Kwa nini Serikali ya Tanzania kutaka kukopa BoT kumeibua mjadala?

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Pendekezo la kuiruhusu Serikali kukopa moja kwa moja kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa dharura limezua mjadala mkubwa miongoni mwa wachumi, wanasiasa na wadau wa sera za umma.

Mabadiliko hayo yamo katika marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, ambapo Serikali inataka BoT iweze kutoa mikopo ya muda mfupi pale kunapotokea upungufu wa mapato au dharura inayohitaji fedha za haraka.

Kifungu hicho kinasema "kwa kuzingatia vifungu vya 34,35 na 37, benki hiyo inaweza kuipa Serikali mkopo wa muda mfupi pale tutakapotokea tukio lisilotarajiwa au lisiloepukika linalosababisha upungufu wa muda wa mapato ya serikali".

Kwa mtazamo wa Serikali, kifungu hicho kinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kukabiliana na misukosuko ya kifedha bila kusubiri taratibu ndefu za kukopa kutoka masoko ya fedha au taasisi nyingine.

Lakini kwa wakosoaji wake, hoja si kuhusu uwepo wa mkopo huo pekee. Wanasema swali kubwa ni nani atakayeamua kuwa kuna dharura, ni mipaka gani itawekwa, na ni kwa kiwango gani Benki Kuu itaendelea kuwa huru katika kusimamia sera za fedha ikiwa pia itakuwa mkopeshaji wa Serikali.

Hofu ni nini hasa?

.

Chanzo cha picha, URT

Maelezo ya picha, Waziri wa Fedha Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar

Miongoni mwa waliokosoa kifungu hicho ni wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole, ambaye ameonyesha wasiwasi kuhusu uwajibikaji wa kutosha katika mfumo huo.

"Hakuna njia za kisheria za kurejesha fedha hizo. Hii ni njia nyingine ya kupora nchi. Ni kama Abdallah anakopa kutoka kwa Dullah."

Ingawa kauli hiyo imezua mjadala wake, msingi wa hoja unaotolewa na wakosoaji wengi ni kwamba Serikali na Benki Kuu (BoT), ni taasisi zinazohusiana kwa karibu, jambo linaloweza kuzua maswali kuhusu usimamizi wa mikopo hiyo na namna ya kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa upande mwingine, wachumi wanaonya kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kwa mfumuko wa bei. Kwa kawaida, Benki Kuu ndiyo taasisi yenye jukumu la kusimamia kiasi cha fedha kinachozunguka kwenye uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei na kulinda thamani ya sarafu.

Iwapo Serikali itategemea kwa kiasi kikubwa fedha kutoka Benki Kuu, baadhi ya wataalamu wanaona kuna hatari ya kuongezeka kwa fedha kwenye uchumi kuliko uzalishaji wa bidhaa na huduma, hali inayoweza kuongeza shinikizo la kupanda kwa bei.

Mchumi Anna Tibaijuka ambaye amewahi kuwa waziri kwa miaka mingi anasema mjadala haupaswi kuwa kama Serikali ikope au isikope kutoka BoT, bali namna ya kuhakikisha utaratibu huo unawekewa mipaka madhubuti.

"Mjadala si Serikali ikope pesa BoT au isikope. Inaweza ikakopa, lakini lazima ifanye hivyo kwa kuwajibika ili kuondoa athari zinazoweza kutokea."

Tibaijuka ametaja Zimbabwe kama mfano unaojulikana zaidi wa nchi ambayo utegemezi mkubwa wa fedha za benki kuu uliambatana na matatizo makubwa ya mfumuko wa bei. Pia ametaja Ghana kama mfano wa hivi karibuni unaoonyesha changamoto zinazoweza kutokea pale ambapo shinikizo za matumizi ya Serikali zinapoongezeka.

Hofu hii pia ipo kwa wanasiasa wa upinzani, Godibless Lema, mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA anasema "mnakwenda kuwa kama Zimbabwe, nguvu ya uzalishaji itapungua, mtakuja kununua hapa sukari kilo moja shilingi laki moja".

Tafiti za uchumi zinasemaje?

G

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwaka 2026, wananchi wa Zimbabwe waliandamana kutokana na mdororo mkubwa wa kiuchumi.

Katika utafiti wake ulioangalia athari za Serikali kukopa Benki Kuu ukilinganisha na benki zingine za kibiashara, akirejea mfano wa nchi ya Pakistan, mtafiti Mobina Yasmeen alibaini kuwa mikopo ya Serikali kutoka Benki Kuu ilikuwa na athari kubwa zaidi kwa mfumuko wa bei kuliko mikopo kutoka benki za biashara.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Benki Kuu inapofadhili matumizi ya Serikali mara nyingi huongeza kiasi cha fedha kinachozunguka kwenye uchumi. Hali hiyo inaweza kuongeza matumizi na mahitaji ya bidhaa, lakini pia inaweza kusababisha ongezeko la bei ikiwa uzalishaji hautaongezeka kwa kiwango kinacholingana.

Hata hivyo, si tafiti zote zinaonyesha upande hasi wa ukopaji wa Serikali. Utafiti wa mwaka 2018 uliofanywa na Benjamin Kabandana na Dk Patrick Mulyungi kuhusu athari za mikopo ya Serikali kwa ukuaji wa uchumi nchini Rwanda ulibaini kuwa ukopaji wa Serikali unaweza kusaidia ukuaji wa uchumi, hasa pale fedha hizo zinapotumika kufadhili miradi ya maendeleo kama miundombinu na huduma za umma.

Lakini watafiti hao pia walionya kuwa ukopaji mkubwa unaweza kuathiri sekta binafsi kwa kupunguza upatikanaji wa mikopo au kupunguza uwekezaji na matumizi ya sekta binafsi kwa wafanyabiashara na wawekezaji, hali inayojulikana kiuchumi kama 'crowding out effect'.

Hivyo basi, mjadala unaoendelea Tanzania unaonyesha pande mbili za sarafu moja. Ukiutizama zaidi mjadala si kama Serikali ikope au isikope kutoka BoT, bali ni masharti gani yatahakikisha nguvu hiyo haitumiki vibaya.