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imesema bado inatafakari pendekezo la Marekani la kumaliza vita vinavyoendelea, huku taarifa zikidai kuwa pande hizo mbili zinaweza kuwa karibu kufikia makubaliano mapya ya amani.

    Kwa mujibu wa ripoti ya Axios, Ikulu ya Marekani inaamini inaweza kufikia makubaliano ya vipengele 14 na Iran, ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa urutubishaji wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa vikwazo na kurejeshwa kwa usafiri huru katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema Tehran bado inapitia pendekezo hilo na baadaye itawasilisha msimamo wake kupitia wapatanishi kutoka Pakistan.

    Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Iran wameonyesha msimamo mkali, wakisema Marekani haitapata kupitia vita kile ambacho imeshindwa kupata kupitia mazungumzo ya moja kwa moja, huku wakionya kuwa Iran iko tayari kujibu mashambulizi yoyote mapya.

    Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump amesema mazungumzo ya saa 24 zilizopita yamekuwa mazuri na kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano, huku akisisitiza kuwa Iran haitaruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia.

  16. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Mei 07, 2026