Marekani yafikiria kuhamisha wanajeshi wake kutoka Saudi Arabia - Gazeti la Wall Street

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal Marekani inatafakari kupunguza au kuhamisha baadhi ya wanajeshi na vifaa vyake vya kijeshi kutoka Saudi Arabia, hatua inayotokana na mvutano unaoongezeka kati ya Washington na Riyadh kuhusu vita vya Iran na usalama wa usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Saudi Arabia ilikataa kuruhusu matumizi ya baadhi ya kambi zake za kijeshi na anga yake wakati Marekani ilipoanzisha operesheni ya kulinda usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz mapema mwaka huu.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani waliozungumza na gazeti hilo, iliiweka Washington katika hali ngumu na kuathiri utekelezaji wa operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la Project Freedom, ambayo Rais Donald Trump alikuwa ameitangaza kwa lengo la kuhakikisha usalama wa meli zinazopita katika njia hiyo muhimu ya baharini.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa miongoni mwa hatua zinazozingatiwa ni kuhamisha baadhi ya wanajeshi na vifaa vya kijeshi kwenda mataifa kama Israel na Jordan, ambayo Washington inaamini yalishirikiana kwa karibu zaidi wakati wa mzozo na Iran.
Hata hivyo, Wall Street Journal imesisitiza kuwa hakuna uamuzi wa mwisho uliotolewa kuhusu uwezekano wa kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Saudi Arabia, na kwamba kwa sasa suala hilo liko katika hatua ya kutathmini hatua mbalimbali.
Hadi sasa, maafisa wa Marekani hawajathibitisha wala kukanusha uwezekano wa kuondolewa kwa wanajeshi wao kutoka Saudi Arabia hivi karibuni.
Unaweza kusoma;


