Mataji 16 katika miaka mitano – kwa nini Uhispania ni nguvu kubwa inayotawala soka

Chanzo cha picha, GETTY
Hispania imeshinda tena.
Baada ya kutawazwa mabingwa wa Ulaya miaka miwili iliyopita jijini Berlin, sasa 'La Roja' ni mabingwa wa dunia baada ya kuifunga Argentina bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Dunia huko New Jersey siku ya Jumapili.
Walifanikiwa kufanya hivyo mwaka wa 2010, miaka miwili baada ya kushinda michuano ya Euro ya mwaka 2008.
Mafanikio haya ya hivi karibuni ya Hispania yanaendeleza utawala wao wa ajabu katika soka la wanaume na wanawake.
Wao ndio taifa la kwanza kushinda Kombe la Dunia la wanaume na wanawake kwa wakati mmoja – huku 'La Roja' wakiishinda Uingereza katika fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake jijini Sydney mwaka wa 2023.
Hayo si yote. Timu ya wanaume ilishinda taji la Nations League mwaka wa 2023 na medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya 2024, huku timu ya wanawake ikishinda Nations League mwaka wa 2024 na 2025.
Kwa hakika, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Hispania imeshinda mataji 16 ya dunia na Ulaya—idadi ya kushangaza—kuanzia ngazi ya vijana chini ya umri wa miaka 17 hadi ngazi ya wakubwa.
"Ni utawala," mtaalamu wa soka la Hispania, Guillem Balague, aliambia BBC Sport.
"Ni kama mchanganyiko kamili wa mambo mazuri yanayotokea kwa wakati mmoja. Kiutamaduni, tunafanya mambo kwa namna fulani. Kila mtu anaamini katika hilo. Jambo la muhimu ni kwamba hatusimami.
"Ni kama kupanda Mlima Everest tena, kwa sababu timu ya wanaume ilishinda Kombe la Dunia mwaka wa 2010, miaka miwili baada ya kushinda Euro. Sasa tumefanya hivyo tena."
Mashine ya ushindi ya Uhispania
Soka la wanawake (mataji 11 kati ya 2022-2026)
Ngazi ya juu: Kombe la Dunia 1 (2023); Ligi ya Mataifa 2 (2024, 2025).
Chini ya miaka 20: Kombe la Dunia 1 (2022).
Chini ya miaka 19: Mabingwa wa Ulaya mara 5 (2022, 2023, 2024, 2025, 2026).
Chini ya miaka 17: Kombe la Dunia 1 (2022); Mabingwa wa Ulaya mara 1 (2024).
Soka la wanaume (mataji 5 kati ya 2022-2026)
Ngazi ya juu: Kombe la Dunia 1 (2026); Mabingwa wa Ulaya mara 1 (2024); Ligi ya Mataifa 1 (2023).
Chini ya miaka 23: Washindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki mara 1 (2024).
Chini ya miaka 19: Mabingwa wa Ulaya mara 1 (2026).
'Ilikuwa hatari kumteua De La Fuente'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hispania ilipomteua Luis de la Fuente kuwa kocha mkuu mnamo Desemba 2022, ni watu wachache walioamini kuwa angefanikiwa kushinda mataji ya Nations League (2023), Ubingwa wa Ulaya (2024) na Kombe la Dunia (2026) ndani ya muda mfupi kiasi hicho.
Hispania ilikuwa imetolewa hivi punde kwenye Kombe la Dunia na Morocco katika hatua ya 16 bora nchini Qatar, na shirikisho lilihitaji mrithi baada ya Luis Enrique kuondoka katika nafasi hiyo.
"Walimchagua mtu huyu [De La Fuente] ambaye alielewa mtindo na mfumo wa timu," aliongeza Balague.
"Ilikuwa uamuzi wenye hatari kubwa - sidhani kama kuna mtu aliyedhani angefanikiwa kiasi hicho."
Hatua hiyo ilionekana kuwa na hatari kwa sababu De La Fuente alichukua jukumu la kuinoa Hispania - timu ambayo imeshinda mataji matatu kati ya matano ya mwisho ya Ubingwa wa Ulaya kwa wanaume (2008, 2012, 2024) - bila kuwa amewahi kufundisha klabu kubwa.
Baada ya kustaafu soka la ushindani mwaka 1994, De La Fuente alitumia miaka 15 katika majukumu mbalimbali kwenye klabu tofauti, ikiwemo kufundisha ligi za daraja la chini nchini Hispania, kufanya kazi na timu za vijana na kuwa kocha msaidizi, kabla ya kuchukua jukumu la kuzinoa timu za vijana za Hispania.
"De la Fuente aliwafahamu wengi wa wachezaji hawa tangu wakiwa katika vituo vya kukuza vipaji (academies) na wanaendelea kukua kama timu," kiungo wa zamani wa Hispania, Juan Mata, aliambia BBC Sport.
"Hii si timu ya sasa pekee, bali pia ni timu ya siku zijazo."
Tangu alipoteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya wakubwa baada ya kuzinoa timu za vijana chini ya umri wa miaka 19, 21 na timu ya Olimpiki, De La Fuente amejenga utamaduni wa kuheshimu wapinzani na mchakato wa maendeleo, huku akihimiza uvumilivu na utulivu.
"Wengi wenu ni wadogo kiumri kuliko mimi na mnapaswa kuheshimu uzoefu," kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa kabla ya mechi jijini New York siku ya Ijumaa. "Baada ya kumaliza mchezo huo, kulikuwa na wachezaji waliohoji, 'Kocha, sasa ni nini kingine kilichobaki kushinda ilhali tumeshinda kila kitu katika makundi yote?'
"Tulihitimisha kuwa kilichosalia ni mechi inayofuata mwezi Septemba, kwani timu hii haichoki kupambana."
Mafanikio ya timu za taifa na makocha wa Kihispania yameenea hadi kwenye soka la ngazi ya klabu.
Licha ya uamuzi wa Pep Guardiola kuondoka Manchester City baada ya miaka 10 iliyojaa mataji mengi, angalau robo ya makocha watakaoanza msimu wa 2026-27 wa Ligi Kuu ya Uingereza ni raia wa Uhispania.
Kwa sasa, Uhispania haijapoteza mchezo wowote kati ya mechi zake 38 zilizopita katika mashindano yote; hii ni rekodi ya muda mrefu zaidi kuwahi kuwekwa na timu yoyote kutoka Ulaya au Amerika Kusini katika historia.
'Tunashinda kila kitu'
Wakati huo huo, soka la wanawake nchini Uhispania limeimarika sana katika muongo uliopita na linaanza kupata mafanikio makubwa katika mechi zenye ushindani mkali na shinikizo kubwa.
Ushindi wa timu hiyo dhidi ya Uingereza miaka mitatu iliyopita katika fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake ulipatikana katika ushiriki wao wa tatu tu kwenye mashindano hayo, wakiwa wameanza kushiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2015.
Baadaye, timu ya wanawake ya Uhispania iliendeleza mafanikio hayo kwa kushinda mataji ya 'Nations League' mfululizo mwaka 2024 na 2025.
"Mabadiliko katika soka la wanawake nchini Uhispania yamekuwa makubwa sana," mchezaji wa zamani Maria Garrido, ambaye sasa ni mwandishi wa habari, aliambia BBC Sport mwaka 2024.
"Miaka kumi iliyopita, nilipokuwa nikichezea FC Barcelona, hakukuwa na La Masia [chuo maarufu cha soka cha Barcelona] kwa ajili ya wasichana. Tulijigharimia usafiri wenyewe, wazazi wetu walitupeleka mazoezini, na hatukulipwa pesa yoyote.
"Lakini katika miaka mitano iliyopita, hali imeboreka sana. Kumekuwa na juhudi kubwa za kukuza soka la wanawake, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa makundi zaidi ya vijana, kuboreshwa kwa miundombinu na mazingira, pamoja na kuanzishwa kwa chuo maalum cha soka kwa ajili ya wasichana.
"Mabadiliko haya hayajaleta mapinduzi makubwa katika mchezo huo tu, bali pia yameongeza heshima kwa soka la wanawake nchini Uhispania."
Mafanikio haya ya timu za wanaume na wanawake yalikuja baada ya kushinda mataji mengi katika ngazi ya vijana katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
'Ushindi huzaa ushindi'

Chanzo cha picha, GETTY
Mustakabali unaonekana kuwa mwema, huku wengi wakiamini kuwa utawala wa Uhispania utaendelea.
Katika nafsi ya Lamine Yamal na Pau Cubarsi, timu hiyo ina vipaji viwili bora vya vijana ambao wamejipatia medali yao ya kwanza ya ushindi wa Kombe la Dunia wakiwa na umri wa miaka 19.
Vicky Lopez, anayechezea timu ya taifa ya wanawake, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa mara tatu akiwa na Barcelona katika umri huohuo.
Mshambuliaji Salma Paralluelo pia ameiwakilisha nchi yake zaidi ya mara 50 kabla ya kufikisha umri wa miaka 23.
Yamal alikuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kucheza fainali ya Kombe la Dunia, akimfuatia Pele wa Brazil mwaka 1958 (miaka 17, siku 249) na Giuseppe Bergomi wa Italia mwaka 1982 (miaka 18 na siku 201).
Huku Cubarsi naye akianza mchezo siku ya Jumapili akiwa na umri wa miaka 19 na siku 178, Uhispania ilikuwa timu ya kwanza kuchezesha vijana wawili walio chini ya umri wa miaka 20 katika fainali moja ya Kombe la Dunia.
"Uhispania ina mtindo wa kucheza ambao hakuna yeyote duniani aliyeonyesha kuwa anaweza kuukaribia," kipa wa zamani wa Uingereza Joe Hart aliambia BBC Sport baada ya ushindi dhidi ya Argentina.
"Hakuna aliyeweza kuwazuia au kuwapa changamoto kubwa katika Kombe hili la Dunia; walikabiliwa na mashuti 10 pekee yaliyolenga lango lao katika michuano yote."
Wakati huo huo, Thierry Henry, mshindi wa Kombe la Dunia la mwaka 1998 akiwa na Ufaransa, aliambia Fox Sports kuwa Uhispania ina uwezo wa kutawala kwa miaka mingi ijayo.
"Nataka kusifu mfumo wao na mambo waliyoyaweka," alisema.
"Kwa sababu hapo awali Uhispania haikuwa ikishinda kwa namna hiyo. Na sasa wanashinda katika kila ngazi."












