Moja kwa moja, UAE na Israel zatofautiana kuhusu ziara ya siri ya Netanyahu nchini humo

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, imetangaza kuwa Netanyahu alifanya ziara ya siri kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu wakati wa vita mashariki ya kati

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Mama aliyemuua mumewe kwa sumu ahukumiwa kifungo cha maisha

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mama mmoja kutoka jimbo la Utah nchini Marekani ambaye aliandika kitabu cha watoto kuhusu huzuni baada ya kifo cha ghafla cha mumewe, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani bila nafasi ya kuachiliwa huru baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mume wake.

    Majaji wa mahakama mwezi Machi walihitimisha kuwa Kouri Richins alimuua mumewe mwaka 2022 kwa kumpa kinywaji kilichochanganywa na dawa ya fentanyl.

    Waendesha mashtaka walisema Richins mwenye umri wa miaka 36 alikuwa na madeni ya mamilioni ya dola, alikuwa amechukua bima za maisha kwa jina la mumewe, na pia alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa.

    Akitoa hukumu Jumatano, siku ambayo marehemu Eric Richins angefikisha miaka 44, Jaji Richard Mrazi alisema:

    “Mtu aliyepatikana na hatia ya makosa haya ni hatari mno kuachiwa huru tena.”

    Mama huyo wa watoto watatu, ambaye hakutoa ushahidi wakati wa kesi yake, alizungumza kwa takriban dakika 30 mahakamani, akielekeza maneno yake zaidi kwa watoto wake.

    “Ninaelewa kuwa leo hamtaki kuzungumza nami na mnanichukia. Hilo ni sawa. Mtakapokuwa tayari, nitakuwa hapa kwa ajili yenu,” alisema.

    Richins pia alipatikana na hatia ya kudanganya ili kupata fedha za bima baada ya kifo cha mumewe nyumbani kwao karibu na mji wa mapumziko wa Park City.

    Waendesha mashtaka walisema aliamini angeurithi utajiri wa mumewe uliokadiriwa kuwa zaidi ya dola milioni nne baada ya kifo chake.

    Mahakama pia ilielezwa kuwa Richins alikuwa akipanga maisha ya baadaye na mwanaume mwingine aliyekuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi.

    Aidha, alipatikana na hatia ya kujaribu kumuua mumewe katika tukio la awali ambapo alidaiwa kuweka sumu kwenye mkate wa nyama aliokuwa akiula.

    Richins alikamatwa Machi 2023, miezi miwili baada ya kuchapisha kitabu cha picha cha watoto kiitwacho Are You With Me?, ambacho alisema kililenga kuwasaidia watu, akiwemo watoto wake watatu, kukabiliana na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao.

    Katika mahojiano aliyowahi kufanya na kituo cha redio cha KPCW kabla ya kukamatwa kwake, alisema alikuwa na matumaini kuwa kitabu hicho kingewafariji familia zinazopitia maumivu ya kumpoteza mtu wa karibu.

    Pia alimuelezea marehemu mumewe kama “mume mzuri na baba bora.”

    Soma zaidi:

  2. Xi atoa wito China na Marekani kuwa 'washirika badala ya wapinzani'

    H

    Chanzo cha picha, CGTN

    Rais wa China Xi Jinping ametoa wito kwa nchi yake na Marekani kushirikiana kama washirika badala ya kuwa wapinzani, akisisitiza haja ya utulivu katika uhusiano wa mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa duniani.

    Akizungumza katika hotuba ya ufunguzi, Xi amesema dunia nzima inafuatilia mazungumzo yao, akibainisha kuwa mabadiliko makubwa ya kimataifa yasiyo ya kawaida yanaendelea kwa kasi na hali ya kimataifa iko katika mzunguko wa mabadiliko na misukosuko.

    Aliongeza kuwa dunia imefika katika njia panda mpya, akihoji iwapo China na Marekani zinaweza kuepuka kile kinachoitwa “mtego wa Thucydides” na badala yake kuanzisha mfumo mpya wa mahusiano unaoweza kuleta utulivu wa kimataifa.

    Xi amehoji pia iwapo mataifa hayo mawili yanaweza kushirikiana kukabiliana na changamoto za dunia na kujenga mustakabali bora wa mahusiano yao kwa maslahi ya watu wao na binadamu kwa ujumla.

    Pia amewapongeza Marekani na Rais Donald Trump kwa kuadhimisha miaka 250 ya uhuru, akisema nchi hizo mbili zina maslahi mengi yanayofanana kuliko tofauti.

    Amesisitiza kuwa mafanikio ya upande mmoja yanaweza kuwa fursa kwa mwingine, na kwamba uhusiano thabiti kati ya China na Marekani ni muhimu kwa utulivu wa dunia.

    “China na Marekani zinanufaika na ushirikiano na hupoteza kupitia migogoro,” amesema, akihitimisha kwa wito wa mataifa hayo kuwa washirika na kusaidiana kufanikiwa katika enzi mpya ya mahusiano ya kimataifa.

    Soma zaidi:

  3. Mazungumzo ya Trump na Xi yaanza rasmi Beijing huku ishara za ukaribu zikionekana

    H

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Ingawa tayari Donald Trump amewasili nchini China, shughuli kuu za ziara yake zimepangwa kufanyika Alhamisi na Ijumaa.

    Hapa ni baadhi ya ratiba muhimu wakati wa ziara hiyo:

    Alhamisi

    Rais wa China Xi Jinping atampokea Rais Trump katika Ukumbi Mkuu wa Watu mjini Beijing.

    Viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi ya pande mbili.

    Pia kutakuwa na karamu ya chakula cha jioni baadaye usiku.

    Ijumaa

    Kutakuwa na picha ya pamoja na kupeana mkono kati ya Rais Xi na Rais Trump katika bustani ya Zhongnanhai mjini Beijing, ambayo ni makao makuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.

    Kualika viongozi wa kigeni katika eneo hilo mara nyingi huchukuliwa kuwa ishara ya ukaribu wa kidiplomasia.

    Baadaye, Trump na Xi watafanya kikao kingine cha mazungumzo ya pande mbili wakinywa chai. Pia kutakuwa na chakula cha mchana kabla ya Rais Trump kuagwa rasmi katika uwanja wa ndege.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Iran yaonya UAE baada ya taarifa za ziara ya siri ya Netanyahu

    h

    Chanzo cha picha, EPA

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameibua hisia kali kufuatia taarifa za ziara ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, nchini United Arab Emirates, akisema hatua hiyo ilikuwa tayari imefahamika na vyombo vya usalama vya Iran muda mrefu uliopita.

    “Netanyahu sasa ameweka hadharani kile ambacho taasisi za usalama za Iran zilikuwa tayari zimewasilisha kwa viongozi wetu,” Araqchi amesema.

    Katika kauli kali zinazoonekana kuelekezwa kwa UAE na mataifa mengine ya Ghuba, Araqchi amesema:

    “Uadui dhidi ya taifa kubwa la Iran ni kamari ya kipumbavu, na ushirikiano au njama na Israel katika mwelekeo huo hauwezi kusameheka. Wale wanaoshiriki kushirikiana na Israel kuleta mgawanyiko wanapaswa kuwajibishwa.”

    Kauli hiyo imekuja wakati taarifa kuhusu ziara ya siri ya Netanyahu nchini UAE wakati wa vita dhidi ya Iran zikiendelea kuzua mjadala mkubwa wa kimataifa.

    Katika siku za hivi karibuni pia, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti madai kuhusu mashambulizi ya siri ya kijeshi yaliyofanywa na UAE pamoja na Saudi Arabia dhidi ya Iran, taarifa ambazo zimevuta uangalizi mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Soma zaidi:

  5. UAE na Israel zatofautiana kuhusu ziara ya siri ya Netanyahu nchini humo

    g

    Chanzo cha picha, Reuters/Getty Images

    UAE imekanusha taarifa zinazoeleza kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alifanya ziara ya siri nchini humo wakati wa vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE, serikali hiyo ilisema: “Umoja wa Falme za Kiarabu unakanusha taarifa zilizochapishwa kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa Israel au kupokea ujumbe wa kijeshi wa Israel.”

    Wizara hiyo iliongeza kuwa uhusiano kati ya UAE na Israel uko wazi na unategemea makubaliano ya Abraham Accords, hivyo ziara zote rasmi na mikutano hutangazwa hadharani na kufanyika kwa uwazi.

    Kauli hiyo imekuja baada ya vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, vikiwemo Reuters na CBS News, kuripoti Jumatano kwa kunukuu Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel kwamba Netanyahu alifanya ziara ya siri nchini UAE wakati wa vita dhidi ya Iran na kukutana na Rais wa UAE Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

    Awali, Ofisi ya Netanyahu ilikuwa imesema ziara hiyo iliashiria “hatua ya kihistoria” katika uhusiano kati ya Israel na UAE.

    Wakati huo huo, gazeti la Israel Hayom liliripoti kuwa Israel iliipatia UAE mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome wakati wa vita vya karibuni, madai yaliyonukuliwa kutoka kwa Mike Waltz ambaye alisema UAE ilionekana kutumia mfumo huo uliotolewa na Israel.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 14 mwezi Mei 2026.