Mtanzania Clara Luvanga avunja rekodi ya usajili wa soka la wanawake duniani?

Clara Luvanga poses in Al-Nassr blue training kit

Chanzo cha picha, Washington Spirit

Maelezo ya picha, Luvanga amekuwa mwiba kwenye ligi ya Saudi na sasa anaelekea Marekani
    • Author, Sally Freedman
    • Nafasi, BBC Sport senior journalist
    • Author, Celestine Karoney
    • Nafasi, BBC Sport Africa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mshambuliaji wa Tanzania Clara Luvanga amejiunga na Washington Spirit akitokea klabu ya Saudi Arabia, Al-Nassr, katika usajili unaoaminika kuwa miongoni mwa usajili wenye gharama kubwa zaidi katika historia ya soka la wanawake.

Ada iliyolipwa na klabu hiyo ya Ligi ya Marekani kwa wanawake (National Women's Soccer League) haijawekwa wazi rasmi.

Baadhi ya taarifa zinaripoti kuwa ni dola milioni 2.3 (takriban pauni milioni 1.7), jambo ambalo lingemfanya Luvanga kuwa mchezaji wa kike aliyesajiliwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia ya soka la wanawake.

BBC haijaweza kuthibitisha kiasi hicho, ingawa chanzo kilicho karibu na suala hilo kimesema kinaamini usajili huo unaingia katika orodha ya usajili ghali zaidi wa soka la wanawake, ukiwa miongoni mwa sajili tano bora na ghali.

Spirit ilikataa kusema kuhusu ada hiyo ya uhamisho ilipowasiliana na BBC Sport.

Luvanga, mwenye umri wa miaka 21, amesaini mkataba utakaomuweka Washington hadi mwisho wa msimu wa 2029 wa NWSL.

Iwapo kiasi hicho cha rekodi kilichoripotiwa ni sahihi, itamaanisha ada hiyo imevuka pauni milioni 1.4 ambazo London City Lionesses inadaiwa kuilipa Paris St-Germain kumsajili Grace Geyoro mwaka jana.

Hata hivyo, ada ya Geyoro imepingwa, jambo linaloonyesha zaidi jinsi takwimu za uhamisho katika soka la wanawake mara nyingi zinavyofanywa kuwa siri.

Kwa uhamisho huo, pia Luvanga anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza katika moja ya ligi kubwa za wanawake duniani ya NWSL.

Luvanga alitwaa taji la ligi kuu la Saudi Arabia kwa wanawake( Saudi Women's Premier League) katika misimu yake yote mitatu akiwa na Al-Nassr, pamoja na Saudi Women's Cup, Saudi Women's Super Cup na Mashindano ya Klabu za Wanawake ya West Asian Football Federation (WAFF).

.

Chanzo cha picha, HabariLeo

Maelezo ya picha, Clara akiwa kwenye moja ya majukumu ya timu ya taifa ya wanawake Tanzania (Twiga Stars)
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Pia alitwaa kiatu cha dhahabu cha ligi msimu uliopita baada ya kufunga mabao 24 katika mechi 14.

Washington Spirit inamilikiwa na Michele Kang, ambaye pia anaimiliki London City Lionesses.

London City ilifanya usajili kadhaa wa wachezaji maarufu wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi, akiwemo mshindi wa Ballon d'Or mara mbili Alexia Putellas, aliyejiunga akitokea Barcelona kwa mkataba wa miaka mitatu.

Luvanga alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na timu ya taifa ya Tanzania mwaka 2024. Kabla ya kujiunga na Al-Nassr mwaka 2023, alichezea DUX Logrono ya Hispania, baada ya kukulia katika mfumo wa vijana wa klabu ya Yanga Princess ya Tanzania.

Akizungumzia klabu yake mpya, Luvanga alisema: "Nimefurahi sana kujiunga na Washington Spirit na kukabiliana na changamoto hii mpya kwenye NWSL.

"Ninajua ninafika wakati msimu tayari umeanza, lakini nimefurahi sana kucheza katika ligi mpya na nchi mpya."

Mkurugenzi wa michezo wa Spirit, James Hocken, alisema: "Clara anaongeza mwelekeo mpya wa kusisimua katika safu yetu ya ushambuliaji tunapoelekea hatua ya mchujo.

"Licha ya umri wake mdogo, ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa njia mbalimbali na ana sifa za kufanya vizuri sana katika ligi hii."

Akivutiwa na Ronaldo anajaribu kufuata nyayo zake

Tanzanian striker Clara Luvanga shakes hands with Portuguese star Cristiano Ronaldo in front of a banner showing the club crest of Saudi club Al-Nassr

Chanzo cha picha, Clara Luvanga

Maelezo ya picha, Mwaka 2023, Luvanga alijiunga na klabu ya ligi kuu ya wanawake ya Saudi, Al-Nassr

Kupanda kwa Luvanga kutoka Tanzania hadi moja ya ligi zenye ushindani mkubwa zaidi duniani kwenye soka la wanawake kumekuwa kwa kasi kubwa.

Alianza maisha yake ya soka na Yanga Princess nchini Tanzania kabla ya kupata mafanikio makubwa ya kimataifa mwezi Agosti 2023, alipojiunga na klabu ya Hispania, DUX Logrono. Lakini Hispania ilikuwa kituo kifupi tu katika safari yake ya soka.

Kufikia Oktoba mwaka huo, Luvanga alielekea Saudi Arabia kujiunga na Al-Nassr, uamuzi ambao umekuwa wa mabadiliko makubwa katika maisha yake ya soka.

Katika misimu mitatu Mashariki ya Kati, aliisaidia Al-Nassr kushinda taji la ligii kuu kwa misimu yote mitatu aliyoichezea na kujijengea jina kama mmoja wa washambuliaji waliofunga mabao mengi zaidi katika ligi hiyo.

Muda wake akiwa Al-Nassr pia ulimpa fursa ya kukutana na mmoja wa nyota wakubwa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anayeichezea timu ya wanaume ya Al-Nassr. Luvanga amezungumzia jinsi anavyoiga baadhi ya mambo katika maisha yake ya soka kutoka kwa mshambuliaji huyo wa Ureno.

"Umakini na azma aliyonayo, unapoangalia maisha yake, natamani kuishi hivyo," aliiambia BBC Sport Africa mwaka 2025.

Kuna upande mwingine wa mshambuliaji huyo wa Tanzania ambao ni zaidi ya kufunga mabao. Aliyekuwa mchezaji mwenzake Luvanga huko Al-Nassr, golikipa Sara Khalid Al-Dossary, alimtaja Luvanga kupitia BBC Sport Africa kuwa mchezaji huyo, anakipaji kingine zaidi ya soka: ana dansi vizuri.

Sasa Luvanga anapeleka soka lake pamoja na haiba yake nchini Marekani. Uhamisho wake kwenda Washington Spirit unamfanya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanzania kucheza katika ligi hiyo ya Marekani (NWSL), hatua nyingine muhimu katika kuifanya soka la wanawake Tanzania kuwa sehemu ya soka la kimataifa.

Pia ataingia katika chumba cha kubadilishia nguo chenye idadi kubwa ya wachezaji kutoka Afrika, huku kikosi cha Washington Spirit sasa kikiwa na wachezaji saba wa timu za taifa za Afrika.

Licha ya mafanikio yake katika ngazi ya klabu, Luvanga hajawa na ushawishi kama huo akiwa na jezi ya Tanzania katika ngazi ya timu ya taifa ya wakubwa.

Mabao yake 12 kwa Tanzania yamefungwa katika ngazi ya vijana - 10 akiwa na timu ya Under-17 na mawili akiwa na timu ya U20, huku matatizo ya utimamu wa mwili yakipunguza ushiriki wake katika kampeni mbili zilizopita za kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON).