Moja kwa moja, Marekani na Iran zarushiana makombora, Trump asema usitishaji wa vita unaendelea

Iran imedai kushambulia meli za kijeshi za Marekani karibu na bandari ya Chabahar kujibu mashambulizi ya Marekani dhdi ya meli zake mbili karibu na Mlango bahari wa Hormuz pamoja na maeneo ya raia katika kisiwa cha Qeshm na pwani ya kusini mwa Iran.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Tshisekedi adokeza kuongeza muhula wa tatu wa urais DRC

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amesema anaweza kuwania muhula wa tatu wa urais baada ya muda wake wa sasa kumalizika mwaka 2028 ikiwa wananchi wataridhia kupitia kura ya maoni. Katiba ya nchi hiyo kwa sasa inaruhusu mihula miwili pekee ya urais.

    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Tshisekedi alisema hajataka muhula wa tatu moja kwa moja, lakini yuko tayari kuendelea kuongoza ikiwa wananchi watamhitaji. Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa nchini humo huku upinzani ukihofia jaribio la kubadili katiba ili kuongeza muda wa utawala wake.

    Rais huyo pia amesema uchaguzi mkuu wa mwaka 2028 unaweza usifanyike kwa wakati kutokana na hali mbaya ya usalama mashariki mwa nchi. Waasi wa M23 wameendelea kudhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, yakiwemo miji muhimu ya Goma na Bukavu.

    Tshisekedi ameilaumu Rwanda kwa kuchelewesha juhudi za amani na kunufaika na rasilimali za madini kutoka DR Congo. Rwanda imeendelea kukanusha kuunga mkono waasi wa M23 licha ya madai na ushahidi kutoka mataifa mbalimbali.

    Kauli za Tshisekedi zimekuja wakati muswada wa kuruhusu kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba ukiendelea kujadiliwa bungeni. Upinzani umeonya kuwa jaribio lolote la kubadili ukomo wa mihula ya urais litakuwa “mapinduzi ya kikatiba” yenye lengo la kumweka madarakani Tshisekedi kwa muda mrefu zaidi.

  2. China yawahukumu vifo Mawaziri wake wawili wa zamani wa Ulinzi kwa rushwa

    sd

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri wa ulinzi wa zamani wa China Wei Fenghe (kulia), wakati huo akiwa kwenye majukumu yake

    Mahakama ya kijeshi nchini China imewahukumu kifo mawaziri wawili wa zamani wa ulinzi baada ya kupatikana na hatia ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Hukumu hiyo ilitangazwa Alhamisi kupitia vyombo vya habari vya serikali ya China.

    Mawaziri hao ni Wei Fenghe na Li Shangfu, ambao walifikishwa katika mahakama ya kijeshi na kuhukumiwa kifo huku adhabu hiyo ikisitishwa kwa miaka miwili. Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, baada ya kipindi hicho hukumu zao zitabadilishwa kuwa kifungo cha maisha bila nafasi ya msamaha au kupunguziwa adhabu.

    Mahakama ilisema viongozi hao walipokea kiasi kikubwa cha rushwa na kutumia nyadhifa zao kujinufaisha binafsi pamoja na kuwapa wengine upendeleo usio halali. Mali zote binafsi za wawili hao pia zimechukuliwa na serikali.

    Li Shangfu alikuwa Waziri wa Ulinzi kuanzia Machi 2023 kabla ya kuondolewa madarakani Oktoba mwaka huo baada ya kutoweka hadharani kwa muda mfupi. Naye Wei Fenghe alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia 2018 hadi 2023 kabla ya kurithiwa na Li.

    Hukumu hizo zinatajwa kuwa sehemu ya kampeni kubwa ya kupambana na rushwa inayoendeshwa na Rais Xi Jinping ndani ya jeshi na serikali ya China. Hata hivyo, wakosoaji wa serikali wanasema kampeni hiyo pia hutumika kuwaondoa wapinzani wa kisiasa wa rais huyo.

  3. Marekani na Iran zarushiana makombora, Trump asema usitishaji wa vita unaendelea

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mvutano kati ya Marekani na Iran umeongezeka tena baada ya pande hizo mbili kurushiana mashambulizi saa 24 zilizopita, katika tukio linalotajwa kuwa jaribio kubwa zaidi kwa sitisho la vita lililodumu kwa mwezi mmoja.

    Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema makubaliano ya kusitisha mapigano bado yanaendelea.

    Iran ilidai kuwa Marekani ilishambulia meli mbili karibu na Mlango wa Hormuz pamoja na maeneo ya raia katika kisiwa cha Qeshm na pwani ya kusini mwa Iran. Jeshi la Iran limesema lilijibu kwa kushambulia meli za kijeshi za Marekani karibu na bandari ya Chabahar.

    Kwa upande wake, Jeshi la Marekani (CENTCOM) limesema lilifanya mashambulizi ya kujibu baada ya Iran kutumia makombora, droni na boti ndogo kushambulia manowari tatu za Marekani. Marekani imesema hakuna meli zake zilizoharibiwa na kwamba haitaki kuongeza mzozo huo.

    Akizungumza mjini Washington, Trump alipunguza uzito wa tukio hilo akisema, “Walitujaribu leo, nasi tukawajibu vikali,” huku akisisitiza kuwa sitisho la vita bado lipo. Marekani pia ilikuwa ikisubiri majibu ya Iran kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano bila kutatua moja kwa moja suala la mpango wa nyuklia wa Iran.

    Baada ya saa kadhaa za mashambulizi, televisheni ya taifa ya Iran iliripoti kuwa hali imerejea kawaida katika visiwa na miji ya pwani karibu na Mlango wa Hormuz, huku Iran ikionya kuwa itajibu kwa nguvu mashambulizi yoyote yajayo.