Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Viongozi wawili wenye kiburi waibua mtafaruku Hormuz, nini kitatokea?" – Uchambuzi
Katika mapitio yetu ya vyombo vya habari leo, magazeti yamejadili kile kinachoitwa "ukaidi" wa Washington na Tehran na athari zake kwa usafiri katika Mlango wa Hormuz, pamoja na "ujumbe wa kidiplomasia usio wa moja kwa moja" uliomo katika barua ya Mfalme Charles III kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Aidha, kuna mjadala kuhusu kupungua kwa ushawishi wa Jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta ya petroli, OPEC kutokana na mabadiliko ya haraka katika soko la nishati duniani.
Tunaanza na gazeti la The New York Times, ambapo Nicholas Kristof ameandika makala akiikosoa kile anachokiita makosa ya mara kwa mara ya Rais Donald Trump katika uhusiano wake na Iran.
Mwandishi anaamini kuwa hatua ya Trump kuondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran mwaka 2018 haikuleta makubaliano bora kama ilivyotarajiwa, bali ilichangia kuharakisha maendeleo ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Anaongeza kuwa mwaka huu serikali ya Marekani ilikosea tena ilipodhani kuwa vita na Iran vitakuwa vifupi na kuleta makubaliano ya haraka, ilhali Tehran ilijibu kwa kuchukua udhibiti wa Mlango wa Hormuz.
Mwandishi Kristof anaeleza kuwa Trump, kwa mtazamo wake, anaendelea kupita kiasi kuamini ufanisi wa shinikizo la kiuchumi na uzuiaji wa majini, akidhani Iran iko karibu kuanguka, jambo linalopingana na tathmini za wataalamu wa nishati.
Ananukuu wachambuzi wakisema Tehran bado ina muda kabla ya kufikia mgogoro wa mafuta, na madai ya kuanguka kwa sekta yake ya mafuta yamezidishwa.
Anaongeza kuwa dau la Marekani kwamba vikwazo vitailazimisha Iran kusalimu amri huenda si la kweli, kwa kuwa uongozi wa Iran mara nyingi hushikilia misimamo yake hata chini ya shinikizo kubwa la kiuchumi.
Hali hii inaweza kurefusha mgogoro na kuongeza athari zake kwa uchumi wa dunia, hasa kutokana na usumbufu wa usafiri katika Mlango wa Hormuz.
Anasema Iran imewasilisha pendekezo la awali la kufungua tena mlango huo huku ikiahirisha masuala mengine kama mpango wa nyuklia, lakini Marekani bado haijaridhishwa, jambo linaloacha mlango wazi wa kuongezeka kwa mvutano.
"Hotuba ya Mfalme Charles kulivyofichua kwa ustadi mambo ya aibu kuhusu Donald Trump"
Tunaelekea gazeti la The Independent, ambapo mwandishi Simon Walters anaandika kuhusu hotuba ya Mfalme Charles III katika Bunge la Marekani na jinsi alivyotoa ujumbe usio wa moja kwa moja kwa Rais Donald Trump.
Mwandishi anaona kuwa kushughulika na Trump ni mojawapo ya changamoto tata zaidi katika diplomasia ya kisasa, kwani viongozi hulazimika kuchagua kati ya kumkabili moja kwa moja au kumsifu ili kuepuka athari kali.
Anaeleza kuwa changamoto hii ilidhihirika zaidi baada ya kile alichokiita aibu ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House mwaka jana.
Anaongeza kuwa Mfalme Charles III, kupitia hotuba iliyopokelewa kwa sifa, aliweza kusawazisha ujumbe mkali bila kuibua mzozo wa moja kwa moja, akipokea makofi kwa ishara ya kusimama mara 13.
Hotuba hiyo ilijumuisha kauli zilizohusu sera za Trump katika masuala kadhaa.
Kuhusu NATO, mwandishi anaeleza kuwa Trump hapo awali alitishia kujiondoa kwenye muungano huo, lakini Mfalme alikumbusha mchango wa nchi wanachama, akisisitiza mshikamano wao na Marekani baada ya mashambulizi ya Septemba 11.
Kuhusu Ukraine, Trump alionyesha mashaka juu ya msaada kwa Kyiv, ilhali Mfalme alitoa wito wazi kwa Marekani kuisaidia Ukraine ili kufanikisha amani ya haki na ya kudumu dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Kwenye masuala ya ulinzi, Trump aliwalaumu washirika wa NATO kwa kutotumia fedha za kutosha, wakati Mfalme alisisitiza ushirikiano wa kiusalama na wajibu wa kuongeza bajeti ya ulinzi.
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Trump alizua mashaka kuhusu hali hiyo, ilhali Mfalme alionya kuhusu athari za uharibifu wa mifumo ya asili kwa usalama na uchumi.
Hotuba hiyo pia iligusia dini, ambapo Trump na makamu wake JD Vance walikosoa ushawishi wa Waislamu barani Ulaya, huku Mfalme akihimiza mazungumzo ya kidini na uelewano.
Kwenye uchumi, Trump alitumia ushuru kama shinikizo la kibiashara, wakati Mfalme alisisitiza umuhimu wa uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Kuhusu matumizi ya madaraka, Mfalme alikumbusha misingi ya sheria za pamoja kati ya Uingereza na Marekani na umuhimu wa mifumo ya kuzuia mamlaka kupita kiasi.
Mwandishi anasema hotuba ya Mfalme Charles III ilikuwa na ukosoaji wa kidiplomasia usio wa moja kwa moja kwa utawala wa Trump, uliowasilishwa kwa ustadi wa kisiasa bila kuibua mgogoro wa wazi.
End of Pia unaweza kusoma:
"Kupungua kwa ushawishi wa OPEC"
Tunaelekea tahariri ya gazeti la Financial Times ambayo inazungumzia kile inachokiita kupungua kwa ushawishi wa OPEC kutokana na mabadiliko ya haraka katika soko la nishati duniani.
Tahariri inaeleza kuwa Jumuiya ya nchi zinazouza petroli OPEC hapo awali ilikuwa na nguvu kubwa, hasa baada ya vikwazo vya mafuta vya mwaka 1973, lakini ushawishi wake umepungua kutokana na kupungua kwa utegemezi wa mafuta duniani na kuongezeka kwa uzalishaji kutoka nchi zisizo wanachama, hasa Marekani kupitia mafuta ya shale.
Inaongeza kuwa kujiondoa kwa Umoja wa Falme za Kiarabu kunaonyesha hatua ya juu ya mabadiliko haya, na kuashiria kile kinachoweza kuwa kipindi cha kudhoofika kwa shirika hilo.
Gazeti linaeleza kuwa Abu Dhabi imekuwa ikipanga kujiondoa kwa muda mrefu baada ya kuwekeza kuongeza uwezo wake wa uzalishaji.
Mabadiliko haya yanaonyesha tofauti kati ya nchi zinazotaka kudumisha bei, kama Saudi Arabia, na zile zinazotaka kuongeza uzalishaji ili kujihakikishia soko la baadaye.
Tahariri inaongeza kuwa mvutano wa kikanda, pamoja na vita na Iran na usumbufu wa usafirishaji kupitia Hormuz, umeharakisha mchakato huu.
Hata hivyo, OPEC bado ina nguvu muhimu kwa kuwa wanachama wake wanamiliki karibu asilimia 75 ya akiba ya mafuta duniani, na gharama ya uzalishaji ni ya chini.
Lakini uwezo wake wa kudhibiti soko unategemea mshikamano wa ndani, ambao umeathiriwa na migogoro ya kisiasa na tofauti za kikanda.
Inaelezwa kuwa kujiondoa kwa UAE kunaongeza mgawanyiko ndani ya OPEC, na kuweka Saudi Arabia katika nafasi ya kujaribu kudumisha umoja huo huku kukiwa na hatari ya kuongezeka kwa uzalishaji usio na udhibiti na kuyumba kwa soko la nishati duniani.