Jinsi utawala wa Iran ulivyoimarika kutokana na vita na Marekani

Chanzo cha picha, EPA
Bado wapo, popote uendapo, televisheni yoyote utakayowasha, unachokiona ni sura za viongozi waliouawa nchini Iran, pamoja na wale wapya waliowekwa, picha zao zikijaa maeneo ya umma.
Maandamano yameisha, vita vimekuja na kuondoka, na sasa ni wakati wa kusitisha mapigano, lakini serikali ya Kiislamu ya Iran bado iko imara.
Kwa mujibu wa baadhi ya Wairani nchini humo waliozungumza na BBC, badala ya kuuangusha utawala wa Kiislamu, vita hivyo vimeuimarisha, na sasa uko katika hali ya kuwakandamiza wale wanaoipinga.
Sana na Diako - sio majina yao halisi - ni wanandoa wachanga wanaoishi Tehran, mji mkuu wa nchi hiyo.
Ni wanandoa waliosoma na wenye kipato cha kati, wanaotarajia kuona mwisho wa serikali yenye msimamo mkali.
Ili kusimulia hadithi zao, tuliondoa baadhi ya taarifa zinazowatambulisha kwenye simulizi hii ili kuwalinda.
Mwandishi wa habari ambaye anasaidia BBC kutunga simulizi hii alikutana na Sana na Diako karibu na eneo la burudani, ambapo familia huja na watoto wao, hasa wakati huu wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Diako anatumai kuwa maisha yataboreka. "Mambo yatabadilika, tuko tayari kwa mabadiliko," alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sana alicheka huku akieleza haya.
"Badilisha?" Aliuliza kwa mshangao. "Nchi inaangukia mikononi mwa majeshi ya mapinduzi, unaongelea mabadiliko. Nchi iko kwenye machafuko." Sana alieleza jinsi alivyohisi baada ya Marekani na Israel kuanza kuishambulia Iran.
"Mwanzoni sikutaka vita kutokea... [lakini] ilipoanza na viongozi wa serikali walikuwa wakiuawa, nilianza kufurahia," alisema.
Lakini vita vilipoendelea, matumaini ya Sana yalianza kufifia, kama yalivyokuwa kwa Ikulu ya White House, kwa sababu mauaji ya Kiongozi Mkuu wa nchi, Ayatollah Ali Khamenei, na vigogo wengine wa serikali haykuleta mabadiliko mapya ya serikali.
"Kwa sababu watu wa serikali bado wapo madarakani. Nilichotarajia hakijatokea. Kila kitu kilianguka. Na tukabaki na serikali ya Kiislamu. Nimehuzunishwa sana na ushindi wao katika vita."
Dola ya Kiislamu ina msingi mkubwa wa uungaji mkono nchini humo.
Mikutano ya kuunga mkono serikali ni ya kawaida kote Iran, wakati mikutano ya kupinga serikali imepigwa marufuku.
Vyanzo vyetu vilizungumza na wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu, wanasheria, na waandishi wa habari wa kujitegemea, ambao walionyesha kutoridhishwa kwao na serikali.
Pia kuna hofu kwamba iwapo vita hivyo vitamalizika, serikali itapanua kampeni yake ya ukandamizaji dhidi ya raia walioipinga hasa wakati wa vita.
Shirika la Human Rights Watch (HRANA) lenye makao yake makuu nchini Marekani lilisema zaidi ya watu 53,000 walikamatwa wakati wa maandamano dhidi ya serikali Januari iliyopita, na kabla ya kuzuka kwa vita.
Na tangu kuanza kwa vita hivyo, maelfu ya wengine wanaaminika kukamatwa na kuwekwa kizuizini.
Pia kuna ripoti kwamba angalau wafungwa 21 wa kisiasa waliuawa kwa kunyongwa wakati wa vita, idadi kubwa zaidi katika muda mfupi katika zaidi ya miaka 30.

Chanzo cha picha, Reuters
Tisa kati ya waliouawa walihusishwa na maandamano ya Januari, 10 walituhumiwa kuwa wanachama wa makundi yanayoipinga serikali, huku wawili wakituhumiwa kwa ujasusi.
Susan - ambaye jina lake limebadilishwa - wakili anayefanya kazi na wafungwa, alisema hali ambayo watu wanazuiliwa ni mbaya sana.
"Kabla ya vita, wale walioongoza maandamano na wale waliokuwa na silaha waliteswa. Lakini wakati wa vita, kila mtu aliyekuwa kizuizini aliteswa," alieleza.
Hadithi yake inaonyesha jinsi vita ilivyosambaratisha familia. Wazazi wake walikuwa waaminifu kwa serikali, na aliogopa kwamba wangekabili matatizo ikiwa serikali ingepinduliwa.
Alipoelezea hofu yake kwa kaka yake - ambaye pia alikuwa mpinzani wa serikali - alionekana kutojali.
"Kwa kuwa wanataka kuwa wafia dini, nani atawazuia?"
Susan anatumaini kwamba vita vitaisha, lakini anahofu kwamba watu kama yeye watakabiliwa na mkazo mbaya sana.
Na anaogopa hatima ya watu kuwa mateka. "Nadhani vita vitakapokwisha, kuna uwezekano kwamba serikali itaondoa hasira zake kwa wale inaowashikilia. Ninahisi kama wakati unasonga."

Chanzo cha picha, EPA
Wanaharakati wa haki za binadamu wanaripoti kuwa watu wanne wameuawa kufikia sasa mwaka huu, wakishutumiwa kuwa na uhusiano na shirika la kijasusi la Israel, Mossad.
Waandishi wa habari wa kujitegemea ni miongoni mwa wale wanaohofia kukamatwa kwa tuhuma za kusaidia Marekani au Israel.
Kuna taarifa za kukamatwa kwa watu kadhaa wanaodaiwa kutuma habari kwenye vyombo vya habari vya nje zinazoonekana kuwa na madhara kwa nchi.
Mmoja wa waandishi wa habari - tutamwita Armin - ambaye alizungumza na mwenzetu huko Tehran, alielezea jinsi kuripoti kwa uaminifu juu ya vita kulivyosababisha kukamatwa kwake.
"Kwanza kabisa, tunashutumiwa kwa uhalifu wa kisiasa. Lakini katika hali hii ya vita, tukiripoti, tunaweza kutuhumiwa kwa uhaini."
Jinai ya uhaini inaweza kubeba hukumu ya kifungo cha maisha katika mahakama chini ya serikali ya Iran.
"Zamani tulikuwa tunajaribu kujua ni watu wangapi wamejeruhiwa au madhara yaliyotokana na maandamano hayo, lakini sasa suala limebadilika, sasa tumejikita katika kubaki hai, sisi wenyewe na familia zetu," alisema Armin.
Wakati familia yake inajaribu kulala, Armin hawezi kulala.
"Mara nyingi mimi hulala nimeketi, nikijiuliza juu ya maisha yetu ya baadaye, na kutokuwa na uhakika husababisha wasiwasi."
Jambo la kushangaza ni kwamba upinzani dhidi ya serikali umetoweka katika mitaa ya nchi. Serikali imekuwa kisu na nyama, inaua imtakaye na kumuacha imtakaye.












