Kenya yathibitisha kisa cha tisa cha Ebola, wagonjwa wengine waimarika

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kenya imethibitisha kisa cha tisa cha ugonjwa wa Ebola, aina ya Bundibugyo, huku Wizara ya Afya ikisema wagonjwa wengine wanaendelea kuimarika na hakuna ushahidi wa maambukizi kusambaa nje ya kundi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, mgonjwa mpya ni mwanamume mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni ndugu wa karibu wa mgonjwa wa kwanza kufariki kutokana na ugonjwa huo.
Mwanamume huyo alithibitishwa kuwa na Ebola Oktoba 19, 2026, baada ya kuanza kuonyesha dalili akiwa tayari amewekwa karantini kwa kuwa alikuwa amekutana na mtu aliyeambukizwa.
Wizara imesema alitengwa mara tu alipoanza kuonyesha dalili, akapimwa na kuanza kupata matibabu baada ya kuthibitishwa kuwa na virusi hivyo.
Wizara ya Afya inasema wagonjwa wote tisa ni sehemu ya kundi moja la maambukizi, huku asilimia 99.3 ya watu waliokuwa katika orodha ya walio karibu na wagonjwa wakifuatiliwa na kuwekwa karantini.
Mamlaka zinasema hadi sasa hakuna ushahidi wa maambukizi nje ya kundi hilo.
Mgonjwa wa kwanza alifariki, huku wagonjwa wengine wanane wakiendelea kupata huduma za matibabu na uangalizi wa karibu. Wizara imesema wagonjwa hao wameonyesha kuimarika kwa kiasi kikubwa na hali zao ni thabiti.
Aidha, Kenya imepokea dozi 500 za dawa kwa ajili ya kusaidia matibabu ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola.
Watu 134 kati ya 135 waliohusishwa na wagonjwa wamefuatiliwa

Chanzo cha picha, Jospin Mwisha / AFP via Getty Images
Wizara ya Afya imesema juhudi za kutambua na kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa zinaendelea, huku orodha ya watu hao ikiongezeka kila kisa kipya kinapothibitishwa.
Hadi sasa, watu 134 kati ya 135 waliotambuliwa kama watu waliokutana na wagonjwa wamefuatiliwa na kuwekwa karantini, sawa na asilimia 99.3.
Wizara imesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya timu za kitaifa na za kaunti zinazofuatilia maambukizi, familia, jamii na washirika wa maendeleo.
Serikali imewashukuru Wakenya kwa ushirikiano wao na kutoa wito kwa umma kuendelea kushirikiana na timu za afya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Hospitali na kaunti zaimarishiwa vifaa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya imesema imesambaza vifaa vya kukabiliana na Ebola katika kaunti 12 zilizo katika hatari kubwa zaidi na kaunti nyingine 16 zilizo katika hatari kubwa.
Vifaa hivyo ni pamoja na mavazi ya kujikinga kwa wahudumu wa afya, glavu, kinga za uso, buti, vifaa vya kuchukulia na kusafirisha sampuli, vifaa vya uchunguzi na vipimajoto.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kusaidia timu za dharura katika kaunti kutambua, kutenga na kupima kwa usalama watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo.
Wizara pia imesema maabara maalumu imeanzishwa katika Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza cha Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ili kushughulikia vipimo vya kawaida vya wagonjwa wanaopata huduma za Ebola.
Hatua hiyo inalenga kuzuia maabara kuu ya hospitali hiyo kulemewa na kazi au kuathiriwa na sampuli zenye virusi vya Ebola, jambo ambalo lingeweza kuvuruga huduma za vipimo kwa wagonjwa wengine.
Wizara imeongeza kuwa inaendelea kufuatilia hatua za kuzuia maambukizi katika vituo vya karantini na matibabu ili kuhakikisha mapungufu yoyote yanashughulikiwa na wahudumu wa afya wanalindwa.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, hakuna maambukizi yaliyosambaa ndani ya vituo vya karantini, na wahudumu wanaowahudumia wagonjwa wamepewa vifaa vya kujikinga.
Baadhi ya watu wanatarajiwa kumaliza karantini
Wizara ya Afya imesema baadhi ya watu walioingia karantini Oktoba 6 na ambao hawajaonyesha dalili wanatarajiwa kukamilisha kipindi cha ufuatiliaji cha siku 21 na kuanza kurejea nyumbani kuanzia Oktoba 25.
Serikali imetoa wito kwa jamii kuwapokea kwa upendo watu hao watakapomaliza kipindi hicho, ikisema hawapaswi kunyanyapaliwa.
Wizara imesema watu wanaokamilisha siku 21 za ufuatiliaji bila kuonyesha dalili hawana hatari ya kuwaambukiza wengine.
Wakati huo huo, serikali imesema Kenya itaendelea kuwa wazi kwa shughuli za usafiri, biashara na mikusanyiko ya umma, bila kuweka vizuizi vinavyohusiana na mlipuko huo.
Wakenya wametakiwa kuendelea kufuata mwongozo wa Wizara ya Afya na kuripoti mapema dalili zinazoweza kuashiria Ebola, zikiwemo homa, uchovu usio wa kawaida, maumivu ya misuli au viungo, maumivu ya koo, kutapika, kuharisha au kutokwa na damu kusikoelezeka.
Mtu anayepata dalili hizo au anayemfahamu mtu anayezionyesha anashauriwa kuripoti katika kituo cha afya kilicho karibu au kupiga simu ya bure kupitia nambari 719.



































