Afrika ilivyoweka historia ya uwakilishi katika uchaguzi wa Marekani

.
    • Author, Basma El Atti
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

JD [Vance], habibi (mpenzi wangu)."

Hayo yalikuwa maneno ya utani yasiyo ya kawaida kusikika katika mkutano wa kusherehekea ushindi wa chama cha Democratic baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.

Aliyeyasema ni Abdul El-Sayed, mwenye umri wa miaka 42, ambaye wazazi wake walihamia Marekani kutoka Misri. Katika mkutano huo wa ushindi, alimzungumzia kwa utani Makamu wa Rais JD Vance, ambaye alikuwa amefanya kampeni dhidi yake, lakini sasa ndiye atakayemwapisha Januari kuwa Seneta mpya wa jimbo la Michigan.

Hata hivyo, El-Sayed si mwanasiasa pekee mwenye mizizi ya Afrika aliyepata mafanikio katika uchaguzi huu. Kuanzia mbunge mwanamke wa kizazi cha Gen Z aliyezaliwa Ethiopia hadi wagombea wenye asili ya Nigeria, wanasiasa wengine kadhaa wenye asili ama uhusiano na Afrika wamefanikiwa kuingia katika nafasi za uongozi.

Uchaguzi wa katikati ya muhula hufanyika baada ya miaka miwili ya kipindi cha urais wa miaka minne. Katika uchaguzi huo, Wamarekani huchagua wawakilishi wao katika Bunge la Congress pamoja na maelfu ya viongozi katika ngazi za majimbo na serikali za mitaa.

Abdul El-Sayed - Misri

s
Maelezo ya picha, El-Sayed akiwa na mkewe Sarah Jukaku mwenye ushungi

El-Sayed, aliyezaliwa Marekani, alitumia sehemu kubwa ya kampeni yake kujibu mashambulizi kutoka kwa vyombo vya habari vya kihafidhina na Rais Donald Trump. Trump alimtuhumu kuwa anaunga mkono Muslim Brotherhood, tuhuma ambazo El-Sayed alizikanusha.

"Jina langu ni Abdul Rahman Mohammed El-Sayed," alisema kwa lafudhi ya Kiarabu cha Misri mbele ya umati wa watu waliokuwa wakishangilia ushindi wake.

Jina lake la Kiislamu lenye asili ya Kiarabu lilikuwa moja ya mambo yaliyotumiwa na wapinzani wake kumshambulia. Ushindi huo unamuweka katika nafasi ya kuwa seneta wa kwanza Muislamu nchini Marekani.

Katika kampeni yake, El-Sayed alitumia zaidi mitandao ya kijamii kuwafikia wapiga kura, hususan vijana. Video zake za TikTok zilionyesha akizungumza moja kwa moja na kizazi cha Gen Z, akitumia vichekesho vinavyopendwa na vijana hao na hata kuvaa bangili za urafiki.

Akiwa na uzoefu wa kusimamia huduma za afya ya umma, ajenda yake ilijikita katika sera za mageuzi, ikiwemo huduma za afya kwa wote kupitia Medicare for All, upatikanaji wa nyumba kwa gharama nafuu na kupunguza ushawishi wa makampuni makubwa katika siasa. Pia amekuwa mkosoaji mkubwa wa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel.

Melat Kiros - Ethiopia

Melat Kiros, wearing a white shirt, speaks on a stage on Colorado election night, with two US flags behind her.
Maelezo ya picha, Akizaliwa Addis Ababa, familia ya Melat Kiros ilikwenda Denver wakati huo akiwa mtoto mchanga
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Akiwa na umri wa miaka 29, Melat Kiros ameweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza wa kizazi cha Gen Z kuchaguliwa kuingia katika Bunge la Congress la Marekani.

Kiros alizaliwa Addis Ababa, Ethiopia, lakini familia yake ilihamia Marekani akiwa bado mtoto mchanga. Alikulia Denver, Colorado.

Kabla ya ushindi wake, hakuwa amewahi kushika nafasi yoyote ya uongozi iliyopatikana kupitia uchaguzi. Hata hivyo, alifanikiwa kumshinda mbunge aliyekuwa amehudumu kwa mihula 15 katika kura za maoni za chama cha Democratic katika jimbo la Colorado, kabla ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Jumanne.

Kama ilivyokuwa kwa El-Sayed, kampeni ya Kiros ilijikita katika masuala yanayowagusa vijana wenye misimamo ya mageuzi, yakiwemo kupanda kwa gharama za maisha, huduma za malezi ya watoto kwa wote na upatikanaji wa huduma za afya kupitia Medicare for All.

Msimamo wake wa kukosoa vikali vita vya Israel huko Gaza umemuingiza katika mijadala yenye utata. Hata hivyo, Kiros amesisitiza kuwa ukosoaji wake unalenga serikali ya Israel, si watu wa dini ya Kiyahudi.

Mwaka 2023, alipoteza kazi katika kampuni kubwa ya uwakili mjini New York baada ya kukataa kuondoa barua ya wazi aliyokuwa ameandika.

Barua hiyo ilikuwa inazungumzia msimamo wa makampuni kadhaa ya uwakili yaliyokuwa yamezitaka taasisi za elimu ya sheria kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya chuki dhidi ya Wayahudi katika vyuo vikuu, wakati wanafunzi walipokuwa wakiandamana kuunga mkono Palestina.

Kiros alilaani vitendo vya chuki dhidi ya Wayahudi, lakini akaziambia kampuni hizo za uwakili, ikiwemo ile aliyokuwa akiifanyia kazi, kuwa hazipaswi kuchanganya chuki hizo na mjadala wa kisiasa kuhusu uhalali wa kuwepo kwa taifa la Israel.

Anasema tukio la kufutwa kazi lilimfanya aanze kufikiria kwa uzito zaidi kuhusu kujihusisha na siasa.

Adrian Boafo - Ghana

Adrian Boafo (left) greets Rep. Steny Hoyer, who is retiring from the seat, during a press conference. Several supporters holding a blue and white signs fearing Boafo's name and the Democratic Party.
Maelezo ya picha, Wazazi wa Adrian Boafo walihamia Marekani kutoka Ghana

Mwanasiasa mwingine aliyeweka historia ni Adrian Boafo, Mmarekani wa kizazi cha pili mwenye asili ya Ghana.

Boafo ataiwakilisha jimbo la tano la uchaguzi la Maryland katika Bunge la Congress, akichukua nafasi ya mwanasiasa mkongwe Steny Hoyer, ambaye amestaafu baada ya zaidi ya miaka 40 katika siasa.

Akiwa na umri wa miaka 32, Boafo alizaliwa Virginia na kukulia katika Kaunti ya Prince George's, Maryland. Wazazi wake walihamia Marekani kutoka Ghana.

Safari yake ya kuingia Congress ilianza katika siasa za serikali za mitaa. Aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Jiji la Bowie kabla ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi katika Bunge la jimbo la Maryland mwaka 2023.

Pia aliwahi kufanya kazi na Hoyer, kabla ya hatimaye kushinda uchaguzi wa kumrithi.

Katika kampeni yake, Boafo alijikita katika kupunguza gharama za maisha, huduma za malezi ya watoto na kulinda ajira za wafanyakazi wa serikali ya shirikisho. Suala hilo lilikuwa muhimu katika eneo analoliwakilisha, ambalo liko karibu na Washington DC na lina maelfu ya wafanyakazi wa serikali.

Katika ujumbe wake baada ya ushindi, Boafo alisema hajawahi kuona umuhimu wa kuwatumikia wapiga kura wake ukiwa mkubwa kama sasa. Alitaja kupunguzwa kwa ajira za serikali, kupanda kwa gharama za maisha na hatua kali za utawala wa Trump dhidi ya wahamiaji kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

Junior Ezeonu na Carol Kazeem - Nigeria

Mafanikio ya wanasiasa wenye asili ya Afrika hayakuishia katika Bunge la Congress. Baadhi yao pia wamepata nafasi muhimu katika uongozi wa majimbo na serikali za mitaa.

Junior Ezeonu alizaliwa Nigeria na kuhamia Marekani akiwa mtoto mdogo.

Akiwa na umri wa miaka 27, tayari alikuwa amekuwa diwani mwenye umri mdogo zaidi katika Jiji la Grand Prairie, kabla ya kushinda kiti katika Bunge la jimbo la Texas.

Naye Carol Kazeem, mwenye umri wa miaka 34, ni mwanasiasa wa jimbo la Pennsylvania mwenye asili ya Nigeria ambaye amefanikiwa kutetea nafasi yake katika jimbo la 159 la uchaguzi.

Kwa jumla, wagombea wasiopungua wanne wenye asili ya Nigeria walishinda katika uchaguzi uliofanyika Novemba 3.

Katika mitandao ya kijamii, watu wamekuwa wakichapisha matokeo hayo kama chanzo cha hamasa, hususan nchini Nigeria na Kenya, ambazo zinatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu mwaka 2027.

Ilhan Omar - Somalia

Ilhan Omar

Miongoni mwa wanasiasa waliorejea katika Bunge la Congress ni Ilhan Omar, mwenye umri wa miaka 44, aliyezaliwa Somalia.

Omar amefanikiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa tano licha ya uchunguzi unaoendelea wa serikali ya shirikisho kuhusu nyaraka zake za uhamiaji.

Maafisa wa serikali walifanya upekuzi katika makazi yake mjini Washington mwezi Oktoba kama sehemu ya uchunguzi huo. Omar amekanusha kufanya kosa lolote na hadi sasa hajafunguliwa mashtaka ya jinai.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia Congress mwaka 2018, na kuwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Somalia pamoja na mmoja wa wanawake wa kwanza Waislamu kuhudumu katika chombo hicho cha kutunga sheria.

Amekuwa pia mmoja wa wanasiasa wanaoshambuliwa mara kwa mara na Trump, ambaye amekuwa akimkosoa yeye pamoja na wahamiaji wengine kutoka Somalia.

Trump aliwahi kutumia lugha ya dharau kuelezea baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Somalia. Hata hivyo, mwezi Oktoba, mshauri wake mwenye asili ya Yemen, Amer Ghalib, alisema rais huyo angeacha kutumia lugha ya aina hiyo.

Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi