Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi mkutano wa kilele wa Trump-Xi unavyoweza kuimarisha uhusiano kwa miaka mingi ijayo
- Author, Anthony Zurcher
- Nafasi, Mwandishi Amerika Kaskazini
- Author, Laura Bicker
- Nafasi, Mwandishi China
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Usalama karibu na uwanja wa kihistoria wa Tiananmen Square mjini Beijing umeimarishwa kwa siku kadhaa, huku uvumi ukienea kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna gwaride maalum au tukio kubwa lililopangwa.
Maandalizi ya tukio hili kuu yameanza kwa minong'ono, lakini China inaonekana tayari kufanya onyesho kwa ajili ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Ziara hiyo itajumuisha mazungumzo, karamu, na kutembelea Hekalu la Mbinguni, ambapo wafalme wangesali kwa ajili ya mavuno mazuri.
Trump na Rais wa China Xi Jinping wana matumaini kwamba ziara hiyo itazaa matunda. Mkutano huu wa kilele kati ya viongozi wawili wenye nguvu zaidi ulimwenguni unatajwa kuwa moja ya mikutano muhimu zaidi kwa miaka.
Kwa miezi kadhaa, uhusiano wa Marekani na China umekuwa wa pata potea kwa Trump. Mtazamo wake umekuwa katika vita vinavyoendelea na Iran, operesheni za kijeshi katika Ulimwengu wa Magharibi na wasiwasi wa ndani. Lakini yote yanabadilika wiki hii. Mustakabali wa biashara ya kimataifa, kuongezeka kwa mivutano nchini Taiwan, na ushindani katika teknolojia ya hali ya juu vyote viko hatarini.
Kiuchumi, vita vya kibiashara vinavyoendelea na Marekani na mzozo wa Iran vinaweza kuwa habari mbaya kwa Xi, lakini kisiasa ni zawadi inayomfanya ajihisi kuwa na ushawishi mkubwa.
Ziara hii inaweza kuweka msingi wa ushirikiano wa siku zijazo - au migogoro - katika miaka ijayo.
Ni mnong'ono wa Iran?
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kabla ya kuelekea China siku ya Jumanne, Trump alisema atakuwa na "mazungumzo marefu" kuhusu Iran na kiongozi huyo wa China.
China inajaribu kuingilia kimya kimya kama mleta amani katika vita, ambayo sasa ni mwezi wa tatu. Beijing imejiunga na Pakistan kama mpatanishi katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Maafisa wa Beijing na Islamabad waliwasilisha mpango wenye vipengele vitano mwezi Machi kwa lengo la kukomesha mapigano na kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz. Na nyuma ya pazia, maafisa wa China wamekuwa wakiwavuta kwa upole wenzao wa Iran kuelekea meza ya mazungumzo.
Hakuna shaka, licha ya kuonyesha nguvu zake thabiti, kwamba China ina hamu ya kukomesha vita hivi.
Uchumi wa nchi hiyo tayari unapambana na ukuaji wa polepole na ukosefu mkubwa wa ajira. Kuongezeka kwa bei ya mafuta kumeongeza gharama ya bidhaa zilizotengenezwa kwa kemikali za petroli, kila kitu kutoka kwa nguo hadi plastiki. Kwa wazalishaji wengine nchini China, gharama zimepanda kwa asilimia 20.
China ina akiba ya mafuta ya kmezewa mate na uongozi ambao umechukua katika kutengeneza upya na magari ya umeme yameizuia kutokana na athari mbaya zaidi za uhaba wa mafuta, lakini vita vinasababisha maumivu zaidi kwa uchumi uliodorora wa China ambao unategemea sana mauzo ya nje. Lakini, ikiwa China itaingilia kati na kusaidia Marekani, bado itataka kitu kama malipo.
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi mjini Beijing wiki iliyopita ilionekana kubuniwa kuonyesha aina ya ushikiliaji na ushawishi ulionao China katika Mashariki ya Kati.
Markani inafuatilia kwa karibu. "Natumai Wachina watamuambia kile anachostahili kuambiwa,'' alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio."Na hicho ndicho kile unachofanya kwenye Mlango-Bahari kinakusababisha kutengwa kimataifa. Wewe ndiye mtu mbaya katika hili."
Marekani pia imejaribu kuishawishi China kutozuia azimio jipya la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalolaani mashambulizi ya Iran dhidi ya meli zinazojaribu kuvuka Hormuz baada yake, na Urusi ilipinga pendekezo la awali.
"Nadhani tukifanikiwa kuirejesha Iran kikamilifu kwenye meza ya mazungumzo, basi Marekani inatambua kuwa China itachukua jukumu fulani," anasema Ali Wyne, Mshauri Mkuu wa Utafiti na Utetezi wa uhusiano wa Marekani na China katika Kundi la Kimataifa la Migogoro.
Trump, kwa upande wake, ameonekana kutokerwa na uhusiano wa karibu wa China na Tehran. Wakati Marekani hivi majuzi iliidhinisha kiwanda cha kusafisha mafuta chenye makao yake nchini China kwa ajili ya kusafirisha mafuta ya Iran, rais wiki iliyopita alipuuza uungwaji mkono wowote wa China kwa Iran wakati wa mzozo huo.
"Ndivyo hali ilivyo, sio?" alimwambia mwandishi wa habari wa Marekani. "Tunafanya mambo, dhidi yao pia."
Hatima ya Taiwan
Utawala wa Trump umekuwa ukituma ishara mseto linapokuja suala la Taiwan.
Desemba mwaka jana, Marekani ilitangaza mkataba wa silaha wa dola bilioni 11 na Taiwan, na kuikera serikali ya China katika mchakato huo. Trump, hata hivyo, amepuuza nia ya Marekani kuitetea Taiwan, ambayo China inadai kuwa eneo lake.
"Anaiona kuwa sehemu ya China," Trump alisema kuhusu Xi, "na hiyo ni juu yake, atafanya nini."
Pia amesema Taiwan hairudishi vya kutosha Marekani kwa dhamana yake ya usalama, na kuongeza kuwa "haitupi chochote". Mwaka jana, alitoza ushuru wa 15% kwa Taiwan na kuishutumu kwa kuiba utengenezaji wa semiconductor kutoka Marekani.
Wiki iliyopita, Rubio alisema kuwa Taiwan itaangaziwa wakati wa ziara hiyo, ingawa lengo litakuwa ni kuhakikisha kuwa suala hilo haliwi chanzo cha mvutano mpya kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu.
"Hatuhitaji matukio yoyote ya kudhoofisha kutokea kwa Taiwan au popote katika
Indo-Pacific," alisema. "Na nadhani hiyo ni kwa manufaa ya pande zote mbili za Marekani na Wachina.
Kwa upande wake, China imeashiria kwamba Taiwan itapewa kipaumbele katika mazungumzo haya. Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi alisema wiki iliyopita kwamba anatumai Marekani itafanya "chaguo sahihi" wakati wa mazungumzo ya simu na Rubio.
Beijing imekuwa ikiongeza shinikizo lake la kijeshi kwa kutuma ndege za kivita na vyombo vya majini kuzunguka Taiwan karibu kila siku.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa maafisa wa China wanaweza kushinikiza kubadilishwa kwa lugha ya maneno kuhusu Taiwan ambayo iliandaliwa kwa uangalifu mwaka wa 1982. Sera ya hivi karibuni ya Washington iliyotangazwa hivi karibuni ni kwamba kwa sasa haiungi mkono uhuru wa Taiwan. Je, Beijing inaweza kushinikiza maneno yenye nguvu kama vile "Marekani inapinga uhuru wa Taiwan"?
"Sidhani kama Rais Xi atakubali hilo," anasema John Delury, mwenzao mkuu kutoka Kituo cha Mahusiano ya Marekani na China katika Jumuiya ya Asia. "Hata kama Trump atasema kitu cha ambacho kinaonekana kama mvuto kwa Taiwan, kwa sababu yeye si mwangalifu sana na matumizi yake ya lugha, Wachina wanajua bora kuliko kuweka matumaini makubwa katika hilo, kwa sababu anaweza kulibadilisha msimamo katika matandao wake wa kijamii wa Truth Social."
Mazungumzo muhimu ya biashara
Sehemu kubwa ya mwaka 2025, Marekani na China zilionekana kuwa karibu kutumbukia katika mzozo mpya wa kibiashara, ambao ingelitikisa misingi ya uchumi wa ulimwengu.
Trump alipandisha na kupunguza ushuru mara kwa mara kwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Marekani, wakati mwingine kufikia viwango vya zaidi ya 100%.
China ilijibu kwa kupunguza mauzo ya madini ya adimu kwa Marekani na ununuzi wake wa mauzo ya nje ya kilimo ya Marekani, na ikiwalenga wakulima katika majimbo muhimu ambayo yalimpigia kura Trump.
Joto hilo kwa sasa limepungua tangu Trump na Xi walipokutana ana kwa ana nchini Korea Kusini Oktoba mwaka jana. Uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Februari uliopunguza uwezo wa rais wa kutoza ushuru wa upande mmoja.
Trump na Xi bado watakuwa na mengi ya kuzungumza wakati wa mkutano wao wa kilele wa Beijing. Hata hivyo kiongozi huyo wa Marekani atashinikiza kuongeza ununuzi wa China wa bidhaa za kilimo za Marekani.
China ina uhakika wa kuishinikiza Marekani kuacha uchunguzi wa kibiashara uliotangazwa hivi majuzi kukagua mienendo isiyofaa ya kibiashara isiyo ya haki katika hatua ambayo inaweza kumpa Trump uwezo wa kuwekea tena bidhaa za Chinaushuru wa juu zaidi.
Katika masuala yote ya sera yatakayojadiliwa na pande zote mbili, huenda ziara ya Trump ya siku mbili (Alhamisi na Ijumaa) inayotarajiwa kusheheni mikutano na shughuli chungu nzima isizae matunda..
Ingawa hakutakuwa na muda wa kutosha kwa viongozi hao wawili kufikia kikamilifu makubaliano muhimu, mkutano huu unatoa fursa ya mazungumzo yatakayoimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili makubwa kwa miaka mingi ijayo.