Waisraeli na Wamarekani kwenye uchaguzi, huku matokeo yakitarajiwa kuwa na athari duniani kote.

Chanzo cha picha, Getty
- Author, James Landale
- Nafasi, Diplomatic correspondent
- Akiripoti kutoka, Jerusalem
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Uchaguzi wa Israel unafanyika leo, huku Marekani ikijiandaa kufanya uchaguzi wa katikati ya muhula wiki ijayo.
Matokeo ya chaguzi hizi mbili yanatarajiwa kuwa na athari kubwa si kwa mustakabali wa nchi hizo pekee, bali pia kwa vita vya Iran, usalama wa Mashariki ya Kati na uchumi wa dunia.
Huenda Tip O'Neill, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Marekani, alikuwa sahihi aliposema kuwa "siasa zote ni za ndani". Hata hivyo, matokeo ya chaguzi hizi bila shaka yatakuwa na athari duniani kote.
Hii ni kwa sababu chaguzi hizo hazitokei tu karibu kwa wakati mmoja; pia zimefungamana kwa namna mbalimbali.
Serikali itakayoongoza Israel itaathiri kwa muda mrefu mustakabali wa Mashariki ya Kati na vita vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo.
Vilevile, mabadiliko yoyote katika uwiano wa vyama ndani ya Bunge la Marekani yanaweza kuathiri si vita hivyo pekee, bali pia mustakabali wa uchumi wa dunia.
Kuna pia uhusiano wa moja kwa moja kati ya wapiga kura wa nchi hizo mbili. Kundi la utetezi wa maslahi ya chama cha Republican nchini Israel, Republicans Overseas Israel, linakadiria kuwa takriban Waisraeli 500,000 wenye pasipoti za Marekani wanaweza kupiga kura katika chaguzi zote mbili.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekuwa akisisitiza uhusiano wake wa karibu na Rais wa Marekani, Donald Trump. Uhusiano huo umeangaziwa pia kwenye bango la kampeni za chama chake cha Likud mjini Tel Aviv.
Marc Zell, mwenyekiti wa kundi hilo, amesema wapiga kura hao wanaweza kushawishi matokeo ya mashindano makali ya uchaguzi nchini Marekani, yakiwemo ya kiti cha Seneti katika jimbo la Michigan.
Anakadiria kuwa wapiga kura 10,000 watatuma kura zao za posta kutoka Israel kwa ajili ya uchaguzi huo.
"Wanaweza kweli kuleta tofauti," aliiambia BBC.
Hata hivyo, uhusiano wa kisera kati ya nchi hizo mbili una uzito mkubwa zaidi, hasa kuhusiana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Mashambulizi makubwa ya anga yaliyoanza mwezi Februari yaliharibu maeneo mengi ya kijeshi na kuwaua viongozi wengi wa Iran. Lakini hayakufanikiwa kuiondoa madarakani serikali ya Iran.
Badala yake, Iran ilijibu kwa mashambulizi makali katika eneo la Ghuba na kutwaa udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya nishati inayosafirishwa katika eneo hilo.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Suala la Iran
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uchaguzi nchini Israel umeanza huku kampeni za kisiasa zikiwa tayari zimeathiri maamuzi kuhusu usalama na vita vya Iran.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametumia kampeni hizo kuzungumzia uwezekano wa kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran.
Pia ametoa madai mapya kuhusu tishio la nyuklia la Iran, bila kuwasilisha ushahidi, huku akisisitiza tena kuwa serikali ya Kiislamu ya Iran lazima iondolewe madarakani.
Hatua hiyo inaonekana kulenga kuimarisha taswira yake kama kiongozi anayeweza kulinda usalama wa Israel, ambayo ilipata pigo kubwa baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel na kusababisha vifo vya watu wengi.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameongeza mjadala kuhusu uwezekano wa mashambulizi mapya dhidi ya Iran baada ya kumuunga mkono Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika jitihada zake za kuchaguliwa tena.
Trump amesema kuwa yeye na Netanyahu wanapaswa "kukamilisha kazi nchini Iran hivi karibuni," kauli inayodokeza kuwa huenda nchi hizo mbili zikaendeleza hatua zao za kijeshi dhidi ya Iran.
Hata hivyo, licha ya matamshi makali ya vitisho vya kijeshi, kuna taarifa zinazokinzana kwamba Trump aliingilia kati kumzuia Netanyahu kuishambulia Iran kabla ya siku ya uchaguzi.
Inaripotiwa kuwa Trump ana hofu kwamba mashambulizi mapya yanaweza kusababisha bei za nishati kupanda tena, hali ambayo ingewakumbusha wapiga kura wa Marekani kuhusu vita dhidi ya Iran ambavyo wengi nchini humo wanavipinga.
Rais Trump amekuwa akifanya kampeni kuwaunga mkono wagombea wa chama cha Republican wanaowania viti katika Congress, ikiwemo kampeni ya Michigan siku ya Jumapili, ambako ushindani wa kiti cha Seneti ni mkali.

Chanzo cha picha, REUTERS/Jonathan Ernst
Je, mashambulizi dhidi ya Iran yanaweza kusubiri hadi baada ya chaguzi hizo?
Vyombo vya habari nchini Israel vimekuwa vikijadili uwezekano wa Netanyahu kujaribu kuimarisha nafasi yake ya kisiasa kwa kuishambulia Iran baada ya uchaguzi, akiwa waziri mkuu wa mpito.
Kwa mujibu wa nadharia hiyo, Netanyahu anaweza kutetea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayomhusisha yeye, badala ya kuruhusu vyama vya upinzani kuunda muungano wa serikali bila yeye.
Kwa muda mrefu, Netanyahu amejulikana kama mwanasiasa anayejua namna ya kunusurika katika misukosuko ya kisiasa nchini Israel.
Akiondolewa madarakani, angekabiliwa na uchunguzi rasmi kuhusu hatua alizochukua kabla ya mashambulizi ya Oktoba 7, pamoja na kuendelea kwa taratibu za kisheria zinazohusiana na madai ya ufisadi dhidi yake.
Mjadala kuhusu uwezekano huo umechukua uzito kiasi kwamba mpinzani wake, aliyekuwa mkuu wa jeshi la Israel Gadi Eisenkot, tayari ametangaza kuwa hatajiunga na serikali yoyote ya umoja wa kitaifa.
Kama ilivyo kwa wanasiasa wengi wakuu nchini Israel, Eisenkot anaiona Iran kama tishio kwa uwepo wa Israel na anaunga mkono hatua za kijeshi dhidi ya serikali ya Iran.
Hata hivyo, ameonya waziwazi dhidi ya kuendeleza vita kwa madhumuni ya kisiasa.
Trump anaangalia urithi atakaoacha
Huenda Trump akawa tayari zaidi kuishambulia Iran baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, iwapo hatakuwa tena na shinikizo kubwa la uchaguzi na akiamini kuwa mashambulizi mengine yanaweza kumwezesha kujiondoa katika vita hivyo.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa uchumi wa Iran umedhoofishwa sana na vita pamoja na vikwazo vya kiuchumi, kiasi kwamba mashambulizi mengine yanaweza kuwachochea Wairani kuipindua serikali yao.
Wengine wanaona mtazamo huo kuwa matumaini yasiyo na msingi wa kutosha.
Ni mkakati ambao umeshindwa mara kadhaa hapo awali, lakini bado una wafuasi ndani ya duru za maamuzi mjini Washington.
"Baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula, atakuwa katika hatua ya kufikiria urithi atakaoacha," mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi mwenye ufahamu wa karibu kuhusu masuala hayo aliniambia.
"Atataka kuonyesha kuwa bado ana uwezo wa kuchukua hatua na kufanikisha mambo katika masuala mengine, badala ya kuendelea kukwama katika matatizo ya ndani ya Marekani."
Nchini Israel, kuna makubaliano mapana miongoni mwa vyama vingi kuhusu tishio linalotokana na Iran na umuhimu wa kuzuia uwezo wake wa kijeshi.
Hata hivyo, iwapo wapiga kura watachagua serikali mpya, huenda wakapata waziri mkuu ambaye hana msukumo mkubwa wa kisiasa au maslahi binafsi ya kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran.
Katika mazingira hayo, Trump amedokeza kuwa msimamo wake pia unaweza kubadilika.
"Ikiwa Israel itakuwa na kiongozi asiyefaa, yaani mtu mwingine yeyote isipokuwa Bibi [jina la utani la Netanyahu], Marekani italazimika kufanya kazi hii yenyewe, na sina mwelekeo wa kufanya hivyo," aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
Netanyahu ametumia kampeni za uchaguzi za mwaka huu kuzungumzia uwezekano wa mashambulizi mapya dhidi ya Iran.
Si ajabu basi kwamba viongozi wa Iran wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kura za maoni nchini Marekani, kama wafanyavyo wachambuzi walioko ndani ya duru za kisiasa mjini Washington.
Hatari kubwa ni kwamba mashambulizi yoyote mapya baada ya uchaguzi yanaweza kuitumbukiza Mashariki ya Kati katika machafuko mapya iwapo Iran itajibu kwa nguvu.
Viongozi wa Iran wametishia hadharani na kwa faragha kushambulia viwanja vya ndege, mabomba ya kusafirisha nishati, nyaya za mawasiliano zilizo chini ya bahari, miundombinu ya nishati, mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari, pamoja na kambi na meli za kivita za Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliandika katika gazeti la Financial Times kwamba mashambulizi mapya yangeweka "maisha ya raia, ustawi wa mataifa yote ya eneo hili na uchumi wa dunia katika hatari kubwa".

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Vita vya Iran vinavyobadili siasa za Marekani
Moja ya matokeo ya vita dhidi ya Iran, pamoja na operesheni za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, ni kudhoofika kwa uungwaji mkono wa Israel ambao kwa muda mrefu ulikuwa ukishirikiwa na vyama vyote viwili vikuu vya Marekani.
Abdul El-Sayed, mgombea wa mrengo wa kushoto wa chama cha Democratic anayewania kiti cha Seneti katika jimbo la Michigan, amefanya kampeni ya kutaka kupunguzwa kwa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel.
"Mshirika anayechukua pesa zako ili kukusukuma kwenye vita ambavyo hupaswi kupigana, si mshirika," aliiambia ABC News.
Awali, Marekani na Israel zilishambulia Iran kwa lengo la kuharibu makombora yake ya masafa marefu, kudhoofisha uwezo wake wa nyuklia, kupunguza uungwaji mkono wake kwa makundi yenye silaha yanayoshirikiana nayo katika ukanda huo, na hata kuiondoa serikali yake madarakani.
Tangu wakati huo, malengo ya vita yamebadilika na kuelekezwa katika kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.
Brad Lander, mgombea wa Democratic anayewania kiti katika Congress mjini New York na ambaye pia yuko upande wa mrengo wa kushoto wa chama hicho, aliamua kwenda Ukingo wa Magharibi siku chache tu kabla ya uchaguzi.
Aliwasaidia Wapalestina kuvuna mizeituni na kwa muda mfupi akazuiliwa na vikosi vya Israel.
Tukio hilo lilimpa pia fursa ya kuendeleza ujumbe wake wa kisiasa kupitia mitandao ya kijamii.
Katika historia ya siasa za Marekani, hali hii si ya kawaida.
Hata Netanyahu mwenyewe ameonya kuwa huenda Israel ikalazimika kujifunza kuishi bila ulinzi wa Marekani katika siku zijazo.
Kiongozi wa chama cha Yashar nchini Israel, Gadi Eisenkot, ametangaza kuwa hatajiunga na serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi.

Chanzo cha picha, Chris Torres / EPA/Shutterstock

Chanzo cha picha, Abir Sultan Credit / EPA/Shutterstock
Nini kitatokea ikiwa Netanyahu au Trump watapoteza nguvu?
Iwapo Netanyahu atashindwa katika uchaguzi na kuondoka madarakani, hilo litamaliza uhusiano wa kisiasa kati yake na Trump ambao umekuwa na vipindi vya ukaribu na misuguano.
Wiki iliyopita, Trump alimwelezea Netanyahu kama "waziri mkuu shujaa mkubwa".
Lakini wakati wa kiangazi, alimtaja kama mtu "mwenye wazimu kupindukia".
Kiongozi mpya wa Israel angelazimika kujenga uhusiano mpya na rais wa Marekani ambaye huenda wakati huo akawa anaelekea kumaliza muda wake madarakani. Hilo lingebadilisha kwa kiasi kikubwa mienendo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Iwapo chama cha Democratic kitapata udhibiti mkubwa zaidi ndani ya Congress, huenda hilo likaweka mipaka fulani kwa uungwaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa Israel.
Congress ina mamlaka ya muda mrefu yanayoweza kutumiwa kudhibiti matumizi ya kijeshi. Pia inaweza kupunguza msaada wa kijeshi kwa Israel.
Hata hivyo, akiwa rais, Trump ataendelea kuwa na mamlaka makubwa ya utendaji na uwezo wa kutumia kura ya turufu kuzuia baadhi ya maamuzi ya Congress, huku akiendelea kuendesha vita kulingana na mtazamo wake.
Uamuzi wa Israel na Marekani kuingia vitani dhidi ya Iran mapema mwaka huu umebadilisha uchumi wa dunia na siasa za kimataifa.
Maamuzi yatakayofanywa na wapiga kura katika nchi hizo mbili katika siku zijazo yanaweza kuamua mwelekeo ambao dunia itachukua kuanzia hapa.




































