Tetesi za soka: Barcelona na Arsenal bado wanamwania Julián Álvarez

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Atletico Madrid hawana mpango wa kukubali ofa yoyote kwa ajili ya mshambuliaji wa Argentina Julián Álvarez, 26, licha ya Barcelona na Arsenal kuendelea kumfukuzia. (Fichajes).
Kocha wa zamani wa Liverpool Jürgen Klopp angependa kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani ikiwa Julian Nagelsmann ataondoka kufuatia kutolewa kwa Ujerumani katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia. (Fabrizio Romano)
Tottenham wanajiandaa kujaribu kumsajili mshambuliaji wa pembeni wa Uholanzi Crysencio Summerville, mwenye umri wa miaka 24, kutoka West Ham, baada ya kumsajili kiungo wa Ureno Mateus Fernandes, 21, kutoka klabu hiyo iliyoshuka daraja. (GiveMeSport)
Juventus wanamfikiria mshambuliaji wa Sunderland na Uholanzi Brian Brobbey, 24, kama mbadala wa chaguo lao la kwanza, mshambuliaji wa Ufaransa Randal Kolo Muani, 27, wa Paris St-Germain. (TuttoMercatoWeb)
Everton watajaribu kumsajili kiungo wa Villarreal na Senegal Pape Gueye, 27, au kiungo wa Parma na Ubelgiji Mandela Keita, 24, iwapo kiungo wao wa Senegal Idrissa Gueye, 36, hataongeza mkataba wake. (Teamtalk)
Aston Villa wanavutiwa na kiungo wa Celta Vigo na Guinea Ilaix Moriba, 23, na wanajiandaa kutoa ofa ya pauni milioni 15 kumsajili. (Football Insider)
Kiungo wa England Curtis Jones, 25, huenda akaendelea kubaki Liverpool baada ya kusita kujiunga na Nottingham Forest, huku Inter Milan wakishindwa kufikia kiwango cha fedha kinachohitajika kumsajili. (Liverpool Echo)
Coventry City wanatarajiwa kumsajili beki wa Uswisi Aurèle Amenda, 22, kutoka Eintracht Frankfurt, ikiwa ni usajili wao wa kwanza tangu kurejea Ligi Kuu England. (Talksport)













