Mama aliyemuua mumewe kwa sumu ahukumiwa kifungo cha maisha
Mama mmoja kutoka jimbo la Utah nchini Marekani ambaye aliandika kitabu cha watoto kuhusu huzuni baada ya kifo cha ghafla cha mumewe, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani bila nafasi ya kuachiliwa huru baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mume wake.
Majaji wa mahakama mwezi Machi walihitimisha kuwa Kouri Richins alimuua mumewe mwaka 2022 kwa kumpa kinywaji kilichochanganywa na dawa ya fentanyl.
Waendesha mashtaka walisema Richins mwenye umri wa miaka 36 alikuwa na madeni ya mamilioni ya dola, alikuwa amechukua bima za maisha kwa jina la mumewe, na pia alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa.
Akitoa hukumu Jumatano, siku ambayo marehemu Eric Richins angefikisha miaka 44, Jaji Richard Mrazi alisema:
“Mtu aliyepatikana na hatia ya makosa haya ni hatari mno kuachiwa huru tena.”
Mama huyo wa watoto watatu, ambaye hakutoa ushahidi wakati wa kesi yake, alizungumza kwa takriban dakika 30 mahakamani, akielekeza maneno yake zaidi kwa watoto wake.
“Ninaelewa kuwa leo hamtaki kuzungumza nami na mnanichukia. Hilo ni sawa. Mtakapokuwa tayari, nitakuwa hapa kwa ajili yenu,” alisema.
Richins pia alipatikana na hatia ya kudanganya ili kupata fedha za bima baada ya kifo cha mumewe nyumbani kwao karibu na mji wa mapumziko wa Park City.
Waendesha mashtaka walisema aliamini angeurithi utajiri wa mumewe uliokadiriwa kuwa zaidi ya dola milioni nne baada ya kifo chake.
Mahakama pia ilielezwa kuwa Richins alikuwa akipanga maisha ya baadaye na mwanaume mwingine aliyekuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi.
Aidha, alipatikana na hatia ya kujaribu kumuua mumewe katika tukio la awali ambapo alidaiwa kuweka sumu kwenye mkate wa nyama aliokuwa akiula.
Richins alikamatwa Machi 2023, miezi miwili baada ya kuchapisha kitabu cha picha cha watoto kiitwacho Are You With Me?, ambacho alisema kililenga kuwasaidia watu, akiwemo watoto wake watatu, kukabiliana na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao.
Katika mahojiano aliyowahi kufanya na kituo cha redio cha KPCW kabla ya kukamatwa kwake, alisema alikuwa na matumaini kuwa kitabu hicho kingewafariji familia zinazopitia maumivu ya kumpoteza mtu wa karibu.
Pia alimuelezea marehemu mumewe kama “mume mzuri na baba bora.”
Soma zaidi: